009-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Vitendo Vya Swalaah Ya Maiti

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Janaazah

 

009-Vitendo Vya Swalaah Ya Maiti

 

Alhidaaya.com

 

 

1- Takbiyrah

 

(a) Idadi ya takbiyrah:

 

Zimepokelewa picha tofauti za takbiyrah toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ya kwanza: Takbiyrah nne

 

- Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwombolezea Negus siku aliyokufa. Alitoka nao kwenda sehemu ya kuswalia, akapanga nao safu, kisha akampigia takbiyrah nne. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy (1333) na Muslim (951)].

 

- Imepokelewa toka kwa Jaabir: "Kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswalia Ashamah Negus, akapiga takbiyrah nne". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy (1334)].

 

- Imepokelewa toka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu Anhumaa) akisema: "Mtu mmoja alikufa, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimzuru, wakamzika usiku. Kulipopambazuka, walimjulisha naye akawauliza: Nini kiliwazuia msinijulishe? Wakasema: Ilikuwa ni usiku na giza, tukahisi tabu kukupa uzito. Akaliendea kaburi lake, akamswalia na akapiga takbiyrah nne”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Muslim (954) na An-Nasaaiy (1/284)].

 

Haya haya yamesemwa na ‘Umar bin Al-Khattwaab, Ibn ‘Umar, Zayd bin Thaabit, Al-Hasan bin ‘Aliy, Ibn Abiy Awfaa, Al-Barraa bin ‘Aazib, Abu Hurayrah, Ibn ‘Aamir, Muhammad bin Al-Hanafiyyah, ‘Atwaa, Ath-Thawriy, Al-Awzaa’iy, Ahmad, Is-Haaq, Maalik, Asw-haab Ar-Raay, Ibn Al-Mubaarak na Ash-Shaafi’iy. [Al-Majmu’u cha An-Nawawiy (5/189), Sharhu As-Sunnah cha Al-Baghawiy (5/342, 343), Al-Ummu cha Ash-Shaafi’iy (1/413), Ad-Dusuwqiy (1/414), na Kash-Shaaful Qina’a (2/112)].

 

Ya pili: Takbiyrah tano

 

- Imepokelewa na ‘Abdul Rahmaan bin Abiy Ya’alaa akisema: “ Zayd alikuwa akipiga takbiyrah nne kwa Swalaah za maiti wetu, na alipiga takbiyrah tano kwenye Swalaah fulani ya maiti, nami nikamuuliza sababu akasema: Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akizipiga”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Muslim (957)].

 

- Imesimuliwa kwamba ‘Aliy alikuwa akipiga takbiyrah sita kwa watu wa Badr, tano kwa Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na nne kwa watu wengineo. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Ibn Abiy Shaybah (11454)].

 

- Imam At-Tirmidhiy amesema kuhusu takbiyrah tano: “ Baadhi ya wasomi katika Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wengineo wameliafiki hili. Wanaona ni takbiyrah tano kwa Swalaah ya Janaazah”. [Angalia Hadiyth nambari (1023)].

 

Ya tatu: Takbiyrah saba

 

Picha hii ina Hadiyth Dhwa’iyf. Nimeitaja ili kuashiria udhwa’iyf wa Hadiyth yake. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu Anhumaa) akisema: “ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru siku ya Uhud waletwe waliouawa, akaanza kuwaswalia. Wakawekwa tisa pamoja na Hamzah, akawapigia takbiyrah saba, kisha wakaondoshwa akabakishwa Hamzah. Kisha wakaletwa wengine tisa akawapigia takbiyrah saba mpaka akawamaliza”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twahaawiy katika Sharhu Ma’aanil Aathaar (1/503)].

 

Ya nne:

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin Az Zubayr (Radhwiya Allaahu Anhu) ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru Hamzah afunikwe kwa burdah siku ya Uhud. Kisha akamswalia, akapiga takbiyrah tisa, kisha wakaletwa waliouawa wakapangwa safu, akawaswalia na akamswalia Hamzah pamoja nao”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twahaawiy katika Sharhu Ma’aanil Aathaar (1/503)].

 

· Faida

 

Imepokelewa toka kwa Maswahaba (Radhwiya Allaahu Anhum) athari Swahiyh kuhusu takbiyrah za Swalaah ya maiti tatu, nne, tano, sita, na saba. [Al-Awsatw (5/429), Ibn Abiy Shaybah (1/497), Sharhul Ma’aaniy (1/497) na Al-Muhalla (5/128)].

