Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
Suwrah Al-Faatihah:
"بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ * الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ * الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ * مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ * إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ * اهْدِنَا الصِّرَاط الْمُسْتَقِيمَ * صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ".
“Kwa Jina la Allaah Ar-Rahmaan, Mwenye Kurehemu • Himdi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu • Ar-Rahmaan, Mwenye Kurehemu • Mfalme wa siku ya malipo • Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada • Tuongoze njia iliyonyooka • Njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea”. [Al-Faatihah: (1-7)]
Du’aa ya kwanza kabisa katika Qur-aan Tukufu iko katika Suwrah hii ya Al-Faatihah. Hii ndio Suwrah Adhimu kabisa kati ya Suwrah za Qur-aan ambayo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam ameiita “Ummul Qur-aan” pale aliposema:
"الْحَمْدُ لِلَّهِ: أُمُّ الْقُرْآنِ، وَأُمُّ الْكِتَابِ، وَالسَّبْعُ الْمَثَانِي"
“Alhamdulil Laahi ni “Ummul Qur-aan, na “Ummul Kitaab” na “As-Sab-‘ul Mathaaniy”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Abu Sa’iyd bin Al-Ma’aliy:
"لأُعَلِّمَنَّكَ أَعْظَمَ سُورَةٍ فِي الْقُرْآنِ... الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ"
“Hakika nitakufundisha Suwrah Adhimu zaidi katika Qur-aan: Alhamdulil Laah Rabbil ‘aalamiyn”. [Al-Bukhaariy: Kitaabut Tafsiyr].
Imeitwa “Ummul Qur-aan” kwa vile inakusanya aina zote tatu za tawhiyd pamoja na du’aa yenye manufaa makubwa zaidi, nayo ni kuomba hidaayah ambayo ndio asili ya furaha na mafanikio katika nyumba mbili za dunia na aakhirah. Na hapa ni pale unaposoma:
"اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ"
“Tuongoze njia iliyonyooka”.
Mbali na uzito wa du’aa hii, unaposimama ndugu Muislamu kuswali, basi usisahau kuhudhurisha moyo wako kwa kukizingatia kila unachokisoma na kila unachokitenda. Unaposoma Suwrat Al-Faatihah ujue kwamba Allaah Anakujibisha neno kwa neno. Ukiyazingatia, basi Naye Atakuzingatia na kukujibu du’aa yako, na usipoyazingatia, basi matunda yake yanakuwa ni madogo mno. Katika Al-Hadiyth Al-Qudsiy, Allaah Anasema:
"قَسَمْتُ الصَّلَاةَ بَيْنِي وَبَيْنَ عَبْدِي نِصْفَيْنِ، وَلِعَبْدِي مَا سَأَلَ، فَإذَا قَالَ الْعَبْدُ: الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ، قَالَ اللَّهُ تَعَالَى : حَمِدَنِي عَبْدِي، وَإذَا قَالَ: الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ، قاَلَ اللَّهُ تَعَالَى: أَثْنَى عَلَيَّ عَبْدِي، وَإذَا قَالَ: مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ، قَالَ : مَجَّدَنِي عَبْدِي،
“Nimeigawa Al-Faatihah kati Yangu na Mja Wangu nusu mbili, na Mja Wangu atapata aliloliomba. Mja akisema:
الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ
Allaah Ta’aalaa Husema: Mja Wangu amenihimidi.
Na akisema:
الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
Allaah Ta’aalaa Husema: Mja Wangu amenisifu.
Na anaposema:
مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ
Allaah Husema: Mja Wangu amenitukuza”. [Muslim: Kitaabu As Swalaat]
Hii ndio nusu ya kwanza ambapo umemhimidi Allaah, umemsifu na umemtukuza. Hayo yote yanahusiana Naye.
Ama nusu ya pili ya kuizingatia zaidi, ni hii ya wewe kumwomba hidaayah. Na hapo Allaah Husema: Hili ni kati Yangu Mimi na Mja Wangu, na Mja Wangu atapata aliloliomba. Na hii ni dhamana Allaah Anatupa kwamba du’aa hii tunayoiomba kila siku katika Swalaah zetu katika Suwrah hii Anatukubalia ikiwa sisi tutaisoma kwa uzingativu, unyenyekevu na ikhlasi, tukijua kwamba tumesimama mbele Yake, Yeye Anatusikiliza, Anatujibisha na Anatuahidi kwamba tuliloliomba tutalipata. Na kwenye Hadiyth hii, Allaah Ameiita Al-Faatihah kwa jina la Swalaah, kwa kuwa Swalaah haitimii bila kuisoma Al-Faatihah.
Hivyo basi, tunapohirimia, tuweke mbali kabisa mawazo yetu na mishughuliko yetu yote ya kidunia na tuizingatie vyema suwrah hii pamoja na yote yanayohusiana na Swalaah.
Kuomba hidaayah tunakuhitajia zaidi kuliko kuomba shida zetu zingine zote. Na kwa ajili hiyo, Allaah Mtukufu Ametuwekea Suwrah hii tuisome katika kila rakaa ya Swalaah zetu. Tumwombe humo hidaayah mara 17 katika Swalaah za faradhi za kila siku kwa moyo uliohudhurishwa, na kwa unyenyekevu na kwenye Swalaah nyingine zote za Sunnah. Na kwa ajili hiyo, Waumini wenye kuswali kwa khushui katika Swalaah zao, Allaah Amewaeleza kuwa ni katika waliofaulu kutokana na du’aa iliyomo humo na mengineyo yote yaliyokusanywa ndani yake.
Muislamu anapoiomba du’aa hii adhimu ni kama vile anasema: “Ee Rabbi wetu! Tuonyeshe na Tuongoze, na Tupe tawfiyq tushikamane na Njia Yako iliyonyooka ambayo itatufikisha sisi katika Nyumba Yako ya Pepo za neema. Kwani mwenye kuthibiti juu ya njia hiyo hapa duniani, basi unyayo wake utathibiti vyema juu ya Swiraat iliyosimamishwa juu ya mgongo wa Jahannamu. Na kwa kiasi cha mtu kutembea juu ya njia hii hapa duniani, ndivyo atakavyotembea juu ya njia hiyo ya Swiraat Siku ya Qiyaamah.
Kisha du’aa inabainisha njia hiyo tunayoiomba. Hapo tunasoma na kusema:
"صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ "
“Njia ya wale Uliowaneemesha”.
Hapa unatawasali kwa Allaah kwa Neema Zake na kwa ihsani Zake kwa wale Aliowaneemesha kwa kuwapa hidaayah hiyo.
Unamwambia Allaah: Hakika Wewe Umewaneemesha hao kwa kuwapa hidaayah, na bila shaka hilo ni kutokana na Neema Zako kwao. Basi na mimi Nijaalie nipate sehemu ya neema hii, na Unijaalie niwe miongoni mwa hawa Uliowaneemsha.
Watu hawa ni akina nani? Hawa ni Manabii, Swiddiqina, Mashuhadaa na Swalihina kama Alivyosema:
"وَمَنْ يُطِعِ اللَّهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ مِنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا "
“Na atakayemtii Allaah na Rasuli, basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah Aliowaneemesha miongoni mwa Manabii na Swiddiqiyna na Mashuhadaa na Swalihina, na uzuri ulioje kuwa pamoja na hao!”. [An-Nisaa: (69)]
Hili ndilo la kuliomba kwa nguvu zote na kulipigania wakati wote wa umri wetu. Ni uzuri ulioje kuwa pamoja na hawa! Beba utajiri wote wa dunia, beba umashuhuri wote wa dunia, beba medali zote za dunia, lakini usipokuwa kwenye kundi hili, basi umekula hasara. Ndipo hapo unapoomba zaidi usiwe katika kundi la walioghadhibikiwa na waliopotea unaposema:
غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ
“Si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea”.
Walioghadhibikiwa ni Mayahudi. Anaingia pia ndani ya kundi hili kila yule aliyeijua haki kisha asiifuate au kuifanyia kazi. Na waliopotea ni Manasara. Makundi yote haya mawili yameingia katika hasara kubwa ya kuishia kwenye moto wa Jahannamu. Na hapa unamwomba Allaah usije kuingia kwenye makundi haya mawili au makundi mengine potovu ambayo mwisho wake ni motoni.
Na imesuniwa vile vile kuitikia “aamiyn” ni sawa mtu akiwa anaswali peke yake, au akiwa ni imamu, au akiwa maamuma, na katika hali zote. Imesimuliwa na Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah amesema:
"إذَا أمَّنَ الإمَامُ فَأَمِّنُوا فَإِنَّهُ مَنْ وَافَقَ تَأْمِينُهُ تَأْمِينَ المَلاَئِكةِ غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ"
“Imamu akisema “aamiyn”, basi nanyi semeni aamiyn, kwani yeyote ambaye “aamiyn yake itawafikiana na ya Malaika, basi ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia”. [Al-Bukhaariy: Kitaabul Aadhaan]
Mbali na kuongozwa katika njia iliyonyooka uliyoiomba, pia unasamehewa madhambi yako yote ya nyuma kwa kusema tu “aamiyn”. Ni Rehma iliyoje ya Allaah kwetu sisi!
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
02-Kutaqabaliwa ‘Amali
"رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ"
“Rabbi wetu Tutakabalie, hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa Yote”. [Al-Baqarah: 127)]
Haya ni maombi ya kwanza kati ya maombi ya Imamu wa waliojiengua na shirki na kushikamana na tawhiyd, kiigizo cha wenye kumpwekesha Allaah na Khaliyl wa Ar Rahmaan Nabii Ibraahiym ‘Alayhis Salaam ambaye Allaah Ta’aalaa Amemsifu kwamba ni mwenye kukusanya mambo yote ya kheri Aliposema:
"إِنَّ إِبْرَاهِيمَ كَانَ أُمَّةً قَانِتًا لِلَّهِ حَنِيفًا وَلَمْ يَكُ مِنَ الْمُشْرِكِينَ"
“Hakika Ibraahiym alikuwa mwenye akhlaaq na maadili yote mema, mtiifu kwa Allaah, aliyeelemea haki, na hakuwa miongoni mwa washirikina”. [An Nahl (120)].
Du’aa hii ya kuomba kukubaliwa ‘amali za vitendo na maneno, ni du’aa muhimu kabisa kwetu. Angalia Nabii huyu Baba wa Manabii akiwa katika kazi ya ujenzi huu muhimu wa Al-Ka’abah ambayo ndiyo Qiblah cha Waumini wanachokielekea katika Swalaah zao zote, akiwa pamoja na mwanaye Ismaa’iyl ‘Alayhis Salaam, anavyomwomba Allaah Awataqabalie kazi yao hii pamoja na cheo chake kikubwa alichonacho mbele ya Allaah. Basi vipi mimi na wewe?
Hebu litaamuli jambo lao hili. Wanaifanya kazi hii waliyopewa na Mola wao huku wakimwomba: “Ee Rabbi wetu! Tutakabalie”. Angalia vipi ilikuwa hali yao ya khofu ya kutokukubaliwa ‘amali yao hiyo!
Msingi muhimu wa kukubaliwa mtu ‘amali yake ni ikhlasi pamoja na kumwomba Allaah Amtakabalie.
Hali hii ya Nabiy Ibraahiym ‘Alayhis Salaam na mwanaye Ismaa’iyl ni kama hali ya Waumini wenye kumtakasia Allaah Aliowaelezea katika Kauli Yake:
"وَالَّذينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوْا وَقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَى رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ"
“Na ambao wanatoa vile wavitoavyo na huku nyoyo zao zina khofu kwamba hakika watarejea kwa Rabbi wao”. [Al-Muuminuuna (23:60)]
Yaani wanatoa swadaqah, matumizi ya familia zao na mengineyo ya kheri huku wakiwa na khofu ya kutokubaliwa hayo. Bibi ‘Aaishah alimuuliza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Aayah hii akisema:
"أَهُمْ الَّذِينَ يَشْرَبُونَ الْخَمْرَ وَيَسْرِقُونَ؟ قَالَ: لَا يَا بِنْتَ الصِّدِّيقِ، وَلَكِنَّهُمْ الَّذِينَ يَصُومُونَ، وَيُصَلُّونَ، وَيَتَصَدَّقُونَ، وَهُمْ يَخَافُونَ أَنْ لَا يُقْبَلَ مِنْهُمْ"
“Je hawa ni wale wanaokunywa ulevi na wanaoiba? Akasema: Hapana ee binti As Swiddiyq. Lakini hawa ni wale wanaofunga, wanaoswali na wanaotoa swadaqah nailhali wao wanaogopa wasikubaliwe (‘amali zao hizo)”. [Sunanu At-Tirmidhiy: Kitaabu Tafsiyril Qur-aan ‘An Rasuwlil Laah]
Kutokana na du’aa hii tunajifunza haya yafuatayo:
1- Umuhimu wa kukubaliwa ‘amali pale ambapo mhimili wa ‘amali njema unasimamia juu yake. Na hii ni pamoja na kumtakasia Allaah na kufuata yale yote Aliyokuja nayo Rasuli.
2- Aayah inatufundisha kwamba tunatakiwa tushikamane na kumwomba Allaah nyakati zote Atutakabalie ‘amali zetu baada ya kuzifanya. Na hili ndilo alilokuwa akilifanya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa akistaghfiri mara tatu baada ya kila Swalaah. Na alikuwa anasema baada ya Swalaah ya Alfajiri:
"اللّهمَّ إنّي أسألك علماً نافعاً، ورزقاً طيباً، وعملاً مُتقبّلاً"
“Ee Allaah! Hakika mimi ninakuomba ‘ilmu nufaishi, riziki safi ya halali, na ‘amali yenye kutaqabaliwa”. [Imesimuliwa na Ummu Salamah]
Na alikuwa anajilinda kwa kusema:
"اللّهمّ إنّي أعوذ بك من علم لا ينفع، ومن عمل لا يُرفع"
“Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na ‘ilmu isiyonufaishi, na ‘amali isiyopandishwa”. [Imesimuliwa na Anas bin Maalik]
3- Kutawassali kwa Allaah kwa kutumia Majina Yake na Sifa Zake kwa mujibu wa ombi. Jina la السميع linanasibiana na Allaah kuwa Anaisikia du’aa yao, na العليم linanasibiana na kuwa Allaah Anazijua niya zao, na ukweli wa unyenyekevu wao.
4- Du’aa ni makimbilio ya Manabii na Mitume wote. Mja anaihitajia katika hali zake zote za kisharia na kidunia.
5- Du’aa inaondosha sifa ya mtu kujiona, kwani kujiona kunaharibu ‘amali ya mtu.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
03-Mema Ya Dunia Na Aakhirah
"رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّار"
“Rabb wetu! Tupe katika dunia mazuri na katika Aakhirah mazuri na Tukinge na adhabu ya moto”. [Al-Baqarah: (201)]
Du’aa hii ndani yake kuna kukiri “Rubuwbiyyah Kuu” ya Allaah Ta’aalaa yenye kuwajibikiana na kumpwekesha Yeye tu katika Uungu. Hili ndilo linalotakikana kwa mwenye kuomba du’aa, ahudhurishe maana hizi njema za Umola Wake Ta’alaa kwa Viumbe Vyake vyote, nalo ni jambo ambalo linamfanya mja awe mnyenyekevu na mwenye kuonja ladha ya kunong’onezana na Mola Wake katika du’aa kama hii ambayo hailingani na kitu chochote katika anavyovipenda.
Katika du’aa hii, anaomba kheri zote za dunia kwa tamshi fupi kabisa na maneno machache mno. Du’aa hii imekusanya kheri zote za dunia anazozitamani mtu, kwani mema katika “Tupe katika dunia mazuri” yanajumuisha matakwa yote mema ya hapa duniani ikiwa ni pamoja na afya njema, nyumba pana yenye wasaa, mke mwema au mume mwema au watoto wema, riziki kunjufu, elimu nufaishi, amali njema, kipando maridhawa, usalama na amani na mengineyo muhimu katika maisha yetu.
Ama mema ya aakhirah, hayo bila shaka ni Pepo, kwani ambaye hatoipata Pepo Siku hiyo, basi huyo amenyimwa kheri zote. Kadhalika, kupata amani kutokana na fazaa kubwa ya kisimamo cha Qiyaamah, kufanyiwa wepesi hisabu, kuweko katika Kivuli cha Allaah huku wengine wakitaabika na kuteseka na mengineyo mengi mema ya Siku hiyo kwa waja wema.
Ama “na Utukinge na adhabu ya moto”, hii inajumuisha kutuwepesishia sababu zake hapa duniani, kujiepusha na maharamisho na madhambi, kuwa na tawhiyd safi, kujiepusha na bid’a na kufuata yale yote aliyokuja nayo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Na kwa vile du’aa hii imekusanya maombi yote ya kidunia na kiaakhirah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikithirisha kuiomba. Anas (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: “Ilikuwa ndio du’aa anayoiomba zaidi Rasuli”.
Na Anas akamuiga Rasuli katika hilo, na akawa haiachi katika du’aa zozote anazoziomba. Baadhi ya Maswahaba walimwomba awaombee, naye akawaombea kwa du’aa hii iliyobarikiwa.
Tunajifunza kutokana na du’aa hii:
1- Kwamba tuombe kheri zote za dunia na aakhirah.
2- Tunapoomba tutawassal kwa Sifa za kivitendo za Allaah Ta’aalaa kama hapa “Tukinge”.
3- Mtu halaumiwi kuomba kheri za dunia pamoja na kheri za aakhirah.
4- Kila mmoja wetu anahitajia mema ya dunia na mema ya aakhirah.
5- Uzuri wa du’aa ni iwe yenye kukusanya utashi: “Tupe duniani mema na aakhirah mema”, na khofu pia: “Utukinge na adhabu ya moto”. Hii inamfanya mtu kuwa kati ya khofu na matumaini.
6- Umuhimu wa kuomba kwa du’aa zilizomo kwenye Qur-aan Tukufu. Du’aa hizi ni toshelezi na jumuishi kwa matakwa yote anayoyatamani mtu katika dini yake, dunia yake na aakhirah yake. Muislamu anatakiwa awajibike nazo pamoja na zile zilizopokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) badala ya kutumia du’aa za kutungwa na watu ambazo mara nyingi zinakuwa na maneno yasiyomridhisha Allaah Ta’aalaa.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
04-Nyoyo Zisipotoshwe
"رَبَّنَا لاَ تُزِغْ قُلُوبَنَا بَعْدَ إِذْ هَدَيْتَنَا وَهَبْ لَنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً إِنَّكَ أَنتَ الْوَهَّابُ"
“Rabb wetu! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kuwa Umetuhidi, na Tutunukie kutoka Kwako rahmah. Hakika Wewe Ni Mwingi wa Kutunuku na Kuneemesha”. [Aal ‘Imraan: (08)]
Kuthibiti katika dini, iymaan na njia iliyonyooka ni takwa muhimu ambalo Muislamu anatakiwa amwombe Mola wake wakati wote. Na kulipata takwa hili hakuwi ila kwa tawfiyq toka kwa Allaah Mtukufu. Kutokana na umuhimu wake, hata Rasuli mwenyewe alikuwa akikithirisha kuomba akisema:
"اللَّهُمَّ مُصَرِّفَ الْقُلُوبِ صَرِّفْ قُلُوبَنَا عَلَى طَاعَتِكَ"
“Ee Allaah! (ee) Mwenye kuzigeuza nyoyo, Zigeuze nyoyo zetu ziwe juu ya utiifu Kwako”. [Sunan At-Tirmidhiy]
Na alikuwa pia anaomba:
"يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِكَ"
“Ee Mwenye Kuzipindua nyoyo, Uthibitishe moyo wangu juu ya Dini Yako”. [Swahiyh Muslim: Kitaabul Qadar]
Na baada ya kuomba kukitwa nyoyo zao juu ya iymaan, hawatosheki na hilo, bali pia wanamwomba Allaah Awatunuku Rahma Zake toka Kwake. Wanamwomba Rahma Zake pana jumuishi zitakazowafanya kupata nuru ya iymaan, tawhiyd na maarifa ndani ya nyoyo zao, na kupata pia utiifu kamili wa viungo. Miongoni mwa matokeo ya rahmah hii ni kudumu juu ya uongofu hapa duniani, na kuzipata neema za kudumu huko aakhirah. Na kwa ajili hiyo, du’aa hii ya kuomba rahmah imekuja kwenye aayah nyingi ndani ya Qur-aan Tukufu. Kuzipata rahmah hizi za Allaah ni ufaulu mkubwa mno kwa Muislamu, kwa kuwa hata kuingia Peponi kunasimamia juu ya msingi wa kuzipata rahmah. Bila rahmah hakuna Pepo, hata mtu awe na mema ya kiasi gani. Hata Rasuli mwenyewe anasema kuwa hawezi kuingia Peponi ila baada ya kufunikwa na Rahma za Allaah.
Kutokana na haya, inatubainikia umuhimu wa kukithirisha kuomba Rahmah za Allaah ili tuweze kufaulu hapa duniani na kesho aakhirah, na tuweze kuingia Peponi kwa Rahmah hizo.
Kutokana na du’aa hii tunajifunza haya yafuatayo:
1- Mwanadamu hana uwezo wa kuumiliki moyo wake, kwani moyo huu uko kati ya Vidole Viwili katika Vidole vya Allaah ambapo Anaugeuza Anavyotaka. Hili limethibitishwa na Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo ni muhimu sana kukithirisha du’aa hii ili moyo uthibiti katika iymaan na wala usiyumbe yumbe au kutoka nje ya duara la iymaan.
2- Kumwomba Allaah kuthibiti juu ya iymaan ni moja kati ya makusudio makubwa anayotakiwa Muislamu ayapupie.
3- Muislamu anatakiwa azihudhurishe wakati wote Neema za Allaah kwake.
4- Umuhimu wa kutawassal kwa Allaah kupitia Neema Zake kwa kusema: “Baada ya kutuhidi”.
5- Viumbe wote hawana budi ila kumwomba Rabbi wao katika kuwaletea manufaa na kuwaondoshea madhara.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
05-Watoto Wema
"رَبِّ هَبْ لِي مِن لَّدُنْكَ ذُرِّيَّةً طَيِّبَةً إِنَّكَ سَمِيعُ الدُّعَاءِ"
“Rabb wangu! Nitunukie kutoka Kwako kizazi chema, hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia du’aa yangu”. [Aal ‘Imraan: (38)]
Nabiy Zakariyya (‘Alayhis Salaam) alipoona kwamba Allaah Ta’aalaa Anamruzuku Maryam matunda ya msimu wa baridi wakati wa kipindi cha joto, na matunda ya majira ya joto kipindi cha baridi, hapo alitamani kupata mtoto. Wakati huo alikuwa ni mzee ambaye mifupa yake imedhoofu na nywele zimejaa mvi. Pamoja na hali hiyo, mkewe pia alikuwa ni tasa. Lakini kutokana na ukamilifu wa iymaan yake na dhana yake njema kwa Mola wake juu ya ukamilifu wa Uwezo Wake, alielekea kumwomba bila kuchelewa.
