04- Wasiya Kumi Katika Mwisho Wa Suwrah Al-An'aam: Kutokukaribia Machafu

 

  Wasiya Kumi Katika Mwisho Wa Suwrah Al-An'aam  

 

04- Kutokukaribia Machafu

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَلَا تَقْرَبُوا الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ

Na wala msikaribie machafu yaliyo dhahiri na yaliyofichika. [Al-An’aam: 151]

 

 

Maana ya الْفَوَاحِشَ

 

Kila tabia na kitendo kibaya ikiwa ni cha kutendwa au cha kutamkwa ambacho kinatoka nje ya fitwrah (maumbile asili) ya mwana Aadam. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameharamisha katika kauli Zake zifuatazo:

 

إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالْإِحْسَانِ وَإِيتَاءِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَيَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَالْبَغْيِ ۚ يَعِظُكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ﴿٩٠﴾

Hakika Allaah Anaamrishia uadilifu na ihsaan na kuwapa (msaada) jamaa wa karibu; na Anakataza machafu na munkari na ukandamizaji. Anakuwaidhini ili huenda mkapata kukumbuka. [An-Nahl: 90]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 إِنَّ اللَّـهَ لَا يَأْمُرُ بِالْفَحْشَاءِ

“Hakika Allaah Haamrishi machafu. [Al-A’raaf: 28]

 

 

Na pia Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

 

 

 اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ

Soma (ee Muhammad Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) uliyoletewa Wahy katika Kitabu na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari [Al-'Ankabuwt: 45]

 

Mara nyingine katika Qur-aan fahshaa (kwa matamshi ya ujumla) inakusudiwa ni zinaa au liwati ambayo yamekatazwa kuyakaribia kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾

Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu umekuwa na ni njia mbaya kabisa. [Al-Israa: 32]

 

Na Anasema pia Allaah ('Azza wa Jalla):

 

وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ أَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ مَا سَبَقَكُم بِهَا مِنْ أَحَدٍ مِّنَ الْعَالَمِينَ ﴿٨٠﴾

Na (Tulimtuma) Luutw, alipowaambia kaumu yake: “Je, mnafanya uchafu (wa liwati) ambao hajakutangulieni nao yeyote katika walimwengu?” [Al-A’raaf: 80]

 

 

Na katika Sunnah:

 

عَنْ اِبْن مَسْعُود رَضِيَ اللَّه عَنْهُ قَالَ : قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ((لَا أَحَد أَغْيَر مِنْ اللَّه مِنْ أَجْل ذَلِكَ حَرَّمَ الْفَوَاحِش مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ)) متفق عليه

Kutoka kwa Ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna mtu mwenye wivu zaidi ya Allaah. Ndio maana Akaharamisha vitendo vichafu vinavyotendwa kwa dhahiri na kwa siri)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Na pia:

 

 

عن سَعْد بْن عُبَادَة قال: لَوْ رَأَيْت مَعَ اِمْرَأَتِي رَجُلًا لَضَرَبْته بِالسَّيْفِ غَيْر مُصَفَّح فَبَلَغَ ذَلِكَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ ((أَتَعْجَبُونَ مِنْ غَيْرَة سَعْد ؟ فَوَاَللَّهِ لَأَنَا أَغْيَر مِنْ سَعْد وَاَللَّه أَغْيَر مِنِّي مِنْ أَجْل ذَلِكَ حَرَّمَ الْفَوَاحِش مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ)) متفق عليه

Kutoka kwa Sa’ad bin ‘Ubaadah ambaye amesema: “Nikimuona mtu na mke wangu [wakifanya zinaa] nitamuua kwa upanga!” Ilipomfikia Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) habari hii alisema: ((Je, mnastaajabu wivu wa Sa’ad? Naapa kwa Allaah, mimi nina wivu zaidi kuliko Sa’ad, na Allaah Ana wivu zaidi yangu. Ndio maana Akaharamisha madhambi machafu yanayotendwa kwa dhahiri na kwa siri)) [Al-Bukhaariy na Muslim]   

 

 

Na pia al-fuhsh (machafu) imetajwa kwa ujumla katika kauli Zake Allaah ('Azza wa Jalla):

 

الَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ إِلَّا اللَّمَمَ

 

Wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu isipokuwa makosa madogo-madogo. [An-Najm: 32]

 

وَالَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ وَإِذَا مَا غَضِبُوا هُمْ يَغْفِرُونَ﴿٣٧﴾

Na wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu na wanapoghadhibika wao wanasamehe. [Ash-Shuwra: 37]

 

 

Dalili kuwa fuhsh (machafu) ina maana ya machafu mengineyo kama kutukana, kulaani, ghiybah (kusengenya) n.k ni kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

  

 إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿١٩﴾

Hakika wale wanaopenda uenee uchafu wa kashfa kwa wale walioamini; watapata adhabu iumizayo duniani na Aakhirah. Na Allaah Anajua nanyi hamjui. [An-Nuwr: 19]

