024-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah Ya Witr

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

024-Swalaah Ya Witr

 

 

· Taarifu Yake:

 

Witr kilugha ina maana ya idadi pweke kama moja, tatu na tano. Ni kama neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaposema:

((Hakika Allaah ni Witr, Anapenda Witr)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6410) na Muslim kutoka kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah].

 

Na neno lake: ((Mwenye kustanji, afanye kwa Witr)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa katika Mlango wa Twahara]

 

Ama kiistilahi, Swalaah ya Witr, ni Swalaah inayoswaliwa kati ya Swalaah ya ‘Ishaa na kuchomoza Alfajiri, na huhitimishiwa Swalaah ya usiku. Imeitwa hivyo kwa kuwa inaswaliwa kwa idadi ya Witr kama rakaa moja, au tatu, au zaidi, na haiwi kwa idadi shufwa.

Baadhi ya Maulamaa wanasema kwamba Swalaah hii ni sehemu ya Swalaatul Qiyaam na Tahajjudi, na wengine wanasema si Tahajjudi. [Al-Majmu’u cha An-Nawawiy (4/480)]

 

· 

Hukmu Yake:

 

Maulamaa wana kauli mbili kuhusiana na hukmu yake:

 

Ya kwanza:

 

Ni wajibu kwa madhehebu ya Abu Haniyfah. [Al-Hidaaya Ma’a Fat-hil Qadiyr (1/300), Al-Majmu’u (3/514) na Naylul Awtwaar (3/38)]

 

 Nao ni msimamo wake peke yake mpaka Ibn Al-Mundhir akasema: “Simjui yeyote aliyekubaliana na Abu Haniyfah katika hili”. Hoja zake ni:

 

1- Hadiyth Marfu’u ya Abu Hurayrah:

((من لم يوتر فليس منا))

((Asiyeswali Witr, si katika sisi)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/443). Kuna Hadiyth kama hii ya Buraydah ambayo ni Dhwa’iyf pia. Angalia Al-Irwaa (417)].

 

2- Hadiyth Marfu’u ya Abu Ayyuub:

((الوتر حق، فمن أحب أن يوتر بخمس فليفعل، ومن أحب أن يوتر بثلاث فليفعل، ومن أحب أن يوتر بواحدة فليفعل))

((Witr ni haki. Mwenye kupenda kuswali Witr rakaa tano afanye, mwenye kupenda kuswali Witr rakaa tatu afanye, na mwenye kupenda kuswali Witr rakaa moja afanye)). [Hadiyth Swahiyh Mawquuf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1422), An-Nasaaiy (8/238) na Ahmad (5/418). Maimamu wameibadili kuwa Swahiyh badala ya Mawquwf].

 

3- Hadiyth Marfu’u ya Abu Baswrah:

(( إن الله زادكم صلاة، وهي صلاة الوتر، فصلوها فيما بين العشاء إلى الفجر))

((Hakika Allaah Amewaongezeeni Swalaah, nayo ni Swalaah ya Witr, basi iswalini kati ya ‘Ishaa mpaka Alfajiri)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (6/397) na At-Twahaawiy (1/250). Angalia njia zake kwenye Al-Irwaa (423)].

 

4- Hadiyth Marfu’u ya Ibn ‘Umar:

(( اجعلوا آخر صلاتكم بالليل وترا))

((Ifanyeni Swalaah yenu ya mwisho ya usiku Witr)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (998) na Muslim (751)].

 

5- Hadiyth Marfu’u ya Abu Sa’iyd:

(( أوتروا قبل أن تصبحوا))

((Swalini Witr kabla hamjapambaukiwa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (754), At-Tirmidhiy (468), An-Nasaaiy (1/247) na Ibn Maajah (1189)]

 

6- Hadiyth ya ‘Aaishah: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali usiku. Na anapotaka kuswali Witr huniambia: ((Simama uswali Witr ee ‘Aaishah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (512) na Al-Bukhaariy kwa namba hii hii (512)]

 

Kauli ya pili:

 

Ni Sunnah iliyokokotezwa. Ni kauli ya Jamhuri ya Maulamaa kati ya Maswahaba, Taabi’iyna, waliowafuatia na maswahibu wa Abu Haniyfah.

 

Wamezijibu dalili zilizotangulia za Abu Haniyfah kwamba Hadiyth zake nyingi ni Dhwaíyf na hazina mashiko. Ama zilizothibiti kuwa Swahiyh  na ambazo amri zake zinaonyesha kuwa ni wajibu, basi amri hizo zinageuzwa kuwa ni Sunnah kutokana na Hadiyth zifuatazo:

 

1- Hadiyth ya Twalha bin ‘Ubaydullaah kuhusu mtu aliyemuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye Rasuli akamwambia: ((Swalaah tano mchana na usiku)). Akamuuliza: “Je, kuna jingine zaidi ya hilo linalonipasa?” Akamwambia: ((Hapana, isipokuwa kama utaswali Sunnah)). Mtu yule akasema: “Wal Laahi! Sitozidisha zaidi ya haya wala sitopunguza”. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Amefaulu kama atakuwa mkweli)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa mara nyingi].

 

Katika Hadiyth hii moja tu, kuna dalili kadhaa kwamba Witr si wajibu, zitaamuli vizuri.

 

2- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomtuma Mu’aadh kwenda Yemen alimwambia: ((Wewe unawaendea watu katika Ahlul Kitaab, basi la kwanza utakalowalingania  liwe ni kumwabudu Allaah. Wakimjua Allaah, basi wajulishe kwamba Allaah Amewafaradhia Swalaah tano mchana na usiku, na wanapolifanya..)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1395) na Muslim (19)].

 

Hadiyth hii ndiyo yenye nguvu zaidi kutolewa dalili, kwa kuwa kutumwa Mu’aadh kwenda Yemen, kulikuwa kabla ya kufariki Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa siku chache. Na lau kama Witr ingelikuwa ni wajibu, au jambo ambalo Allaah Amewaongezea watu katika Swalaah zao, basi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angelimwamrisha Mu’aadh awajulishe kwamba Allaah Amewafaradhishia Swalaah sita na si tano.

 

3- Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( الصلوات الخمس، والجمعة إلى الجمعة، كفارات لما بينهن ما لم تغش الكبائر))

((Swalaah tano, na Ijumaa hadi Ijumaa, ni kafara ya yaliyoko kati yake madhali hayakufanywa madhambi makubwa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (233), At-Tirmidhiy (214) na Ibn Maajah (1086)],

 

Hapa hakuitaja Witr katika Swalaah zilizotajwa  ambazo ni wajibu.