Akamwomba Mola wake, akamwita mwito wa siri kama Alivyosema Allaah katika Suwrat Maryam:
"إِذْ نَادَى رَبَّهُ نِدَاءً خَفِيًّا"
“Alipomwita Rabb wake mwito wa siri”. [Maryam: (3)]
Tunamwona akimwomba Allaah Amtunuku, kwa kuwa kutunuku ni ihsani anayofanyiwa mtu bila ya mkabala wowote au kwa njia isiyo ya kawaida. Na hili linanasibiana na hali yake ya utu uzima na utasa wa mkewe ambaye hazai. Ni kana kwamba amesema: “Nipe mimi bila kupitia njia zilizozoeleka”. Yeye hapa hakuangalia njia wala visababisho kwa mazingira yake ya kawaida, bali alimwangalia Muumba wake na Mpatishaji wake. Na hii ndio iymaan safi ya kweli kwa Allaah Ta’aalaa, na ndio dhana njema ya mja kwa Mola wake.
Katika du’aa yake hii, Nabiy Zakariyyah ‘Alayhis Salaam amemwomba Allaah Amtunuku watoto wema. Hakuomba tu watoto, bali kafungamanisha ombi lake hilo na wema. Wema huu ni wa hapa duniani na aakhirah. Wema uwe katika maneno yao, matendo yao na hata pia katika miili yao. Ni wema wa kihisia na kidhahania.
Du’aa yake ameimalizia kwa kusema: “Hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia maombi”. Hapa anatoa sababu ya ombi lake. Kana kwamba anasema: “Mimi sikukimbilia Kwako na kukuomba isipokuwa kwa kujua kwangu kwa yakini kwamba Wewe Unajibu maombi na wala Humwangushi mtu”. Kaimalizia kwa Jina Lake Tukufu la “Mwenye Kusikia” ambalo Linanasibiana na ombi lenyewe. Na hapo moja kwa moja ikamjia bishara ya kukubaliwa ombi lake.
Tunajifunza kutokana na du’aa hii:
1- Kwamba viumbe wote wakiwemo Mitume na Manabii wanamhitajia Allaah Ta’aalaa. Wanahitajia kumwomba katika hali zao zote.
2- Haitakikani mtu aombe tu mtoto, bali aombe watoto wema. Watoto tu wanaweza kuwa fitnah na kiini cha matatizo kwake yeye mwenyewe. Watoto wema watamfaa duniani na aakhirah.
3- Dhana njema kwa Allaah ni ‘ibaadah njema pia. Allaah Humlipa Mja Wake na Humpa kwa mujibu wa nguvu ya dhana yake njema Kwake. Kutokana na dhana yake njema kwa Allaah, Zakariyah alimwomba Allaah hapo hapo kutokana na yale aliyoyaona kwa Maryam, na Allaah Akamjibu hapo hapo.
4- Mwenye kutamani jambo kubwa, au akaona kitu kikubwa anachokitamani, basi aelekee hapo hapo kwa Allaah amwombe, na wala asicheleweshe. Nabiy Zakariyyah alipoyaona ya Maryam, hapo hapo akaomba la kwake analolitamani ambalo alikuwa amelikatia tamaa kutokana na hali yake na hali ya mkewe.
5- Hapa kuna kiashirio kwamba du’aa inarejesha qadhwaa. Hii ni kwa vile, kwa sababu za kawaida tu, mwanamke tasa na mzee hawazai. Naye alipomwomba Allaah Amruzuku mtoto, bishara ilikuwa moja kwa moja.
"فَنَادَتْهُ المَلائِكَةُ"
“(Hapo hapo) Malaika akamwita”.
6- Umuhimu wa kutawassal kwa Majina Matukufu ya Allaah pamoja na Vitendo Vyake. Aliposema: هَبْ لِي “Nitunuku”, hapo alitawassal kwa Sifa ya Allaah ya Kutunuku, nayo ni Sifa ya kivitendo, na inanyambulika kutokana na Jina lake la “Al-Wahhaab”.
7- Kwa kutajwa kisa hiki cha ajabu pamoja na ombi jema la Zakariyyah, tunatakiwa tusikate kabisa tamaa na Fadhla za Allaah na Rahma Zake.
8- Inapendeza kuomba du’aa kwa siri. Hili limeashiriwa na Kauli Yake Ta’aalaa:
"إِذْ نَادَى رَبَّهُ نِدَاءً خَفِيًّا"
“Alipomwita Rabb wake mwito wa siri”.
9- Katika njia bora kabisa za kumfikia Allaah, ni mwombaji kutawassal Kwake kwa kuelezea udhaifu wake, uhitajio wake Kwake na udhalili wake ingawa yote hayo Allaah Anayajua. Lakini hapa ni kama anakiri hilo kwa kinywa chake kwamba yeye hawezi lolote ila kwa Nguvu na Msaada Wake Allaah. Angalia Nabiy Zakariyyah anavyojieleza:
"رَبِّ إِنِّي وَهَنَ الْعَظْمُ مِنِّي وَاشْتَعَلَ الرَّأْسُ شَيْبًا"
“Rabb wangu! Hakika mimi mifupa imeninyong’onyea na kichwa kimeng’aa mvi.” [Maryam: (04)]
10- Kumshtakia Allaah hakupingani na subira, bali ni ukamilifu wa utumwa kwa Allaah Ta’aalaa.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
06- Kuandikwa Pamoja Na Wenye Kushuhudia Haki
"رَبَّنَا آمَنَّا بِمَا أَنزَلَتْ وَاتَّبَعْنَا الرَّسُولَ فَاكْتُبْنَا مَعَ الشَّاهِدِينَ"
“Rabb wetu! Tumeamini Uliyoyateremsha na tumemfuata Rasuli, basi Tuandike pamoja na wanaoshuhudia (haki). [Aal ‘Imraan: (53)]
Du’aa hii iliombwa na wafuasi na wasaidizi waaminifu wa Nabiy ‘Iysaa ‘Alayhis Salaam wajulikanao kama “Al-Hawaariyyuwn”. Wameitwa hivi kutokana na usafi na weupe wa iymaan zao kwa Allaah Mtukufu wakawa katika daraja za juu kabisa za usafi kwa nje yao na ndani yao.
Du’aa yao hii wameianza kwa kutumia Jina Takatifu la Allaah la Rabb wakisema:
"رَبَّنَا آمَنَّا بِمَا أَنْزَلْتَ"
“Rabb wetu! Tumeamini Uliyoyateremsha”.
Waombaji wengi wakiwemo Mitume, Manabii na Waumini wema walikuwa wakitawassal kwa Allaah Ta’aalaa kwa kutumia Jina hili. Hili linaonekana pia kwenye du’aa nyingi zilizoko ndani ya Qur-aan Tukufu na hususan Aayah za mwisho za Suwrat Al-Baqarah.
Kisha wakaanza kujieleza wakisema kwamba wao wameamini yale yote Aliyoyateremsha katika Injiyl, na wamemfuata Rasuli wao ‘Iysaa (‘Alayhis Salaam) katika yale yote aliyowaletea – na haya yote Allaah Anayajua- na kwa ajili hiyo basi wanamwomba Awaandike pamoja na wenye kushuhudia. Na hii ndiyo iymaan kamili, kwani iymaan ndio msingi wa kila kitu, na ndiyo inayotangulizwa kabla ya yote. Kwanza kumwamini Allaah, kuamini Ubwana Wake, kuamini Uungu Wake na kuamini Majina Yake na Sifa Zake Tukufu.
Wamekusanya katika du’aa yao hii tawassulati mbalimbali adhimu; tawassuli kwa Ubwana wa Allaah, iymaan yao pamoja na matendo yao mema. Baada ya kujieleza kwao huko, mwisho wakataja ombi lao. Wakamwomba Allaah Awaandike pamoja na wenye kushuhudia. Hawa ni wale wenye kushuhudia haki, walioikubali tawhiyd, waliowasadiki Mitume, waliofuata Maamrisho ya Allaah na kujiepusha na makatazo Yake. Wakamwomba Allaah Awajumuishe katika kundi moja na hawa na Awakirimu pamoja nao.
Hili ndilo ambalo kila mmoja wetu anatakiwa aliombe na alipupie ili kuwa katika kundi hilo la wenye kushuhudia.
Tunajifunza kutokana na du’aa hii:
1- Kwamba iymaan ni lazima ikusanye yote Aliyoyateremsha Allaah.
2- Mtu kujishuhudishia mwenyewe kwamba yeye ni Muumini au ni Muislamu au mfano wa hayo, hakuzingatiwi kama ni riyaa na hususan katika kumfuata Rasuli na yote aliyokuja nayo. Kwa kuwa hilo lina faida, nayo ni kumtia nguvu mfuatwa.
3- Kuna umuhimu mkubwa wa kutawassal kwa Allaah kwa wasiylah zaidi ya moja. Manabii walitawassal kwa Allaah kwa wasiylah mbili kuu ambazo ni kumwamini Yeye na kufuata yote Aliyowateremshia.
4- Muislamu awe na pupa ya kusuhubiana na watu wema, kwa kuwa katika hilo kuna utengefu kwake duniani na aakhirah.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
07-Maghfirah, Kuimarishwa Miguu Na Ushindi Dhidi Ya Makafiri
"رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَإِسْرَافَنَا فِي أَمْرِنَا وَثَبِّتْ أَقْدَامَنَا وَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ "
“Rabb wetu! Tughufurie madhambi yetu na upindukaji wetu mipaka katika mambo yetu, na Ithibitishe miguu yetu na Tunusuru dhidi ya watu makafiri”. [Aal ‘Imraan: (147)].
Du’aa hii adhimu Waumini walikuwa wakiiomba katika uwanja wa vita kabla ya kukabiliana na adui au wakati vita vinapopamba moto. Na Allaah Ametueleza hili ili tuigize kitendo chao hicho pamoja na du’aa hii wakati tunapokabiliana na makafiri au wakati tunapopitiwa na misukosuko migumu. Vita vya kupigania Uislamu (Jihaad) –hata kabla ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba zake Al Kiraam- vilifanywa na Manabii wengi mno wakiwa na wafuasi wao Waislamu wakipambana kwa pamoja na makafiri ili kulinyanyua juu kabisa Neno la Allaah la Tawhiyd na Dini Yake. Allaah Anatuambia:
"وَكَأَيِّنْ مِنْ نَبِيٍّ قَاتَلَ مَعَهُ رِبِّيُّونَ كَثِيرٌ فَمَا وَهَنُوا لِمَا أَصَابَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّه وَمَا ضَعُفُوا وَمَا اسْتَكَانُوا وَاللَّهُ يُحِبُّ الصَّابِرِينَ"
“Na Manabii wangapi walipigana vita wakiwa pamoja nao Waumini wengi waliojaa Imani ya kikweli, basi hawakulegea kwa yaliyowasibu katika Njia ya Allaah, wala hawakudhoofika na wala hawakunyong’onyea. Na Allaah Anapenda wanaosubiri”. [Aal ‘Imraan: (146)]
Hawakunyong’onyea, hawakukata tamaa wala hawakuvunjika moyo hata kama matokeo ya vita hayakuwa mazuri, bali walirudi, wakajipanga upya, wakajiimarisha tena na kuwa tayari kwa raundi zijazo. Na hii yote ni kutokana na ungangari wao na nguvu ya iymaan yao. Na wakati huo mgumu wa kuumana vita, hawakuwa na jingine la kuomba isipokuwa kusema:
"رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَإِسْرَافَنَا فِي أَمْرِنَا وَثَبِّتْ أَقْدَامَنَا وَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ "
“Rabb wetu! Tughufurie madhambi yetu na upindukaji wetu mipaka katika mambo yetu, na Ithibitishe miguu yetu na Tunusuru dhidi ya watu makafiri”. [Aal ‘Imraan: (147)].
Walijiongezea wenyewe ombi hili pamoja na inavyoonesha kwamba wao ni wawajibikaji wazuri wa Maamrisho ya Allaah na katika kuipigania Dini Yake kwa ajili ya kujinyenyekeza na kujikusurisha kwa Allaah. Na huu ndio ukamilifu wa utumwa kwa Allaah Rabbi wa walimwengu.
Walijua kwa yakini kwamba madhambi na kupetuka Mipaka ya Allaah ni katika sababu kubwa za kufeli na kushindwa, na kwamba kuepukana na madhambi ni moja kati ya sababu za ushindi dhidi ya maadui au kupata mafanikio yoyote ya kidunia au ya kiaakhirah. Hapo ndipo walipomwomba Mola wao Awaghufurie madhambi yao yote. Na hizi ndizo sifa za Waumini wachaji. Wao daima wanakuwa katika hali ya kati ya matarajio na khofu hata pale wanapokuwa kwenye misukosuko mikubwa.
Kadhalika, walimwomba Allaah Aithibitishe miguu yao, yaani Azitie nguvu nyoyo zao ili miguu iweze kusimama imara. Nyoyo zikilegea, basi miguu haiwezi kusimama. Muislamu anamhitajia Allaah Amthibitishe moyo wake katika hali tatu:
1- Amthibitishe wakati wa kupambana na maadui. Kama Hakumthibitisha, basi atakimbia vita. Na kukimbia vita ni katika makosa makubwa sana kwa Muislamu.
2- Amthibitishe kwenye mambo ya shubha. Kama Hakumthibitisha basi atapotea.
3- Amthibitishe mbele ya matamanio ya nafsi. Asipomthibitisha basi ataangamia.
Na kwa vile wapiganaji hawa wakiwa na Manabii wao walikusanya matano wakati wa hali hizo ngumu; subra, kutonyong’onyea na kutokata tamaa, kuomba maghfirah, kuomba du’aa kwa adabu na unyenyekevu na kuomba nusura toka Kwake tu Allaah, Allaah Aliwajibu hapo hapo. Allaah Anasema:
"فَآتَاهُمُ اللَّهُ ثَوَابَ الدُّنْيَا وَحُسْنَ ثَوَابِ الْآخِرَةِ وَاللَّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ"
“Basi Allaah Akawalipa malipo ya dunia na thawabu nzuri za Aakhirah. Na Allaah Anapenda wafanyao ihsaan”. [Aal ‘Imraan: (148)]
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Muislamu anatakiwa amwombe Allaah kwa du’aa hii na hususan wakati wa kupambana na makafiri. Si katika vita tu, bali katika pambano lolote la kuitetea na kuipigania dini. Ni kama kwenye midahalo au katika kuwanusuru Waislamu wanaonyanyaswa kwa ajili ya dini yao.
2- Mwanadamu anamhitajia Allaah katika hali zake zote.
3- Mwanadamu hakosi kuvuka mipaka juu ya nafsi yake; ima kwa kuzidisha yasiyotakiwa, au katika kukusuru kwa kufanya jambo chini ya kiwango chake kinachotakiwa. Hivyo anatakiwa akithirishe du’aa hii kwa kuwa inanasibiana na hali yake.
4- Kutanua du’aa ni vizuri zaidi kuliko kuifupisha. Lau wao wangelisema: “Tughufirie” basi ingelitosha. Lakini wametanua zaidi du’aa yao wakiomba Awaghufirie madhambi yao madogo madogo, na kuvuka kwao mipaka kwa kutenda madhambi makubwa. Na kila mtu anavyozidi kutanua wigo wa du’aa yake na kuirefusha, basi anazidi kudhihirisha utumwa wake kwa Allaah. Na huu ndio ukomo wa unyenyekevu kwa Allaah Ta’aalaa.
5- Madhambi ndio sababu kuu ya udhaifu na kukosa Msaada wa Allaah. Na kwa ajili hiyo, walimwomba Allaah Awafutie madhambi yao ili mlango wa Msaada Wake ufunguke kwao waweze kuwashinda maadui zao makafiri.
6- Du’aa ni katika sababu kuu za mtu kupata muradi wake na kuondoshewa adha. Baada ya kuomba, Allaah Akawatimizia pale Anaposema: “Basi Allaah Akawalipa malipo ya dunia na thawabu nzuri za Aakhirah”.
7- Muislamu anatakiwa asitegemee tu nyenzo alizonazo, bali amtegemee Muumba wake na Mpatishaji wake. Waumini hao pamoja na wingi wao, hawakuangalia wingi huo kama ndio mwega, bali walitegemeza kusimama kwao imara mbele ya adui na kushinda kwa Allaah Ta’aalaa.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
08-Kukingwa Na Moto, Maghfirah Na Kufishwa Pamoja Na Watu Wema
"رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَذا بَاطِلاً سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ * رَبَّنَا إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ * رَّبَّنَا إِنَّنَا سَمِعْنَا مُنَادِيًا يُنَادِي لِلإِيمَانِ أَنْ آمِنُواْ بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا وَتَوَفَّنَا مَعَ الأبْرَارِ * رَبَّنَا وَآتِنَا مَا وَعَدتَّنَا عَلَى رُسُلِكَ وَلاَ تُخْزِنَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّكَ لاَ تُخْلِفُ الْمِيعَادَ"
“Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu Ni Wako, basi Tukinge na adhabu ya moto • Rabb wetu! Hakika Umuingizaye motoni, kwa yakini Umemhizi, na madhalimu hawana wasaidizi wa kuwanusuru • Rabb wetu! Hakika sisi tumemsikia mwitaji anaita kwenye iymaan kwamba mwaminini Rabb wenu basi tukaamini. Rabb wetu! Tughufurie madhambi yetu na Tufutie mabaya yetu na Tufishe pamoja na Waumini wema • Rabb wetu! Tupe pia Uliyotuahidi kupitia Rusuli Wako, wala Usituhizi Siku ya Qiyaamah, hakika Wewe Huendi kinyume na miadi”. [Aal ‘Imraan (191-194)].
Du’aa hizi tukufu zinatoka kwa watu waliojaa iymaan. Inatakikana kwa kila Muislamu asimame kidogo kuzitaamuli na kuzizingatia kutokana na mengi muhimu yaliyoko ndani yake.
Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) alimuuliza Mama yetu Swiddiyqah bint As Swiddiyq (Radhwiya Allaah ‘anhaa):
"أَخْبِرِينَا بِأَعْجَبِ شَيْءٍ رَأَيْتِيهِ مِنْ رَسُولِ اللَّهِ ، قَالَ: فَسَكَتَتْ ثُمَّ قَالَتْ: لَمَّا كَانَ لَيْلَةً مِنَ اللَّيَالِيِ قَالَ: يَا عَائِشَةُ، ذَرِينِي أَتَعَبَّدُ اللَّيْلَةَ لِرَبِّي، قُلْتُ: وَاَللَّهِ إنِّي لَأُحِبُّ قُرْبَك، وَأُحِبُّ مَا يَسُرُّك، قَالَتْ: فَقَامَ فَتَطَهَّرَ، ثُمَّ قَامَ يُصَلِّي، قَالَتْ: فَلَمْ يَزَلْ يَبْكِي حَتَّى بَلَّ حِجْرَهُ، قَالَتْ: وَكَانَ جَالِسًا، فَلَمْ يَزَلْ يَبْكِي حَتَّى بَلَّ لِحْيَتَهُ، قَالَتْ: ثُمَّ بَكَى، فَلَمْ يَزَلْ يَبْكِي حَتَّى بَلَّ الْأَرْضَ، فَجَاءَ بِلَالٌ يُؤْذِنُهُ بِالصَّلَاةِ، فَلَمَّا رَآهُ يَبْكِي قَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، لِمَ تَبْكِي وَقَدْ غُفِرَ لَك مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِك وَمَا تَأَخَّرَ؟ قَالَ: أَفَلَا أَكُونُ عَبْدًا شَكُورًا؟ لَقَدْ نَزَلَتْ عَلَيَّ اللَّيْلَةَ آيَةٌ وَيْلٌ لِمَنْ قَرَأَهَا وَلَمْ يَتَفَكَّرْ فِيهَا : إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ......."
“Tueleze jambo la ajabu zaidi uliloliona kwa Rasuli wa Allaah. Anasema: Akanyamaza (kukumbuka moja kati ya mambo hayo) kisha akasema: Ulipokuwa usiku mmoja kati ya nyusiku alisema: Ee ‘Aaishah! Niruhusu nifanye ‘ibaadah usiku huu kwa ajili ya Mola wangu. Nikamwambia: Wa Allaah, mimi napenda kuwa nawe karibu, na ninapenda linalokufurahisha. Akaenda kujitwaharisha, kisha akasimama na kuanza kuswali. Na hakuacha kuendelea kulia mpaka akailowesha nguo yake. Alikuwa amekaa, na akaendelea kulia mpaka akazitotesha ndevu zake. Kisha akalia, na akaendelea kulia mpaka akailowesha sakafu. Halafu Bilaal akaja kumjulisha wakati wa Swalaah. Alipomwona analia alimwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Kwa nini unalia nailhali wewe umeshasamehewa madhambi yako yaliyopita na yajayo?! Akamwambia: Kwa nini nisiwe mja mwingi wa kushukuru! Hakika imeniteremkia usiku huu aayah. Ole wake atakayeisoma na asiyataamuli yaliyomo humo: (Akasoma): Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana; bila shaka ni Aayaat (ishara, zingatio) kwa wenye akili.” [Imesimuliwa na Ibn Hibaan katika Swahiyh yake. Al-Albaaniy kasema: Isnaad yake ni nzuri]
Yaani, hizi mbingu zilivyonyanyuliwa na zilivyotanuliwa bila mipaka wala bila nguzo, na ardhi ilivyokuwa chini ya mbingu kwa masafa yasiyoweza kukokoteka, mbali na yaliyomo ndani ya viwili hivi na vilivyo baina yake kati ya tunavyovijua na tusivyovijua, bila shaka kwa wenye akili zingativu ni ishara ya wazi ya uwepo wa Allaah Ta’aala. Wenye akili hawa ni wale wanaomdhukuru Allaah katika hali zao zote kwa siri na hadharani.
Na wanatafakuri na kutaamuli uumbaji huu usio na mfano ambao hawezi yoyote kuufanya isipokuwa Allaah Mtukufu. Hii inadulisha kwamba kutafakuri huku ni katika sifa za Mawalii wa Allaah Ta’aalaa, na pia ni katika ‘ibaadah kubwa kabisa za moyo. Ni kutafakuri kwa kina kila kile unachokiona kwa macho yako katika maisha yako ya kila siku. Vyote hivyo vinaonyesha Uwezo wa Allaah na Uumbaji wake usio na kombo.
“Subhaanak” ni neno linalotokana na “Tasbiyh”. Maana yake ni kutakasa na kuweka mbali na ubaya au kasoro. Tunaposema “Subhaanah”, ni kuwa tunamtakasa Allaah Ta’aalaa kutokana na upungufu au kufanana na Viumbe Vyake. Tunamtakasa Yeye kuumba kitu kwa mchezo tu bila hikmah au lengo maalum.
Maneno yote haya yanaonyesha uzuri wa kutawassuli kwao wakati wa kuomba du’aa kwa kuyaeleza hayo kabla ya kusema ombi lao. Ni uzuri ulioje wa kuitandaza du’aa kwa tawasuli badala ya kuifupisha!
Na baada ya kutafakuri kwa kina, na kumtakasa Allaah kutokana na upungufu au kasoro yoyote, au kufanana na kiumbe Chake chochote, moja kwa moja wakamwomba Allaah Awakinge na adhabu ya moto. Kisha wakaeleza sababu ya kuomba kinga dhidi ya moto huo wakisema:
"رَبَّنَا إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ"
“Rabb wetu! Hakika Umuingizaye motoni, kwa yakini Umemhizi. Na madhalimu hawana wasaidizi wa kuwanusuru”.
