Skip navigation.
Home kabah

Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) 9 - Hali Inayoruhusu Ghiybah


10-Rabiy'ul Aakhir  1428
 

Tumebainishiwa katika sheria yetu ya Kiislamu kuwa iko hali inayojuzu Ghiybah kwa sababu ya maslaha yanayopatikana.

 

Kupinga dhulma ya Qaadhi au Kiongozi au kuzuia dhulma isitendeke

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((لاَّ يُحِبُّ اللّهُ الْجَهْرَ بِالسُّوَءِ مِنَ الْقَوْلِ إِلاَّ مَن ظُلِمَ))

((Allaah Hapendi uovu uenezwe kwa maneno ila kwa mwenye kudhulumiwa)) [An-Nisaa: 148].  

 

Katika kushitaki kudhulumiwa haki yako

 

Kutoa aibu ya mtu inapohitajika mfano kushtaki kwa mhusika (mkuu atakayeweza kutatua matatizo) kuwa 'fulani kanidhulumu kadhaa na kadhaa, au kanifanyia kadhaa na kadhaa, au fulani hanipi haki yangu kadhaa na kadhaa". Hii ni kutokana na dalili ya Hadiyth ifuatayo:

 

عن عائشة رضي الله عنها : أن هنداً زوجة أبي سفيان قالت : يارسول الله إن أبا سفيان رجل شحيح وليس يعطيني ما يكفيني وولدي إلا ما أخذت منه ، وهو لا يعلم ، فقال :  ((خذي ما يكفيك وولدك بالمعروف))  متفق عيه

Kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba Hind mke wa Abu Sufyaan alisema: "Ewe Mjumbe wa Allaah, Hakika Abu Sufyaan ni mtu bakhili, wala hanipi kinachonitosha mimi na mwanangu ila ninachokichukua ilihali hajui" (ni sawa hivi nifanyavyo?)" Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Chukua kwa wema kinachokutosha wewe na mwanao)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Katika hali ya kubadilisha maovu

 

Huenda Muislamu akaona maovu yanatendeka na hatoweza kuyaondosha ila aulizie sababu, na huenda atakayeulizwa amseme aliyetenda maovu mfano 'fulani ndiye aliyefanya ovu hili kadhaa na kadhaa"

 

Kujikinga na shari, na kunapotolewa nasiha kwa Waislamu

 

عن فاطمة بنت قيس رضي الله عنها قالت أتيت النبي صلى الله عليه وسلم فقلت إن أبا الجهم ومعاوية خطباني فقال رسول الله صلى الله عليه وسلم ((أما معاوية فصعلوك لا مال له وأما أبو الجهم فلا يضع العصا عن عاتقه))  متفق

وفي رواية لمسلم ((وأما أبو الجهم فضراب للنساء)) وهو تفسير لرواية لا يضع العصا عن عاتقه وقيل معناه كثير الأسفار

Faatwimah binti Qays (Radhiya Allaahu 'anha) amesimulia: "Nilimuendea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nikamuambia: "Abul-Jahmi na Mu'aawiyah wameniposa". Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia: ((Ama Mu'aawiyah ni mtu fukara hana mali. Ama Abul-Jahmi haondoi fimbo juu ya shingo yake)) [Al-Bukhaaariy na Muslim]

 

Katika riwaaya nyingine ya Muslim imesema: ((Na ama Abul-Jahmi anawapiga mno wanawake))

Riwaaya hii ni tafsiyr ya riwaaya isemayo: ((…haondoi fimbo juu ya shingo yake)) Na pia imesemekana kuwa maana ya kutoondosha fimbo juu ya shingo yake ni kuwa, anasafiri mno.

Ibnu Taymiyyah amesema: Huenda anapotajwa kwa ubaya mtu kukawa ni kwa ajili ya nasiha kwa Waislamu kwa usalama au manufaa ya Dini yao na dunia yao.

 

Kuwasengenya mafisadi na watu wenye shaka

Kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo ambayo Al-Bukhaairy ametoa hoja kuwa Hadiyth hii yafaa kuwasengenya wafisadi na watu wenye shaka.

 

عن عائشة رضي الله عنها أن رجلا استأذن على النبي صلى الله عليه وسلم فقال ((ائذنوا له بئس أخو العشيرة)) متفق

Kutoka kwa 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) amesimulia kuwa mtu mmoja aliomba idhini ya kuingia kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Mruhusuni, ni mtu mbaya katika kabila lake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kuihami Dini na wanafiki

 

  عن عائشة رضي الله عنها قالت قال رسول الله صلى الله عليه وسلم ((ما أظن فلانا وفلانا يعرفان من ديننا شيئا))   رواه البخاري

قال الليث بن سعد أحد رواة هذا الحديث هذان الرجلان كانا من المنافقين

 

 

Kutoka kwa 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Sidhani fulani na fulani wanajua chochote katika Dini yetu)) [Al-Bukhaariy]

Allayth bin Sa'ad ambaye ni mmoja wa wapokezi wa Hadiyth hii amesema: "Watu hawa wawili walikuwa ni katika wanafiki"

 

Mwisho wa Mada Ya Ghiybah

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala Atuhidi tuweze kutunza ndimi zetu ili tujiepushe hatari na dhambi za Ghiybah. Aamiyn