 

4- Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Witr juu ya mnyama. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (999), Muslim (700) na wengineo].

 

Na lau kama Witr ingelikuwa ni wajibu, basi isingelijuzu kuiswali juu ya mnyama kama ilivyotangulia.

 

5- Hadiyth ya Ibn Muhayriyz toka kwa Al-Mukhaddajiy aliyesema: “Mtu mmoja alimuuliza Abu Muhammad (ambaye ni katika Ma-Answaar) kuhusu Witr akasema: “Witr ni wajibu kama wajibu wa Swalaah”. Akamwendea ‘Ibaadah bin Swaamit akamwelezea hilo, naye akasema: “Ameongopa Abu Muhammad, nimemsikia Rasuli wa Allaah akisema: ((Swalaah tano Allaah Amezifaradhisha kwa Waja Wake)). [Ni Dhwa’iyf kwa kauli yenye nguvu. Imeshafanyiwa “ikhraaj” katika mlango wa Hukmu ya mwenye kuacha Qur-aan. Angalia takhriyj yake kiuchambuzi katika kitabu cha Ta’adhiym Qadrus Swalaahat kwa takhriyj yangu].

 

6- Hadiyth ya Jaabir aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituswalisha katika mwezi wa Ramadhwaan rakaa nane, na akaswali Witr. Ulipokuja usiku wa pili, tulikusanyika Msikitini tukitaraji kwamba atatoka ili atuswalishe. Tukakaa humo mpaka asubuhi ikaingia tukasema: Ee Rasuli wa Allaah! Tulitaraji utatoka utuswalishe. Akasema: ((Nilichukia – au nilihofia – Witr ifaradhishwe kwenu)). [Ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Khuzaymah (1070), Abu Ya’alaa (1802) na Ibn Hibaan (2409)].

 

· Faida

 

Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah (Rahimahul Laahu) amekhitari kwamba Witr ni wajibu kwa mtu ambaye ni mazoea yake kuswali usiku. [Al-Ikhtiyaarat uk. 64]

 

Ninasema: “Huenda kigezo chake ni kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ifanyeni Swalaah yenu ya mwisho ya usiku Witr)).

 

· Wakati Wa Witr

 

Maulamaa wote wamekubaliana kwamba muda wa kati ya Swalaah ya ‘Ishaa mpaka kuchomoza Alfajiri ni wakati wa Swalaah ya Witr. Kisha wakakhitalifiana kuhusu kujuzu kuswaliwa kwake baada ya Swalaah ya Alfajiri kwa kauli tano. Zilizo mashuhuri zaidi ni kauli mbili:  [Al-Awsatw, At-Tamhiyd (2/349 – Fat-hul Maalik), Bidaayatul Mujtahid (1/294) na Al-Majmu’u (3/518)]

 

Ya kwanza:

 

Haijuzu baada ya kuchomoza Alfajiri. Hii ni kauli ya Abu Yusuf, Muhammad bin Al-Hasan, Maswahibu wawili wa Abu Haniyfah, Sufyaan Ath-Thawriy, Is-Haaq, ‘Atwaa, An-Nakh’iy na Sa’iyd bin Jubayr. Kauli hii pia imehadithiwa toka kwa Ibn ‘Umar, na hoja yao ni:

 

1- Hadiyth ya Khaarijah bin Hudhaafah – iliyotangulia karibuni – isemayo: ((Basi iswalini muda wa kati ya ‘Ishaa mpaka kuchomoza Alfajiri)).[Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh. Tumeshaitaja na angalia Al-Irwaa (423)].

 

2-Hadiyth Marfu’u ya Abu Sa’iyd isemayo: ((Swalini Witr kabla hamjapambaukiwa)).[Hadiyth Swahiyh: Imetajwa hivi karibuni.]

 

Na katika tamshi lake: ((Mwenye kuingiliwa na Alfajiri na hakuwahi kuswali Witr, basi hana Witr tena)). [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Khuzaymah (1092), Ibn Hibaan (2409), Al-Haakim (1/301) na Al-Bayhaqiy (2/478)].

 

3- Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Harakisheni kuswali Witr kabla ya Alfajiri)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (750), Abu Daawuud (1436), At-Tirmidhiy (467) na Ahmad (2/37)].

 

4- Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swalaah ya usiku ni rakaa mbili mbili. Akichelea mtu kuingia Alfajiri, ataswali rakaa moja iwe ni Witr kwa zile alizoziswali)). [Hadiyth Swahiyh: Imetangulia hivi karibuni].

 

5- Imepokelewa na Ibn ‘Umar akisema: “Alfajiri ikiingia, basi Swalaah ya usiku na Witr zinakuwa hazipo tena, kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ((Swalini Witr kabla ya Alfajiri)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (469), Ibn Khuzaymah (2/148), Al-Haakim (1/302) na Al-Bayhaqiy (2/478)].

 

Ya pili:

 

Inajuzu baada ya kuchomoza Alfajiri madhali mtu bado hajaswali Alfajiri. Ni kauli ya Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Abu Thawr. Wametoa dalili kwa athar zilizopokelewa toka kwa Maswahaba kwamba walikuwa wakiswali Witr baada ya Alfajiri wakiwemo akina Ibn Mas-’oud, Ibn ‘Abbaas, ‘Ubaadah bin As-Swaamit, Abud Dardaa, Hudhayfah na ‘Aaishah. Na haikuhadhithiwa kinyume na hivyo kutoka kwa Maswahaba wengine zaidi yao.

 

· Lenye nguvu

 

Kauli ya kwanza inaonyesha kuwa ni madhubuti zaidi kutokana na uimara wa dalili zake. Ama athar toka kwa Maswahaba, inavyoonyesha kama anavyosema Ibn Rushd ni kuwa athar hizi haziendani kinyume na athar zilizotangulia, bali kujuzisha kwao hilo ni katika mlango wa kulipa, na si mlango wa kutekeleza. Lakini kauli yao itakuwa ni kinyume cha athar lau kama watazifanya Swalaah zao baada ya Alfajiri kuwa ndio wakati wake wa kuziswali. Liangalie hilo kwa makini. Kisha inatakikana itaamuliwe sifa ya Sunnah yao katika hilo vipi walitenda!!.

 

· Wakati Wake Mwafaka Zaidi

 

Tumeshasema kwamba inajuzu kuswali Witr kuanzia baada ya Swalaah ya ‘Ishaa mpaka kuchomoza Alfajiri, lakini wakati bora zaidi ni katika theluthi ya mwisho ya usiku.