Yaani Umemdhalilisha na Umemkhizi mbele ya halaiki katika “Mahshar”. Atakayekumbwa na hali hiyo, basi hatopata msaidizi yeyote, kwani Ufalme Siku hiyo ni Wake tu Allaah Al-Waahid Al-Qahhaar. Hiyo ndiyo Siku ambayo Waumini wanaiogopa ya kusimamishwa mbele ya Allaah na kuhisabiwa. Hao kwa khofu hiyo, jazaa yao itakuwa ni Jannah.
"وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَىٰ • فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَىٰ"
“Ama yule aliyekhofu kisimamo mbele ya Rabb wake, na akaikataza nafsi yake na hawaa • Basi hakika Jannah ndio makaazi yake”. [An-Naazi’aat: (40-41)]
Na baada ya kuomba kinga dhidi ya moto, wakaendelea kutawassuli zaidi kwa kujieleza kwa Allaah kwamba wamemsikia mwitaji anaita kwenye iymaan, naye ni Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nao bila kusita wakamwamini. Baada ya kujielezea kwa hili, hapo hapo wakaunganisha du’aa ya kuomba waghufuriwe madhambi yao, wafutiwe mabaya yao na wafishwe pamoja na Waumini wema wakisema:
"رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا وَتَوَفَّنَا مَعَ الأبْرَارِ"
“Rabb wetu! Basi Tughufurie madhambi yetu na Tufutie mabaya yetu na Tufishe pamoja na Waumini wema”.
Yaani, kwa sababu ya sisi kumsikia Rasuli akiulingania Uislamu, nasi tukamwamini na kukuamini Wewe, basi Tupe haya tuliyoyaomba. Wameitanguliza tawassuli hiyo huku wakijenga dhana njema kwa Allaah ili iwe njia ya kupatiwa lengo lao kuu la kupata maghfira na kuokoka Siku hiyo ya Qiyaamah.
Wakaendelea kuomba Allaah Awatekelezee yale Aliyowaahidi kupitia Rusuli Wake ya kuwanusuru, kuwamakinisha ardhini, kuzipata Radhi Zake na Jannah Yake aakhirah. Na pia Asiwakhizi Siku ya Qiyaamah. Wakaongezea hapa tawassuli nyingine ya kumwambia Allaah kwamba Yeye Hakhalifu Ahadi Yake.
* رَبَّنَا وَآتِنَا مَا وَعَدتَّنَا عَلَى رُسُلِكَ وَلاَ تُخْزِنَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّكَ لاَ تُخْلِفُ الْمِيعَادَ"
“Rabb wetu! Tupe pia Uliyotuahidi kupitia Rusuli Wako, wala Usituhizi Siku ya Qiyaamah, hakika Wewe Huendi kinyume na miadi”.
Na kutokana na kutawassuli kwao kwa kujieleza kwa mambo tofauti waliyoyafanya, na kutumia kwao Jina la Rabbi linalobeba maana ya ubwana, ulezi na usimamizi kwa viumbe vyote, kuwa kwao na ikhlasi na kuwa na dhana njema kwa Allaah, Allaah Aliwajibu du’aa yao.
Aayah hizi bainifu zinazotufafanulia du’aa njema wanazoziomba watu wenye akili angavu, zinatuhimiza tujitahidi kuziomba kwa unyenyekevu na udhalili. Na kutokana na umuhimu wake, imethibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akizisoma anaposimama usiku.
Tunajifunza kutokana na du’aa hizi:
1- Kuna umuhimu mkubwa sana wa kutaamuli uumbwaji wa mbingu na ardhi, kwa kuwa Allaah Ta’aalaa Ametaja ndani yake ishara nyingi.
2- Kutaamuli uumbaji wa Allaah kunamfanya Muislamu afanye ‘ibaadah kwa uzuri zaidi ikiwa ni pamoja na dhikri, du’aa, unyenyekevu na iymaan kuongezeka.
3- Fadhla ya kudumu katika kumdhukuru Allaah kwenye hali zote.
4- Umuhimu wa kumtakasa Allaah kutokana na kasoro yoyote au upungufu wowote (Kumsabbih).
5- Viumbe bora watakasifu wakiwemo Watu Wema na Manabii wanahitaji kuomba du’aa ya kulindwa na moto sembuse watu wa kawaida.
6- Du’aa kama inavyokuwa kwa tamko la ombi, inakuwa vile vile kwa tamko taarifu lenye kumaanisha ombi. Ni katika Kauli Yake Ta’aalaa:
رَبَّنَا إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ
“Rabb wetu! Hakika Umuingizaye motoni, kwa yakini Umemhizi”… kwa maana: Usitukhizi, Ukatuingiza motoni.
7- Kumwomba Allaah Ta’alaa mahitajio ya kidini, kidunia na kiaakhirah, ndio du’aa bora zaidi na ya ngazi ya juu zaidi.
8- Ubora wa kuikunjua du’aa badala ya kuifupisha, kwa kuwa kuikunjua kunasisitiza utumwa zaidi wa mja kwa Allaah. Kila mtu anavyokithirisha kuomba na kurefusha, hapo utumwa wake kwa Allaah unazidi kuongezeka pamoja na shauku. Pia kunadulisha mtu kutochoka na kukata tamaa, na hili ni katika visababisho vya kujibiwa.
9- Ni vizuri mwombaji ataje baadhi ya Neema za Allaah kwake wakati anapoomba kutokana na Neno Lake Ta’aalaa:
"أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا"
10- Mtu kuitaja amali yake njema hakuipomoshi. Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
"أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا"
11- Inafaa kutawassal kwa amali njema katika du’aa. Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
"رَبَّنَا إِنَّنَا آمَنَّا"
12- Umuhimu wa kutawassal kwa Allaah kwa kutumia Majina na Sifa Zake.
13- Katika uzuri wa du’aa ni mwombaji kueleza sababu ya ombi lake. Ni kama walivyosema:
إِنَّكَ مَنْ تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ[ ،]إِنَّكَ لَا تُخْلِفُ الْمِيعَادَ
14- Kusifu sana pamoja na tawassulati kubwa ni sababu kubwa ya kujibiwa du’aa.
15- Uhalali wa kutawassali kwa Allaah kwa kutumia Sifa Zake Kanushi kama vile: "إِنَّكَ لَا تُخْلِفُ الْمِيعَادَ" Hakika Wewe Huendi kinyuke na ahadi.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
09-Bila Maghfirah Na Rahma Hatima Ni Khasara
"رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ"
“Rabb wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu, bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika”. [Al-A’araaf: (23)].
Du’aa hii ya barakah ni ya baba na mama yetu Aadam na Hawaa (‘Alayhimas Salaam). Inatuonyesha namna ya kutubia na kurejea kwa Allaah baada ya kufanya makosa. Na kwa ajili hiyo, Allaah Ameitaja ili iwe ni mwangaza kwetu mpaka Siku ya Qiyaamah.
Katika du’aa hii, baba yetu na mama yetu baada ya kukiri kwamba wamezidhulumu nafsi zao, wameomba kwanza wasamehewe na kisha warehemewe, yaani wameomba maghfirah kabla ya rahmah, kwa kuwa rahmah haipatikani ila kwa maghfirah. Na mpangilio huu umekuja kwenye aayaati nyingi ndani ya Qur-aan Tukufu. Na ndio maana kuomba maghfirah kumehimizwa sana ndani ya Qur-aan na faida zake nyingi kutajwa ndani yake pamoja na kwenye Hadiyth za Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Tunajifunza kutokana na du’aa hii:
1- Kwamba kukiri kwanza kosa kisha kukubali kujidhulumu kabla ya kuomba msamaha, kuna matarajio makubwa zaidi ya kukubaliwa du’aa.
2- Umuhimu wa kutawassali kwa Jina la Allaah la Rabb wakati wa kuomba du’aa.
3- Du’aa hii imekusanya aina nne za tawassul:
Kwanza: Kutawassali kwa Jina la Rabb.
Pili: Kutawassali kwa hali ya waombaji kwa kukiri kwao: “Tumezidhulumu nafsi zetu”.
Tatu: Kulitegemeza jambo kwa Allaah waliposema: “Na kama Hutotughufuria na Kuturehemu”.
Nne: Kuelezea hatima yao itakavyokuwa kama Hatowasamehe na Kuwarehemu, nayo ni kwamba watakuwa wenye kukhasirika.
4- Du’aa hii ni katika miundo bora zaidi ya kuomba maghfirah. Allaah Ndiye Aliyemfundisha Aadam ‘Alayhis Salaam na itaendelea kuombwa mpaka Siku ya Qiyaamah.
5- Ukamilifu wa du’aa ni mwombaji kukusanya kati ya utashi, hofu na tawbah. Hapa ni pale waliposema:
"وَإِنْ لَمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ"
6- Dhambi lolote ni lazima tulikuze na tulione kubwa, kwani dhambi lolote kwa haki ya mkubwa ni kubwa.
7- Du’aa ndio makimbilio kwa Manabii na Mitume wote. Hakuna awezaye kughafilika nayo au kutoijali isipokuwa waovu.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
10-Kuepushwa Kuwa Kundi Moja Na Madhalimu
"رَبَّنَا لاَ تَجْعَلْنَا مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ"
“Rabb wetu! Usitujaalie kuwa pamoja na watu madhalimu”. [Al-A’araaf: (23)]
Hii ni du’aa ya watu wa “Al-A’araaf”, napo ni mahala kati ya Pepo na moto. Si mahala pa kutulia hapo, bali ni pa watu ambao mema yao yamelingana na mabaya yao. Watakaa hapo kwa muda Aupendao Allaah, kisha hatimaye wataingia Peponi baada ya roho kuwa juu juu. Watakuwa wakiogopa hata kutupa jicho kuwaangalia watu wa motoni kutokana na kitisho kikubwa cha moto wenyewe na hali za waliomo humo. Hapo macho yao yatageuziwa huko waangalie, na kutokana na watakayoyaona, ndipo wataomba du’aa hii Allaah Asiwapeleke huko wakajumuika na hao madhalimu.
"وَإِذَا صُرِفَتْ أَبْصَارُهُمْ تِلْقَاءَ أَصْحَابِ النَّارِ قَالُوا رَبَّنَا لَا تَجْعَلْنَا مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ"
“Na yatakapogeuzwa macho yao kuelekea watu wa motoni watasema: Rabb wetu! Usitujaalie kuwa pamoja na watu madhalimu”. [Al-A’araaf: (47)]
Hakika ni kisimamo kigumu mno hapo! Hali hii inatuzindusha kuwa tujitahidi kiasi tuwezavyo kufanya amali zote njema ili mizani yetu iwe nzito tusije kukwama hapo, na tujiepushe na yote mabaya hata kama tunayaona ni madogo vipi. Pengine tasbiyha moja tu inaweza ikailaza miyzaan akaokoka mtu, au kosa moja dogo tu linaweza kupindua mizani na kumfanya mtu kuingia Motoni. Tusidharau jema lolote, tusidharau baya lolote.
Muumini anatakiwa aendelee kumwomba Allaah Ta’aalaa Asimjaalie kuwa pamoja na watu madhalimu hapa duniani na huko aakhirah. Anatakikana aepukane nao hapa hapa duniani ili asije kuwa nao kundi moja Siku ya Qiyaamah, kwani watakuwa mahala pabaya kabisa kwenye adhabu ya kuwadhalilisha.
Tunajifunza kutokana na du’aa hii:
1- Kwamba Muislamu anatakiwa ajiepushe na kila lile litakalompelekea katika hatima mbaya ya kuishilia Jahannam –tunajilinda nayo kwa Allaah- katika maneno, vitendo na mwenendo.
2- Muislamu anatakiwa akithirishe kuomba du’aa hii muhimu kwa kuwa imekusanya ndani yake kuomba kinga ya hatima mbaya zaidi.
3- Muislamu ajiepushe awezavyo kushirikiana na madhalimu kwa kuwa atakuwa pamoja nao ndani ya moto.
4- Dhulma si tu kuchukua mali za watu kinyume na sheria, bali ni kila kitendo kitakachomsababishia mtu kuishilia pabaya. Kwani dhulma ni kukiweka kitu mahala ambapo si pake. Ukiweka utupu wako sehemu isiyo halali, basi umedhulumu, ukipetuka Mipaka ya Allaah, basi umedhulumu na kadhalika. Allaah Alipomkataza Baba yetu Aadam asile mti Alimwambia: “Wala msiukaribie mti huu, mtakuwa katika madhalimu”. Mtu akifanya katazo lolote hata la kidunia, au akavunja sheria, basi anakuwa amejidhulumu mwenyewe kwa kuwa atakabiliwa na vyombo vya sheria. Na siku hiyo, kila dogo na kubwa litahisabiwa, na hatima ya mtu itakuwa kwa mujibu wa matokeo ya hisabu.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
11- Kuandikiwa Mema Ya Dunia Na Ya Aakhirah
"أَنتَ وَلِيُّنَا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا ۖ وَأَنتَ خَيْرُ الْغَافِرِينَ • وَاكْتُبْ لَنَا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ"
“Wewe Ni Mlinzi wetu, basi Tughufurie na Turehemu, Nawe Ni Mbora wa wenye kughufuria • Na Tuandikie katika dunia hii mazuri na katika Aakhirah”. [Al-A’araaf (155-156)]
Hii ni du’aa iliyoombwa na Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam). Aliiomba pale alipokwenda na watu wema 70 katika Baniy Israaiyl kwa ajili ya miadi maalum na Allaah ili kumwomba msamaha baada ya kuabudu ndama. Walipofika mahala pa miadi, watu wake hao walimwambia Muwsaa: “Hatutokuamini mpaka tumwone Allaah wazi wazi, kwani wewe umezungumza Naye, basi tuonyeshe nasi tumwone”.
Hapo ikawachukua radi na umeme angamizi wakafa. Na Muwsaa (‘Alayhis Salaam) akaomba du’aa hii. Akamwomba Allaah Awaghufirie madhambi yao na Awarehemu kwa Rehma Zake ambazo zimekienea kila kitu. Akatanguliza du’aa kwa Jina Tukufu la Allaah la “Al-Waliyy” lenye maana ya kuwa Allaah Ndiye Mwenye Kuyasimamia mambo ya viumbe vyote ya duniani na aakhirah, na Ndiye Mwenye Kuwalinda na Kuwahifadhi. Akatanguliza pia kiwakilishi “Wewe” ili iwe ni ufunguo wa kupenyeza ombi lake la maghfirah na rahma. Hii ni adabu njema kabisa ya kutawassali kwa Majina ya Allaah Mtukufu.
Kisha baada ya kuomba maghfirah na rahmah, akamwomba Allaah Awaandikie mema hapa duniani na aakhirah. Ameomba kuandikiwa kwa kuwa chenye kuandikwa kinakuwa ni cha kudumu, cha kuendelea na chenye kukariri mara kwa mara. Ama kitu cha muda tu, hicho hakiandikwi. Na mema ni neno jumuishi kwa kila lile analolitamani mtu katika dini yake, dunia yake na aakhirah yake.
Tunajifunza katika du’aa hii:
1- Kwamba mwombaji anatakiwa atumie matamshi matukufu zaidi, maana nzuri zaidi na utukuzo kwenye du’aa yake. Ni kama kutumia kiwakilishi cha “Wewe” kwa Allaah Mtukufu.
2- Kutawassali kwa Jina kati ya Majina Matukufu ya Allaah kama "الولي" . Ni kama ilivyo katika aayah: "وَلِيُّنَا".
3- Kuzingatia maombi yenye umuhimu zaidi ya kidunia na kiaakhirah. Nayo ni kuomba maghfirah na rahmah. Ni kama pale waliposema: "فاغفر لنا وارحمنا".
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
12-Toshelezo La Allaah
"حَسْبِيَ اللَّهُ لا إِلَـهَ إِلاَّ هُوَ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَهُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ"
“Amenitosheleza Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Kwake nimetawakali. Naye Ni Rabb wa ‘Arsh Adhimu”. [At-Tawbah: (129)]
Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifundishwa kuisema du’aa hii wakati makafiri wanapompinga na kukataa haki aliyowaletea, na pale walipokataa nasaha zake na mawaidha ya haki. Du’aa hii ni ya kutaka Msaada wa Allaah dhidi ya wapingaji hao, na kutawakali kwa Allaah pamoja na matatizo yote yanayomsumbua mtu.
Du’aa hii ina maana: “Rabbi wangu Ndiye Mwenye Kunitosha mimi na yote yenye kunipa ghamu, na hakuna mwingine wa kuabudiwa kwa haki ila Yeye tu, na Kwake tu nimetegemea, na Ni Yeye Pekee tu ninayemwamini katika kuniletea yenye kunifaa na kuniondoshea yenye kunidhuru”.
Na Yeye pia Ndiye Anayemiliki ‘Arshi ambayo ndiyo kiumbe kikubwa zaidi kuliko vyote, chenye kuzunguka kila kitu, na Yeye Yuko juu yake kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye Mwenyewe Allaah.
Du’aa hii iko katika muundo taarifu lakini ndani yake kuna ombi. Kana kwamba mwombaji anasema: Nitosheleze ee Rabbi wangu na kila kitu kinachonisumbua na kinachoniogopesha”. Imekusanya dhana kamili njema, yakini kwa Allaah, kumpwekesha Allah, kumtegemea Yeye tu na kumsifu. Yeye tu Ndiye Astahikiye kuogopwa, na Kwake tu mambo yote yanarejea.
Du’aa hii ina fadhila kubwa sana. Imepokelewa toka kwa Abud Dardaai kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنْ قالَ فِي كُلّ يَوْمٍ حِينَ يُصْبحُ، وَحِينَ يُمْسِي : حَسْبِيَ اللَّهُ لا إِلهَ إِلاَّ هُوَ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَهُوَ رَبُّ العَرْشِ العَظِيمِ، سَبْعَ مَرَّاتٍ كَفَاهُ اللَّهُ تَعالى ما أهمَّهُ مِنْ أمْرِ الدُّنْيا والآخِرَة"
“Mwenye kusema kila siku anapopambaukiwa na anapoingiliwa na jioni: Amenitosheleza Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Kwake nimetawakali. Naye Ni Rabb wa ‘Arsh Adhimu, mara saba, Allaah Ta’aalaa Atamtosheleza na kila linalomletea ghamu katika mambo ya dunia na aakhirah”. [Imesimuliwa na Ibn As-Sunniyy katika kitabu chake cha “Amalul Yaymi wa Al Laylati]
Tunajifunza kutokana na du’aa hii yafuatayo:
1- Du’aa hii ina umuhimu mkubwa kutokana na fadhila zake zilizoelezewa kwenye Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni muhimu sana kuisoma asubuhi na jioni mara saba kila siku, itakuondoshea ghamu na hamu zote za dunia na aakhirah.
2- Kutawakali ni sababu ya Allaah kumtosheleza Mja Wake. Ni kama Alivyosema:
"وَمَنْ يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَهُوَ حَسْبُهُ"
“Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza”. [At-Twalaaq: (3)]
3- Ubora wa neno la Tawhiyd. Kuna uokozi ndani yake duniani na aakhirah.
4- Umuhimu wa kutawassali kwa Allaah kwa Tawhiyd Yake, kutawakkali Kwake, na Ubwana Wake kwa Kiumbe Chake kikubwa zaidi kuliko vyote (‘Arshi).
5- Du’aa kama inavyokuwa kwa tamshi la ombi, pia inakuwa kwa tamshi taarifu.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
13-Tusiwe Fitnah Kwa Watu Madhalimu
"رَبَّنَا لَا تَجْعَلْنَا فِتْنَةً لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ● وَنَجِّنَا بِرَحْمَتِكَ مِنَ الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ"
“Ee Rabb wetu! Usitujaalie kuwa ni mtihani kwa watu madhalimu ● Na Tuokoe kwa Rahmah Yako na watu makafiri”. [Yuwnus: (85-86)].
Hii ni miongoni mwa du’aa nyingi za Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) wakati akikabiliana na Fir-‘awn. Inatuonyesha namna Muislamu anavyokabiliana na makafiri na madhalimu ambapo la kwanza kulifanya ni kutawakkal kwa Allaah kwa kufanya maandalizi yote yanayohitajika na kubeba nyenzo zote, halafu kuelekea kwa Allaah kwa du’aa.
Fir-‘awn kwa jeuri yake, aliikataa miujiza yote aliyokuja nayo Muwsaa kuthibitisha Utume wake, hoja zisizopingika na dalili bayana alizomtolea. Lakini pamoja na hivyo, vijana wachache katika Baniy Israaiyl walimwamini Muwsaa kutokana na ukweli waliouona kama Anavyosema Allaah:
"فَمَا آمَنَ لِمُوسَىٰ إِلَّا ذُرِّيَّةٌ مِّن قَوْمِهِ عَلَىٰ خَوْفٍ مِّن فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِمْ أَن يَفْتِنَهُمْ ۚ وَإِنَّ فِرْعَوْنَ لَعَالٍ فِي الْأَرْضِ وَإِنَّهُ لَمِنَ الْمُسْرِفِينَ"
“Basi hawakumwamini Muwsaa isipokuwa dhuriya (vijana) katika kaumu yake kwa sababu ya kumkhofu Fir’awn na wakuu wao wasiwatese. Na hakika Fir’awn ni jeuri katika ardhi, na hakika yeye bila shaka ni miongoni mwa wapindukao mipaka”. [Yuwnus: (83)].
Wengi kwa kumwogopa Fir-‘awn, walishindwa kuamini au kutangaza iymaan yao hadharani.
Kisha Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) aliwaamuru watawakkal kwa Allaah tu.
"وَقَالَ مُوسَىٰ يَا قَوْمِ إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ فَعَلَيْهِ تَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّسْلِمِينَ"
“Na Muwsaa akasema: Enyi kaumu yangu! Ikiwa mmemwamini Allaah, basi Kwake mtawakali, mkiwa ni Waislamu”. [Yuwnus: (84)]
Kwa kuwa Allaah Pekee Ndiye Mwenye Kumtosha Mja Wake kwa kila lile analoliogopa au kila linalomletea ghamu.
"وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ"
“Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza”.
Na ili mja aweze kupata toshelezo kamili la Allaah, basi ni lazima asimamie vyema ‘ibaadah zake zote, kisha atawakkal. Allaah kwenye aayah nyingi Amekutanisha ‘ibaadah na tawakkul. Anasema:
"فَاعْبُدْهُ وَتَوَكَّلْ عَلَيْهِ"
“Basi mwabudu Yeye na tawakali Kwake”. [Huwd: (123)].
Muwsaa akawaambia: “Kama nyinyi mmemwamini kikweli Allaah ikiwa pamoja na Nusra Yake kwenu, basi tawakalini Kwake tu”. Ameikariri sharti kwao kusisitizia na kubainisha kwamba ukamilifu wa iymaan unakuja kwa kutegemeza mambo yote kwa Allaah. Hapo hapo nao wakajibu na kutii wakisema: “Tumetawakali kwa Allaah”.
Kisha wakamwomba Allaah wakisema: “Usitujaalie kuwa ni mtihani kwa watu madhalimu”. Kwa maana: Usiwape usaidizi dhidi yetu wakatushinda, likawa hilo ni mtihani kwetu kwa dini yetu, au makafiri wakafitinika kwa ushindi wao dhidi yetu wakasema: Kama (Waislamu) wangelikuwa juu ya haki, basi wasingelishindwa”.