 

An-Nawawiy (Rahimahul Laahu) ameiashiria tofauti hii kisha akasema: “ Halafu tofauti hiyo ilitoweka, na Umma kwa sasa umekubaliana kwa pamoja kwamba ni takbiyrah nne bila kuongeza wala kupunguza”. [Al-Majmu’u (5/187). Ibn Hazm kaikadhibisha Ijma’a hii katika Al-Muhalla (5/126) kwa namna niliyoitaja hapo juu].

 

Ninasema: “ Haitolewi hoja ambayo wamo humo akina ‘Aliy, Ibn Mas-’oud, Anas, Ibn ‘Abbaas, Maswahaba wa Sham na Taabi’iyna. La sahihi ni kuwa kila lililothibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndilo litumikalo, na mwenye kupinga hatiwi maanani. Ijapokuwa linaloonekana kuwa na uzito zaidi katika Hadiyth zilizotajwa kwenye mlango huu ni kuwa, kuongeza zaidi ya takbiyrah nne ni jambo linalowahusu wanachuoni wenye kuheshimika kama alivyolizungumzia hilo At-Twahaawiy kwenye mlango maalumu. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

· Akiacha Takbiyrah Moja Kati Ya Takbiyrah

 

[Al-Mughniy (3/451), Ibn ‘Aabidiyn (1/613), na Ad-Dusuwqiy (1/411)].

 

Mwenye kuacha takbiyrah moja kati ya takbiyrah za Swalaah ya maiti, kama ameiacha kwa kusahau, ataipiga kisha atatoa tasliym. Imeripotiwa kwamba Anas alipiga takbiyrah tatu kwenye Swalaah ya maiti, kisha akaondoka. Akazungumza, na watu wakazungumza, wakasema: “ Ee Abu Hamzah! Umepiga takbiyrah tatu tu! Akasema: Pangeni safu. Wakapanga, akapiga ya nne. [Kuna maneno kuhusu isnadi yake. Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (6417) kupitia kwa Mu’ammar toka kwa Qataadah. Kuna walakini kwenye riwaya hii].

 

Na kama imamu ataiacha kwa kusudi, Swalaah yake itabatilika, na sijdah ya sahau hairuhusiwi kwa hali yoyote.

 

· Je, Atanyanyua Mikono Yake Sambamba Na Takbiyrah?

 

Hakuna Hadiyth yoyote Marfu’u ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayogusia hili, lakini Maulamaa wamegawanyika makundi mawili: [Al-Mabsuwt (2/46), Al-Mudawwanah (1/160), Al-Majmu’u (5/232), Kash-Shaaful Qina’a (2/72), Al-Awsatw (5/426), Al-Muhalla (5/128), Kitabu cha Raf-’u Al Yadayn cha Al-Bukhaariy (uk. 175) na Ahkaamul Janaaiz (uk. 148)].

 

La kwanza: Wanasema atanyanyua mikono yake katika takbiyrah ya kwanza tu. Ni kauli ya Ath-Thawriy, na riwaya toka kwa Abu Haniyfah, Malik na Ibn Hazm. Al-Albaaniy kaikhitari. Dalili yao ni:

 

1- Yaliyoripotiwa Marfu’u toka kwa Abu Hurayrah: “Kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipiga takbiyrah katika Swalaah ya maiti, akanyanyua mikono yake kwenye takbiyrah ya kwanza, na akaweka mkono wa kulia juu ya wa kushoto”. [Ni Dhwa’iyf mno: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (1077), Ad-daaraqutwniy (2/75), na Al-Bayhaqiy (4/38)].

Sanad yake pia ni mbovu.

 

2- Yaliyoripotiwa toka kwa Ibn ‘Abbaas: “ Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ananyanyua mikono yake katika Swalaah ya maiti katika takbiyrah ya kwanza, kisha hafanyi tena”. [Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-daaraqutwniy (2/75) na Al-Uqayliy (3/449)].

Sanad yake pia ni Dhwa’iyf.

 

3- Wote wameitafikiana kunyanyua mkono katika takbiyrah ya kwanza. Hakuna jingine zaidi ya hilo lililofanywa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo, haifai kufanya ambalo hakulifanya.

