002-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Wanayoyafanya Waliopo Akishakufa Na Kukata Roho

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Janaazah

 

002-Wanayoyafanya Waliopo Akishakufa Na Kukata Roho

 

Alhidaaya.com

 

 

1- Wayafunge macho yake

 

Imepokelewa toka kwa Ummu Salamah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia kwa Abu Salamah macho yake yakiwa yamefunguka, akayafunga, kisha akasema: ((Hakika roho inapotwaliwa, macho huifuatilia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (920) na Abu Daawuud (3102) kwa ufupi].

 

Hikma ya kuyafunga macho ni kuwa kama hayakufungwa, uso wa maiti utatisha.

 

2- Mambo mengine waliyoyataja Mafuqahaa

 

[Al-Badaai-’i (1/300), Ibn ‘Aabidiyn (2/194), Mawaahibul Jaliyl (2/222), Al-Ummu (1/248), Al-Mughniy (2/451) na Al-Furu’u (2/192)].

 

(a) Akazwe taya zake mbili kwa kitambaa kipana kifungwe toka juu ya kichwa chake ili taya lake la chini lisilegee, mdomo ukafunguka na kukauka usiweze kufunga.

 

(b) Vilainishwe viungo vyake na vidole vyake kwa kuukunjia mkono wake kwenye kifupa panya, muundi wake kwenye paja lake, na paja lake kwenye tumbo lake, kisha litakaririwa hilo ili vilainike zaidi na iwe sahali kumwosha na kumsarifu.

 

(c) Avuliwe nguo ili kisije kikamtoka kitu kitakachomharibu kwa nguo hizo au kumchafua atakapovuliwa.

 

(d) Alazwe juu ya kitanda na mfano wake ili aweze kuhifadhika zaidi. Asiachwe juu ya ardhi kwani ataharibika haraka.

 

(e) Awekewe kitu kizito juu ya tumbo lake ili lisifure.

 

3- Aombewe du’aa

 

Ni kutokana na Hadiyth ya Ummu Salamah iliyotangulia inayomalizia kwa kusema: “Watu katika jamaa zake wakalalama kwa sauti akasema: Msijiombee wenyewe vibaya ila kwa kheri, kwani Malaika huitikia “aamiyn” kwa yale mnayoyasema”. Kisha akasema: “ Ee Allaah! Mghufirie Abu Salamah, Inyanyue daraja yake ndani ya walioongoka, na Umpe badali mwishoni mwake kwa wenye kubakia, na Utughufirie sisi na yeye ee Mola wa walimwengu wote, na Umkunjulie katika kaburi lake na Umnawirishie  humo”.

 

4- Ufunikwe mwili wake wote kwa nguo

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah: “Kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipofariki, alifunikwa kwa burda la Kiyemen”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1241) na Muslim (942) na tamko ni lake].

 

5- Maiti ishughulikiwe haraka na itolewe

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (( Iharakisheni jeneza. Ikiwa ni njema, basi ni kheri mnayoitanguliza kwake. Na kama si hivyo, basi ni shari mnayoitua toka shingoni mwenu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1315) na Muslim (944)].

 

Kuishughulikia haraka maiti ni pamoja na kuiosha haraka, kuivisha sanda na kuitayarisha, na kuibeba kuipeleka haraka makaburini.

 

6- Kulipa haraka madeni yake

 

Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Nafsi ya Muumini hufungiwa kwa sababu ya deni lake mpaka alipiwe)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (1078) na wengineo. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Al-Mishkaat (2915)].

 

Imepokelewa toka kwa Salamah bin Al-Akwa’a akisema: “ Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliletewa jeneza la maiti, na watu wakamwambia: Ee Rasuli wa Allaah liswalie. Akauliza: ((Je, ameacha deni analodaiwa?)) Wakasema: Ndio. Akauliza: (( Je, ameacha chochote?)) Wakasema: Hapana. Akasema: ((Mswalieni mwenzenu)). Mtu mmoja wa Kianswari aitwaye Abu Qataadah akasema: Mswalie, mimi nitalipa deni lake, naye akamswalia”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2291) na An-Nasaaiy, na tamko ni lake].