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameswali Witr katika kila sehemu ya usiku; kuanzia mwanzo wake, katikati yake na mwisho wake, akamalizia Witr yake mwisho wa usiku”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (996) na Muslim (745).].

 

Na imesuniwa – kwa makubaliano ya wote – mtu aifanye Witr kuwa ndiyo Sunnah yake ya mwisho anayoiswali usiku kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ifanyeni Swalaah yenu ya mwisho ya usiku Witr)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa nyuma kidogo].

 

Lakini hii ni pale mtu atakapokuwa na uhakika wa kuweza kuamka mwisho wa usiku. Kama ni hivyo, imesuniwa aicheleweshe Witr yake mpaka mwisho wa usiku. Na kama atachelea kwamba hatoweza kuamka kwa ajili ya Witr mwisho wa usiku, basi imesuniwa hapo aswali Witr kabla hajalala. Na hii ni kwa Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdullaah (Radhwiya Allaahu Anhu) aliyesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Mwenye kuchelea kati yenu kwamba hatoweza kuamka mwisho wa usiku, basi aswali Witr mwanzoni mwake kisha alale. Na mwenye matumaini kati yenu ya kuamka mwishoni mwa usiku, basi aswali Witr mwishoni mwake, kwani Swalaah ya mwishoni mwa usiku huhudhuriwa, na hilo ni bora zaidi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (755), At-Tirmidhiy (455) na Ibn Maajah (1187)].

 

Imepokelewa toka kwa Abu Qataadah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza Abuu Bakr: ((Wakati gani unaswali Witr?)) Akajibu: “Ninaswali Witr kisha nalala”. Kisha alimuuliza ‘Umar: ((Wakati gani unaswali Witr?)). Akajibu: “Ninalala kisha naswali Witr”. Kisha akamwambia Abu Bakr: ((Umefanya kwa umadhubuti, au kwa kujiamini)) na ‘Umar akamwambia: ((Umefanya kwa nguvu ya kujiamini)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1421), Ibn Maajah (1202) na Ibn Khuzaymah (1084)].

 

· Je, Inajuzu Kuswali Sunnah Nyingine Baada Ya Kuswali Witr? Je, Witr Inaweza Kuswaliwa Zaidi Ya Mara Moja?

 

Mwenye kuswali Witr, kisha baada ya hapo akapata utashi wa kuswali Sunnah nyingine, basi Maulamaa wana kauli mbili juu ya suala hili:  [Fat-hul Qadiyr (1/312), Az-Zarqaaniy (1/285), Al-Majmu’u (3/521), Kash-Shaaf Al-Qinaa (1/427) na Bidaayatul Mujtahid (1/297)]

 

Ya kwanza:

 

Inajuzu, na mtu ana khiyari ya kuswali Sunnah azitakazo, lakini asiswali tena Witr. Ni msimamo wa Maulamaa wengi wakiwemo Hanafiy, Maalik, Hanbali na mashuhuri kwa Ash-Shaafi’iy. Pia ni kauli ya  akina An-Nakh’iy, Al-Awzaa’iy na ‘Alqamah. Nayo imehadithiwa toka kwa Abu Bakr, Sa’ad, ‘Ammaar, Ibn ‘Abbaas na ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anhaa).

Dalili ya kujuzisha hili ni haya yafuatayo:

 

1- Hadiyth ya ‘Aaishah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitoa tasliym kwa sauti ya wao kusikia, kisha huswali rakaa mbili baada ya kutoa tasliym akiwa amekaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (749)].

 

2- Hadiyth ya Ummu Salamah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali rakaa mbili baada ya Witr akiwa amekaa. [Isnadi yake ni laini: At-Tirmidhiy (471) na Ibn Maajah (1195). Ipo Hadiyth mwenza katika As-Swahiyh].

 

3- Hadiyth iliyotangulia ya Jaabir kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Mwenye kuchelea kati yenu kwamba hatoweza kuamka mwisho wa usiku, basi aswali Witr mwanzoni mwake kisha alale )). [Hadiyth Swahiyh: Tumeieleza karibuni]

 

Inafahamika kutokana na Hadiyth hii kwamba anapoamka – akiwa ashaswali Witr kabla ya kulala – basi anaweza kuswali.

 

Ama zuio la kuswali Witr zaidi ya mara moja, ni kutokana na Hadiyth ya Twaliq bin ‘Aliyy kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna Witr mbili usiku mmoja)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (468), Abu Daawuud (1439), An-Nasaaiy (3/229) na wengineo].

 

Ya pili:

 

Haijuzu kuswali Sunnah nyingine baada ya Witr ila kama ataitengua Witr yake, aswali tena, kisha amalizie kwa Witr. Maana ya kuitengua ni kuianza Sunnah yake kwa rakaa moja azifanye mbili kujumlisha na ile moja ya Witr yake, kisha aswali idadi ya shufwa kiasi apendacho, kisha amalizie kwa Witr. Na hii ndiyo kauli ya mwisho ya Ash-Shaafi’iy, nayo imehadithiwa toka kwa ‘Uthmaan, ‘Aliyy, Usaamah, Ibn ‘Umar, Ibn Mas-’oud na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu Anhum). Hoja yao ni neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ifanyeni Swalaah yenu ya mwisho ya usiku Witr)). [Hadiyth Swahiyh: Tumeieleza karibuni].

 

Kauli Yenye Nguvu:

 

Ni ya kwanza kutokana na kuthibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Sunnah baada ya kuswali Witr. Kitendo hicho kimetutaarifu kwamba inajuzu kufanya hivyo. Kuitengua Witr kwa picha tuliyoielezea hakuna nguvu kwa sababu mbili:

 

1- Witr iliyoswaliwa mwanzo inahesabiwa kuwa ishakuwa sahihi, hivyo hakuna maana kuitengua baada ya kuiswali, na haiwezekani ikageuka kuwa ni Sunnah nyingine kwa kuzifanya rakaa shufwa.

 

2- Sunnah ya rakaa moja haijulikani katika sharia, na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

· Idadi Ya Rakaa Za Witr Na Namna Yake

 

Inajuzu kuiswali Witr rakaa moja, au tatu, au tano, au saba, au tisa.

