003-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Yanayowapasa Jamaa Wa Maiti – Na Hususan Akina Mama- Inapowajia Habari Ya Kifo

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Janaazah

 

003-Yanayowapasa Jamaa Wa Maiti – Na Hususan Akina Mama- Inapowajia Habari Ya Kifo

 

Alhidaaya.com

 

 

· Kusubiri, kulirejesha jambo kwa Allaah na kuiridhia Qadhwaa ya Allaah

 

Allaah Anasema:

(( وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗوَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ ))

((Na bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Na wabashirie wenye kusubiri ● Wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea” ● Hao zitakuwa juu yao Barakah kutoka kwa Rabb wao na rahmah, na hao ndio wenye kuongoka)). [Al-Baqarah (2:155-157)]

 

Dada yangu Muislamu! Jua kwamba subira ambayo mtu anastahiki kusifiwa kwayo, ni ile ya wakati anaposhtukizwa na msiba, kinyume na ya baada ya hapo, kwani kwa kupita muda, machungu hupoa. [Ameyanukuu katika Fat-hul Baariy (3/149) toka kwa Al-Khatwwaabiy].

 

Imepokelewa toka kwa Anas akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpitia mwanamke mmoja akilia mbele ya kaburi akamwambia: ((Mche Allaah na fanya subira)). Akasema: “Achana na mimi, msiba wangu haukuhusu”. Hakumjua kwamba ni Rasuli. Akaambiwa kwamba huyo ni Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye moja kwa moja akamwendea na hakukuta kwake walinzi. Akamwambia: Sikukujua. Akasema: ((Hakika subira, ni kwenye kishindo cha mwanzo)). [Al-Bukhaariy (1283) na Muslim (926)].

 

Imepokelewa toka kwa Ummu Salamah akisema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:  ((Hakuna Muislamu yeyote anayepatwa na msiba na akasema yale Aliyoamrishwa na Allaah: Innaa lil-Laahi wainnaa ilayhi raaji’uwna. Ee Allaah! Nilipe katika msiba wangu huu, na Unipe badali iliyo bora kuliko hiyo, isipokuwa Allaah Humpa badali bora zaidi kuliko hiyo)). [Muslim (918) na Abu Daawuud (3115)].

 

· Yaliyoharamishwa Kwa Wanawake Wa Jamaa Ya Maiti Na Wanawake Wengineo

 

1- Kuomboleza kwa vilio

 

Hili ni haramu, kwa sababu hukoleza huzuni na huondosha subira. Pia huenda kinyume na kuiridhia Qadhwaa na kuwa chini ya Amri ya Allaah Mtukufu. [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (2/598)].

 

Imepokelewa toka kwa Abu Maalik Al ‘Ash-ariy ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Manne katika Umma wangu ni katika mambo ya kijahiliya, hawayaachi: Kujifaharisha kwa aliyonayo mtu au ya wahenga, kudharau nasaba za wengine na kuiona yake ni bora, kuomba mvua kwa nyota na kuomboleza vibaya)). Na amesema: (( Mwanamke mwenye kuomboleza vibaya ikiwa hakutubia kabla hajafa, atasimamishwa Siku ya Qiyaamah avikwe guo la lami na deraya la pele)). [Muslim (934), Ahmad (5/342), Al-Haakim (1/383) na Al-Bayhaqiy (4/63)].

 

Imepokelewa toka kwa Ummu ‘Atwiyyah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichukua ahadi kwetu wakati wa bay-’a kwamba tusiomboleze vibaya kwa sauti. Hakulitekeleza hilo mwanamke yeyote kati yetu isipokuwa wanawake watano”. [Al-Bukhaariy (1306) na Muslim (936)].

 

2,3- Kupiga mashavu na kurarua nguo

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (( Si katika sisi aliyejipiga mashavu, aliyerarua nguo kifuani na akaomboleza maombolezo ya kijahilia)). [Al-Bukhaariy (1294) na Muslim (103)].

 

Kurarua nguo ni mwanamke kuipasua nguo yake kwenye mpasuo wa kifua, na maombolezo ya kijahilia ni kulia kwa sauti, kuelezea mazuri na sifa za aliyekufa na kuomba vibaya. [Hili ni maarufu kwa wanawake. Ni kama anavyosema mmoja wao: Ee simba wangu! Ee ngamia wangu! na mengineyo mashuhuri. Katika  Al-Bukhaariy (4268) inaelezwa kwamba ‘Abdullah bin Rawwaah alipoteza fahamu, na dada yake akaanza kulia akisema: “Ee jabali langu! Ee kadha wa kadha!”. Alipozindukana alimwambia: Hakuna ulichosema ila niliambiwa: Je wewe ni kweli uko hivyo? Alipokufa, dada yake hakumlilia”].

 

4,5- Kunyoa nywele, kuzisambaza na kuzitawanya

 

Imepokelewa toka kwa Abu Burdah bin Abu Muusa akisema: “ Abu Muusa alihisi maumivu makubwa mno, akapoteza fahamu na kichwa chake kiko juu ya paja la mwanamke mmoja katika jamaa zake. Mwanamke mwingine katika jamaa zake akapiga ukelele, naye hakuweza kumjibisha kwa lolote. Alipozindukana alisema: Mimi niko mbali na yale aliyojiweka mbali nayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amejiweka mbali na mwanamke mwenye kupiga makelele wakati wa msiba, mwanamke mwenye kunyoa wakati wa msiba na mwanamke mwenye kurarua nguo wakati wa msiba”. [Al-Bukhaariy kaitolea maelezo (1296) na Muslim (103)].

 

Na mwanamke mmoja kati ya waliompa Bay-’a Rasuli amesema: “ Kati ya ahadi alizozichukua Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwetu katika mema tuliyoyaahidi ya kwamba hatutomwasi, ilikuwa ni: tusiparuze uso, tusiombe mabaya, tusirarue nguo na tusivuruge nywele”. [Abu Daawuud (3131) kwa Sanad iliyo karibu na uzuri].

 

Kuvuruga nywele ni pamoja na kuzitimuatimua, kuzifumua fumua na kuzinyambuanyambua wakati wa msiba. Na haya pamoja na mengineyo yaliyotangulia ni haramu, inabidi akina mama watahadhari nayo.

 

 

Share