 

La pili: Wanasema atanyanyua mikono yake katika takbiyrah zote. Hili wamelisema Maulamaa wengi kama Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-Haaq na riwaya toka kwa Abu Haniyfah na Maalik. Dalili yao ni:

 

1-Yanayosimuliwa toka kwa Ibn 'Umar: "Kwamba Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaposwalia maiti, ananyanyua mikono yake miwili kwa kila takbiyrah". [Imetiwa dosari kwa waqfu. Imefanyiwa "ikhraaj" na Ad-daaraqutwniy katika Al-'Ilal].

La sahihi ni kuakifishiwa Ibn ‘Umar, nalo ni lenye kufuatia.

 

2- Yaliyothibiti toka kwa Ibn 'Umar: "Kwamba alikuwa akinyanyua mikono yake miwili katika kila takbiyrah katika Swalaah ya maiti, na anaposimama toka kwenye rakaa mbili". [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy katika Kitabu cha Raf-'u Al Yadayn (110) na Al-Bayhaqiy (4/44)].

 

3- Na mfano wa Hadiyth hii toka kwa Ibn 'Abbaas, Al-Haafidh ameiashiria kwenye At-Talkhiysw (2/147), na amesema kuwa ni Swahiyh.

 

Ninasema: " Uwanja katika suala hili ni mpana ingawa kauli ya pili ndiyo yenye nguvu zaidi kutokana na kitendo cha Ibn 'Umar – kwa kuwa ndiye Swahaba mwenye kufuata zaidi Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) – na hususan kwa anayeona kwamba yeye hafanyi hilo ila kwa tawqiyf".

 

· Je, Du’aa Ya Ufunguzi Wa Swalaah Ipo Katika Swalaah Ya Maiti?

 

[Al-Majmu'u (5/193), na Al-Mughniy (3/410)].

 

Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba du’aa ya ufunguzi wa Swalaah haipo katika Swalaah ya maiti. Bali Ash-Shaafi'iy na Hanbali wamesema: Hupiga takbiyrah, kisha husoma isti'aadhah, na halafu husoma.

 

Ath-Thawriy kasema: "Atasoma du’aa ya ufunguzi wa Swalaah kwenye Swalaah hiyo, na imesimuliwa mfano wa kauli hiyo toka kwa Ahmad".

 

Ninasema: "Kauli yenye nguvu ni kuwa du’aa hiyo haikatazwi".

 

· Kusoma Al-Faatihahh Kwenye Swalaah Ya Maiti

 

Maulamaa wana kauli mbili kuhusiana na hukmu ya kusoma Suwrat Al-Faatihahh katika Swalaah ya maiti: [Al-Majmu'u (5/191), na Al-Mughniy (3/411), Al-Muhalla (5/131), Ibn 'Aabidiyn (1/611), Zaadul Ma'aad (1/192), na Bidaayatul Mujtahid (1/188)].

 

Ya kwanza: Ni lazima kuisoma. Hii ni kauli ya Ash-Shaafi'iy, Ahmad, Is-Haaq, Daawuud na Ibn Hazm. Pia kaisema Ibn 'Abbaas na Abu Umaamah. Dalili yao ni:

 

1- Ujumuishi wa kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hana Swalaah ambaye hakusoma Faatihahtul Kitaab)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa mara nyingi katika mlango wa Swalaah].

 

Wamesema: Jina Swalaah ni pamoja na Swalaah ya maiti.

 

2- Imepokelewa toka kwa Abu Umaamah akisema: " Sunnah katika Swalaah ya maiti, asome mtu katika takbiyrah ya kwanza Ummul Kitaab kwa sauti ya chini, kisha apige takbiyrah mara tatu, na atoe tasliym wakati wa takbiyrah ya mwisho". [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na An-Nasaaiy (4/75), ‘Abdul Razzaaq (6428) na Al-Bayhaqiy (4/39)].

 

3-Twalha bin ‘Abdallah bin 'Awf amesema: " Niliswali Swalaah ya maiti nyuma ya Ibn 'Abbaas, akasoma Faatihahtul Kitaab, na akasema: "Ili mjue kwamba ni Sunnah". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy (1335), Abu Daawuud (3182), At-Tirmidhiy (1032) An-Nasaaiy (4/75) na Ibn Maajah (2495)].

 

Ama kwa upande wa Sheikh wa Uislamu, yeye anaona kwamba kuisoma ni Sunnah na si wajibu katika Swalaah ya maiti.

 

Ya pili: Hakisomwi chochote katika Qur-aan katika Swalaah ya maiti. Ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Al-Awzaaiy, Abu Haniyfah, na Maalik. Ni kauli pia ya Ibn 'Umar na 'Ubaadah bin As-Swaamit katika Maswahaba. Hoja yao ni:

 

1- Watu wa Madiynah hawasomi katika Swalaah ya maiti (kwa mujibu wa Maalik).