 

1- Kwa rakaa moja:

 

Inajuzu kwa mujibu wa kauli ya Jamhuri ya Maulamaa kwa kuwa rakaa moja inatosheleza makusudio, na kwa kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Swalaah ya usiku ni rakaa mbili mbili. Akichelea mtu kuingia Alfajiri, ataswali rakaa moja iwe ni Witr kwa zile alizoziswali)). [Hadiyth Swahiyh: Tumeieleza karibuni].

 

Na kwa Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Witr ni rakaa moja ya mwishoni mwa usiku)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (752) na wengineo].

 

Na ‘Aaishah anasema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali usiku rakaa kumi na moja, huifanya moja kati yake Witr”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (736), Abu Daawuud (1335), At-Tirmidhiy (440) An-Nasaaiy (3/234) na Ahmad (6/35)].

 

Ama Abu Haniyfah, yeye anasema kuwa Witr haiwi ila kwa rakaa tatu kutokana na Hadiyth isemayo:

(( المغرب وتر النهار))

((Maghrib ni Witr ya mchana)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/30,41), Ibn Abu Shaybah (2/81) na ‘Abdul Raaziq (4675) kutoka kwa Hadiyth Marfu’u ya Ibn ‘Umar. Maalik ameifanyia “ikhraaj” ikiwa Marfu’u (276). Hakuna madhara kuifanya Mawquwf, kwani Maalik huzifanya Hadiyh Marfu’u kuwa Mawquwf. Hadiyth hii ina wenza wake toka kwa ‘Aaishah na Ibn Mas-’oud]

 

Na kwa kuwa Maghrib – yenye rakaa tatu - imefananishwa na Witr ya Swalaah ya usiku, ni lazima Witr ya usiku iwe rakaa tatu!!

 

Ninasema: “Swalaah ya Magharibi - yenye rakaa tatu – kuwa Witr, hakuzuii nyinginezo kuwa Witr pia. Na kama Magharibi ni Witr ya mchana, basi dalili zilizotangulia zinatuarifu kwamba rakaa moja ni Witr ya usiku, na hili liko bayana.

 

2- Kwa rakaa tatu:

 

Nayo inajuzu kwa njia mbili, na zote zinafaa kisharia. Njia hizo ni:

 

Ya kwanza:

 

Aswali rakaa mbili kisha atoe tasliym, halafu aswali rakaa ya tatu peke yake.

 

Imepokelewa kwamba Ibn ‘Umar alikuwa akitoa tasliym kati ya rakaa mbili na Witr mpaka aagize baadhi ya mahitaji yake. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (991) toka kwa Maalik (1/125)].

 

Imepokelewa toka kwake kwa njia Marfu’u akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitenganisha shaf-’i na Witr kwa tasliym anayoisema kwa sauti tukaisikia”. [Swahiyh Bituruqihi: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/76), At-Twahaawiy (1/278) na Ibn Hibaan (2433-2435). Al-Haafidh ameitia nguvu katika Al-Fat-h (2/482)].

 

Linatolewa ushahidi hili na Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anasoma katika rakaa mbili ambazo baada yake huswali rakaa moja (Sabbihisma Rabbika Al-A’alaa) na (Qul yaa ayyuhal kaafiruwna), na katika rakaa ya Witr anasoma (Qul Huwa Allaah) na (Qul a’uwdhu birabbil Falaq) na (Qul a’uwdhu birabbin Naas). [Dhwa’iyf kwa nyongeza hii: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twahaawiy (1/285), Al-Haakim (1/305), Ad-daaraqutwniy (2/35) na Ibn Hibaan (3432). Hadiyth hii imekuwa Swahiyh bila kutaja “Mu’awwadhatayn” toka Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas na Ubayya bin Ka’ab kama itakavyokuja. Angalia At-Talkhiysw (533)]

 

Katika Swahiyh Ibn Hibaan kuna mlango maalumu usemao: (Kutaja habari zinazoonyesha kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitenganisha tasliym kati ya rakaa mbili na rakaa ya tatu).

 

Ya pili:

 

Aswali rakaa tatu kwa tashah-hudi moja

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa katika Ramadhwaan au mwezi mwingineo wowote akizidisha zaidi ya rakaa 11. Anaswali nne, basi usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha anaswali nne, basi usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha anaswali tatu….”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1147), Muslim (738) na wengineo].

 

Pia ‘Aaishah amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Witr rakaa tatu, hakai isipokuwa katika rakaa ya mwisho”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik (466), An-Nasaaiy (3/234), At-Twahaawiy (1/280), Al-Haakim (1/304) na Al-Bayhaqiy (3/31)].

 

· Tanbihi

 

Hairuhusiwi kuswali rakaa tatu kwa tashah-hudi mbili na tasliym moja kama ilivyo katika Swalaah ya Magharibi. Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Msiswali Witr ya rakaa tatu, bali swalini Witr ya rakaa tano au saba, wala msiifananishe na Swalaah ya Magharibi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Haakim (1/304), Al-Bayhaqiy (3/31), Ibn Hibaan (2429), na Ad-daaraqutwniy (2/24). Al-Haafidh katika At-Talkhiys anasema kuwa watu wa Isnadi yake wote wanaaminika. Hakuna dhara kwa waliosema kuwa ni Mawquwf].

 

· Sura Zinazosomwa Katika Rakaa Tatu

 

Anaposwali mtu rakaa tatu, basi imesuniwa ayasome yaliyomo katika Hadiyth hizi mbili:

 

- Ya Ibn ‘Abbaas asemaye: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema alikuwa akisoma katika Witr (Sabbihisma Rabbika Al-A’alaa) na (Qul yaa ayyuhal kaafiruwn) na (Qul Huwa Allaahu Ahad) katika rakaa rakaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (461) na An-Nasaaiy (3/236)].  Yaani katika kila rakaa Suwrah moja kati ya hizo tatu.

 

- Ya Ubayya bin Ka’ab aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika Witr (Sabbihisma Rabbika Al-A’alaa) na (Qul yaa ayyuhal kaafiruwn) na (Qul Huwa Allaahu Ahad), na anapotoa tasliym husema: (Subhaana Al-Maliki Al Qudduws) mara tatu. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1423), An-Nasaaiy (3/244) na Ibn Maajah (1171). Kuna makhitilafiano ndani yake yasiyo na madhara yoyote kwa Tawfiyq ya Allaah].