Fitnah hii ndio sasa imetawala baada ya sisi Waislamu kuwa katika hali ya udhaifu wa mwisho kabisa. Kila mmoja ametulenga sisi kutokana na udhaifu huo.
Na baada ya kumwomba Allaah Ailinde Dini kutokana na ufisadi, wakaandamizia kumwomba usalama kwa nafsi zao kutokana na watu makafiri wakisema: “Na Tuokoe kwa Rahmah Yako na watu makafiri”. Wameikhusisha tawassul yao kwa Rahma za Allaah, kwa kuwa kwa Rahmah hizo, ombi hujibiwa. Na kwa ajili hii, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anajilinda kutokana na misiba ya dini, kwani hiyo ndio misiba na maangamio makubwa zaidi. Alikuwa anasema:
"وَلَا تَجْعَلْ مُصِيبَتَنَا فِي دِينِنَا"
“Wala Usijaalie msiba wetu ndani ya dini yetu”.
Tunajifunza kutokana na du’aa hizi:
1- Kwamba iymaan ya kweli inapelekea kutawakkal kwa Allaah Pekee.
"يَا قَوْمِ إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ فَعَلَيْهِ تَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّسْلِمِينَ"
“Enyi kaumu yangu! Ikiwa mmemwamini Allaah; basi Kwake mtawakali, mkiwa ni Waislamu”.
2- Du’aa haipingani na tawakkul, bali ni kipengele kisaidizi cha kufanikisha tawakkul.
3- Muislamu anatakikana ajilinde na fitna kutokana na hatari yake kwa dini. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"تعوَّذوا باللَّه من الفتن: ما ظهر منها، وما بطن"
“Jilindeni kwa Allaah na fitnah, zilizodhihiri kati yake, na zilizofichika”. [Swahiyh. Imesimuliwa na Zayd bin Thaabit]
Na alikuwa pia anasema katika du’aa yake kabla ya kumaliza Swalah yake:
"اللَّهُمَّ إني أعوذ بك من عذاب جهنم، ومن عذاب القبر، ومن فتنة المحيا والممات"
“Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na adhabu ya Jahannam, na adhabu ya kaburi, na fitnah ya uhai na umauti”. [Swahiyh. Muslim]
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
14-Kufishwa Na Uislamu Na Kuunganishwa Na Watu Wema
"تَوَفَّنِي مُسْلِمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ"
“Nifishe hali ya kuwa Muislamu na Unikutanishe na Swalihina”. [Yuwsuf: (101)]
Du’aa hii ya barakah ni ya Nabiy Yuwsuf (‘Alayhis Salaam) aliyomwomba Mola wake ilipotimia kwake neema ya kukutana na kujumuika na wazazi wake na nduguze, pamoja na neema ya Utume na Ufalme. Alimwomba Mola wake ‘Azza wa Jalla, kama Alivyomtimizia neema hizo hapa duniani, Amtimizie pia huko aakhirah, na Amfishe hali ya kuwa ni Muislamu wakati atakapokufa, na Amkutanishe na Swalihina ambao ni pamoja na nduguze Manabii na Mitume Rehma na Amani za Allaah ziwe juu yao wote.
Hii inatuonyesha umuhimu wa du’aa, na kwamba du’aa ndio mwenendo wa Manabii na Mitume wote (‘Alayhimus Swalaat was Salaam), na ndio makimbilio yao wakati wa dhiki na faraja na katika hali zao zote. Na kwamba du’aa inatakikana iwe ndio makimbilio ya mja katika maisha yake na katika mambo yake yote, na kila dogo lake na kila kubwa lake.
Du’aa hii ameianza kwa kutaja Jina Tukufu la Allaah la Rabb na kuelezea Neema Alizoneemeshwa na Allaah ya kupewa ufalme na kufundishwa kutegua ndoto. Kisha akaandamiza Sifa nyingine ya Allaah ya uumbaji wa mbingu na ardhi na halafu Jina la “Al-Waliyy” (Mlinzi na Msaidizi). Hizi zote ni katika tawassulaat na adabu njema za kuomba du’aa, na ni mihimili ya kujibiwa. Haya yote yanadhihirika katika aayah kamili isemayo:
"رَبِّ قَدْ آتَيْتَنِي مِنَ الْمُلْكِ وَعَلَّمْتَنِي مِن تَأْوِيلِ الْأَحَادِيثِ ۚ فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَنتَ وَلِيِّي فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۖ تَوَفَّنِي مُسْلِمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ"
“Rabb wangu! Kwa yakini Umenipa utawala, na Umenifunza katika tafsiri za masimulizi (ya ndoto na matukio). Muanzilishi wa mbingu na ardhi. Wewe Ni Mlinzi, Msaidizi wangu duniani na Aakhirah. Nifishe hali ya kuwa Muislamu na Unikutanishe na Swalihina”. [Yuwsuf: (101)]
Amemwomba Allaah Amkite na Amthibitishe imara juu ya Uislamu mpaka Atakapomfisha. Hali hii inahitajia Msaada wa Allaah na tawfiyq kutoka Kwake, na mja anatakiwa afuate na ashikamane na miongozo yote ya kumfanikishia hilo huku Akimwomba Allaah Amwafikishe hilo. Na mtu kufa na Uislamu wake na tawhiyd safi, ni katika mafanikio makubwa ambayo sote tunatakikana tuyaendee mbio. Hiyo ndiyo “Husnul Khaatimah”. Tuendelee pia kumwomba Allaah Atuepushe na fitnah ya uhai na fitnah ya wakati wa kufa ambapo shaytwaan hufanya juhudi zake zote za mwisho za kumteteresha Muislamu na iymaan yake ili afe kafiri. Tunaomba salama.
Hata Rasuli mwenyewe, pamoja na kwamba ndiye Kipenzi cha Allaah na mwisho wa Manabii na Mitume, alikuwa akimwomba Allaah Amkite na Amthibitishe juu ya Uislamu mpaka afe. Alikuwa anasema:
"يا وليَّ الإسلام وأهله، مسكني بالإسلام حتى ألقاك عليه"
“Ee Mlinzi (na Msimamizi) wa Uislamu na watu wake! Nikite na Nithibitishe kwenye Uislamu mpaka Nikutane Nawe nikiwa bado niko nao”. [Imesimuliwa na Anas bin Maalik na kukharijiwa na At-Twabaraaniy]
Kisha Nabiy Yuwsuf (‘Alayhis Salaam) akamwomba Allaah Amkamilishie neema hizi kwa kumkutanisha na watu wema katika Pepo ya Kudumu.
Faida ya du’aa hii:
Du’aa hii imejumuisha:
1- Kukiri tawhiyd.
2- Kujisalimisha kwa Rabb ‘Azza wa Jalla.
3- Kudhihirisha uhitajio wa mja Kwake.
4- Kujiweka mbali na ulinzi usio wa Allaah.
5- Kufa juu ya Uislamu kuwa ndio lengo kuu la Muislamu, na kwamba hilo liko mkononi mwa Allaah tu, na si mkononi mwa kiumbe chochote.
6- Kukiri marejeo ya aakhirah.
7- Kuomba usuhuba wa watu wema.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
15- Amani Kwa Makkah Na Kuepushwa Na Masanamu
"رَبِّ اجْعَلْ هَـٰذَا الْبَلَدَ آمِنًا وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ"
“Ee Rabb wangu! Ujaalie mji huu (Makkah) uwe wa amani, na Uniepushe na wanangu kuabudu masanamu. [Ibraahiym: (35)]
Ni katika du’aa za baba yetu Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam). Inabeba ndani yake maana na makusudio makubwa.
Amemwomba Allaah Aujaalie mji wa Makkah uwe mji wa amani, na Allaah Akamtakabalia du’aa yake kisharia na kiqadar, hata ikawa ni marufuku mtu kubeba silaha ndani ya mji huu. Na hata yule anayekusudia ubaya kwa mji huu, Allaah Humvunjilia mbali na Humwonjesha adhabu kali kama Alivyowafanya watu wa tembo na wengineo.
"وَمَن يُرِدْ فِيهِ بِإِلْحَادٍ بِظُلْمٍ نُّذِقْهُ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ"
“Na yeyote anayekusudia humo kufanya upotofu kwa dhulma Tutamuonjesha adhabu iumizayo”. [Al-Hajj: (25)]
Mbali na kuuombea mji huu amani, Nabiy huyu kutokana na huruma na ukarimu wake uliopitiliza, aliwaombea watu na wakazi wake kwa Allaah Awaruzuku mazao na matunda kwa wingi ambayo ni moja kati ya neema kubwa.
"وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ اجْعَلْ هَـٰذَا بَلَدًا آمِنًا وَارْزُقْ أَهْلَهُ مِنَ الثَّمَرَاتِ مَنْ آمَنَ مِنْهُم بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ قَالَ وَمَن كَفَرَ فَأُمَتِّعُهُ قَلِيلًا ثُمَّ أَضْطَرُّهُ إِلَىٰ عَذَابِ النَّارِ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ"
“Na pindi aliposema Ibraahiym: Rabb wangu! Ufanye mji huu (Makkah) kuwa wa amani, na Waruzuku watu wake matunda, atakayemwamini Allaah miongoni mwao na Siku ya Mwisho. (Allaah) Akasema: Na atakayekufuru basi Nitamstarehesha kidogo kisha Nitamsukumiza katika adhabu ya moto. Na ubaya ulioje mahali pa kuishia!”. [Al-Baqarah: (126)]
Na baada ya kuuombea mji huu amani ambayo ni moja kati ya neema kubwa, alijiombea mwenyewe pamoja na wanawe Allaah Awaepushe na ibada ya masanamu. Akamwomba Amkite juu ya tawhiyd safi takasifu kutokana na uchafu wote wa shirki, na kila lile ambalo linaweza kuichafua tawhiyd yake na ya kizazi chake. Huu ndio Uislamu wa kweli. Muislamu asijiangalie yeye tu, bali na wanawe pia, mkewe na nduguze Waislamu.
"وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا”
“Na wale wanaosema: Rabb wetu! Tutunukie katika wake zetu na dhuria wetu viburudisho vya macho yetu, na Tujaalie kuwa waongozi kwa wenye taqwa. [Al-Furqaan: (74)].
Ibn Kathiyr (Rahimahul Laah amesema: “Kila mwenye kuomba anatakiwa ajiombee mwenyewe, wazazi wake wawili na watoto wake”.
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Kwamba kila Muislamu anatakiwa akithirishe sana du’aa hii ili kupata kinga kutokana na dhambi kubwa na ya hatari zaidi ambayo ni shirki. Shirki ni dhulma kubwa zaidi kuliko zote, na ni dhambi isiyosamehewa mtu akifa nayo bila kutubia.
2- Mwombaji anatakiwa ayatupe malalamiko yake kwa Allaah kwa yale anayoyaogopa na kuyahofia. Huu ndio mwenendo wa Manabii katika maombi yao. Katika mwendelezo wa du’aa, Nabi Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) anasema:
"رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ ۖ فَمَن تَبِعَنِي فَإِنَّهُ مِنِّي ۖ وَمَنْ عَصَانِي فَإِنَّكَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ"
“Rabb wangu! Hakika hao (masanamu) wamepoteza watu wengi. Basi atakayenifuata, huyo yuko nami, na atakayeniasi, basi hakika Wewe Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu”. [Ibraahiym: (36)]
Naye Nabiy Ya’aquwb (‘Alayhis Salaam) baada ya kupata mtihani wa kupotelewa na mwanawe Yuwsuf (‘Alayhis Salaam) alimlalamikia Rabbi wake akisema:
"قَالَ إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّـهِ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ"
“Akasema: Hakika mimi nashitakia dhiki ya majonzi yangu na huzuni zangu kwa Allaah. Na najua kutoka kwa Allaah yale msiyoyajua”. [Yuwsuf: (86)]
Naye Ayyuwb baada ya kuugua muda mrefu, aliomba huku akisema:
"وَأَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ "
“Na Ayyuwb, alipomwita Rabb wake: Hakika mimi imenigusa dhara, Nawe Ndiye Mbora zaidi wa Kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu”. [Al-Anbiyaa: (83)]
3- Ni lazima Muislamu aziepuke sababu na hali zote zinazowapoteza watu kuacha dini yao.
"رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ”
“Rabb wangu! Hakika hao (masanamu) wamepoteza watu wengi”.
4- Inatakikana kwa kila mmoja wetu ajiombee mwenyewe salama na watoto wake kutokana na madhambi makubwa vyovyote yeye afikiavyo kwa utiifu kwa Allaah na kufanya ‘ibaadah.
5- Umuhimu wa kulipa hima suala la tawhiyd na aqiydah, na katika ujumla wake kuomba du’aa Kwake Allaah tu.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
16- Kusimamisha Swalah Pamoja Na Watoto
"رَبِّ اجْعَلْنِي مُقِيمَ الصَّلَاةِ وَمِن ذُرِّيَّتِي ۚ رَبَّنَا وَتَقَبَّلْ دُعَاءِ"
“Rabb wangu! Nijaalie niwe mwenye kusimamisha Swalaah pamoja na baadhi ya dhuria wangu. Rabb wetu! Nitakabalie du’aa yangu”. [Ibraahiym: (40)]
Hii pia ni du’aa ya Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam). Muislamu anatakikana awe na hima na du’aa hii na ashikamane nayo kutokana na umuhimu wake mkubwa.
Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) amemwomba Allaah Amjaalie awe ni mwenye kuihifadhi Swalaah katika wakati wake, nguzo zake na masharti yake pamoja na yote yenye kuifanya Swalaah kuwa kamili yenye kukubaliwa. Na hapa ameikhusisha Swalaah kutokana na umuhimu wake na kuwa kwake nembo ya iymaan na kichwa cha Uislamu. Amewaombea pia baadhi ya dhuria wake wawe pia ni wenye kuisimamisha Swalaah kwa ukamilifu wake unaotakikana. Amewakhusu baadhi ya dhuria wake kwa du’aa hii pasina wengine kwa kujua kwake baada ya kujuvywa na Allaah kuwa baadhi ya dhuria wake hawatosimamisha Swalaah, na wengine watakuwa ni makafiri na wengine mafasiki.
Kisha akamwomba Allaah kwa kutumia Jina la Rabbu kuonyesha utumwa wake Kwake na kutawassali kwa Jina hilo Tukufu akimwomba Amtakabalie du’aa yake hii.
Du’aa hii ni katika du’aa bora kabisa anazoomba Muislamu kujiombea mwenyewe na wanawe. Ni uzuri ulioje yeye na wanaye kuwa ni wenye kusimamisha Swalaah kama inavyotakikana! Haya ni katika mafanikio makubwa kabisa ya kumshukuru Allaah.
Faida kutokana na du’aa hii:
1- Umuhimu wa Swalaah. Ameikhusisha hapa pasi na ‘ibaadah nyinginezo.
2- Umuhimu wa kutawassali kwa Urabb wa Allaah Ta’aalaa kwa kuwa kujibiwa du’aa kwalo ni katika mihimili muhimu.
3- Umuhimu wa kukazania jambo katika du’aa. Katika sentensi moja ya du’aa hii, Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) amekariri neno la Rabb mara mbili.
4- Mwombaji anatakiwa akithirishe kumwomba Allaah Amtakabalie du’aa yake.
5- Kila mwombaji anatakiwa ajiombee mwenyewe, wazazi wake na dhuria wake.
6- Du’aa ndio makimbilio ya Manabii wote, Mitume na Swalihina, bali viumbe vyote.
7- Kama unawajibika kuswali Swalaah tano, basi usivimbe kichwa na kuwadharau wengine wasiowajibika. Jua kwamba hiyo ni tawfiyq ya Allaah kwako. Jaribu kuwakumbusha na kuwaombea Allaah Awahidi. Hao ni nduguzo katika dini ingawa ni mafasiki.
8- Jaribu kuwazoeza watoto Swalaah tokea udogoni mwao. Uwafundishe pia namna ya kuswali kama inavyotakikana, uwapeleke chuoni wakajifunze Qur-aan kuisoma kwa kurattil, kwani kisomo sahihi ndani ya Swalaah ni katika vipengele vya kuikamilisha.
Wewe pia jifunze kuswali Swalaah sahihi. Watu wazima wengi wanaswali kwa makosa, kisomo chao ni cha mashaka mashaka na hukmu nyingi hawazijui. Tumia muda wako kujifunza yote yanayotakikana katika Swalaah, kwani Swalaah ikikubaliwa, ‘amali zako zote zitakubaliwa, na ikikataliwa, basi ‘amali zako nyingine zote zitakataliwa. Tahadhari ndugu Muislamu kwa hili.
Kama hujui, usione haya kumtaka Shekhe wako akufundishe kivitendo hata kama kwa kumlipa. Pia ondosha ujinga wa kutoweza kuisoma Qur-aan kama inavyotakikana. Ni mangapi ya kidunia tunayalipia na kupoteza muda wetu kwayo?! Chunga sana hatima yako ndugu yangu Muislamu.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
17-Maghfirah Kwa Wazazi Na Waumini
"رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ"
“Rabb wetu! Nighufurie mimi na wazazi wangu wawili na Waumini Siku itakayosimama hesabu”. [Ibraahiym: (41)]
Hii pia ni katika du’aa za Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam). Ndanimwe kuna maombi ya kupata uokozi katika nyumba ya aakhirah kwake yeye na kwa Waumini wote. Inaonyesha huruma kubwa aliyopewa Nabiy huyu kwa Waumini wote; wa mwanzo wao hadi wa mwisho wao.
Ameanza akitawasali kwa Jina la Rabbu kwa kusema: “Rabbi wetu! Nighufurie mimi”. Amejikhusisha mwenyewe kwa kujiombea maghfirah kuonyesha taksiri ambayo hakuna mwanadamu anayeweza kusalimika nayo. Halafu akawaombea wazazi wake wawili maghfirah kutokana na haki yao kubwa kwake. Alimwombea baba yake maghfirah kutokana na ahadi aliyoahidiana naye. Nayo ni pale alipomwambia:
"قَالَ سَلَامٌ عَلَيْكَ ۖ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي ۖ إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا"
(Ibraahiym) akasema: Salaamun ‘Alayka (Amani iwe juu yako). Nitakuombea maghfirah kwa Rabb wangu. Hakika Yeye daima Ni Mwenye Kunihurumia sana. [Maryam: (47)]
Lakini baba yake huyo aliposhikilia ukafiri, alijivua naye kama Anavyosema Ta’aalaa:
"وَمَا كَانَ اسْتِغْفَارُ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ إِلَّا عَن مَّوْعِدَةٍ وَعَدَهَا إِيَّاهُ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ أَنَّهُ عَدُوٌّ لِّلَّـهِ تَبَرَّأَ مِنْهُ ۚ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَأَوَّاهٌ حَلِيمٌ "
“Na haikuwa Ibraahiym kumuombea maghfirah baba yake isipokuwa kwa sababu ya ahadi aliyoahidiana naye. Lakini ilipombainikia kwamba yeye ni adui wa Allaah, alijiepusha naye. Hakika Ibraahiym ni mwenye huruma mno na mvumilivu”. [At-Tawbah: (114)]
Aayah hii inadulisha kwamba haijuzu kuwaombea washirikina maghfirah madhali bado wako kwenye ukafiri na ushirikina, ni sawa wakati wa uhai wao au baada ya kufa. Lakini inajuzu kuwaombea hidaayah na tawfiyq ya kumwamini Allaah.
Halafu akawaombea na Waumini wote wa kiume na wa kike Allaah Awaghufirie madhambi yao siku hiyo ngumu ya kusimama mbele ya Allaah kuhisabiwa. Kila mtu atateseka sana kwa makosa na madhambi yaliyosajiliwa kwenye daftari lake, kwa kuwa atakuwa hajui hatima yake itakuwaje. Kwa kuling’amua hili, Nabiy Ibraahiym akatuombea sote tughufiriwe hapo. Na hii ni bishara kubwa kwa kila Muumini, kwa kuwa Allaah Ta’aala Hairejeshi du’aa hii aliyoiomba Kipenzi Chake.
Na kwa ajili hiyo, Muislamu anatakikana akithirishe kuwaombea nduguze Waislamu maghfirah wa tokea Aadam (‘Alayhis Salaam) hadi kusimama Qiyaamah. Mbali na kuonyesha penzi lake kwa nduguzo hao, ataandikiwa jema kwa kila Muislamu. Ni mabilioni mangapi ya mema ataandikiwa kwa idadi ya Waislamu tokea Aadam hadi Qiyaamah! ‘Ubaadah bin Swaamit anasema: Nimemsikia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
"من استغفر للمؤمنين والمؤمنات كتب اللَّه له بكل مؤمن ومؤمنة حسنة"
“Atakayewaombea Waumini wanaume na Waumini wanawake maghfirah, Allaah Atamwandikia jema kwa kila Muumini mwanamume na kila Muumini mwanamke”.
Na kama tujuavyo, Allaah Huongeza jema moja hadi kumi mfano wake. Basi hongera kwa atakayejumuishwa ndani ya du’aa hii.
Tunayojifunza katika du’aa hii:
1- Umuhimu wa kuomba maghfirah. Maghfirah ndiyo salama na mafanikio kwa Muislamu duniani na aakhirah.
2- Mwombaji anatakiwa atenge sehemu ya du’aa yake kwa wazazi wake wawili. Yeye ni chumo lao, nao wana fadhila kubwa kwake.
3- Thawabu kubwa zitokanazo na du’aa hii kutokana na:
(a) Kuwa imetajwa ndani ya Kitabu cha Allaah kama Qur-aan itakayosomwa mpaka Siku ya Qiyaamah.
(b) Malipo yake kuwa makubwa. Kwani mwombaji huandikiwa jema moja kwa kila Muislamu mwanamume na Muislamu mwanamke. Na kila jema moja Allaah Hulipa kumi mfano wake. Ni mabilioni mangapi ya Waislamu waliotangulia, waliopo hivi sasa, na watakaokuja baadaye hadi Siku ya Qiyaamah! Bila shaka si du’aa ya Muislamu kuisahau hata kidogo.
(c) Ni du’aa ya Kipenzi cha Allaah (Khaliylur Rahmaan), na Allaah Hairejeshi du’aa ya Kipenzi Chake.
(d) Ni du’aa yenye kujibiwa. Kwa kuwa du’aa ya Muislamu kwa nduguye Muislamu kwa siri ni yenye kujibiwa.
4- Mwombaji anatakiwa atenge sehemu ya du’aa zake kuwaombea nduguze Waislamu. Na haya ndio mapenzi ya dhati na udugu wa kweli kati ya Waislamu. Ni vizuri pia aanze kujiombea yeye mwenyewe kisha nduguze.
5- Mwombaji aombe zaidi mambo ya aakhirah.
