04-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Akidhikika Pindi Waumini Wanapopata Shida, Akiwajali, Mpole Na Mwenye Huruma Mno

  

Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

004-Akidhikika Pindi Waumini Wanapopata Shida,

Akiwajali, Mpole Na Mwenye Huruma Mno  

 

www.alhidaaya.com

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٢٨﴾

Kwa yakini amekujieni Rasuli anayetokana na nyinyi wenyewe, yanamtia mashaka (na huzuni) yanayokutaabisheni, anakujalini, mwenye huruma kwa Waumini ni mwenye huruma mno, mwenye rahmah. [At-Tawbah: 128]

 

Imaam As-Sa’diy amesema: 

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ

Kwa yakini amekujieni Rasuli anayetokana na nyinyi wenyewe, yanamtia mashaka (na huzuni) yanayokutaabisheni.

 

Yaani: Wanamjua hali yake na wanajimakinisha kuchukua (ujumbe) kutoka kwake wala hawamwendei kinyume katika utiifu, naye ni (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwanasihi nasaha nzuri kabisa na akiwaendea mbio kuwafanikishia maslahi yao. Akidhikika na yale yanayokutieni mashaka na yanayokutaabisheni.

حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

anakujalini, mwenye huruma kwa Waumini ni mwenye huruma mno, mwenye rahmah.

 

Akikupendeleeni khayr na akifanya juhudi kukufikieni hizo khayr na akitilia hima kuongoka kwenu kufikia iymaan na akichukia shari kukufikieni na akifanya juhudi zisikufikieni shari hizo. Mpole na mwenye huruma mno, akiwahurumia kuliko wazazi wao wanavyowahurumia.

[Tafsiyr Imaam As-Sa'dy]

 

Katika ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anayojali na kuyakhofia kwa Waumini ni kuwakinga na moto. Kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

عَنْ جَابِرٍ، قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((مَثَلِي وَمَثَلُكُمْ كَمَثَلِ رَجُلٍ أَوْقَدَ نَارًا فَجَعَلَ الْجَنَادِبُ وَالْفَرَاشُ يَقَعْنَ فِيهَا وَهُوَ يَذُبُّهُنَّ عَنْهَا وَأَنَا آخِذٌ بِحُجَزِكُمْ عَنِ النَّارِ وَأَنْتُمْ تَفَلَّتُونَ مِنْ يَدِي)) مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mfano wangu na mfano wenu ni kama mtu ambaye anayewasha moto kisha wadudu na nondo wala nguo wakawa wanaanguka humo kisha yeye (huyo mtu) anajaribu kuwatoa humo nami huku nawazuia migongo yao isiangukie katika moto lakini mnateleza mikononi mwangu)) [Muslim]

 

Share