 

Mahanbali wamezishikilia Hadiyth hizi mbili. Maalik na Ash-Shaafi’iy wanaona ni mustahabu aongeze mtu “Mu’awwadhatayn” katika rakaa ya tatu kwa mujibu wa Hadiyth ya ‘Aaishah iliyotangulia, lakini isiwe ni ada yake. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

3- Kwa rakaa tano:

 

Inajuzu, na imesuniwa kama ataswali, asikae kwa tashah-hudi ila katika rakaa ya tano. Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali usiku rakaa 13, kati ya hizo akiswali Witr tano, na hakai isipokuwa katika rakaa ya mwisho”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (737), Abu Daawuud (1324) na At-Tirmidhiy (457)].

 

4- Kwa rakaa saba au tisa:

 

Inajuzu. Ikiwa ataswali kwa idadi hizi, imesuniwa aandamishe rakaa na asikae kwa tashah-hudi isipokuwa katika rakaa ya kabla ya mwisho – na asitoe tasliym – halafu asimame kwa rakaa ya mwisho, akae tashah-hudi halafu atoe tasliym.

 

Bi ‘Aaishah akiizungumzia namna ya Swalaah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: “Tulikuwa tukimtayarishia Rasuli mswaki wake, kisha Allaah Humwamsha wakati wowote Apendapo kumwamsha usiku. Huamka akapiga mswaki na kutawadha, kisha huswali rakaa tisa, na hakai katika rakaa hizo isipokuwa katika rakaa ya nane. Hapo humdhukuru Allaah, akamhimidi na kumwomba. Halafu hunyanyuka bila ya kutoa tasliym kwa rakaa ya tisa. Kisha hukaa akamdhukuru Allaah, akamhimidi na kumwomba. Halafu hutoa tasliym ya sisi kuisikia. Kisha huswali rakaa mbili baada ya kutoa tasliym nailhali amekaa. Hizo ndizo rakaa kumi na moja ee mwanangu. Na Rasuli wa Allaah alipowanda na kupata mwili, alikuwa akiswali Witr rakaa saba, na akafanya katika rakaa mbili kama alivyokuwa akifanya mwanzo, na hizo ni tisa ee mwanangu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (746), Abu Daawuud (1328) na An-Nasaaiy (3/199)].

 

· Je, Ni Sharti Swalaah Ya Witr Itanguliwe Na Swalaah Ya (Shaf-’i)?

 

Kwa maana kwamba, je mtu anaweza kuswali rakaa moja au tatu za Witr na zaidi ya hapo bila kuswali kabla yake chochote? Maalik na Ash-Shaafi’iy – wanaona kwamba Witr kwa rakaa moja haiwi ila baada ya kutanguliwa na shaf-’i. [Al-Muntaqaa cha Al Baajiy (1/223) na vitabu rejea husika]

 

Wanasema kwamba asili ya hilo ni ni Hadiyh isemayo: ((Swalaah ya usiku ni rakaa mbili mbili. Akichelea mtu kuingia Alfajiri, ataswali rakaa moja iwe ni Witr kwa zile alizoziswali)).

 

Lakini Mashafii na Mahanbali wanaona kwamba inajuzu kuswali Witr kwa rakaa moja tu ingawa hilo litakuwa ni kinyume cha ubora, na uchache wa ukamilifu ni rakaa tatu. [Haashiyat Al-Qalyouniy (1/212), Kash-Shaaf Al-Qinaa (1/416) na Al-Mughniy (2/150)]

 

Ninasema: “Huenda dalili za kujuzisha ni hizi zifuatazo:  [Bidaayatul Mujtahid cha Ibn Rushd (1/293) chapa ya Al-Kutub Al-‘Ilmiyyah]

 

1- Hadiyth ya ‘Aaishah asemaye: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali nami nimelala na kumkinga juu ya tandiko lake, na anapotaka kuswali Witr, huniamsha nami nikaswali Witr”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (512) na Muslim (512)].

 

Hadiyth hii inaonyesha kwamba Bi ‘Aaishah alikuwa akiswali Witr bila ya kutanguliza Shaf-’i.

 

2- Hadiyth ya ‘Aaishah tuliyoitaja karibuni kuhusiana na kuswali kwake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Witr rakaa saba na tisa, kisha kuswali kwake rakaa mbili akiwa amekaa. Tunafahamu katika Hadiyth hiyo kwamba Witr ni yenye kuitangulia Shaf-’i, na pia tunapata humo hoja kwamba si sharti Witr itanguliwe na Shaf-’i. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

· Qunuwt Katika Witr

 

Qunuwt ina maana mbalimbali. Kati ya maana hizo ni kusimama, kunyamaza, kutoacha ‘ibaadah, du’aa, tasbiyh na khushui. Ama kiistilahi, ni jina la du’aa katika Swalaah katika mahala mahsusi na katika kisimamo. [Al-Futuwhaat Ar Rabbaaniya ‘Alal Adhkaar An Nawawiyyah (2/286) na Baswaair Dhawiyt Tamyiyz (4/298)]

 

Qunuwt katika Swalaah ya Witr inaruhusika kisharia kwa mujibu wa Jamhuri ya Maulamaa kinyume na Maalik. [Ni mashuhuri kwamba yeye anasema ni karaha kufanya qunuwt katika Witr. Riwaya iliyopokelewa toka kwake inasema kwamba Qunuwt hufanywa katika nusu ya mwisho ya Ramadhwaan (Al-Kaafiy) cha Ibn ‘Abdul Barri (uk.74), Al-Qawaaniyn (uk.66), Al-Mughniy (2/580) na Al-Majmu’u (4/24)]

 

Lakini wamekhitalifiana kama qunuwt hiyo ni wajibu au Sunnah. [Abu Haniyfah anasema kwamba ni wajibu kinyume na Maswahibu wawili na Jamhuri. Al-Badaai-’i (1/273) na Al-Bahr Ar Raaiq (2/43)]

 

Au kama inakuwa katika Swalaah zote za Sunnah au katika Ramadhwaan tu. [Kwa Mahanafi ni mwaka wote, na kwa Mashaafi’i ni nusu ya mwisho ya Ramadhwaan hasa, nao wanaona kuwa inakuwa vyema kuifanya katika mwezi wote wa Ramadhwaan. Ama kwa Mahanbali, ni katika mwaka wote. Al-Badaai-’i (1/273), Al-Majmu’u (4/15), Al-Mughniy (2/58) na Al-Muhallaa (4/145)]

 

Au kama inakuwa kabla ya kurukuu au baada yake.  [Kwa Mahanafi, ni kabla ya kurukuu, na kwa Mashaafi’i na Mahanbali ni baada ya kunyanyuka toka kwenye rukuu [Vitabu rejea vilivyotangulia]

 