6- Umuhimu wa du’aa za kisharia toka kwenye Qur-aan au kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ndani yake kuna makusudio adhimu na maana ambazo zinakusanya mahitajio yote anayoyatamani mtu kwa matamshi mafupi na maneno mazuri.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
18- Rahmah Na Kutengenekewa Mambo
"رَبَّنَا آتِنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً وَهَيِّئْ لَنَا مِنْ أَمْرِنَا رَشَدًا"
“Rabb wetu! Tupe kutoka Kwako rahmah, na Tutengenezee katika jambo letu mwongozo wa sawa. [Al-Kahf: (18)]
Hii ni du’aa ya vijana waliokimbilia pangoni (Ahlul Kahf). Walikimbilia huko kuokoa dini yao na iymaan yao kutokana na watu wao, ili wasije kuwakamata, wakawatesa na kuiingiza iymaan yao katika hatari. Walipoingia ndani, walimwomba Allaah Ta’aalaa kwa unyenyekevu wa hali ya juu kabisa Awape rahmah maalum kutoka Kwake, kwa kuwa viumbe vyote viko ndani ya Rahmah ya Allaah. Hivyo wakaomba rahma maalum kwa ajili yao kutokana na hali yao ngumu ya kuandamwa na makafiri. Wakamwomba pia Awarahisishie jambo lao hilo la kufikia kwenye njia ya uongofu na ulingamanifu katika maneno na vitendo.
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Muislamu anatakiwa aondoke au akimbie toka sehemu ambayo hawezi kutekeleza maamrisho ya dini yake kwa mujibu wa hali. Hilo ni katika nyajibu kubwa.
2- Mwenye kuacha jambo kwa ajili ya Allaah, Allaah Humpa badali bora kuliko jambo aliloliacha.
3- Mwenye kumcha Allaah, Allaah Humpa fumbuzi za matatizo yake, na Humruzuku kwa njia asiyoitarajia.
4- Mja anatakiwa atumie nyenzo za kidunia na kisharia ili kufanikisha malengo yake. Vijana hao badala ya kusubiri, walichakarika na kukimbia, kisha wakamwomba Allaah Awakunjulie Rahmah Zake maalum kwao.
5- Rahmah za Allaah ziko aina mbili: Rahmah jumuishi kwa viumbe wote; Waumini na makafiri, na Rahmah maalum kwa Waja Wake wema. Muislamu anatakiwa amwombe Allaah daima Rahmah hii maalum itokayo kwenye Hazina Zake.
6- Du’aa inatakiwa iende sambamba na mchakariko. Walikimbilia pangoni kujificha, kisha wakaelekea kwa Allaah kumwomba.
7- Malipo ni kwa mujibu wa kitendo. Wao walilinda iymaan yao, na Allaah Akawalindia iymaan yao na miili yao isiharibike ndani ya pango.
8- Du’aa iwe ndiyo kazi ya muumini katika majukumu yake yote katika maisha yake.
9- Du’aa za kisharia zinakusanya kila analolitamani mja katika dini yake na dunia yake. Hivyo basi Muislamu anatakiwa azitumie na ashikamane nazo kuliko du’aa za kutungwa
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
19-Kukunjuliwa Kifua Na Kuwepesishiwa Jambo
"رَبِّ اشْرَحْ لِي صَدْرِي* وَيَسِّرْ لِي أَمْرِي* وَا حْلُلْ عُقْدَةً مِّن لِّسَانِي * يَفْقَهُوا قَوْلِي"
“Rabb wangu! Nikunjulie kifua changu • Na Niwepesishie shughuli yangu • Na Fungua fundo (la kigugumizi) katika ulimi wangu • Ili wafahamu kauli yangu”. [Twaahaa : (25-28)]
Hii ni du’aa ya Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam). Alimwomba Allaah kutokana na jambo kubwa wakati Allaah Alipomwamuru aende kumlingania kafiri mkubwa zaidi duniani, aliyechupa mipaka na mwenye nguvu kubwa za jeshi na zana. Naye ni Fir-‘awn aliyedai uungu kwa uongo na uzushi.
Na kutokana na umuhimu mkubwa wa jukumu lenyewe na hatari yake, alimwomba Allaah Amsaidie na Amwepesishie. Kwani du’aa ni silaha ya Muumini ambayo anaombea kwayo msaada huku akiegemeza dhana njema kwa Allaah Ta’aalaa.
Akamwomba Amkunjulie kifua chake kwa nuru, iymaan na hekima ili aweze kubeba adha zote za maneno na vitendo toka kwa Fir-‘awn. Kifua kinapokunjuka, hugeuza mazito ya jukumu kuwa pumziko na wepesi.
Akamwomba Amsahilishie kila jambo analolipitia, kila njia anayoikusudia kufikia kwa Allaah, na mazito yote yaliyo mbele yake.
Na kwa vile ufasaha wa ulimi ni nyenzo kubwa ya kufikisha ujumbe, Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) alimwomba Allaah Amwezeshe kuzungumza maneno bayana na ya hikmah yatakayoziathiri akili na hisia za Fir-‘awn na watu wake. Mlinganiaji akiwa fasaha wa ulimi, ameiva kielimu, mkali wa hoja na msomaji mzuri wa wakati na mazingira, basi bila shaka kazi yake itafanikiwa.
Walinganiaji wa dini, watoaji mihadhara na hotuba elimishi, ni vizuri sana kwao kusoma du’aa hii ili Allaah Awawezeshe na Awasaidie katika kufikisha ujumbe wao kwa walengwa.
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Du’aa ni ‘ibaadah ambayo viumbe wameumbwa kwa ajili yake.
2- Du’aa ni silaha ya Muislamu wakati anapoelekea kutekeleza jukumu lolote lile zito au jepesi.
3- Du’aa hii inawafaa walinganiaji, watoa hotuba, wahadhiri, waalimu na kila mwenye kuhitajia jambo la kheri lenye uzito ndanimwe.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
20-Kuzidishiwa ‘Ilmu
رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا"
“Rabbi wangu! Nizidishie ‘ilmu”. [Twaahaa: (114)]
Allaah ‘Azza wa Jalla Amemwamuru Nabiy Wake Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amwombe Amzidishie elimu. Amri hii inayoelekezwa kwa Nabiy wetu, inaelekezwa pia vile vile kwetu, isipokuwa amri maalum yenye vielelezo vya kumhusisha yeye tu pasina sisi.
Elimu muhimu zaidi hapa ya kuombwa ni elimu ya Kitabu Chake Kitukufu Qur-aan. Elimu hii humpandisha mtu kufikia kuyajua mambo ya kumnufaisha hapa duniani na kesho aakhirah. Allaah Hakumwamuru amwombe ziada katika jambo jingine lolote isipokuwa kwenye elimu. Na hii inaonyesha fadhila ya elimu, na kwamba elimu ni katika amali bora kabisa.
Kuna Hadiyth nyingi zinazohimizia jambo hili tukufu. Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa katika du’aa zake:
"اللَّهُمَّ انْفَعَني بِمَا عَلَّمْتنِي، وَعَلِّمْنِي مَا يَنْفَعُني، وَزِدْنِي عِلْمًا"
“Ee Allaah! Ninufaishe kwa yale Uliyonifundisha, na Unifundishe ya kuninufaisha, na Nizidishie elimu”. [Sunan At-Tirmidhiy. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Muislamu anatakiwa asichoke kutafuta elimu, bali aendelee kusoma umri wake wote na hususan elimu ya dini. Rasuli pamoja na elimu pana aliyopewa, lakini hata hivyo Allaah Amemwamuru amwombe Amzidishie elimu.
2- Elimu bora ya kupewa kipaumbele ni elimu ya dini. Elimu hii itamfanya Muislamu kumwabudu Mola wake kama inavyotakikana na kufuzu kesho aakhirah.
3- Taaluma nyingine pia ni muhimu sana kwa maisha yetu kama uhandisi, udaktari, udereva, urubani na kadhalika. Hizi pia Muislamu anatakiwa amwombe Allaah Amzidishie ili aifanye kazi kwa ufanisi zaidi. Kazi ni ‘ibaadah muhimu kwa Muislamu, na kila anavyoifanya kwa ufanisi, Allaah Humpenda zaidi na kumlipa thawabu zaidi. Lakini elimu ya dini asiisahau kabisa, bali aipe kipaumbele.
4- Kwa sasa hakuna udhuru tena kwa Muislamu wa kutafuta au kusoma elimu yake ya dini kutokana na teknolojia wezeshi tuliyonayo. Tovuti za kidini na mitandao ya kijamii imesheheni taaluma zote za dini. Ni yeye tu kuamua.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
21- Kukiri Kosa Kwa Kumtakasa Allaah
"لا إِلَهَ إِلا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ"
“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak! Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu”. [Al-Anbiyaa: (87)]
Dhulma maana yake ni kukiweka kitu mahala pasipo pake; ima kwa kukipunguza au kukiongeza, au kukitoa nje ya wakati wake au mahala pake. Dhulma ziko za aina tatu:
Ya kwanza: Dhulma kati ya mtu na Allaah Ta’aalaa. Dhulma kubwa hapa ni shirki na ukafiri.
Ya pili: Dhulma kati ya mtu na mtu.
Ya tatu: Dhulma kati ya mtu na nafsi yake mwenyewe.
Hii ni du’aa ya Nabiy Yuwnus (‘Alayhis Salaam). Allaah ‘Azza wa Jalla Alimtuma kwa watu wa Naynawa nchini Iraki. Akawalingania wamwamini Allaah na wamwabudu, lakini watu hao walikataa na kubobea zaidi kwenye ukafiri. Akawaahidi kwamba adhabu ya Allaah itawashukia baada ya siku tatu. Naye akatoka kujitenga nao akiwa amewaghadhibikia kabla Allaah Hakumwamuru kufanya hivyo huku akidhani kwamba Allaah Hatomtia mtihanini. Watu wake hao walipopata uhakika kuwa Nabiy wao ameondoka na kuwaacha na huku wanajua kwamba Nabiy hasemi uongo, walitoka pamoja na watoto wao, wanyama wao na mifugo yao kwenda jangwani. Huko wakamwomba Allaah msamaha kwa unyenyekevu mkubwa na kumlilia. Allaah Akawaondoshea adhabu waliyoahidiwa. Allaah Anasema:
" فَلَوْلَا كَانَتْ قَرْيَةٌ آمَنَتْ فَنَفَعَهَا إِيمَانُهَا إِلَّا قَوْمَ يُونُسَ لَمَّا آمَنُوا كَشَفْنَا عَنْهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَتَّعْنَاهُمْ إِلَى حِينٍ"
“Basi kwa nini usiweko mji mmoja ukaamini na iymaan yake ikawafaa - (haukutokea) isipokuwa kaumu ya Yuwnus. Walipoamini, Tuliwaondoshea adhabu ya hizaya duniani, na Tukawasterehesha mpaka muda maalumu”. [Yuwnus: (98)]
Ama Yuwnus, yeye alikwenda na kupanda jahazi pamoja na watu wengine. Jahazi likazidiwa uzito na wakahofia kughariki. Ikabidi wapige kura ya kumtosa mtu mmoja baharini. Kura ikaangukia kwa Yuwnus, lakini walikataa kumtosa. Wakairudia mara tatu, lakini ikaangukia kwake vile vile. Allaah Anasema:
"فَسَاهَمَ فَكَانَ مِنَ الْمُدْحَضِينَ"
“Akapiga kura ya vishale, akawa miongoni mwa walioshindwa”. [As-Swaaffaat: (141)]
Yuwnus akajitupa mwenyewe baharini. Allaah Akampelekea nyangumi mkubwa, Akamwamuru asimle bali ammeze tu ili tumbo lake liwe ni jela kwake. Hapo akawa ndani ya magiza matatu; la tumbo la nyangumi, la bahari na la usiku. Naye bila kuchelewa akaelekea kwa Mola wake kumwomba Amwokoe toka ndani ya zahama hii ngumu akisema:
"لا إِلَهَ إِلا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ"
“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak! Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu”.
Naye Allaah Ta’aalaa Akamkubalia du’aa yake na kumwokoa toka ndani ya tumbo hilo.
Ameitaja dhulma kwa nafsi yake mwenyewe, na kwamba yeye mwenyewe amepita njia ya wenye kujidhulumu wenyewe. Naye hakuomba toka kwa Allaah msamaha kwa tamko wazi la kuomba ili kumhisisha kwamba yeye ni mwovu dhalimu, naye ndiye aliyejiletea madhara kwa nafsi yake mwenyewe na Allaah Hakumdhulumu. Ni kana kwamba anamwambia Allaah Ta’aalaa: “Ukiniadhibu, basi ni kutokana na Uadilifu Wako, na kama Utanisamehe, basi ni kutokana na Rahma Zako”.
Du’aa hii imekusanya mambo matatu makuu:
1- Imethibitisha Uungu wa Allaah ‘Azza wa Jalla; (Laailaaha illaa Anta).
2- Imethibitisha ukamilifu wa kumtakasa Allaah na kila kasoro; (Subhaanak).
3- Kukiri kosa na kuomba maghfirah kwa kusema kwamba yeye amekuwa katika madhalimu kwa kosa tu la kuondoka kabla ya kupewa idhini na Allaah.
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Du’aa kama inavyokuwa kwa tamko wazi la ombi, inakuwa vile vile kwa tamshi la kuashiria.
2- Tamshi hili limekusanya adabu za du’aa na sababu za kujibiwa. Inapendeza kama Muislamu atalikithirisha wakati anapoomba du’aa na hususan anapozongwa na matatizo na misukosuko.
3- Ndani yake kuna tawhiyd kamili na iymaan kwa Allaah. Inapendeza kwa mwombaji ayajumuishe haya kwenye du’aa yake yoyote.
4- Kuna dalili kwamba kumsabbih Allaah kunatakikana zaidi mtu anapokabiliwa na misukosuko mikubwa, ghamu na hamu. Ni kama Anavyosema Allaah:
"وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ * فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُنْ مِنَ السَّاجِدِينَ"
“Na kwa yakini Tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema ● Basi sabihi na mhimidi Rabb wako na uwe miongoni mwa wanaosujudu”. [Al-Hijri: (97)]
5- Kwamba tawhiyd, iymaan kamili na kukiri madhambi ni moja ya sababu kubwa za kuokoka kutokana na maafa ya dunia na aakhirah.
6- Madhambi ni katika sababu kubwa zinazopelekea kuondoka neema na kuandamwa mtu na nakama.
7- Majanga yanayomwandama mtu sababu yake ni kutowajibika ipasavyo na makalifisho ya kisheria.
8- Viumbe wote vyovyote daraja zao ziwavyo, wanamhitajia Allaah. Hivyo ni lazima wakimbilie Kwake Pekee.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
22-Kuomba Mtoto
"رَبِّ لا تَذَرْنِي فَرْدًا وَأَنتَ خَيْرُ الْوَارِثِينَ"
“Rabb wangu! Usiniache pekee. Nawe Ndiye Mbora wa wenye kubaki”. [Al-Anbiyaa: (89)].
Hii ni du’aa nyingine ya Nabiy Zakariyyaa (‘Alayhis Salaam). Ndani ya maneno yake kwa mujibu wa aayah, ipo du’aa ya kuomba mtoto. Ni muundo mzuri murua uliojaa adabu katika kuwasilisha ombi kwa Mola wa walimwengu.
Katika du’aa hii anasema: “Ee Rabbi wangu! Usiniache mpweke bila mtoto wala wa kunirithi, kwani Wewe Ndiye Mbora Utakayesalia baada ya viumbe vyote kufa”.
Hapa amemsifu Allaah kwa Sifa hiyo ya kubakia milele bila mwisho sambamba na ombi lake hilo la kutaka aruzukiwe mtoto wa kumrithi baada ya yeye kufa na kuendeleza mema yake.
Na hapo hapo Allaah Akamjibu ombi lake hilo, na Akamruzuku Nabiy mwema Aliyemuita Yahyaa. Si hivyo tu, bali Alimpa mkewe uzazi mwingi baada ya kuwa tasa kuonyesha Ukamilifu wa Uwezo Wake Ta’aalaa Ambaye hakuna kiwezacho kumshinda ardhini na mbinguni. Anatuambia:
"فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَوَهَبْنَا لَهُ يَحْيَىٰ وَأَصْلَحْنَا لَهُ زَوْجَهُ"
“Basi Tukamuitikia na Tukamtunukia Yahyaa, na Tukamtengenezea mke wake”. [Al-Anbiyaa: (90)]
Kisha Allaah Ta’aalaa Akabainisha sababu ya kwa nini Alimjibu du’aa Akisema:
"إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ"
“Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya khayr na wanatuomba kwa raghba na khofu, na walikuwa wenye kutunyenyekea”. [Al-Anbiyaa: (90)]
Kuharakia mambo ya kheri ni katika sababu za kujibiwa du’aa ya Muislamu. Hawa walikuwa wakiyaharakia mambo yote ya kheri kwa aina zake na maumbo yake yote katika nyakati zake bora. Si hivyo tu, bali walikuwa wakiyatenda kwa ufanisi utakiwao huku wakiwa wanyenyekevu katika hali zote na katika nyakati zote. Na hili ndilo ambalo Muislamu anatakiwa aliige toka kwa watu hawa wema.
Katika aayah, tamshi la kuomba limekuja kwa muundo wa kitenzi cha wakati uliopo “wanatuomba” kwa faida mbili:
Ya kwanza: Ni kwamba walikuwa wakikithirisha sana hilo na kudumu nalo.
Ya pili: Kuleta picha yao nzuri katika akili zetu. Ni kama vile msemeshwa anaiona picha yao hivi sasa ikimwathiri na kumfanya aige kitendo chao hicho.
Tunajifunza yafuatayo kutokana na du’aa hii:
1- Muislamu hatakiwi kukata tamaa kwa jambo lolote. Ni lazima awe na yakini kamili kuwa Allaah Ana uwezo wa kulifanya lisilowezekana kwa nadhari zetu kuwa linawezekana.
2- Kuruzukiwa watoto ni katika neema kubwa. Neema hiyo hukamilika ikiwa watoto ni wema watakaowafaa wazazi duniani na aakhirah.
3- Miongoni mwa sababu za kujibiwa du’aa ni kuwa na shime na mambo ya kheri kwa mujibu wa uwezo wa mtu, na kudumu kumwomba Allaah nyakati zote na mahala popote.
4- Du’aa huombwa kwa raghba ya kuomba maslaha ya dunia na aakhirah, na khofu ya kuomba hifadhi ya mambo yanayoogopwa ya duniani na ya aakhirah.
5- Unyenyekevu ni dalili ya iymaan ya kweli ya mja kwa Mola wake.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
23-Kinga Dhidi Ya Udokezi Wa Mashaytwaan
"رَبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ * وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَنْ يَحْضُرُونِ"
“Rabb wangu! Najikinga Kwako kutokana na udokezi wa mashaytwaan ● Na najikinga Kwako Rabb wasinihudhurie”. [Al-Muuminuuna: (97-98)]
Kwanza, ni muhimu mno kujua kwamba kujilinda kwa Allaah ni katika aina za du’aa.
Pili, Allaah kwa Hikmah Yake Ameumba shari katika nyumba hii ya dunia. Ameumba shari kubwa zaidi, chimbuko lake, asili yake na sababu yake kuu ambaye ni shaytwaan aliyewekwa mbali na Rahmah Zake. Kati ya hikmah za hili, ni kututahini na kutujaribu ili tuweze kukabiliana na shari hizi tuweze kufaulu duniani na aakhirah. Pepo ya Allaah ni ghali mno, na cha ghali hakiwezekani kupatikana kwa urahisi.
Na kwa vile Mashaytwan wanatuona lakini sisi hatuwaoni kama Alivyosema Allaah:
"إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ"
“Hakika yeye (Ibliys) anakuoneni, yeye na kabila lake (la mashaytwaan) na hali ya kuwa nyinyi hamuwaoni”… Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Ametuamuru tujilinde nao Kwake kutokana na shari yao kubwa iliyo karibu yetu.
Katika aayah, wametajwa mashaytwani, na si shaytwani mmoja. Hii inaonyesha kuwa ni wengi na wako wa aina mbalimbali, na inatupa picha zaidi kuhusu hatari yao kwetu. Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijilinda na aina zote za shari za mashaytwaan akisema:
"أَعُوذُ بِاللَّهِ مِنَ الشَّيْطَانِ: مِنْ نَفْخِهِ، وَنَفْثِهِ، وَهَمْزِهِ"
“Najilinda kwa Allaah na shaytwaan; kutokana na kiburi chake, mashairi yake na ujununi wake”. [Abu Daawuwd: Kitaabu As-Swalaat]
Haya ambayo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda nayo, yanaingia kiujumla kwenye udokezi wa mashaytwan uliotajwa kwenye aayah. Mbali ya udokezi huo, mashaytwaan hawa wanaingia kwenye kila jambo katika mambo yetu. Na hii ni hatari kubwa sana! Hilo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelieleza akisema:
"إنَّ الشَّيْطَانَ يَحْضُرُ أَحَدَكُمْ عِنْدَ كُلِّ شَيْءٍ مِنْ شَأْنِهِ، حَتَّى يَحْضُرَهُ عِنْدَ طَعَامِه..."
“Hakika shaytwaan anamhudhuria mmoja wenu kwenye kila jambo katika mambo yake. Hata anamhudhuria wakati anapokula”. [Swahiyh. Imesimuliwa na Jaabir bin ‘Abdillaah]
Kila jambo katika jambo lake! Hebu angalia hatari hii kubwa kwetu!. Ukila uko nao! Ukilala uko nao! Ukiswali uko nao! Ukiingia msalani uko nao, na hao ni wa aina nyingine! Na kitambo kibaya na hatari zaidi unachokuwa nao ni pale kabla ya kutoka roho. Hapa hutumia mbinu zote kukuzuga ili ufe ukiwa si Muislamu. Tunamwomba Allaah Atupitishe salama hapo. Ni kwamba shughuli yoyote uifanyayo, basi ujue uko nao! Hawakuachi! Ila tu kama utajilinda kwa Allaah. Na hapo unakuja umuhimu wa kujilinda na kiumbe huyu katika hali zote.
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwafundisha Maswahaba maneno ya kusema wakati wanaposhtuka usingizini. ‘Abdullaah bin ‘Amri bin Al-‘Aaswiy amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إذا فَزِعَ أحَدُكم في النوم فَلْيَقُلْ: أَعوذ بكلمات اللَّه التَّامَّة من غضبه، وعِقَابِهِ، وشرِّ عِبادِهِ، ومن هَمَزَاتِ الشَّياطينِ، وأنْ يَحضُرونِ، فإنَّها لَنْ تَضُرَّهُ"
“Akishtuka mmoja wenu usingizini basi aseme: Najilinda kwa Maneno ya Allaah Yaliyotimia kutokana na Ghadhabu Yake na Adhabu Yake, na shari ya waja Wake, na kutokana na uchochezi wa mashaytwaan na kunihudhuria mimi. Hakika hawatomdhuru”. [At-Tirmidhiy: Kitaabu Ad-Da’awaat].