 

· Yanayojuzu Kwa Waliopo Na Wengineo Kuyafanya Kwa Maiti

 

1- Kufunua uso wake na kuubusu

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha): “Ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia kwa ‘Uthmaan bin Madh’uun akiwa maiti, akaufunua uso wake, kisha akamwinamia na kuubusu. Alilia mpaka nikayaona machozi yakimiminika juu ya mashavu yake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3147), At-Tirmidhiy (994) na Ibn Maajah (1456)].

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas: “Kwamba Abu Bakr alimbusu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kufariki”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4457), An-Nasaaiy (4/11) na Ahmad (6/55)].

 

2- Kumlilia maiti kimya kimya bila sauti wala kelele, bila kulalama, bila kujipiga mashavu na mfano wa hayo

 

Katika Hadiyth ya Anas kuhusu kisa cha kufariki Ibrahiym mwana wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamchukua Ibrahiym, akambusu na kumshumu. Kisha baadaye tukaingia hapo alipo na Ibrahiym anakaribia kukata roho, na macho ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yakaanza kutoa machozi. ‘Abdul Rahmaan bin ‘Awf akasema: “ Na wewe pia (unalia) ee Rasuli wa Allaah?!” Akasema: ((Ibn ‘Awf! Hakika hii ni rahma)).  Kisha akaongeza akisema: ((Hakika jicho linatoa machozi, na moyo wahuzunika, nasi hatusemi isipokuwa lenye kumridhisha Mola wetu, na sisi kwa kuondoka kwako ee Ibrahiym, hakika ni wenye kuhuzunishwa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1303)].

 

Na alipougua Sa’ad bin ‘Ubaadah, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilia, na watu walipomwona analia, nao walilia akasema: ((Hivi hamsikii? Hakika Allaah Haadhibu kwa chozi la jicho, wala kwa huzuni ya moyo, lakini Anaadhibu kwa huu - akaashiria ulimi wake- au Anarehemu. Na hakika maiti huadhibiwa kwa kuliliwa na watu wake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1304) na Muslim (924)].

 

Na Jaabir bin ‘Abdullaah aliufunua uso wa baba yake, akamlilia na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yuko hapo. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy na Muslim].

 

· Faida Mbili

 

1- Hakuna ubaya kumlilia tu maiti 

 

Bali linalokatazwa ni kutamka maneno ya kutoridhia Qadari ya Allaah na maombolezo yaliyoharamishwa. Pia hakuna ubaya kuungulika kwa ajili ya maiti wakati anapokaribia kukata roho. Ni kama alivyosema Faatwimah Alayhas Salaam wakati Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa karibu kukata roho: Ooh! Masikini baba yangu!!”. Akasema Rasuli: ((Hakuna tena mateso kwa baba yako baada ya leo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4462) na Ibn Maajah (1630)].

 

Ikajulikana kwamba maneno ya Faatwimah si katika maombolezo mabaya, kwa kuwa Rasuli aliyaridhia. [Fat-hul Baariy (7/756). Maktabah ya Salafiyyah].

 

2- Je, maiti huadhibiwa akililiwa na watu wake au wakimwombolezea?

 

Katika hili, kuna mvutano kati ya Maulamaa katika Maswahaba na waliofuatia baada yao. ‘Umar bin Al-Khatwwaab na mwanawe ‘Abdullaah na wengineo, walikuwa wanaona kwamba maiti huadhibiwa kwa kuliliwa na watu wake. Lakini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anhaa) amekhalifiana nao akisema: “Rasuli wa Allaah alipita kwa mwanamke wa Kiyahudi ambaye watu wake wanamlilia akasema: ((Hakika wao wanamlilia, naye bila shaka anaadhibiwa ndani ya kaburi lake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1289) na Muslim (932)].

 

Nao Jamhuri wanasema kwamba anayeadhibiwa kwa kuliliwa na watu wake, ni yule aliyeusia kwamba aliliwe na aombolezewe baada ya kufa, na wasiya wake ukatekelezwa. Ama anayeombolezewa bila kutoa wasiya, basi huyo haadhibiwi. Na wengine wanasema kwamba bali huadhibiwa kwa kuzembea kwake kuwaelimisha watu wake jambo lililowafanya kufanya hayo, kwani yeye ana jukumu juu ya watu wake. [Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/462) kwa muhtasari].

 

 

Share