 

2- Yaliyothibiti kwa Ibn 'Umar kwamba yeye: "Alikuwa hasomi akimswalia maiti". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Ibn Abiy Shaybah katika Muswannaf wake (11404)].

 

3- Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba alimuuliza 'Ubaadah bin As-Swaamit kuhusiana na Swalaah ya maiti, naye akajibu: " Mimi Wal-Laahi nitakueleza: Utaanza kwa takbiyrah, kisha utamswalia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), halafu utasema: Allaahumma, inna ‘Abdallah fulaan kaana laa yushriku bika shay-an, Anta A-'alamu bihi. In kaana muhsinan Fazid fiy ihsaanihii, wain kaana musiy-an Fatajaawaz anhu. Allaahumma laa Tahrimnaa ajrahu, wala Tudhwillanaa ba'adahu". [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa "ikhraaj" na  Al-Bayhaqiy (4/40)].

 

Ninasema: " Kauli ya kwanza ndio yenye nguvu kutokana na yaliyotangulia. Ama athar ya Ibn 'Umar, inawezekana ikachukulika kama yeye hasomi kingine chochote isipokuwa Ummul Qur-aan. Aidha, athar ya 'Ubaadah, hakuna ndani yake hoja na hususan kutokutajwa takbiyrah nyinginezo na tasliym. Je, itasemwa si wajibu?! La sahihi ni kwamba inasomwa. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

· Kumswalia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Baada Ya Takbiyrah Ya Pili

 

Imesuniwa kumswalia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya takbiyrah ya pili kutokana na Hadiyth ya Abu Umaamah ya kwamba mtu mmoja katika Maswahaba wa Rasuli alimjulisha: "Ya kwamba Sunnah katika Swalaah ya maiti ni imamu kupiga takbiyrah, kisha asome kimya kimya mwenyewe Faatihahtul Kitaab baada ya takbiyrah ya kwanza, halafu amswalie Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na amwombee du’aa maiti katika takbiyrah ya tatu, hasomi chochote katika takbiyrah hizo, kisha atoe tasliym kimya kimya ". [Ash-Shaafi'iy katika Al-Ummu (1/270) na Al-Bayhaqiy (4/39). Al-Haafidh ameipasisha isnadi yake].

 

Ukamilifu wa kumswalia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kwa tamko lile la tashah-hud.

 

· Kumwombea Maiti Du’aa Baada Ya Kumswalia

 

Ni Sunnah kwa kila mmoja kumwombea maiti du’aa baada ya kumswalia. Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema: "Nimemsikia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Mkimswalia maiti, basi kila mmoja amwombee du’aa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Abu Daawuud (3197), Ibn Maajah (1497), Al-Bayhaqiy (4/40 na Ibn Hibaan (3077)].

 

· Miundo Ya Du’aa Katika Swalaah Ya Maiti

 

- (( Allaahumma Ighfir lahuu wa R-hamhu wa 'Aafihii wa 'Afu anhu, wa Akrim nuzulahu wa Wassi'i madkhalahu, wa Ghsilhu bilmaai wath-thalji wal barad, wa Naqqihii minal khatwaayaa kamaa Naqqayta ath-thawba al abyadh minad danas, wa ‘Abdilhu daaran khayran min daarihii, wa ahlan khayran min ahlihi, wa zawjan khayran min zawjihi, wa Adkhilhul Jannah, wa A'idh-hu min 'adhaabil qabri, aw min 'adhaabin naar)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Muslim (963)].

 

- ((Allaahumma Ighfir lihayyinaa wa mayyitinaa, wa shaahidinaa wa ghaaibinaa, wa swaghiyrinaa wa kabiyrinaa, wa dhakarinaa wa unthaanaa. Allaahumma man Ahyaytahuu minnaa fa Ahyihii 'alal Islaam, waman Tawaffaytahuu minna fa Tawaffahuu 'alal iymaan. Allaahumma laa Tahrimnaa ajrahuu walaa Tudwillanaa ba'adahuu)). [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Abu Daawuud (3201), At-Tirmidhiy (1024), Ibn Maajah (1498)].