Tunajifunza kutokana na isti’aadhah hii haya yafuatayo:
1- Kujilinda kwa Allaah ni katika aina za du’aa, na Mlinzi wa yote ni Allaah Pekee. Haijuzu kabisa kujilinda kwa asiye Allaah kwani hilo ni katika shari mbaya. Allaah Anasema:
"وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِنَ الْإِنْسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا"
“Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa wana Aadam wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia madhambi, uvukaji mipaka ya kuasi na khofu. [Al-Jinn: (06)]
2- Shaytwaan ana hatari kubwa kwa mwanadamu. Anamvizia katika hali zake zote. Na kwa ajili hiyo, ni muhimu sana kujilinda naye nyakati zote.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
24-Iymaan, Maghfirah Na Rahmah
"رَبَّنَا آمَنَّا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ"
“Rabb wetu! Tumeamini, basi Tughufurie na Uturehemu, Nawe Ndiye Mbora wa wenye kurehemu”. [Al-Muuminuuna: (109)]
Hii ni du’aa ya Waumini wenye iymaan ya kweli. Imekusanya ndani yake kumwomba Allaah kwa Jina Lake Tukufu la Rabbi pamoja na kujieleza waombaji kuwa wao wamemwamini Yeye na yote waliyokuja nayo Mitume Wake. Hii kama tulivyoashiria nyuma ni wasiylah ya kupelekea kujibiwa du’aa.
Sababu ya kuja du’aa hii njema ni kwamba makafiri motoni wataomba watolewe humo ili warejeshwe duniani. Na Allaah Atawaambia:
" اخْسَئُوا فِيهَا وَلَا تُكَلِّمُونِ"
“Hizikeni humo! Na wala msinisemeshe!”
Halafu Allaah Akabainisha sababu ya kuadhibiwa kwao Akisema:
"إِنَّهُ كَانَ فَرِيقٌ مِّنْ عِبَادِي يَقُولُونَ رَبَّنَا آمَنَّا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ"
“Hakika lilikuwa kundi miongoni mwa Waja Wangu, wakisema: Rabb wetu! Tumeamini, basi Tughufurie na Uturehemu, Nawe Ndiye Mbora wa wenye kurehemu”. [Al-Muuminuwna: (109)].
Na walipokuwa wakisema hivi na kushikamana na iymaan yao, makafiri hao walikuwa wanawacheza shere na kuwadharau.
"فَاتَّخَذْتُمُوهُمْ سِخْرِيًّا حَتَّىٰ أَنسَوْكُمْ ذِكْرِي وَكُنتُم مِّنْهُمْ تَضْحَكُونَ • إِنِّي جَزَيْتُهُمُ الْيَوْمَ بِمَا صَبَرُوا أَنَّهُمْ هُمُ الْفَائِزُونَ"
“Mkawafanyia dhihaka, hadi wakakusahaulisheni kunidhukuru, na mlikuwa ni wenye kuwacheka • Hakika Mimi Nimewalipa leo (Jannah) kwa vile walivyosubiri, hakika wao ndio wenye kufuzu”. [Al-Muuminuuna: (110-111)].
Waombaji katika du’aa hii wamejumuisha iymaan, kuomba maghfirah na rahmah, kutawassal kwa Allaah kwa Jina Lake Tukufu la Rabb na kumsifu kwa Rahmah pana zisizo na mipaka.
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Kutawassal kwa Allaah kwa ‘amali njema ni katika tawasulati zenye kuvuta matarajio makubwa zaidi ya kujibiwa du’aa. Na kutawassal Muislamu kwa iymaan yake ni katika tawasulati bora zaidi.
2- Kuomba maghfirah ni katika maombi muhimu ambayo Muislamu anatakiwa awe na pupa nayo. Ukipata maghfirah, utasalimika na adhabu na yote ya kuchukiza.
3- Maghfirah huombwa kwanza kabla ya rahmah. Bila maghfirah, hakuna rahmah. Maghfirah kwanza, halafu rahmah.
4- Hatari ya kuwacheza shere Waumini. Hatima ya hili ni motoni. Mbaya zaidi ni Muislamu kumcheza shere nduguye Muislamu.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
25-Maghfirah Na Rahmah
" رَّبِّ اغْفِرْ وَارْحَمْ وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ "
“Rabb wangu! Ghufuria na Rehemu, Nawe Ni Mbora wa wenye kurehemu”. [Al-Muuminuwn: (118)].
Allaah Ta’aalaa Amemwamuru Nabiy Wake Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuomba du’aa hii. Amemwamuru aombe maghfirah na rahmah. Mambo haya mawili yamekariri kwenye du’aa nyingi zilizopo ndani ya Qur-aan kutokana na umuhimu wake. Nabiy ameamuriwa ayaombe mawili hayo pamoja na kuwa amesamehewa madhambi yake yaliyopita na yajayo, basi je sisi itakuwaje?
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na sisi tumeamuriwa kuomba du’aa hii kutokana na faida yake kubwa duniani na aakhirah. Na ndio maana Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamfundisha Abu Bakr As-Swiddiyq (Radhwiya Allaah ‘anhu) mfano wa du’aa hii. Abu Bakr alimwambia Rasuli: “Nifundishe du’aa ya kuomba katika Swalah yangu. Rasuli akamwambia sema:
"اللَّهُمَّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي ظُلْمًا كَثِيرًا، وَلَا يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا أَنْتَ، فَاغْفِرْ لِي مَغْفِرَةً مِنْ عِنْدِكَ، وَارْحَمْنِي، إِنَّك أَنْتَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ"
“Ee Allaah! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu dhulma nyingi, na hakuna yeyote anayeghufuria madhambi isipokuwa Wewe tu. Basi Nighufurie mimi maghfirah itokayo Kwako na Unirehemu. Hakika Wewe Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwingi wa Kurehemu”. [Al-Bukhaariy: Kitaabul Aadhaan]
Faida kutokana na du’aa hii:
1- Du’aa hii ni muhimu mno kwa kuwa Rasuli kaamriwa na Allaah Mtukufu kuiomba.
2- Umuhimu wa kutawassal kwa Jina la Rabbu.
3- Mwombaji aanze kuomba maghfirah kwanza kabla ya rahmah. Maghfirah ni ufunguo wa rahmah.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
26-Kuepushwa Na Adhabu Ya Jahannam
"رَبَّنَا اصْرِفْ عَنَّا عَذَابَ جَهَنَّمَ إِنَّ عَذَابَهَا كَانَ غَرَامًا*إِنَّهَا سَاءَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا"
“Rabb wetu! Tuepushe adhabu ya Jahannam. Hakika adhabu yake ni yenye kugandamana daima; isiyomwacha mtu • Hakika hiyo (Jahannam) ni mahali paovu mno pa kustakiri na mahali pa kuishi”. [Al-Furqaan: (65-66)]
Hii ni du’aa ya Waja wema wa Allaah. Amewasifu kwa sifa njema kabisa zilizotukuka, na Akawategemezea Kwake mtegemezo wa tashrifa na taadhima kwa ajili ya kunyanyua hadhi yao Akisema:
"وَعِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الْأَرْضِ هَوْنًا وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلَامًا"
“Na Waja wa Ar-Rahmaan ni wale wanaotembea katika ardhi kwa unyenyekevu na upole, na majahili wanapowasemesha, wao husema: Salaam! [Al-Furqaan: (63)].
Waja hawa wema katika du’aa yao hii wamemwomba Awaepushe na adhabu ya Jahannamu pamoja na sababu zake za kuweza kufanikisha mwepusho huo hapa duniani kwa kuwepesishiwa utendaji wa ‘amali njema na kuepushiwa machafu yenye kupelekea huko.
Waja hawa pamoja na kuwajibika kwao vyema katika makalifisho yote na pupa yao kubwa ya kumcha Allaah, lakini hata hivyo, bado wanaiogopa adhabu ya Allaah ya Jahannamu na wanaendelea kumlilia Allaah Awaepushe nayo bila kujinata kwa ‘amali zao hizo wala kujiona bora kuliko wengineo. Na hii ni katika uzuri wa ‘ibaadah na ukamilifu wake. Muislamu hatakiwi kabisa kujiona kwa matendo yake mema vyovyote yawavyo. Hapa waja hawa wanamwomba Allaah kana kwamba wao wamezamia kwenye maasia na madhambi. Hofu imewatamalaki. Ni kama Allaah Alivyosema kuhusiana na Waumini:
"وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوْا وَقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَى رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ"
“Na ambao wanatoa vile wavitoavyo na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika watarejea kwa Rabb wao”. [Al-Muuminuwna: (60)].
Kisha wakaeleza sababu ya ombi lao hilo, nayo ni kuwa adhabu hiyo ni shari ya kudumu milele, na ni maangamivu yasiyomwacha atakayeingia ndani ya Jahannam. Hakuna mapumziko wala kutoka isipokuwa kwa Waumini walioingia humo kwa muda, na wale watakaotolewa humo kwa shifaa ya Rasuli na baadhi ya Waumini wema. Isitoshe, Jahannam hiyo ni mashukio yenye mwonekano mbaya kabisa wa kutisha na kuchefua.
Bila shaka haifichikani kwetu umuhimu wa kujilinda na moto kwa kuwa ndio shari mbaya zaidi Aliyowahadharisha watu nayo Allaah. Na hapa tunajulishwa kuwa ni vizuri kwa mwombaji aelezee sababu ya akiombacho kama walivyoeleza Waja hawa wema.
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Umuhimu wa du’aa hii kwa vile:
(a) Allaah Ta’aalaa Ameitaja kwa watu ambao Yeye Mwenyewe Amewasifu na Kuwategemezea kwa Nafsi Yake kwenye Qur-aan ambayo itasomwa mpaka Siku ya Qiyaamah.
(b) Imekuja kwa muundo wa kitenzi cha wakati uliopo katika Neno Lake: "وَالَّذِينَ يَقُولُون"َ kinachoonyesha kukithirisha kwao na kudumu kwao kuomba hilo.
2- Inapendeza zaidi kwa mwombaji kueleza sababu ya ombi lake. Hii pia ni katika kuitanua du’aa, na Allaah Analipenda hili.
3- Kutawassal kwa Jina la Rabbu ni katika tawassulaati bora zaidi kuliko zote.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
27-Wake Na Watoto Kuwa Kitulizo Cha Jicho
"رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا"
“Rabb wetu! Tutunukie katika wake zetu na dhuria wetu viburudisho vya macho yetu, na Tujaalie kuwa waongozi kwa wenye taqwa”. [Al-Furqaan: (74)].
Hii ni du’aa ya pili katika du’aa za Waja wema wa Ar-Rahmaan. Wanamwomba Allaah Awatunuku wake na watoto wema katika Matunukio Yake makubwa na mengi kwao. Wanamwomba hawa wawe ni wenye kumtii Yeye na hivyo kuwa ni viburudisho vya macho yao hapa duniani na huko aakhirah. Viburudisho vya macho ni kinaaya ya furaha na sururi. Muislamu hufurahika sana anapoona watoto wake wako kwenye mstari wa taqwaa, wako mbali na marafiki wabaya, na wako mbali na tabia zote chafu za vijana. Furaha hii ataipata duniani, na akifa watoto hawa wema watakuwa wanamwombea maghfirah, wanamtolea swadaqah, wanatekeleza wasiya wake, wanaendeleza mema yake na kadhalika, na Siku ya Qiyaamah watakutana na kujumuika pamoja Peponi. Pia hufurahi sana kwa mke mwema ambaye anapomwangalia humfurahisha, akimwamrisha humtii na anapokuwa naye mbali humlindia heshima yake na mali yake.
Na du’aa hii ya kuwaombea wake zao na watoto wao ni du’aa kwa wao wenyewe pia, kwa kuwa manufaa yake yatawarudia wao wenyewe, na yanadumu duniani na aakhirah. Ni kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"إِذَا مَاتَ الْإِنْسَانُ انْقَطَعَ عنه عَمَلُهُ إِلَّا مِنْ ثَلَاثَةٍ: صَدَقَةٍ جَارِيَةٍ، أَوْ عِلْمٍ يُنْتَفَعُ بِهِ، أَوْ وَلَدٍ صَالِحٍ يَدْعُو لَهُ"
“Anapokufa mwanadamu ‘amali zake hukatika ila kwa matatu: Swadaqah endelevu, au elimu inayopatiwa manufaa, au mtoto mwema anayemwombea”. [Swahiyh Muslim. Hadiyth Swahiyh]
Na huko aakhirah kwa kuwa pamoja nao kwenye Pepo ya Kudumu. Allaah Amesema:
"وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاتَّبَعَتْهُمْ ذُرِّيَّتُهُم بِإِيمَانٍ أَلْحَقْنَا بِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَمَا أَلَتْنَاهُم مِّنْ عَمَلِهِم مِّن شَيْءٍ ۚ كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ"
“Na wale walioamini na wakafuatwa na dhuriya wao kwa iymaan, Tutawakutanisha nao dhuriya wao na Hatutawapunguzia katika ‘amali zao kitu chochote. Kila mtu atafungika kwa yale aliyoyachuma”. [At-Tuwr: (21)].
Na kama hiyo haitoshi, manufaa haya yatarudi pia kwa Waislamu wote. Kwa wema wa waliotajwa, utakuwa ni sababu ya wema kwa wale wote watakaotangamana nao. Na hawa hawa pia ndio watawaombea du’aa njema Waislamu wote walio hai na waliokufa.
Hii ndio hisia ya maumbile asili ya kiiymaan. Hisia ya kuongezeka idadi ya wapitao katika njia ya kuelekea kwa Allaah ‘Azza wa Jalla wake zao na watoto wao wakiwa katika ngazi ya kwanza. Hao ndio watu wa karibu zaidi na mtu, nao ndio amana ya kwanza atakayoulizwa Siku ya Qiyaamah.
Mbali na kumwomba Allaah Awatunukie watoto na wake wa kuyatuliza macho yao, wamemwomba Allaah pia Awajaalie kuwa viongozi na maimamu wa kuigwa na watu wema katika vitendo vyao, maneno yao na kuisimamisha kwao dini. Ni ombi kwa Allaah Awahidi, Awape tawfiyq, Awafadhili kwa elimu nufaishi na vitendo vyema vya dhahiri na fiche vitakavyowafikisha katika ngazi hii ya juu. Kuigwa kwa mema athari yake chanya ni ndefu na pana duniani na aakhirah, na kuigwa kwa mabaya athari yake hasi ni ndefu na pana duniani na aakhirah.
Ombi lao hili pia vile vile ni la kuomba daraja za juu kabisa za utumwa. Ni daraja za uongozi na uimamu katika dini. Daraja hii ya juu haipatikani bila subira na yaqini ya kweli kama Alivyosema Allaah:
"وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا ۖ وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يُوقِنُونَ"
“Na Tukawajaalia miongoni mwao Maimamu wanaongoza kwa Amri Yetu waliposubiri, na walikuwa wakiziyakinisha Aayaat (na Ishara) Zetu”. [As-Sajdah: (24)].
Faida za du’aa hii:
1- Ni du’aa muhimu kama iliyotangulia nyuma kutokana na kusifiwa waombaji na Allaah. Pia kutoiacha kwao na kuikariri mara kwa mara kutokana na kitenzi cha wakati uliopo: (يقولون)
2- Tunukio la Allaah ni katika neema kubwa. Na kwa ajili hiyo wametawassali kwalo.
3- Kumwomba Allaah ‘Azza wa Jalla kutengenea mke na watoto ni katika makusudio muhimu ambayo mwombaji anatakiwa asiyasahau.
4- Mwombaji anatakiwa akuze utashi wake katika du’aa, na amwombe Allaah matakwa yake ya juu kabisa. Ni kama alivyotuusia Rasuli kuwa tusiombe tu Pepo, bali tuombe Al-Firdaws ambayo ndio Pepo ya daraja la juu kabisa. Au tusiombe tu watoto mradi watoto, bali tuombe watoto wema.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
28-Hikmah Na Kukutanishwa Na Watu Wema
"رَبِّ هَبْ لِي حُكْمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ* وَاجْعَلْ لِي لِسَانَ صِدْقٍ فِي الآخِرِينَ * وَاجْعَلْنِي مِن وَرَثَةِ جَنَّةِ النَّعِيمِ"
“Rabb wangu! Nitunukie hikmah (elimu ya Dini) na Unikutanishe na Swalihina • Na Nijaalie kusifika kwa heshima kwa vizazi watakaokuja baadaye • Na Nijaalie miongoni mwa warithi wa Jannah ya neema”. [Ash-Shu’araa: (83-85)].
Baada ya Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) kuzielezea Sifa kochokocho za Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa kama kuwa Yeye Amemuumba na Anamwongoza, Anamlisha na Anamnywesha, anapokuwa mgonjwa Anamponyesha, Anamfisha na kisha Atamfufua, na yeye anatumai kuwa Atamghufuria makosa yake Siku ya malipo, baada ya yote hayo, akaleta du’aa yake hii. Hii ni katika tawassulaat kubwa kabisa zenye kuwajibisha kujibiwa na kukubaliwa du’aa kama tulivyogusia katika du’aa zilizopita.
Amemwomba Allaah Amtunukie hikmah. Hikmah hapa ni kumjua Allaah, kujua Mipaka Yake, na kujua Hukmu Zake. Yaani anaomba Allaah Amtunuku ‘ilmu ya kujulia ahkaam, halali na haramu ili aweze kuhukumu kwayo baina ya watu. Hikmah ni jambo la kuliomba sana, kwani mwenye kupewa hikmah anakuwa amepewa kheri nyingi sana kama Alivyolielezea hilo Allaah Ta’aalaa.
Amemwomba pia Amkutanishe na Swalihina. Yaani awe pamoja na watu hao hapa duniani na kesho aakhirah. Ni kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipokuwa karibu kukata roho:
اللَّهُمّ في الرفيق الأعلى
“Ee Allaah! Pamoja na Ar-Rafiyq Al-A’alaa [Uliowaneemesha katika Manabii, Swiddiyqiyna, Shuhadaa na Swalihina katika daraja za juu za Jannah]”. [Muslim: Kitaabu Fadwaailis Swahaabah]
Na takwa hili lilikuwa vile vile ni katika maombi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa anaomba:
"اللَّهُمَّ تَوَفَّنَا مُسْلِمِينَ، وَأَحْيِنَا مُسْلِمِينَ، وَأَلْحِقْنَا بِالصَّالِحِينَ، غَيْرَ خَزَايَا وَلَا مَفْتُونِين"
“Ee Allaah! Tufishe tukiwa Waislamu, Tuhuishe tukiwa Waislamu, na Tukutanishe pamoja na Swalihina bila kuwa wenye kuhizika wala kufitinika”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]
Muislamu anatakiwa asuhubiane na watu wema hapa duniani, kwani rahmah, amani na uongofu vinawazunguka watu hao. Afanye hivyo ili aweze kusuhubiana nao huko aakhirah na kuwa ngazi moja nao hata kama hakufanya matendo yao kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"الْمَرْءُ مَعَ مَنْ أَحَبَّ"
“Mtu atakuwa pamoja na anayempenda”. [Al-Bukhaariy 6169 na Muslim 2640]
Amemwomba pia Allaah Amjaalie awe mwenye kusifika kwa heshima kwa vizazi watakaokuja baadaye. Awe na utajo mzuri wa kheri kati ya watu, na sifa njema kwa vizazi vijavyo baada yake. Utajo mwema huvutia du’aa za watu kwake na kumfanya kiigizo chema kwao. Na hii ni faida kwao na kwake hadi Siku ya Qiyaamah. Allaah Ta’aalaa Akamjibu du’aa yake hii, Akampa ‘ilmu kubwa na hikmah, Akamfanya kuwa katika Mitume bora, Akamfanya mwenye kupendwa na kukubalika, na mwenye kutukuzwa na kusifiwa katika mila zote na zama zote.
Na kwa muktadha huu, hakuna ubaya mtu kupenda kusifiwa kwa ‘amali zake njema, na kuonekana kwenye ‘amali za Swalihina kama atakusudia kwa hilo Wajihi wa Allaah. Wanasema: “Watu wamekufa nailhali wako hai kati ya watu”, yaani kwa kutajwa kwa mema yao, na wasifu wao uliotukuka.
Na baada ya Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) kumwomba Allaah furaha ya dunia, alimwomba pia furaha nyingine ya milele akisema: “Na Nijaalie miongoni mwa warithi wa Jannah ya neema”. Allaah Akamjibu ombi lake hili, na kuinyanyua ngazi yake juu kwenye Pepo za kudumu milele. Tunamwomba Allaah Atujaalie tuingie ndani ya du’aa hii ya Khaliylur Rahmaan. Aamiyn.
Katika hili, Allaah Anawahimiza Waja Wake wawe na hima ya nguvu katika kuomba mfano wa du’aa hizi za barakah zilizokusanya kheri za dunia na aakhirah.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
29-Kutohizishwa Siku Ya Qiyaamah
"وَلا تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ * يَوْمَ لَا يَنْفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ * إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ"
“Na wala Usinihizi Siku watakayofufuliwa • Siku hayatofaa mali wala watoto • Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika”. [Ash-Shu’araa: (87-89)].
Huu ni mwendelezo wa du’aa zilizotangulia za Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam). Anamwomba Allaah Asimkhizi Siku ya Qiyaamah watu wakatapofufuliwa. Khiizaya ni udhalili na unyonge. Anaomba akingwe na udhalili na unyonge wa Siku hiyo. Hakuna udhalili na unyonge wa mfano wa Siku hiyo. Watu watanyongeka na kudhalilika kutokana na kashfa ya madhambi yao makubwa waliyokuwa wakiyafanya kwa siri na dhahiri. Madhambi hayo yatawatesa mno kabla ya adhabu yenyewe kuwafikia. Na hata hii pia ilikuwa ni du’aa ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa akiomba:
" اللَّهُمَّ لا تُخْزِنِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ , وَلا تُخْزِنِي يَوْمَ الْبَأْسِ ؛ فَإِنَّ مَنْ أَخْزَيْتَهُ يَوْمَ الْبَأْسِ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ "
“Ee Allaah! Usinikhizi Siku ya Qiyaamah, wala Usinikhizi Siku ya adhabu kali, kwani Utakayemkhizi Siku ya adhabu kali, basi kwa hakika Umemkhizi”. [Riwaayah ya Imam Ahmad. Al-Arnaauwtw kasema ni Swahiyh katika Musnad wa Ahmad]
Halafu akataja sababu ya ombi lake hilo kwa Siku hiyo ngumu akisema: “Siku hayatofaa mali wala watoto ● Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika”. Kwa maana kuwa hakuna chochote kitakachoweza kumkinga mtu na adhabu ya Allaah hata kama ataijaza ardhi dhahabu na watu isipokuwa atakayemjia Allaah na moyo uliosalimika na kila mabaya, maradhi ya shubha kama shirki, shaka, unafiki, na kushabikia mambo ya bid’a, hawaa za kinafsi na mengineyo angamizi. Moyo umetajwa hapa kwa kuwa ndio chimbuko la uzuri na ubaya wa kiwiliwili cha mtu. Ukiwa salama, basi viungo vyote vinakuwa salama, na ukiharibika basi viungo vyote vinaharibika. Na hili ndilo lililokuwa ombi la Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) la kuwa na moyo salama. Alikuwa akiomba:
"اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الثَّبَاتَ فِي الْأَمْرِ، وَالْعَزِيمَةَ عَلَى الرُّشْدِ، وَأَسْأَلُكَ شُكْرَ نِعْمَتِكَ، وَحُسْنَ عِبَادَتِكَ، وَأَسْأَلُكَ قَلْبًا سَلِيمًا، وَلِسَانًا صَادِقًا"
“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba uthabiti katika jambo (Dini ya Allaah) bila kutetereka, na azima ya kupania mambo ya kheri yenye kufaulisha. Na ninakuomba kuzishukuru Neema Zako, kukuabudu kama inavyotakikana, na ninakuomba moyo uliosalimika na ulimi usemao kweli”. [Sunan An-Nasaaiy. Al-Arnaauwtw kasema ni Hasan Lighayrih]
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Kuwa inapendeza zaidi kwa mwombaji akusanye katika du’aa yake kheri za dunia na aakhirah, na nyumba ya aakhirah iwe ndio makusudio yake makuu.