Au ni yepi yaliyosuniwa aombe kwayo katika qunuwt hiyo.  [Kwa Mahanafi na Mashaafi’i: Du’aa ni kwa (Allaahumma Ihdinaa fiyman Hadayta….), na kwa Mahanbali ni (Allaahumma innaa nasta’iynuka wa nastahdiyka…)]

 

Lililo sahihi ni haya yafuatayo:

 

1- Qunuwt imesuniwa baadhi ya nyakati katika wakati wowote wa mwaka

 

Asili ya hili ni Hadiyth ya Al-Hasan bin ‘Aliyy (Radhwiya Allaahu Anhu) aliposema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinifundisha maneno ya mimi kuyasema katika Witr:

((Allaahumma Ihdiniy fiyman Hadayta, wa ‘Aafiniy fiyman ‘Aafayta, wa Tawallaniy fiyman Tawallayta, wa Baariyk liy fiymaa A’atwayta, wa Qiniy sharra maa Qadhwayta, fainnaka Taqdhwiy walaa yuqdhwaa ‘alayka, wa innahuu laa yadhillu man Waalayta, Tabaarakta Rabbanaa wa Ta’alayta)).  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1425), At-Tirmidhiy (464), An-Nasaaiy (3/248) na Ibn Maajah (1178). Angalia Al-Irwaa (429)].

 

Na imepokelewa toka kwa “Ubayya bin Ka’ab akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Witr na kusoma Qunuwt kabla ya rukuu”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1425), At-Tirmidhiy (464), An-Nasaaiy (3/248) na Ibn Maajah (1178). Angalia Al-Irwaa (426)].

 

Nasi tumesema: “Qunuwt imesuniwa katika Witr “baadhi ya nyakati”, kwa kuwa Maswahaba waliohadithia kuhusu Witr, hawakuelezea kusomwa qunuwt ndani yake. Na lau kama Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angelikuwa anaifanya siku zote, basi wote wangelinukuu hilo kutoka kwake. Tunakubali kwamba ‘Ubayya bin Ka’ab peke yake amehadithia kuhusu hilo likifanywa na Rasuli, na hii inaonyesha kwamba Rasuli alikuwa akilifanya baadhi ya nyakati, na kwamba hilo si wajibu. Na hii ndio kauli ya Jamhuri ya Maulamaa kinyume na Abu Haniyfah”.  [Al-Albaaniy amebainisha na kufafanua mfano wa haya katika Swifatus Swalaat (uk. 179)]

 

2- Qunuwt katika Witr ni bora zaidi ifanywe kabla ya kurukuu na baada ya kisomo

 

Ni kwa Hadiyth iliyotangulia ya Ubayya bin Ka’ab isemayo: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Witr na kusoma Qunuwt kabla ya rukuu”.

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaswim akisema: “Nilimuuliza Anas bin Maalik kuhusu qunuwt akasema: “Qunuwt ilikuwepo”. Nikamwambia: “Je, ni kabla ya kurukuu au baada ya kurukuu?”. Akasema: “Ni kabla”. Nikamwambia: “Fulani kanieleza kwamba wewe umesema ni baada ya kurukuu”. Akasema: “Ni mwongo. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiifanya baada ya rukuu mwezi mzima. Alikuwa amepeleka watu 70 wanaosemekana kuwa ni wasomaji wakubwa mahiri kwa washirikina. Washirikna hawa walikuwa na mkataba na Rasuli wa Allaah, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawasomea qunuwt ya kuwaombea laana mwezi mzima”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1002) na Muslim (677)].

 

Al-Haafidh katika Al-Fat-h (2/569) amesema: “Mjumuiko wa yaliyokuja toka kwa Anas kuhusiana na hayo ni kuwa qunuwt ni kwa ajili ya haja [yaani kwa janga] baada ya rukuu, na hilo halina mvutano wowote. Ama ikiwa si kwa haja, basi lililo sahihi ni kuwa hufanywa kabla ya kurukuu. Maswahaba walitofautiana katika utendaji wa hilo, na kiilivyo hayo ni makhitilafiano yanayoruhusika”.

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdur Rahmaan bin Al-Aswad toka kwa baba yake akisema: “ ‘Abdullaah – yaani Ibn Mas-’oud – alikuwa hafanyi qunuwt kwa lolote katika Swalaah, isipokuwa katika Witr kabla ya rakaa”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr (9/238). Angalia Al-Irwaa (2/166)].

 

3- Yaliyosuniwa kuombwa ndani ya qunuwt

 

Katika qunuwt ya Witr, imesuniwa kuomba kwa yale ambayo Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimfundisha Al-Hasan bin ‘Aliy: ((Allaahumma Ihdiniy fiyman Hadayta…)) mpaka mwisho kama ilivyotangulia.

 

Inajuzu kumswalia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika qunuwt kwa kuthibiti hilo toka kwa Maswahaba. Limethibiti hilo wakati Ubayya bin Ka’ab alipowaswalisha watu katika Qiyaam ya Ramadhwaan, na pia wakati Abu Haliymah Mu’aadh Al-Answariy alipowaswalisha watu, naye ni mmoja wa wale ambao ‘Umar aliwateua kuswalisha Tarawehe. [Swifatu Swalaatin Nabiyy (uk.180)]

 

4- Si katika Sunnah kurefusha du’aa ya qunuwt

 

Yaliyothibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kumfundisha Al-Hasan du’aa ya qunuwt katika Witr, ni kuwa du’aa yenyewe ni nyepesi na haina urefu.

 

5- Je, inajuzu kughani kwa du’aa ya qunuwt?

 

Haijanukuliwa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala toka kwa Swahaba yake yoyote – kwa ninavyojua – kwamba alighani kwa du’aa, si katika qunuwt wala katika du’aa nyingine yoyote, nami nachelea kuwa ni uzushi hili wanaloliona Maimamu wengi kuwa ni jambo zuri hivi leo!!

 

Ibn Al-Hammaam amesema: “Sioni kuiachilia na kuvuta tuni katika du’aa – kama wanavyofanya baadhi ya wasomaji hivi leo – kunafanywa na yule aliyefahamu maana hasa ya du’aa na kuomba. Hilo si jinginelo bali ni aina ya mchezo. Tukichukulia uhalisia wa mambo kwa mtu mwenye ombi lake kwa Mfalme, ikiwa atawasilisha ombi lake kwa kuvuta tuni, kunyanyua sauti, kushusha, kukurubisha na kukariri kariri kama wimbo, basi hilo litazingatiwa moja kwa moja kama ni masikhara na mchezo. Manzili ya kuomba, inahitaji unyenyekevu na si kughani.” [Fat-hul Qadiyr (1/370, 371)]

 

6-Imesuniwa kunyanyua mikono miwili katika qunuwt

 

Imepokelewa toka kwa Anas kuhusiana na kisa cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwaapiza waliowaua wasomaji wake akisema: “Hakika nilimwona Rasuli wa Allaah kila anaposwali Alfajiri, hunyanyua mikono yake miwili akiwaapizia”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (3/137) na Al-Bayhaqiy (2/211)].

