01-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Alijulikana Kabla Ya Unabii Kuwa Ni Mkweli Na Mwaminifu

 

 Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم)

01-Alijulikana Kabla Ya Unabii Kuwa Ni Mkweli Na Mwaminifu

 

www.alhidaaya.com

 

 

Khulqah yake ya Asw-Swaadiq (mkweli) na Al-Amiyn (Mwaminifu) ilijulikana kabla ya kupewa Unabii kutokana na ukweli wake na uaminifu wake hata akapewa jina la “Asw-Swaadiqul-Amiyn” (Mkweli Mwaminifu):

 

1-Maquraysh wa Makkah walipokuwa wakiijenga upya Al-Ka’bah baada ya kutokea mafuriko makubwa yaliyosababisha maji kuingia ndani ya Msikiti na kubomoka, na pindi walipomaliza kujenga, wakataka kuirudisha Al-Hajar Al-Aswad (Jiwe jeusi) katika kona ya Ka’bah. Makabila manne ya ki-Quraysh  yalikaribia kupigana vita vikubwa kwa kuzozana nani kati yao anayepaswa kuliweka jiwe hilo katika kona yake. Mvutano  huo ukaendelea takriban masiku manne au matano.

Abuu Umayyah bin Mughiyrah Al-Makhzuwmiy ambaye alikuwa mtu mzima wao, akashauri kuwa liwekwe na mtu wa kwanza atakayeingia katika lango la Msikiti, na wote wakaridhika na rai hiyo. Allaah ('Azza wa Jalla) Akajaalia kuwa ni Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aingie na hapo wote wakapiga ukulele: "Huyu Mwaminifu! Sote tumeridhika naye huyu Muhammad."

 

Naye Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa hikma aliyojaaliwa na Allaah ('Azza wa Jalla) akaamrisha kiletwe kitambaa (kikubwa) kisha iwekwe Al-Hajar Al-Aswad katikati kisha akawataka viongozi wa makabila yote; kila mmoja wao akamate kona moja ya kitambaa hicho kisha wanyanyue kwa pamoja, na walipofikia mahali pa kuliweka, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akainyanyua Al-Hajar Al-Aswad kwa mikono yake miwili na kuiweka katika kona ya Al-Ka’bah. Mzozo ukamalizika na watu wakaridhika. [Ar-Rahiyq Al-Makhtuwm, Muhammad Rahmatul-Lil-’Aalamiyn]

 

 

2-Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alipomteremshia amri hii:

 

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ ﴿٢١٤﴾

Na onya (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) jamaa zako wa karibu. [Ash-Shu’araa: 214]

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipapanda juu ya jabali Swafaa akawaita watu wake na kuwaambia: "Enyi Maquraysh (na riwaayah nyingine enyi Banuu Manaaf, Enyi Banuu fulani na fulani). Je, ikiwa nitawaambieni kuwa wapanda farasi wapo nyuma ya jabali hili wakijitayarisha kukushambulieni, mtanisadiki?" Wote kwa pamoja wakamjibu:

"Bila shaka tutakusadiki, kwa sababu hatujapata kusikia kutoka kwako isipokuwa maneno ya kweli." Akasema: "Basi mimi ni mwonyaji kwenu juu ya adhabu kali iliyo mbele yenu. Okoeni nafsi zenu kutokana na moto…" [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo kwa riwaayah tofauti]

 

 

3-Kauli ya Abu Jahl:

 

“Wa-Allaahi mimi najua vilivyo kuwa yeye ni Mkweli….Tulikuwa tukimwita katika ujana  wake Asw-Swaadiq Al-Amiyn.” (Mkweli Mwaminifu). [Tafsiyr Al-Qurtwubiy]

 

 

4-Imepokelewa kutoka kwa Maswahaba mbali mbali wakihadithia Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakisema: “Amesema Asw-Swaadiq Al-Maswduwq” (mkweli aliyesadikishwa). Mfano ni Hadiyth ya ‘Abdullah bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu):

 

عن أبي عبْدِ الرَّحْمن عبدِ الله بنِ مسعودٍ رضي الله عنه قال: حدَّثَنا رسولُ الله صلى الله عليه وسلم وهُوَ الصَّادقُ المَصْدوق: ((إنَّ أَحَدَكُمْ يُجْمَعُ خَلْقُهُ في بَطْنِ أُمِّه أرْبعينَ يوْماً نُطْفَةً، ثُمَّ يَكُونُ عَلَقَةً مِثْلَ ذلك، ثُمَّ يَكُونُ مُضْغَةً مِثْلَ ذلك، ثُمَّ يُرْسَلُ إليه المَلكُ فَيَنْفخُ فيه الرُّوحَ ويُؤمَرُ بأرْبَعِ كلماتٍ: بِكَتْبِ رِزْقِهِ وأَجَلِهِ وعَمَلِهِ وشَقيٌّ أو سَعيدٌ، فَوَاللهِ الَّذي لا إله غَيْرُهُ إنَّ أَحَدَكُمْ ليَعْمَلُ بعَمَلِ أهْلِ الجَنَّةِ حتى ما يكُونَ بَيْنَهُ وبَيْنَها إلا ذِرَاعٌ، فَيَسْبِقُ عَليْه الكِتابُ فَيَعْمَلُ بعَملِ أَهْلِ النَّارِ فَيَدْخُلُها. وإنَّ أَحَدَكُمْ لَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهل النَّارِ حتى ما يَكُونَ بَيْنَهُ وبَيْنَها إلا ذِرَاعٌ، فَيَسْبِقُ عَلَيْهِ الكتابُ، فَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أهل الجنَّةِ فَيَدْخُلُها)) رواه البخاري ومسلم

 

Kutoka kwa Abuu 'Abdir-Rahmaan 'Abdillaah bin Mas‘uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba: “Ametusimulia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ambaye ni mkweli mwenye kuaminiwa: “Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arubaini zifuatazo huwa ni donge la damu, kisha arubaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah Humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho (yake). Na (Malaika huyo) anaamrishwa maneno manne; Kuandika rizki yake, ajali yake (umri atakaoishi duniani), amali zake, mtu muovu au mwema. Wa-Allaahi naapa kwa Yule Ambaye hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, hakika mmoja wenu huenda afanye ‘amali za watu wa Jannah hadi ikawa baina yake na Jannah ni dhiraa na kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya ‘amali ya watu wa motoni akaingia motoni. Na mmoja wenu hufanya ‘amali za watu wa motoni hadi ikawa baina yake na moto ni dhiraa na hapo kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya ‘amali ya watu wa Jannah akaingia Jannah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Pia Hadiyth ya   Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) Al-Bukhaariy Kitaab Al-Fitan, na wengineo.

 

 

5-Allaah ('Azza wa Jalla) Mwenyewe Amethitibisha kuwa ni Asw-Swaadiq (mkweli) Anaposema:

 

وَالَّذِي جَاءَ بِالصِّدْقِ وَصَدَّقَ بِهِ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ﴿٣٣﴾

Na yule aliyekuja na ukweli na wakausadikisha - hao ndio wenye taqwa. [Az-Zumar: 33]

 

Amesema Mujaahid na Qataadah na wengineo kuhusu: “Na yule aliyekuja na ukweli “Huyo ni Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)” [Tafsiyr Ibn Kathiyr]  

 

 

Share