 

 

Na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عبد الله بن مسعود  رضي الله عنه  أن رسول الله  صلى الله عليه وسلم  قال: ((ليس المؤمن بالطعان ولا اللعان ولا الفاحش ولا البذيء))  رواه أحمد و إسناده صحيح

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Muumini siye mwenye kutukana, wala kulaani, wala al-faahish [mwenye kufanya machafu] wala mwenye ujeuri)) [Imesimuliwa na Imaam Ahmad kwa isnaad Swahiyh]

 

 

Na pia,

 

عَنْ عَائِشَة قَالَتْ دَخَلَ عَلَى رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَهُود فَقَالُوا: السَّام عَلَيْك يَا أَبَا الْقَاسِم" فَقَالَتْ عَائِشَة : وَعَلَيْكُمْ السَّام قَالَتْ : فَقَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ " ((يَا عَائِشَة إِنَّ اللَّه لَا يُحِبّ الْفُحْش وَلَا التَّفَحُّش)) قُلْت أَلَا تَسْمَعهُمْ يَقُولُونَ السَّام عَلَيْك" ؟ فَقَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  (( أَوَمَا سَمِعْت أَقُول وَعَلَيْكُمْ)) البخاري

 

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ambaye amesema: Baadhi ya Mayahudi walikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakamuamkia kwa kumwambia: “As-saam ‘alayka yaa Abal Qaasim” [kwa maana mauti yakufikie Ee baba wa Qaasim]. Basi nikasema: “Wa ‘alaykumus-saam” [kwa maana na mauti yakufikieni]. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ee ‘Aaishah, hakika Allaah, Hapendi al-fuhsh wala at-tafahhush [uchafu na kutoa maneno machafu)). Nikasema: Je, hukuwasikia walivyosema “As-saam ‘alayka?” Akasema: ((Je, hukusikia nimewajibu “Wa ‘alaykum” [Na juu yenu])) [Al-Bukhaariy] 

 

 

Hadiyth hii inatufunza kwamba mtu anapokutukana ni bora kunyamaza au kumjibu lakini bila ya kurudia maneno machafu aliyotamka yeye, lakini sio kutamka maneno machafu.

 

Pia Hadiyth nyengine Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametahadharisha:

 

وعن أبي هريرة أن رسول الله صلى الله عليه و سلم قال  ((إياكم و الفحش؛ فإن الله لا يحب الفاحش و المتفحش)) رواه أبو داود و أحمد و إسناده صحيح.

 

((Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Tahadharini na uchafu, kwani Allaah Hapendi mwenye kufanya uchafu na mwenye kutamka machafu)) [Abu Daawuwd, Ahmad kwa isnaad Swahiyh]

 

 

Na pia mara nyengine al-fuhsh (machafu) ina maana ya ubakhili kama katika kauli za Allaah ('Azza wa Jalla):

 

الشَّيْطَانُ يَعِدُكُمُ الْفَقْرَ وَيَأْمُرُكُم بِالْفَحْشَاءِ

Shaytwaan anakutishieni ufukara na anakuamrisheni machafu, (ubakhili), [Al-Baqarah: 268]

 

Na pia:

 

  يَا أَيُّهَا النَّاسُ كُلُوا مِمَّا فِي الْأَرْضِ حَلَالًا طَيِّبًا وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿١٦٨﴾

Enyi watu! Kuleni katika vilivyomo ardhini vya halali, vizuri; na wala msifuate hatua za shaytwaan. Hakika yeye kwenu ni adui wa wazi.

 

 

إِنَّمَا يَأْمُرُكُم بِالسُّوءِ وَالْفَحْشَاءِ وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿١٦٩﴾ 

Hakika hakuna isipokuwa anakuamrisheni maovu na machafu (na ubakhili) na mseme dhidi ya Allaah msiyoyajua.  [Al-Baqarah: 168-169]. 

 

 

Baadhi ya madhara ya al-fuhsh (machafu)

 

 

1-Kujitenga mbali na Allaah ('Azza wa Jalla) kwa sababu Yeye (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hapendi wenye kutenda uovu huu kutokana na makatazo Yake.

 

 

2-Machafu ya zinaa na liwati 

 

Uislamu umeharamisha starehe za haraam, umeharamisha zinaa, ushoga, na kumuendea mke kinyume na maumbile. Taathira zake ni nyingi zikiwemo maradhi mabaya, kashfa na aibu, mtoto atakayezaliwa katika zinaa ataleta taathira kubwa mbaya katika jamii nzima.

 

 

3-Kujitenga mbali na watu kwani husababisha magomvi, chuki na uadui, mfarakano na kukhasimikiana.

 

 

4-Kujipatia malipo mabaya duniani na Akhera.

 

 

 

 

 

 

 

Share