 

Pia imepokelewa toka kwa Abu Raafi’i akisema: “Niliswali nyuma ya ‘Umar bin Al-Khattwaab, akasoma qunuwt baada ya kurukuu, akanyanyua mikono yake na akasoma du’aa kwa sauti”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (3/137) na Al-Bayhaqiy (2/211)].

 

Abu Hurayrah alikuwa akinyanyua mikono yake katika qunuwt ya mwezi wa Ramadhwaan. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Nasr katika Kitabu cha Qiyaamul Layl ukurasa wa 138]

 

7- Hakuna usharia wa kupangusa uso au kifua kwa mikono miwili baada ya qunuwt

 

Hii ni kwa vile hakuna dalili yoyote inayothibitisha hilo. Al-Bayhaqiy anasema katika Sunanih (2/212): “Ama kupangusa mikono miwili usoni wakati wa kumaliza du’aa, sikulihifadhi hili kutoka kwa yeyote katika Masalaf katika du’aa ya qunuwt”.

 

Ninasema: “Si sahihi vile vile Hadiyth inayozungumzia kupangusa uso baada ya du’aa nje ya Swalaah. Sheikh wa Uislamu (22/519) anasema: “Ama kupangusa kwake uso wake kwa mikono yake, hilo halikufanywa na Rasuli. Kuna Hadiyth moja au Hadiyth mbili zinazogusia hilo lakini hazifai kama dalili. Allaahu Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

· Kufanya Tasbiyh Na Kuomba Du’aa Baada Ya Witr

 

Imesuniwa baada ya kutoa tasliym ya Witr, kufanya tasbiyh kutokana na Hadiyth ya Ubayya bin Ka’ab aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika Witr (Sabbihisma Rabbika Al-A’alaa) na (Qul yaa ayyuhal kaafiruwn) na (Qul Huwa Allaahu Ahad). Anapotoa tasliym husema: (Subhaana Al-Malik Al-Qudduuws) mara tatu. [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa karibuni].

 

Imepokelewa pia toka kwa ‘Aliy kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema mwishoni mwa Witr yake:

(( اللهم إني أعوذ برضاك من سخطك، وبمعافاتك من عقوبتك وأعوذ بك منك، لا أحصي ثناء عليك، أنت كما أثنيت على نفسك))

((Allaahumma inniy a’uwdhubika min sakhatwika, wa bimu’aafaatika min ‘uquwbatika wa a’uwdhubika minka, laa uhswiy thanaan ‘alayka, Anta kamaa Athnayta ‘alaa Nafsika)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1427), At-Tirmidhiy (3566), An-Nasaaiy (1/252) na Ibn Maajah (1179)].

 

· Kuilipa Witr

 

Mtu akilala akapitwa na Witr au akasahau kuswali, basi ataiswali anapoamka au anapoikumbuka wakati wowote ule. Hii ni kwa Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriyy aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Aliyelala akapitwa na Witr au akaisahau, basi aiswali anapopambazukiwa au anapokumbuka)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (465), Abu Daawuud (1431), Ibn Maajah (1188) na Ahmad. Angalia Al-Irwaa (2/153)].

 

Na kutokana na ujumuishi wa kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwenye kulala akapitwa na Swalaah, au akaisahau, basi aiswali anapokumbuka)).

 

Ujumuishi huu unakusanya Swalaah zote za faradhi na Sunnah. Kwa Swalaah za faradhi ni amri ya faradhi, na kwa Swalaah za Sunnah ni amri ya Sunnah. Aidha, atailipa Witr kama ilimpita kutokana na sababu yoyote kama ugonjwa na mfano wake.

 

Ninasema: “Anayefanya makusudi kuiwacha Witr bila ya udhuru wowote mpaka ikaingia Alfajiri, basi haruhusiwi kuilipa kwa mujibu wa uhakiki tulioufanya katika mlango wa kulipa qadhwaa. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

· Ni Rakaa Ngapi Za Kulipiwa Witr?

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapolala usiku au akaugua, huswali rakaa 12 mchana..”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (746) na wengineo].

 

Na imejulikana kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali usiku rakaa 11, na ikajulikana  kwamba kulipa kwake Witr mchana ilikuwa ni kwa shaf-’i. Kwa hiyo, mwenye mazoea ya kuswali Witr rakaa moja, atalipa mchana kwa kuswali rakaa mbili, na mwenye mazoea ya kuswali rakaa tatu, atazilipa nne na kadhalika.

 

Imesuniwa mtu afanye haraka kuilipa kabla ya Adhuhuri ili aandikiwe thawabu za Swalaah ya Usiku. Imepokelewa toka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( من نام عن حزبه أو عن شيئ منه، فقرأه بين صلاة الفجر وصلاة الظهر، كتب له كأنما قرأه من الليل))

(( Mwenye kulala asifanye uradi wake, au sehemu ya uradi huo, halafu akaja kuusoma kati ya Swalaah ya Alfajiri na Swalaah ya Adhuhuri, huandikiwa kama aliyeusoma usiku)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (747), At-Tirmidhiy (578), Abu Daawuud (1299), An-Nasaaiy (3/259) na Ibn Maajah (1343)].

 

Hadiyth hii inatuhimizia kuwahi haraka, na pia inaonyesha uweze

kano wa kwamba ubora wa kutenda jambo pamoja na kuzidishiwa maradufu, kunafungamana na ule wakati wake uliopangwa.  [Haashiyat As-Suyuutwiy ‘Ala An-Nasaaiy (3/259)]

 

· Rakaa Baada Ya Witr

 

‘Aaishah akizungumzia kuhusu namna Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akiswali usiku anasema: “Alikuwa anaswali rakaa 13; huswali rakaa nane, na Witr rakaa moja. Anapotoa tasliym, hupiga takbiyr akaswali rakaa mbili akiwa amekaa, na huswali rakaa mbili kati ya adhana ya Alfajiri na iqaamah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1159), Muslim (738) na wengineo].