 

Faida: Kisomo na du’aa ni kimya kimya

 

Kisomo na du’aa ni kimya kimya katika Swalaah ya maiti, ingawa imepokelewa toka kwa Ibn 'Abbaas [Al-Bukhaariy (1335). Imetajwa nyuma] kwamba alisoma kwa sauti Faatihahtul Kitaab isipokuwa hilo lilikuwa kwa lengo la kuwafunza watu kama alivyosema Ahmad kuwa alifanya hivyo ili kuwafundisha. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (3/412)].

 

· Kutoa Tasliym

 

Maulamaa wamekhitalifiana; je ni tasliym moja au mbili?

 

Wenye kusema tasliym moja: Imepokelewa kwa njia sahihi toka kwa Ibn 'Umar [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Ibn Abiy Shaybah (11491)] na Waailah bin Al-Asqu'i [Sanad yake ni Hasan: Imefanyiwa "ikhraaj" na Ibn Abiy Shaybah (11505)] kwamba walikuwa wakitoa tasliym moja.

 

Pia limesimuliwa hilo toka kwa 'Aliy, Ibn 'Abbaas, Jaabir, Abu Hurayrah, Anas bin Maalik na Ibn Abiy Awfaa. Kadhalika, limesemwa na Sa'iyd bin Jubayr, Al-Hasan, Ibn Syriyna, Abu Umaamah bin Sahl, Al-Qaasim bin Muhammad, Al-Haarith, Ibrahiym An-Nakh'iy, Ath-Thawriy, Ibn 'Uyaynah, Ibn Al-Mubaarak, ‘Abdul Rahmaan bin Mahdiy, Maalik, Ahmad na Is-Haaq. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (3/418) na Al-Mudawwanatul Kubraa (1/170)].

Nayo ni kauli iliyosimuliwa toka kwa Ash-Shaafi'iy. [Al-Majmu'u cha An-Nawawiy (5/198-200)].

 

Wenye kusema tasliym mbili: Hili kalisema Ash-Shaafi'iy na Aswhaabu Ar Raay, na limwekhitariwa hili na Al-Qaadhwiy. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (3/418)].

Pia Abu Haniyfah ana msimamo huu. [Al-Mawsuu'at Al-Fiqhiyyah (16/28)].

 

Hoja yao katika hili ni kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Swalini kama mnavyoniona naswali)).

 

Na Hadiyth ya ‘Abdullah bin Abiy Awfaa ya kwamba alimswalia binti yake akapiga takbiyrah nne, kisha akatoa tasliym kulia kwake na kushoto kwake. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bayhaqiy katika Sunani zake (4/43)].

 

Hadiyth hii imerufaishwa kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ninasema: "Hadiyth hii ni Dhwa’iyf".

 

· Aliyepitwa Na Baadhi Ya Takbiyrah

 

Baadhi ya Maulamaa wanaona kwamba maamuma akipitwa na baadhi ya takbiyrah, basi atazilipa zilizompita. Limesimuliwa hilo toka kwa Sa'iyd bin Al-Musayyib, 'Atwaa, An-Nakh'iy, Az-Zuhriy, Ibn Syriyn, Qataadah, Maalik, Ath-Thawriy, Ash-Shaafi'iy, Is-Haaq, Asw-Haab Ar Raay, na Ibn Hazm. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (3/423), Al-Muhalla cha Ibn Hazm (5/179)].

 

Lakini wamekhitalifiana kama atalipa; je ataomba du’aa kati ya takbiyrah au haombi? Abu Haniyfah anasema kwamba ataomba kati ya takbiyrah inayolipwa, lakini Maalik na Ash-Shaafi'iy wanaona kwamba atailipa bila kusoma au kuomba chochote. [Bidaayatul Mujtahid cha Ibn Rushd (1/190)].

 

Na hoja ya wanaosema kwamba alipe ni kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mlichokipata kiswalini, na kilichowapiteni kikamilisheni)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy (635), na Muslim (602)].

 

Baadhi ya Maulamaa wanaona kwamba halipi takbiyrah zilizompita. Yameelezwa hayo kwa njia sahihi toka kwa Al-Hasan. [Hadiyth Swahiyh: ‘Abdul Razzaaq (5/64)].

 

 Na inasimuliwa kuwa Ibn 'Umar hakuwa akilipa takbiyrah. Na kama atapiga takbiyrah mfululizo, basi hakuna ubaya. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (3/423)].

Imepokelewa toka kwa Ahmad akisema: "Kama hakulipa, basi hakuna ubaya". [As-Saabiq].

 

 

 

Share