2- Mwombaji amwombe Allaah Amzidishie ‘ilmu na hikmah kwa yatakayomnufaisha katika dini yake, dunia yake na aakhirah yake.
3- Mwombaji anatakiwa amwombe Allaah Ta’aalaa Amjaalie kuwa pamoja na watu wema duniani na aakhirah. Pia Amruzuku utajo mwema hapa duniani kutokana na faida zifuatazo:
(a) Kufanywa kiigizo chema na watu.
(b) Kuombewa du’aa na watu.
(c) Kukubaliwa kirahisi katika ushahidi, kutoa nasaha, kutatua migogoro na kadhalika.
4- Umuhimu wa kutawassal kwa Sifa za Allaah Ta’aalaa ikiwemo Sifa ya kivitendo ya Kutunuku kama ilivyo katika du’aa nyingi za Qur-aan Tukufu. Katika hili kuna ukamilifu wa adabu, utukuzaji na usifuji kwa Allaah Ta’aalaa.
5- Kutaja sababu ni katika uzuri wa du’aa.
6- Ni vizuri kwa mwombaji awaombee wazazi wake wawili hata kama hawako kwenye hali ya uongofu au hali tengefu.
7- Manabii na Mitume wote wanaiogopa Siku ya Qiyaamah.
8- Moyo ni kinofu muhimu zaidi mwilini. Kikiwa kizima, basi mwili wote unapata uzima, na kikiharibika, nao mwili wote unaharibika.
9- Mja anatakiwa asighurike kwa matendo yake. Ikiwa Imamu wa Manabii ambaye amepewa mambo makubwa ya kuhimidiwa anaiogopa Siku hiyo, basi sisi ndio tunatakiwa tuiogope zaidi.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
30- Kuzinduliwa Kuzihisi Na Kuzishukuru Neema
"رَبِّ أَوْزِعْنِي أَنْ أَشْكُرَ نِعْمَتَكَ الَّتِي أَنْعَمْتَ عَلَيَّ وَعَلَى وَالِدَيَّ وَأَنْ أَعْمَلَ صَالِحًا تَرْضَاهُ وَأَدْخِلْنِي بِرَحْمَتِكَ فِي عِبَادِكَ الصَّالِحِين"
“Rabb wangu! Nipe ilhamu na uwezo nishukuru Neema Yako ambayo Umenineemesha juu yangu na wazazi wangu, na nipate kutenda mema Utakayoridhia, na Niingize kwa Rahmah Yako katika Waja Wako Swalihina. [An-Naml: (19)]
Hii ni du’aa ya Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis Salaam). Allaah Alimpa Utume na ufalme, Akamfundisha lugha za ndege, naye akawa ni mwingi wa kushukuru neema zote hizo.
Katika du’aa hii, amemwomba Allaah Amzindushe na Ampe tawfiyq ya kuendelea kuzishukuru Neema Zake kwake zisizokokoteka wala kuhesabika. Katika hili amewajumuisha pia wazazi wake wawili kwa ajili ya kukithirisha neema hizo, kwani neema aliyo naye yeye manufaa yake yanarejea kwao vile vile.
Huu ndio ukamilifu na uzuri wa kushukuru Neema za Allaah ambapo neema kubwa zaidi ni Uislamu ambao ni tunu isiyolinganishwa na chochote Aliyotutunukia sisi Allaah bila kumwomba. Na wengi neema hii hawaihisi wala hawaithamini kabisa. Mtu Muislamu lakini Uislamu hataki kujifunza. Anaitupa bahati kubwa aliyonayo mkononi.
Kadhalika, amemwomba Allaah Mtukufu Amwezeshe kutenda amali yoyote ile njema ya kumridhisha Allaah iwe kwa ulimi, kwa moyo, au kwa viungo. Si kila amali aifanyayo mtu inamridhisha Allaah Subhaanah kwani inaweza kuwa na mapungufu ya riyaa, kujiona, shirki na kadhalika. Mtu lazima ajiepushe na hayo na aifanye amali yake kwa ikhlasi safi.
Akamwomba pia Amuingize Peponi Nyumba ya Rahmah Zake pamoja na Waja Wake wema ambapo haingii yeyote isipokuwa kwa Rahma za Allaah na si kwa amali zake vyovyote ziwavyo. Na ndipo akaomba akisema: “Na Niingize kwa Rahmah Zako”, na si kwa amali zangu, pamoja na Waja Wako wema kwenye Jannaat Zako za daraja ya juu kabisa ambazo haingii isipokuwa Swalihina.
Nabiy huyu ameomba ukamilifu wa furaha za dunia na aakhirah ambazo ni:
- Kuwezeshwa kuzishukuru Neema za Allaah zisizokokoteka.
- Kufanya ‘amali zenye kuridhiwa.
- Kusuhubiana na viumbe wema.
Kuna faida kadhaa kutokana na du’aa hii:
1- Umuhimu wa kumwomba Allaah Atusaidie katika kumtii na hususan kumshukuru ambako kunawajibisha kuzilinda neema za dunia na aakhirah. Na haya ndiyo makusudio ambayo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiyaomba akisema:
"اللَّهُمَّ أَعِنِّي عَلَى ذِكْرِكَ وَشُكْرِكَ وَحُسْنِ عِبَادَتِكَ"
“Ee Allaah! Nisaidie katika kukudhukuru, kukushukuru na kukuabudu itakikanavyo”. [Abuu Daawuwd: Kitaabul Witr. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]
2- Neema ya Uislamu ndio neema kubwa zaidi kuliko zote. Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah (‘Alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimwomba Allaah Ta’aalaa Amtimizie na Amhifadhie neema hii akisema:
“Ee Allaah! Nijaalie mwenye kushikamana na Uislamu katika hali ya kusimama kwangu, Nijaalie mwenye kushikamana na Uislamu katika hali ya kukaa kwangu, na Nijaalie mwenye kushikamana na Uislamu katika hali ya kulala kwangu”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyhul Jaami’i].
3- Sifa ya kuridhia ni katika Sifa za Allaah Ta’aalaa. Nayo ni Sifa ya kivitendo inayohusiana na Matakwa Yake ‘Azza wa Jalla.
4- Kuziamini Sifa za Allaah Ta’aalaa ni chachu ya ‘amali na kauli njema.
5- Sifa ya utumwa kwa Allaah ndio sifa kubwa zaidi kuliko zote.
6- Umuhimu wa kuomba kusuhubiana na kuwa pamoja na Swalihina.
7- Kuzingatia zaidi kuzitengeneza ‘amali na vitendo na maneno ili zikubaliwe na ziridhiwe na Allaah Ta’aalaa.
8- Inapendeza zaidi kwa mwombaji awajumuishe wazazi wake wawili ndani ya du’aa yake kutokana na fadhila kubwa yao kwake.
9- Wazazi wawili ni miongoni mwa neema kubwa zaidi za Allaah kwa mtu.
10- Umuhimu wa kuomba du’aa za Qur-aan kwa kuwa zimekusanya maneno mafupi yenye maana pana.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
31-Kukiri Kuidhulumu Nafsi Kwa Makosa Na Kuomba Maghfirah
"رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي فَاغْفِرْ لِي"
“Rabb wangu! Hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu”. [Al-Qaswas: (16)]
Ni du’aa ya Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam). Ni du’aa muhimu ambayo inabidi tuizingatie. Inabainisha litakiwalo kwa mtu kushikamana nalo wakati wa fitnah na misukosuko, na namna ya kuamiliana na hali kwa mujibu wa Manhaj ya Allaah isiyo na kombo na njia iliyonyooka ambayo mwenye kushikamana nayo hatopotea duniani na wala hataishia pabaya aakhirah.
Sababu ya du’aa hii ni kuwa Muwsaa (‘Alayhis Salaam) alimuua Mkoptik kwa makosa bila kukusudia. Ni pale Muizrael ambaye ni katika watu wake alipomwomba amsaidie dhidi ya Mkoptik. Muwsaa akampiga ngumi moja akafa pale pale. Akalichukulia hilo ni dhambi kwa kuua nafsi ambayo Allaah Hakumwamuru kuiua.
Katika du’aa hii, Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) ameanza kwa kukiri kosa lake na kuonyesha majuto. Majuto yake yalimsukuma kunyenyekea kwa Mola wake na kumwomba maghfirah. Na kwa kuwa kosa lenyewe si la kukusudia, basi bila shaka alijua kwamba Allaah Atamsamehe, lakini pamoja na hivyo akaomba maghfirah. Hii ndiyo hali ya Nabiy wa Allaah. Basi vipi hali yetu sisi tunaofanya madhambi usiku na mchana bila kujali wala kuhisi lolote?!
Bila shaka kila mmoja wetu anatakikana asimame na kuitaamuli hali yake na hatima yake. Kila mtu atawajibishwa kwa kila dogo na kubwa. Leo ni matendo hakuna hisabu, na kesho ni hisabu hakuna matendo.
Tunayojifunza kutokana na du’aa hii:
1- Kukiri kosa ni toba pamoja na kulijutia, kuachana nalo kabisa na kuweka azima ya kutolirudia tena.
2- Kukiri kwanza kosa na kukiri kuidhulumu nafsi kabla ya du’aa, ni katika viwajibisho vya kujibiwa du’aa.
3- Aliyefanya dhambi anatakiwa aharakie kutubia na kurejea kwa Allaah hapo hapo.
4- Kukiri kwamba mtu kaidhulumu nafsi yake na kuomba maghfirah toka kwa Allaah, ni katika nyenendo za Manabii na Mitume. Ni kama walivyosema baba na mama yetu Aadam na Hawwaa:
"قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنْفُسَنَا وَإِنْ لَمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ"
“Wakasema: Rabb wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu, bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika”. [Al A’araaf: (23)].
5- Du’aa hii inadulisha namna ambavyo Allaah Anapenda kuikubali tawbah ya Mja Wake na kumghufuria. Muwsaa baada tu ya kuomba du’aa hii, Allaah Alimsamehe kosa lake. Aayah kamili inasema:
قَالَ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي فَاغْفِرْ لِي فَغَفَرَ لَهُ ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ
“Akasema: Rabb wangu! Hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu, basi Nighufurie; Akamghufuria. Hakika Yeye Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu”. [Al-Qaswas: (16)].
6- Kutawassal kwa Jina la Rabbu kunanasibiana na du’aa za haja zote.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
32- Kuokolewa Na Watu Madhalimu
"رَبِّ نَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ"
“Rabb wangu! Niokoe na watu madhalimu”. [Al-Qaswas: (28)].
Ni katika du’aa za Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) zilizokariri kwenye Kitabu cha Allaah ‘Azza wa Jalla. Ndani yake kuna maelekezo toka kwa Allaah Ta’aalaa kwetu ya kushikamana na njia ya kheri na kujiepusha na njia za baatwil ili tuwe katika Hifadhi ya Allaah katika dini yetu na dunia yetu.
Ameanza du’aa yake kwa kutawassali kwa Allaah kwa Jina Lake la Rabb. Akamwomba Amwokoe kutokana na dhulma za Fir-‘awn na kundi lake. Fir-‘awn huyu na wasaidizi wake hawa walijidhulumu wenyewe kwa kukataa wito wa iymaan wa Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) pamoja na miujiza dhahiri waliyoishuhudia wenyewe yenye kuthibitisha ukweli wa wito wake. Na hii ni mbali na jeuri yao na dhulma zao nyingi walizokuwa wakiwafanyia Bani Israel. Allaah Alimjibu du’aa yake kama ilivyo Ada Yake kwa Manabii na Vipenzi Vyake ambao wanakimbilia Kwake kwenye mambo yao yote na katika hali zao zote.
Kumwomba Allaah uokozi kutokana na madhalimu, kama ilivyo ada na mwenendo wa Manabii na Mitume, ilikuwa pia ni sehemu ya du’aa za Waumini wema. Bibi Aasiyah mke wa Fir-‘awn alimwomba Allaah pia vile vile Amwokoe kutokana na mumewe Fir-‘awn na vitimbi vyake na watu madhalimu. Qur-aan inatuambia:
"وَضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا لِّلَّذِينَ آمَنُوا امْرَأَتَ فِرْعَوْنَ إِذْ قَالَتْ رَبِّ ابْنِ لِي عِندَكَ بَيْتًا فِي الْجَنَّةِ وَنَجِّنِي مِن فِرْعَوْنَ وَعَمَلِهِ وَنَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ"
“Na Allaah Amewapigia mfano wale walioamini, mke wa Fir’awn, aliposema: Rabb wangu! Nijengee nyumba Kwako kwenye Jannah, na Niokoe na Fir’awn na vitendo vyake, na Niokoe na watu madhalimu”. [At-Tahriym: (11)].
Bi huyu ameomba aokolewe kutokana na Fir-‘awn dhalimu, kisha akaeneza ombi la kuokolewa kutokana na kila mwenye sifa hii mbaya ya udhalimu.
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Muislamu anatakiwa awe na pupa ya kuomba himaya toka kwa Allaah dhidi ya madhalimu. Hii ni kutokana na hatari yao kwa dini na nafsi.
2- Hakuna kinachovuta neema na kuondosha mabalaa kama du’aa. Ndio maana ikawa ni kimbilio la Manabii na Vipenzi vya Allaah nyakati zote na mahala popote.
3- Umuhimu wa kutawassal kwa Sifa za Allaah wakati wa kuomba du’aa. Ni kama alivyotawasali Muwsaa (‘Alayhis Salaam) kwa kusema: “Niokoe”, na hii ni Sifa Tukufu ya kivitendo ya Allaah inayoonyesha ukamilifu wa nguvu, matakwa na utoaji misaada.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
33- Njia Iliyo Sawa
"عَسَى رَبِّي أَن يَهْدِيَنِي سَوَاءَ السَّبِيلِ"
“Asaa Rabb wangu Akaniongoza njia iliyo sawa”. [Al-Qaswas: (22)].
Hii ni du’aa nyingine ya barakah ya Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) ndani ya Qur-aan Tukufu. Ni du’aa iliyo katika muundo wa sentensi taarifu.
Alipomuua Mkoptik bila kukusudia kwa kumpiga konde, alipambaukiwa kuwa mwenye khofu katika mji ule huku anaangaza kwa tahadhari. Akaja mtu kutoka mwisho wa mji ule akiwa anakimbia, akamhabarisha kuwa wakuu wanashauriana kumuua, kwa hiyo atoke haraka, na asidharau ushauri wake huo.
Muwsaa bila kusita akatoka mjini hapo kuelekea Madyana. Alitoka bila maandalizi yoyote ya safari. Hana masurufu, hana kipando, hana viatu na hata huko anakoelekea hamjui yeyote. Akiwa katika hali hii ngumu ya ghafla iliyochanganyika na khofu ya kuuawa, hapo alielekea kwa Mola wake na kumwomba du’aa hii akisema: “Asaa Rabb wangu Akaniongoza njia iliyo sawa”.
Yaani njia iliyonyooka na fupi ya kumfikisha kwa urahisi aendako. Na hapo Allaah ‘Azza wa Jalla Akamwongoza njia hiyo, na Akamwongoza katika njia iliyonyooka duniani na aakhirah. Akafika aendako, akapata ukaribisho wa heshima na akaozeshwa. Halafu akapata Utume, na kurudi tena kwa Fir-a’wn akiwa na miujiza. Na yeye akawa ndio sababu ya Fir’awn kuangamia pamoja na jeshi lake.
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Katika aayah hii, kuna maelekezo na mafundisho kuwa Muislamu anatakiwa atoe juhudi zake za mwisho za kutumia nyenzo alizonazo, kisha aelekee kwa Allaah kumwomba Amwepesishie kufikia lengo lake kupitia nyenzo hizo. Huu ndio ukamilifu wa kutawakkal.
2- Muislamu anatakiwa amwombe Mola wake ‘Azaa wa Jalla hidaayah ya kihisia na kidhahania mpaka Allaah Amwongoze kwenye njia nyepesi na karibu zaidi itakayomfikisha kwenye kusudio lake katika dini yake na dunia yake.
3- Viumbe vyote vinamhitajia Allaah Ta’aalaa kuvihidi na kuviwezesha.
4- Ubora wa du’aa katika kuvuta manufaa na kuondosha madhara.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
34- Kheri Yoyote Wakati Wa Dhiki Mbaya
"رَبِّ إِنِّي لِمَا أَنزَلْتَ إِلَيَّ مِنْ خَيْرٍ فَقِيرٌ"
“Rabb wangu! Hakika mimi ni mhitajia wa kheri yoyote Utakayoniteremshia”. [Al-Qaswas: (24)].
Ni mlolongo wa du’aa za Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) baada ya kuua mtu na kukimbilia Madyana. Allaah Amezitaja kutokana na umuhimu wake. Ndanimwe kuna kheri na manufaa mengi ya kidunia na kiaakhirah. Hivyo tuzizingatie na tuzifahamu.
Baada ya kuchoka sana kwa safari ya muda mrefu kwa miguu na kupata njaa kali huku akiwa hana chochote cha kula, Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) alijua wapi aelekee na wapi pa kutokea. Akaelekea kwa Mola wake Ambaye Alimwangalia na kumhifadhi tokea udogoni mpaka hapo alipofikia. Hapo ndipo akaomba du’aa hii tukufu, kwa maneno laini kabisa yenye kuhisisha dhiki aliyonayo na msaada wa haraka wa faraja kwake.
Allaah kama Anavyopenda kwa mwombaji atawassal Kwake kwa Majina Yake, Sifa Zake na Neema Zake, pia Anapenda atawassali Kwake kwa udhaifu wake, ajizi yake, uhitajio wake, na kukosa uwezo wa kupata maslaha yake na kujiondoshea madhara. Kwa hayo, mwombaji anaonyesha udhalili wake na uhitajio wake Kwake tu pasi na mwingine.
Ndani ya Kitabu cha Qur-aan, kuna aina tofauti za namna ya kuomba du’aa. Kuna du’aa ya ombi la moja kwa moja kama:
"وَقُلْ رَبِّ اغْفِرْ وَارْحَمْ وَأَنْتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ"
“Na sema: Rabb wangu! Ghufuria na Rehemu, Nawe Ni Mbora wa wenye kurehemu”. [Al-Muuminuwn: (118)].
Na pia kuna ombi la muundo wa sentensi taarifu kama la Nabiy Ayyuwb:
"وَأَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ"
“Na Ayyuwb, alipomwita Rabb wake: Hakika mimi imenigusa dhara, Nawe Ndiye Mbora zaidi wa Kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu”. [Al-Anbiyaa: (83)].
Au la Nabiy Zakariyyaa:
"قَالَ رَبِّ إِنِّي وَهَنَ الْعَظْمُ مِنِّي وَاشْتَعَلَ الرَّأْسُ شَيْبًا وَلَمْ أَكُن بِدُعَائِكَ رَبِّ شَقِيًّا"
“Akasema: Rabb wangu! Hakika mimi mifupa imeninyong’onyea na kichwa kimeng’aa mvi, na wala sikuwa mwenye kunyimwa katika kukuomba du’aa, ee Rabb wangu”. [Maryam: (04)].
Na ikiwa Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) alimwomba Allaah kheri kwa muundo wa kugusia hali mbaya aliyokuwa akiipitia, basi pia imethibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwomba Allaah kwa muundo wa ombi la moja kwa moja. Ni kama katika Hadiyth Adhimu ambapo Rasuli alimwambia Mama yetu ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa):
“Shikamana na du’aa kusanyifu jumuishi. (Omba):
"اللَّهمَّ إنِّي أسألُكَ مِنَ الخيرِ كلِّهِ عاجلِهِ وآجلِهِ ، ما عَلِمْتُ منهُ وما لم أعلَمْ ، وأعوذُ بِكَ منَ الشَّرِّ كلِّهِ عاجلِهِ وآجلِهِ ، ما عَلِمْتُ منهُ وما لم أعلَمْ ، اللَّهمَّ إنِّي أسألُكَ من خيرِ ما سألَكَ عبدُكَ ونبيُّكَ ، وأعوذُ بِكَ من شرِّ ما عاذَ بِهِ عبدُكَ ونبيُّكَ ، اللَّهمَّ إنِّي أسألُكَ الجنَّةَ وما قرَّبَ إليها من قَولٍ أو عملٍ ، وأعوذُ بِكَ منَ النَّارِ وما قرَّبَ إليها من قولٍ أو عملٍ ، وأسألُكَ أن تجعلَ كلَّ قَضاءٍ قضيتَهُ لي خيرًا"
“Ee Allaah! Hakika mimi ninakuomba kheri zote; za karibu yake na za mbali yake, ninazozijua kati yake na nisizozijua. Na najilinda Kwako na shari zote; za karibu yake na za mbali yake, ninazozijua kati yake na nisizozijua. Ee Allaah! Hakika mimi ninakuomba kheri alizokuomba Mja Wako na Nabiy Wako, na najilinda Kwako na shari alizojilinda nazo Kwako Mja Wako na Nabiy Wako. Ee Allaah! Hakika mimi ninakuomba Jannah na yote ya kuniwezesha kuifikia katika maneno au vitendo. Na najilinda Kwako na moto na yote ya kunisogeza kuukaribia katika maneno au matendo. Na ninakuomba Uifanye kila qadhwaa Uliyoipitisha kwangu kuwa kheri”. [Imesimuliwa na ‘Aaishah na kukharijiwa na Ibn Maajah. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Kumshtakia Allaah hali yako hakupingani na subra, bali hilo ni katika ukamilifu wa iymaan kwa Allaah Ta’aalaa na kuridhia Qadar Yake. Tatizo ni kuwashtakia viumbe. Hapo ndipo linapokuja kosa.
2- Ni juu ya mwombaji atawassal kwa Allaah kwa aina tofauti za tawassulaat za kisheria. Hilo ni katika ukamilifu wa utumwa Anaoupenda Allaah ‘Azza wa Jalla.
3- Uhalali wa kujilinda na umasikini. Huo ni mwenendo wa Manabii na Mitume. Pia ilikuwa ni katika du’aa za Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akiomba:
"اللّهُمَّ إنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْفَقْرِ، وَالْقِلَّةِ، وَالذِّلَّةِ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ أَنْ أَظْلِمَ أو أُظْلَمَ"
“Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako kutokana na ufukara, uhaba (wa kila kinachohitajia ukamilifu) na udhalili. Na najilinda Kwako kudhulumu au kudhulumiwa”. [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1544), Ahmad (8294) na tamko ni lao, na Ibn Maajah (3842)]
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
35- Usaidizi Dhidi Ya Mafisadi
"رَبِّ انصُرْنِي عَلَى الْقَوْمِ الْمُفْسِدِينَ"
“(Luutw) akasema: Rabb wangu! Ninusuru dhidi ya watu mafisadi.” [Al-‘Ankabuwt: (30)].