 

Maulamaa wana miono mitatu kuhusiana na rakaa hizi mbili baada ya Witr:

 

1- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameziswali ili kubainisha kwamba inajuzu, naye hakudumu nazo, bali aliziswali mara moja au mara chache sana, na kwamba neno la ‘Aaishah “Alikuwa anaswali”, hakulazimishi kuwa alidumu au alikariri mpaka ije dalili inayothibitisha hivyo. [Sharhu Muslim ya An-Nawawiy (6/21) chapa ya Ihyaau At-Turaath Al-‘Arabiy]

 

2- Rakaa hizi mbili zinapita mapitio ya Sunnah na makamilisho ya Witr, kwani Witr ni ‘ibaadah kando, nazo zinakuwa ni kama rakaa mbili baada ya Magharibi, na hiyo ndiyo Witr ya mchana. Na rakaa mbili baada yake ni ukamilisho wake, pia na rakaa mbili baada ya Witr ya usiku.  [Zaadul Ma’adiy ya Ibn Al-Qayyim (1/318, 319)]

 

3- Rakaa hizi mbili ni mahsusi kwake Rasuli basi. Hivyo Hadiyth haiwi mahsusi kwa amri ya kuifanya Swalaah ya mwisho ya usiku Witr!! [Naylul Awtwaar (3/48) chapa ya Al-Hadiyth]

 

Ninasema: “Kauli mbili za mwanzo, kila moja ina uzito wa nguvu, ama ya tatu, hii ni lazima iangaliwe. Umahususi hauthibiti ila kwa dalili, na asili ya vitendo vyake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kufuatwa na kuigwa nasi. Ikiwa itasemwa: “ Kitendo chake Rasuli hakulifanyi agizo lake la kuifanya Swalaah ya mwisho ya usiku kuwa Witr kuwa ni agizo mahsusi”, basi sisi tunasema: “Ni kweli, lakini agizo hilo linageuzwa kuwa Sunnah kutokana na kauli yake iliyotangulia isemayo: ((Mwenye kuchelea kati yenu kutoweza kuamka mwishoni mwa usiku, basi aswali Witr mwanzoni mwake halafu alale..)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa karibuni].

 

Na kwa kumkubalia kwake Abu Bakr aswali Witr kabla ya kulala.  [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa karibuni].

 

Kwa mujibu wa Hadiyth hizi mbili, ni halali kuswali kwa aliyeamka baada ya kuwa aliswali Witr kabla ya kulala. Kisha nililidadisi agizo la Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) la kuswali rakaa mbili baada ya Witr katika Hadiyth Marfu’u ya Thawbaan isemayo:

(( إن هذا السفر جهد وثقل، فإن أوتر أحدكم فليركع ركعتين، فإن استيقظ وإلا كانتا له ))

((Hakika safari ni tabu na uzito, ikiwa mmoja wenu ataswali Witr, basi aswali rakaa mbili. Na ikiwa ataamka (itakuwa vyema), na kama hakuweza basi zitamtosheleza)). [Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-daaramiy (1594) na kwake limetumika neno "السهر" badala ya "السفر" , Ibn Khuzaymah (1106) na Ad-daaraqutwniy (2/36). Angalia Asw-Swahiyhah (1993)] ….nikakuta agizo limekutana na kitendo, na usharia ukathibiti. Hivyo agizo la kuifanya Witr mwisho wa usiku, ni agizo la kupendelewa hivyo. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

· Suwrah Zinazosomwa Katika Rakaa Mbili Baada Ya Witr

 

Imepokelewa toka kwa Abu Umaamah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali rakaa mbili baada ya Witr akiwa ameketi akisoma ndani ya rakaa hizo: (Idhaa zulzilatil ardhu) na (Qul yaa ayyuhal kaafiruwn). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (5/260), At-Twahaawiy (1/280-341), At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr (8/277) na Al-Bayhaqiy (3/33). Ina Hadiyth mwenza ya Anas].

 

· Imesuniwa Kulala  Baada Ya Rakaa Mbili

 

Imesuniwa kulala baada ya rakaa mbili za baada ya Witr – au baada ya Swalaah ya Usiku – mpaka iadhiniwe Alfajiri. Ibn ‘Abbaas katika Hadiyth yake ambapo anaelezea namna Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyoswali usiku wakati yeye alipolala kwa khalati yake Maymuwnah anasema: “Kisha akasimama kuswali, nami nikasimama nikafanya kama alivyofanya, halafu nikaondoka na kwenda kusimama kandoni mwake. Naye akauweka mkono wake wa kulia juu ya kichwa changu na akalikamata sikio langu la kulia na kulisokota. Halafu akaswali rakaa mbili, kisha rakaa mbili, kisha rakaa mbili, kisha rakaa mbili, kisha rakaa mbili, kisha rakaa mbili, halafu akaswali Witr. Baadaye alilala mpaka alipojiwa na mwadhini, akasimama, akaswali rakaa mbili nyepesi, kisha akatoka, akaswali Alfajiri”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj“ na Al-Bukhaariy (1146) na Muslim (739)]

 

Na katika riwaya ya Ibn Khuzaymah anasema: “Akaswali Witr tisa au saba, kisha akaswali rakaa mbili, halafu akaulaza ubavu wake mpaka nikasikia mkoromo wake, kisha Swalaah ikaqimiwa, akaondoka, akaenda kuswali”. Rakaa hizi mbili, inawezekana ni zile alizokuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiziswali baada ya Witr, na pia inawezekana zikawa ni rakaa mbili za Alfajiri. [Swahiyh ya Ibn Khuzaymah (2/157-158)].

 

Ninasema: “Uwezekano wa kwanza unatiliwa nguvu na Hadiyth ya Al-Aswad aliposema: “Nilimuuliza ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha): Ni vipi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaswali Swalaah ya usiku? Akasema: Alikuwa akilala mwanzo wake, anasimama mwishoni mwake akaswali, kisha hurejea kwenye tandiko lake. Na mwadhini anapoadhini hutoka haraka. Na kama ana kitu hivi huoga, na kama hana, hutawadha akatoka”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1146) na Muslim (739)].

 

Na hili halipingi uhalali wa kulala baada ya rakaa mbili za Sunnah ya Alfajiri, bali inavyoonyesha ni kuwa mara alikuwa akilala kati ya Swalaah ya usiku na Swalaah ya Alfajiri, na mara nyingine baada ya rakaa mbili za Sunnah ya Alfajiri, na huenda alikuwa akilala katika mwahala kote kuwili. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

 

Share