Skip navigation.
Home kabah

Utaratibu Sahihi Wa Kufanya Ruqya - 4 Malipo ya fedha kwa ajili ya kufanya Ruqya

(Na Fathi Al-Jundii)

Imefasiriwa na Ummu Ashraf

 

 

Je Ni Halali Kutoza Au Kupokea Malipo Ya Ruqya?

 

Qur’an na Sunna zinakemea isirafu

  ya fedha lakini ni watu wachache mno wanaozingatia makemeo hayo, hii yote ni kwa sasabu ya huba ye fedha waliyopandikizwa wanadamu.

Mbwa mwitu wawili wenye njaa waliotumwa kumwinda kondoo hawaleti madhara makubwa kulinganisha madhara yanayoipata dini kutokana na tamaa ya mali aliyonayo binadamu.” (Ahmad na Tirmidhi).

Yahya ibn Muath kasema, “pesa ni kama nnge, kama hustahiki, basi usiichukue, kwani ikikutafuna,  kwa hakika sumu yake itakuua” Alipoulizwa ni kwa vipi mtu anastahiki, akajibu, ‘Ni kuichukua kwa kutumia njia halali na kuitumia katika njia sahihi.’ Pia akasema, ‘Mwanadamu atafikwa na misiba miwili akiwa na fedha katika sakaratimauti’. Alipoulizwa ni ipi misiba hiyo, akajibu, ‘Fedha zote zitachukuliwa kwake na ataulizwa kuhusu fedha zote hizo. (Mukhtasari Minhaj Al-Qasidiin) 

Wanazuoni wa Kiislamu wanakubali kuwa ni halali kuchukua fedha kwa kufanya Ruqya. Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni wanasema kuwa ni bora zaidi kutopokea malipo yoyote zaidi ya malipo ya MwenyeziMungu.

Hapa lazima tutofautishe kati ya mtu anayetoza fedha na mtu anayepewa fedha bila kuiomba. Umar ibnul-Khattab kasimulia hivi: “Mtume wa Allah alikuwa na kawaida ya kunipa kitu lakini mimi nikawa namwambia, “si ungempa mtu masikini na mwenye kuhitaji zaidi kuliko mimi?’ Mtume (Salallahu alaihi wasalam) akaniambia, ‘kama unapewa kitu fulani bila kukiomba au bila ya kuwa na tamaa nacho, basi kichukue na kama hukupewa basi usikikimbilie (usikipupie)’. (Bukhari).

Lakini haina maana kuwa mtu apokee malipo ya Ruqya kutoka kwa watu ambao yeye anajuwa wako katika hali ngumu ila wanalazimika kutoa malipo ili kuepuka aibu. Katika mazingira haya ni kheri kuepuka kuchukua malipo hayo hasa hasa kama mtu anayefanya ruqya hana shida sana na malipo hayo.

Kuna ushahidi unaothibitisha kuwa malipo ya ruqya yatolewe iwapo mgonjwa amepona kabisa ugonjwa wake. Kwa maneno ya Abdul Barr  ‘...malipo ya kitu ambacho hakileti tija yoyote ni dhuluma na haramu” (At-Tamhiid).

Hii ni kinyume kabisa na vile wafanyavyo  ‘waganga’ wengi hivi leo ambao hutoza malipo ya kazi zao bila kutibu ugonjwa. Wengine wanazo kliniki na hospitali kabisa kupokea wagonjwa na kutoza malipo tofauti ya huduma kama vile malipo ya kufungua faili, kumuona daktari na malipo ya kusomewa ruqya!

Watu wamefanya hii ndio shughuli yao maalum wakiwahadaa watu wenye matatizo kuwa wao ni watu waliojaaliwa uwezo wa kutibu na kuponya. Kwa kuwa watu hawa hujipa haiba ya kuonekana kama ni watu wenye elimu kubwa ya dini, basi huweza kuwavuta watu wengi wenye matatizo.

                            Je Ruqya inaweza kuwa kazi ya kudumu?

Kwa kuangalia historia ya Mtume, historia ya Maswahaba na wanazuoni wachaMungu ambao wanafahamika kwa elimu yao ya dini, na kwa kazi waliyoifanya kwa jamii ya Waislamu, tutaona kuwa hakuna hata mmoja kati yao aliyejiajiri kutibu wagonjwa kwa njia ya ruqya.

Na wala hakuna yeyote miongoni mwao aliyekifanya kisomo cha ruqya kuwa ndiyo shughuli au kazi yake na kutambulika rasmi kwa kazi hiyo. Hakuna ubishi kuwa magonjwa yalikuwa mengi katika kila zama, lakini hakuna ushahidi  wowote kuwa Khalifa yeyote aliwahi kuteua “wasomaji wa ruqya” ili kuwasomea wagonjwa kama vile alivyoteua Mahakimu.

Kwa maana hiyo, 

ni muhimu kwa mgonjwa  kujisomea mwenyewe na kama akipata mtu mwenye ilimu ambaye ni mwaminifu na mchaMungu, si vibaya kumuomba amfanyie ruqya huku na yeye mwenyewe akishiriki kiimani na si kubweteka tu ‘asomewe’ na kubakia na imani potofu kuwa kisomo ndicho kinachomsaidia badala ya MwenyeziMungu. 

Watu wanaofanyiwa ruqya bila ya wao wenyewe kuwa na imani wako katika hatari ya kuangukia katika shirki ya kuwategemea wale wanaowafanyia hiyo ruqya badala ya kumtegemea MwenyeziMungu.

Inafahamika kuwa matendo halali, wakati mwingine, huharamika iwapo yanafanywa kwa utaratibu unaopingana na mafundisho ya Sharia. Lau kungelikuwa na kheri katika kufanya kazi ya kudumu katika fani ya tiba ya ruqya basi basi sote tungeshindana kufanya kazi hiyo.

Tumalize makala hii kwa nukuu hii kutoka  kitabu kiitwacho, Sincere Devotion cha Mwandishi Saddiiq Hassan Khan;

Matendo yote na maombi yote ya kutibu ugonjwa yanajuzu kufanyika iwapo maneno yanayotumika yanatoka katika Qur’an na Sunna au kama maneno hayo yanatoka kwa wachaMungu wa jamii za nyuma za Waislamu ambayo yameepukana na shirki . Lakini kinyume chake mambo hayo huwa haramu na husababisha ushirikina.

Vipo vitabu vingi vinavyohusiana na ruqya lakini muumini anashauriwa kutafuta mambo sahihi katika vitabu hivi na kuachana na yale yanayopingana na mafundisho ya Uislamu. Haya ni pamoja na maandiko ya waganga wadanganyifu wanaoandika hirizi . Mambo haya hayafai kabisa.

“Kwa hakika MwenyeziMungu Anawatosha waja watiifu ikiwa hawategemei chochote isipokuwa Yeye na ambao hawatafuti njia nyingine kujitibu ila kwa dua alizofundisha Mtume (Salallahu alaihi wasalam) na tiba halali. Yeyote anayejiepusha na mambo ya shaka huitakasa dini na kuipamba heshima yake lakini yule anayejiingiza katika mambo ya shaka hujitumbukiza katika jambo la haramu. Kwa hiyo, shirki yaweza kufanywa bila kutambua, mtu achukue tahadhari mno ili kuiepuka”. 

-Mwisho-