09-Wasiya Kumi Katika Mwisho Wa Suwrah Al-An'aam: Kutekeleza Ahadi Ya Allaah

 

Wasiya Kumi Katika Mwisho Wa Suwrah Al-An'aam  

 

09- Kutekeleza Ahadi Ya Allaah

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَبِعَهْدِ اللَّـهِ أَوْفُوا

 

Na timizeni ahadi ya Allaah. [Al-An’aam: 152]

 

Kutimiza ahadi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), ni kutimiza amri Zake Alizotuamrisha na kujiepusha na makatazo yote katika Qur-aan na Sunnah.

 

 

Mojawapo ya ahadi baina yetu na baina ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni ile ahadi iliyopokelewa na wana Aadam wote kabla ya kuumbwa.   Tukashuhudia na kuchukua ahadi kwamba tutamtii Muumba wetu na hatutamshirikisha. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):  

 

 

 وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖ قَالُوا بَلَىٰ ۛ شَهِدْنَا ۛ أَن تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَـٰذَا غَافِلِينَ﴿١٧٢﴾

  Na pindi Rabb wako Alipochukua katika wana wa Aadam kutoka migongoni mwao, kizazi chao, na Akawashuhudisha juu ya nafsi zao, “Je, Mimi siye Rabb wenu?” Wakasema: “Ndio bila shaka, tumeshuhudia!” (Allaah Akawaambia): “Msije kusema Siku ya Qiyaamah: hakika sisi tulikuwa tumeghafilika nayo haya." [Al-A'araf : 172]

 

 

 

Ahadi nyengineyo ni kuunga undugu. Allaah ('Azza wa Jalla) Anawaonya wanaovunja ahadi Zake kwamba watakuwa miongoni mwa waliokhasirika:

 

 الَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ اللَّـهِ مِن بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٢٧﴾

Wale wanaovunja ahadi ya Allaah baada ya kuifunga Kwake na wanakata Aliyoyaamrisha Allaah kuungwa, na wanafanya ufisadi katika ardhi, hao ndio wenye khasara. [Al-Baqarah: 27]

 

 

Kutimiza nadhiri pia ni miongoni mwa kutimiza ahadi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema:

 

 يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا﴿٧﴾

Wanatimiza nadhiri na wanaiogopa siku ambayo shari yake ni yenye kuenea kwa upana. [Al-Insaan: 7]

 

 

Vile vile kutimiza ahadi tunazoahidiana sisi waja Wake. Mfano ahadi baina ya wanandoa, ahadi katika deni, ahadi katika kuamiliana kwa aina yoyote, kwa sababu ahadi hizo ni jukumu lipasalo kutimizwa. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَأَوْفُوا بِالْعَهْدِ ۖ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْئُولًا ﴿٣٤﴾

Na timizeni ahadi; hakika ahadi itakuwa ni ya kuulizwa [Al-Israa: 34]

 

 

Ahadi pia ni kutimiza miadi ya kukutana mahali kwa muda fulani.   Swala hili ni tatizo sugu katika jamii kwa vile imekuwa ni kawaida watu kutokutimiza miadi mpaka imepewa msemo kuwa ‘miadi ya Kiswahili’ kwa sababu ya kuchelewa katika mahali na muda walioahidiana watu kwa masaa kadhaa!  Mpaka imekuwa wenye shughuli kutaja nyakati za uongo za mialiko kwa kukhofu watu kuchelewa. Na wale wachache wenye kutimiza ahadi wanapofika mapema kwenye shughuli iwe wamepoteza muda wao kuwasubiri wale wanaochelewa kufika.  Kisha watu huona kuwa miadi ya kweli ni miadi ya Kizungu na hali mafunzo haya tumepewa sisi Waislamu kabla ya hao Wazungu kuja kuyatimiza.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuhusu Nabiy Ismaa’iyl ‘('Alayhis-Salaam):

 

وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِسْمَاعِيلَ ۚ إِنَّهُ كَانَ صَادِقَ الْوَعْدِ وَكَانَ رَسُولًا نَّبِيًّا ﴿٥٤﴾

Na mtaje katika Kitabu Ismaa’iyl. Hakika yeye alikuwa mkweli wa ahadi na alikuwa Rasuli na Nabiy. [Maryam: 54]

 

 

Mfano wa kutokutimiza ahadi ni kuahidi kumpa mwenzio kitu fulani, au kumuahidi kumsaidia tatizo lake fulani, kisha unapofika wakati unamkimbia usitimize ahadi yako. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameonya kuwa hiyo ni miongoni mwa alama za unafiki:     

 

((آية المنافق ثلاث : إذا حدث كذب ، وإذا وعد أخلف ، وإذا اؤتمن خان)) رواه البخاري ومسلم.

((Alama za Mnafiki ni tatu; anapozungumza huongopa, anapotoa ahadi huenda kinyume [hatimizi], na anapoaminiwa hufanya khiyana)) [Al-Bukhaariy na Muslim]  

 

 

Share