Skip navigation.
Home kabah

Mashairi - Nguzo Za Kiislamu, Ihsaan Na Imaan

Mtungaji: 'Aliy 'Umar 'Uthmaan

NGUZO ZA UISLAMU,

Nguzo za u-islamu,       idadi yake ni tano

Shahadayo muhimu,         ulimi na moyo mfano

Upwekesho Karimu,             na Muhammad bora mno

 

Nguzo ya pili ni swala,      idumishe maishani

Na ukilekee kibula,        kusimamisha dini

Ndilo kwanza suala,       taulizwa kaburini

 

Tatu nayo ni saumu,        faradhi Ramadhani

Baleghe memlazimu,         popote ulimwenguni

Wenye akili timamu,       ielezavyo Qurani

 

Nguzo ya nne ni zaka,     kwa wale wenye mali

Lazima sidhihaka,     si khiari tukubali

Wale waloneemeka,     kutofanya ubakhili

 

Tano kuhiji Makka,              kwa yule mwenye uwezo

Mara moja kumbuka,        ni ya mtume mafunzo

Mefaulu bila shaka,       atimizae hii nguzo

 

NGUZO YA IHSANI

 

Nguzo nayo ya ihsani,       ni moja tu uielewe

Umuabudu Manani,           kwamba umuonawe

Kama wewe humuoni,        akuonawe utambue

 

NGUZO ZA IMANI

 

Nguzo sita za imani,               uzipige makamama

Mola wetu muamini,               imara nawe simama

Alotukuka yakini,                  alotangu ya daima

 

Amini kuna malaika,               japo nawe huwaoni

Uwe na nzito hakika,              iyakinishe moyoni

Uondoe zote shaka,                msingi wa yetu dini

 

Kuna vitabu vinne,                  lazima uvikubali

Tafuta kweli uone,                  usiwe nawe jahili

Quran ndicho cha nne,             Zabur,Taurat,Injili

 

Usiwabugue mitume,                meteremsha Qadimu

Nyuma yao tusimame,            kutoka baba Adamu

Muhammadi tumsome,           na babuye Ibrahimu

 

Tuamini na qadari,                  mipango yake Mola

Asokuwa na mshauri,             kumuuliza masuala

Mwenye vazi kiburi,                arshini metawala

 

Kheri zote na shari,                   zatoka kwake Rabana

Hatuna sisi khiari,                   lolote yeye kinena

Shukuru na usubiri,                 upate mama kuvuna