Hii ni du’aa ya Nabiy Luutw (‘Alayhis Salaam). Nabiy huyu alitumwa kwa watu waliokuwa wamejumuisha kati ya ushirikina, ukafiri na kitendo kibaya mno cha kuchukiza. Walikuwa wakiwaendea wanaume kinyume na maumbile kitendo ambacho hakijawahi kufanywa na yeyote katika waliotangulia. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Ametuhadithia ulinganio wa Nabiy huyu. Watu hawa walikaidi na kuukataa ulinganio huo hata mkewe ambaye ndiye mtu wa karibu zaidi. Alipokata tamaa, Nabiy Luutw aliwaapiza baada ya kuzidi kubobea kwenye uchafu wao na ukafiri. Na hata walithubutu kuwataka kimatamanio Malaika wa adhabu walipomjia Nabiy Luutw na habari ya furaha wakiwa katika maumbile ya kibinadamu. Alipoona hali hiyo, Nabiy Luutw alielekea kwa Mfalme, Mwenye uwezo na Mwenye Kusikia kila kitu na kuomba akisema: “Rabb wangu! Ninusuru”.
Alimwomba Allaah Amnusuru wasiweze kufikia dhamira yao kwa kuwateremshia adhabu iliyoahidiwa. Akatawassali kwa Jina Tukufu la Allaah la Rabb lenye maana ya ulezi, usimamizi, kuleta manufaa, kuondosha madhara, na kudabiri mambo. Akawaelezea watu wake kuwa ni mafisadi kwa kuwa ufisadi wao huo ulifungua njia kwa vizazi vilivyofuatia hadi leo kama hali tunavyoiona. Kampeni zimechachamaa kuhalalisha jambo hilo ili kionekane kitu cha kawaida, ndoa za jinsia moja zinatangazwa hadharani bila kukemewa na hata baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wamehudhuria kwenye mikutano au minasaba mikubwa na wake zao waume.
Na kutokana na kitendo hicho chao kibaya na kichafu mno cha kuwaingilia wanaume, Allaah Aliwaadhibu adhabu kali mno ya kuupindua mji wao juu chini, chini juu:
"فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا جَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ مَّنضُودٍ"
“Basi ilipokuja Amri Yetu, Tuliupindua (mji wao) juu chini, na Tukauteremshia mvua ya mawe ya udongo mgumu uliookwa yenye kuandamana”. [Huwd: (82)].
Kama walivyopindua maumbile asili, Allaah Naye Akapindua miili yao, nyumba zao na mji wao kiujumla kama adhabu inayowafikiana na matendo yao.
Katika kisa hiki, kuna mazingatio na maelekezo kwetu kwamba tukimbilie kwa Allaah kuomba hifadhi, na tujilinde Kwake kutokana na munkarati potoshi zenye kuharibu moyo, akili, mwili na silka salimu.
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Hakuna mwenye uwezo wa kuhifadhi isipokuwa Allaah Pekee.
2- Mwombaji anatakiwa aepukane na mafisadi ili yasimkute yaliyowapata watu wa Luutw, na pia amwombe Allaah Amsaidie kufanikisha hilo.
3- Umuhimu wa kutawassali kwa Allaah kwa kuwaapiza mafisadi. Ni kama lilivyodulisha tamshi: “Ninusuru”, na hakusema: “Nilinde”, na hii inaonyesha hatari yao kubwa, na kwamba mwenye kunusuriwa na watu hao, basi kwa hakika amenusuriwa nusra ya nguvu kutoka kwa Allaah Ta’aalaa.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
36- Maghfirah Kwa Waumini Waliotangulia
"رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ"
“Rabb wetu! Tughufurie pamoja na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan, na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Rabb wetu! Hakika Wewe Ni Mwenye huruma mno, Mwenye Kurehemu”. [Al-Hashr: (10)].
Du’aa hii ina umuhimu mkubwa mno. Allaah Ta’aalaa Ameitaja kwa watu wa iymaan safi baada ya Maswahaba (Allaah Awaridhie wote) kati ya Taabi’iyna na waliowafuatia kwa wema hadi Siku ya Qiyaamah. Ni du’aa inayoonyesha mapenzi ya kweli na udugu uliojikita ndani ya nyoyo za Waislamu. Kwani haki za Muislamu juu ya nduguye Muislamu ni nyingi. Kati ya haki hizo ni kumwombea nduguye kwa siri katika uhai wake na baada ya kufa kwake. Udugu wa dini ndio udugu uliotukuka zaidi na wenye faida za kudumu zaidi kuliko udugu wa damu. Udugu wa kidini ni wa kufaana duniani na aakhirah, lakini wa damu unaweza usiwe na faida yoyote; si duniani wala aakhirah.
Al-‘Allaamah bin Sa’adiy (Rahimahul Laah) amesema: “Du’aa hii inawajumuisha Waumini wote waliotangulia kati ya Maswahaba, waliopita kabla yao na watakaokuja baada yao. Na hii ni katika fadhwaail za iymaan kwamba Waumini wananufaishana wao kwa wao, na wanaombeana wao kwa wao kwa kuwa iymaan yao ni moja. Iymaan hii imewafunga wote ndani ya duara la udugu ambao moja kati ya matawi yake ni kuombeana wao kwa wao na kupendana wao kwa wao. Na kwa ajili hiyo, Allaah Ta’aalaa Ametaja katika du’aa hii mafundo ya chuki ambayo kama yataondoka, kinyume chake huthibiti, nayo ni mapenzi ya kweli kati ya Waumini”.
Hivyo wamekusanya ndani ya du’aa hii ya barakah kati ya usalama wa moyo na usalama wa ndimi zao. Hakuna ndani ya nyoyo zao chuki yoyote, hikdi yoyote wala kumtaja yeyote kwa ubaya. Na hili ndilo jumuiko la mapenzi ya kweli kati ya Waumini kwa ajili ya Rabbi wa walimwengu.
Abu Mudhwaffar As-Sam’aaniy (Rahimahul Laah) amesema: “Katika aayah, kuna dalili kwamba kuwaombea rahmah waliotangulia, kuwaombea kheri na kuacha kuwataja kwa ubaya, ni alama ya Waumini wa kweli”.
Na Waislamu wenye sifa hii ya kupendana, kuombeana na kuwataja kwa wema ndugu zao, Allaah Atawalipa malipo mema kabisa. Allaah Anatuambia:
"وَنَزَعْنَا مَا فِي صُدُورِهِم مِّنْ غِلٍّ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ ۖ وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي هَدَانَا لِهَـٰذَا وَمَا كُنَّا لِنَهْتَدِيَ لَوْلَا أَنْ هَدَانَا اللَّـهُ"
“Na Tutaondosha mizizi ya mafundo ya kinyongo yaliyomo vifuani mwao, itapita chini yao mito. Na watasema: AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Ambaye Ametuongoza kwa haya, na tusingelikuwa wenye kuhidika kama Allaah Asingetuongoza”. [Al-A’raaf: (43)].
Haifichikani ee ndugu yangu Muislamu kwamba kuna kheri nyingi za dunia na aakhirah katika kukithirisha du’aa hii. Kwanza, kufanya hivyo ni kuitikia Agizo la Allaah Ta’aalaa. Pili, kuna thawabu nyingi anazozipata mwombaji. Tatu, du’aa hii hukuza mapenzi kwa nduguze Waislamu ndani ya moyo wake. Nne, humweka mbali na chuki, hasadi, mafundo na kinyongo. Na kwa hivyo, nyoyo husafika, na hii ni moja kati ya makusudio makubwa ya dini.
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Ni kuwa du’aa hii ina umuhimu mkubwa sana kwa Muislamu ambaye anatakiwa aikithirishe mchana na usiku, kwani matunda na manufaa yake hayakokoteki duniani na aakhirah.
2- Kati ya haki kubwa za Muislamu kwa nduguye Muislamu, ni kumwombea du’aa.
3- Kuna umuhimu mkubwa wa kumwomba Allaah Ta’aalaa maghfirah. Kati ya matunda makubwa ya maghfirah ni kuondoka mabaya, kupatikana kheri, na kufuzu Jannah.
4- Muislamu asisahau fadhla za waliomtangulia katika iymaan. Awataje kwa wema na awaombee.
5- Du’aa hii imekusanya tawassuli mbili muhimu ambazo ni:
(a) Kutawassal kwa Umola wa Allaah (Rubuwbiyyah) waliposema: “Rabbi wetu”, na kwa Majina Yake Mawili Matukufu; “Rauwf” na “Rahiym”.
(b) Kutawassal kwa neema Aliyowapa ya iymaan wao na waliowatangulia.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
37-Kutimiziwa Nuru Na Kughufuriwa
"رَبَّنَا أَتْمِمْ لَنَا نُورَنَا وَاغْفِرْ لَنَا إِنَّكَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ"
“Rabb wetu! Tutimizie Nuru yetu, na Tughufurie, hakika Wewe juu ya kila kitu Ni Muweza”. [At-Tahriym: (66)].
Du’aa hii yenye manufaa ni ya Waumini Siku ya Qiyaamah wakati nuru ya wanafiki itakapozimika (tunajilinda kwa Allaah na hilo). Na nuru hii, ni moja kati ya alama ambazo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atawatambua kwayo umati wake. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَنَا أَوَّلُ مَنْ يُؤْذَنُ لَهُ بِالسُّجُودِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، وَأَوَّلُ مَنْ يُؤْذَنُ لَهُ أَنْ يَرْفَعَ رَأْسَهُ، فَأَرْفَعُ رَأْسِي فَأُنْظِرُ بَيْنَ يَدَيَّ، فَأَعْرِفُ أُمَّتِي مِنْ بَيْنِ الْأُمَمِ))، فَقَالَ رَجُلٌ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، فَكَيْفَ تَعْرِفُ أُمَّتَكَ مِنْ بَيْنِ الْأُمَمِ؟ مَا بَيْنَ نُوحٍ إِلَى أُمَّتِكَ؟ قَالَ: ((غُرٌّ مُحَجَّلُونَ مِنْ أَثَرِ الْوُضُوءِ، ولَا يَكُونُ لِأَحَدٍ مِنَ الْأُمَمِ غَيْرِهِمْ، وَأَعْرِفُهُمْ أَنَّهُمْ يُؤْتَوْنَ كُتُبَهُمْ بِأَيْمَانِهِمْ، وَأَعْرِفُهُمْ بِسِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِمْ مِنْ أَثَرِ السُّجُودِ، وَأَعْرِفُهُمْ بِنُورِهِمُ الَّذِي بَيْنَ أَيْدِيهِمْ، وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ، وَعَنْ شَمَائِلِهِمْ"
“Mimi ndiye wa mwanzo atakayeruhusiwa kusujudu Siku ya Qiyaamah, na ndiye wa mwanzo atakayeruhusiwa kunyanyua kichwa chake. Nitanyanyua kichwa changu na moja kwa moja nitaonyeshwa mbele yangu. Hapo nitautambua umati wangu kati ya nyumati nyinginezo. Mtu mmoja akauliza: Ee Rasuli wa Allaah! Vipi utautambua umati wako katikati ya nyumati zinginezo? Kipindi cha kati ya Nuwh hadi umati wako? Akasema: Watakuwa na nuru usoni mwao, mikononi na miguuni mwao kutokana na athari za wudhuu, na hatakuwa nayo yeyote katika nyumati nyinginezo isipokuwa wao tu. Na nitawajua kwamba wao watapewa madaftari yao kwa upande wao wa kuume. Na nitawajua kwa alama zao kwenye nyuso zao kutokana na athari ya sijdah. Na nitawajua kwa nuru yao ambayo itakuwa mbele yao, kuliani mwao na kushotoni mwao”. [Imekharijiwa na Ahmad. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]
Waumini hawa watamwomba Allaah wakisema: “Ee Rabbi wetu! Tutimizie nuru yetu”. Wataomba waendelee kuwa na nuru yao hiyo mpaka pale watakapofika Jannah Nyumba ya amani. Na hii ni pale watakapoona nuru ya wanafiki imewazimikia, nao wataingia khofu nuru yao nayo isije kuzima.
Imenukuliwa toka kwa Adh-Dhwahhaak akisema: “Hakuna yeyote isipokuwa atapewa nuru Siku ya Qiyaamah. Watu watakapofika kwenye Swiraat, nuru ya wanafiki itazima. Na Waumini wakiona hivyo, wataingia khofu ya kuzimikiwa nuru yao kama ilivyozimika nuru ya wanafiki hao”.
Halafu Waumini hao wataelezea sababu ya wao kuomba hilo wakisema: “Hakika Wewe juu ya kila kitu Ni Muweza”.
Kana kwamba wanasema: “Ee Rabbi wetu! Hatukukuomba hili isipokuwa tu kwamba sisi tunajua kuwa Wewe ni Muweza wa kila kitu. Hakikushindi chochote, basi Tutimizie kheri hii na Ibakishe mpaka tufike kwenye Nyumba ya amani (Daarus Salaam) Uliyotuahidi”.
Na nuru hii ee ndugu yangu Muislamu, itakuwa kwa mujibu wa ‘amali zako hapa duniani. Malipo ni kwa mujibu wa kazi. Imesimuliwa toka kwa ‘Abdullaah bin Mas-‘uwd (Radhwiya Allaah ‘anhu) akiizungumzia aayah hii: “Watagaiwa nuru yao kwa mujibu wa ‘amali zao wakipita juu ya Swiraat. Kati yao kuna ambaye nuru yake itakuwa mfano wa mlima, na wengineo kuna ambaye nuru yake mfano wa mtende. Mwenye nuru ya chini zaidi ni yule itakayokuwa mfano wa kidole chake cha gumba; mara inazimwa, mara inawashwa”.
Na Muislamu anatakiwa amwombe Allaah Ta’aalaa Amtimizie nuru yake kamili hapa hapa duniani ili Amtimizie nuru kamili Siku ya Qiyaamah juu ya Swiraat. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimwomba Mola wake Tabaaraka wa Ta’alaa Amruzuku nuru kwenye sehemu zote za mwili wake mtukufu ili ikamilike kwake ‘ilmu, maarifa na uongofu. Alikuwa akiomba:
"اللهُمَ اجعَل فِي قَلبِي نُوراً وفِي سَمعي نُوراً وعَن يَمينِي نُوراً وعن يَسارِي نُوراً وفَوقِي نُوراً وتَحتِي نُوراً وأَمامِي نُوراً وخَلفِي نُوراً وأَعظِم لِي نُوراً"
“Ee Allaah! Jaalia ndani ya moyo wangu nuru, na kwenye masikio yangu nuru, na kuliani kwangu nuru, na kushotoni kwangu nuru, na juu yangu nuru, na chini yangu nuru, na mbele yangu nuru, na nyuma yangu nuru, na Nikuzie nuru yangu”. [Al-Bukhaariy: Kitaabu Ad Da’awaat, na Muslim: Kitaabu Swalaatil Musaafiriyn wa Qaswrihaa. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]
Du’aa hii ina faida zifuatazo:
1- Kuna umuhimu mkubwa sana wa kumwomba Allaah du’aa hii, kwani ndani yake kuna maombi mawili yanayohusu dini, dunia na aakhirah:
(a) Kutimiziwa nuru, yaani kuenezewa, ambapo kati ya athari zake ni ‘ilmu, uongofu na iymaan. Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiiomba nuru wakati anapokwenda kwenye Swalah, wakati anaposujudu na wakati anaposimama usiku kwa ‘ibaadah.
(b) Kumwomba Allaah maghfirah ya madhambi. Ndani ya hili kuna kinga dhidi ya shari zote ambapo kubwa yake zaidi ni moto (Allaah Atulinde nao).
3- Kutawassul kwa Jina la Allaah la “Al-Qadiyr” kunanasibiana na ombi lolote liwalo.
4- Kwamba kati ya matunda makuu ya tawbah ya kweli iliyokamilisha masharti, ni kufaulu na kupata amani kwenye Nyumba ya Amani.
5- Du’aa ina fadhla kubwa, na kwamba manufaa yake ya kidunia na kiaakhirah, yanarudi kwa mwombaji mwenyewe. Haijalishi cheo chake wala nafasi yake.
Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu
Na Sharh Yake
Alhidaaya.com [2]
38- Maghfirah Kwako, Wazazi Na Waumini
"رَّبِّ اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِمَن دَخَلَ بَيْتِيَ مُؤْمِنًا وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَلَا تَزِدِ الظَّالِمِينَ إِلَّا تَبَارًا"
“Rabb wangu! N ighufurie mimi, na wazazi wangu wawili, na kila aliyeingia nyumbani mwangu akiwa Muumini, na Waumini wa kiume na Waumini wa kike, na wala Usiwazidishie madhalimu isipokuwa kuteketea kabisa”. [Nuwh: (28)].
Hii ni du’aa miongoni mwa du’aa za Nabiy Nuwh (‘Alayhis Salaam). Imekusanya maombi ya dunia na aakhirah. Amejiombea mwenyewe maghfirah, amewaombea wazazi wake, na amewaombea waumini wote walio hai na waliokufa kuanzia Aadam (‘Alayhis Salaam) mpaka kitakaposimama Qiyaamah. Aliiomba wakati alipojua kupitia Wahyi kwamba hakuna yeyote katika umati wake atakayeamini zaidi ya wale waliokwisha muamini.
Akaanza kujiombea mwenyewe maghfirah. Hili linatakiwa kwa Muislamu ajianze yeye mwenyewe kabla ya mwingine yeyote. Nafsi yake ina haki zaidi kwake kuliko mwingine yeyote.
Akawaombea pia maghfirah wazazi wake wawili kutokana na fadhla yao kubwa kwake. Hili pia tumeamuriwa sisi tulifanye kwa wazazi wetu.
Halafu maghfirah hiyo hiyo akamwombea kila Muumini anayeingia nyumbani kwake. Kwa kuwa kusuhubiana nao kuna usalama na uthabiti katika dini. Na hili linatudokeza kuwa marafiki zetu ni lazima wawe watu wema ambao kama wataingia nyumbani kwako utahisi utulivu kwa kila jambo. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لاَ تُصَاحِبْ إِلاَّ مُؤْمِنًا، وَلاَ يَأْكُلْ طَعَامَكَ إِلاَّ تَقِيٌّ"
“Usiandamane isipokuwa na Muumini, na asile chakula chako isipokuwa mchaji”. [Abu Daawuwd: Kitaabul Adab]
Du’aa hii kwa hakika ina umuhimu mkubwa mno. Na hii ni kwa haya:
(a) Ni kwamba du’aa za Manabii zinajibiwa. Nasi tunatumai kwa yakini Allaah Atazijibu du’aa walizotuombea.
(b) Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametoa bishara njema ya kupata malipo makubwa kwa du’aa hii. Amesema:
"مَنِ اسْتَغْفَرَ لِلْمُؤْمِنِيْنَ وَالْمُؤْمِنَاتِ، كَتَبَ اللهُ لَهُ بِكُلِّ مُؤْمِنٍ وَمُؤْمِنَهٍ حَسَنَةً"
“Mwenye kuwaombea maghfirah Waumini wa kiume na Waumini wa kike, Allaah Atamwandikia jema kwa kila Muumini wa kiume na Muumini wa kike”. [Musnad Ash-Shaamiyyiyn cha At-Twabaraaniy. Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan]
Hebu angalia ukubwa wa malipo haya! Kila jema moja malipo ni kumi mfano wake hadi nyongeza nyingi maradufu kwa mabilioni ya Waumini wa tokea Aadam hadi Siku ya mwisho. Na hii inaonyesha ukubwa wa Fadhla za Allaah kwa Waumini.
Kisha Nabiy Nuwh akaimalizia du’aa yake kwa kusema: “Na wala Usiwazidishie madhalimu isipokuwa kuteketea kabisa”. Du’aa hii inamjumuisha kila dhalimu tokea alipoiomba hadi Qiyaamah. Na kwa vile du’aa za Manabii hujibiwa, basi kila dhalimu itampata tu.
Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:
1- Kuna umuhimu mkubwa sana wa kumwomba Allaah Ta’aalaa maghfirah. Maghfirah ni katika sababu kubwa za kuingia Jannah.
2- Mwombaji aombe la muhimu zaidi kisha linalofuatia kwa umuhimu.
3- Kuna umuhimu mkubwa wa kuwaombea wazazi wawili maghfirah. Ni wema kwao wakiwa hai au maiti.
4- Muislamu anatakiwa asiwasahau nduguze Waislamu katika du’aa zake pamoja na dhuria wake.
5- Mwenye kukithirisha du’aa hii basi atajibiwa bila shaka kutokana na mambo mawili:
(a) Ni du’aa ya Nabiy ambaye ni katika wale Watano (Ulul ‘Azm).
(b) Ni du’aa ya siri, kwa kuwa anaowaombea wakiwa hawamjui wala yeye hawajui.
6- Umuhimu wa kutawassal kwa Jina la Rabb. Ni mwenendo wa Manabii na Mitume wote.
7- Inajuzu kuwaombea mabaya madhalimu, na hasa madhara yao yanapowagusa watu.
8- Inapendeza mwombaji aeleze sababu ya du’aa yake.
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/24
[2] http://www.alhidaaya.com/
[3] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11107&title=Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20%20Na%20Sharh%20Yake
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11108&title=01-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Al-Faatihah
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11109&title=02-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kutaqabaliwa%20%27Amali
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11110&title=03-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Mema%20Ya%20Dunia%20Na%20Aakhirah%20
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11111&title=04-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Nyoyo%20Zisipotoshwe%20
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11112&title=05-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Watoto%20Wema
[9] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11113&title=06-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kuandikwa%20Pamoja%20Na%20Wenye%20Kushuhudia%20Haki
[10] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11114&title=07-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Maghfirah%2C%20Kuimarishwa%20Na%20Ushindi%20Dhidi%20Ya%20Makafiri
[11] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11115&title=08-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kukingwa%20Na%20Moto%2C%20Maghfirah%2C%20Kufishwa%20Pamoja%20Na%20Wema%20
[12] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11116&title=09-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Bila%20Maghfirah%20Na%20Rahma%20Hatima%20Ni%20Khasara
[13] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11117&title=10-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kuepushwa%20Kuwa%20Kundi%20Moja%20Na%20Madhalimu
[14] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11118&title=11-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kuandikiwa%20Mema%20Ya%20Dunia%20Na%20Ya%20Aakhirah
[15] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11119&title=12-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Toshelezo%20La%20Allaah%20%20%20
[16] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11120&title=13-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Tusiwe%20Fitnah%20Kwa%20Watu%20Madhalimu
[17] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11121&title=14-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kufishwa%20Na%20Uislamu%20Na%20Kuunganishwa%20Na%20Watu%20Wema
[18] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11122&title=15-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Amani%20Kwa%20Makkah%20Na%20Kuepushwa%20Na%20Masanamu
[19] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11123&title=16-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kusimamisha%20Swalah%20Pamoja%20Na%20Watoto
[20] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11124&title=17-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Maghfirah%20Kwa%20Wazazi%20Na%20Waumini
[21] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11125&title=18-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Rahmah%20Na%20Kutengenekewa%20Mambo
[22] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11126&title=19-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%2019-Kukunjuliwa%20Kifua%20Na%20Kuwepesishiwa%20Jambo%20
[23] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11127&title=20-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kuzidishiwa%20%E2%80%98Ilmu
[24] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11129&title=21-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kukiri%20Kosa%20Kwa%20Kumtakasa%20Allaah
[25] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11130&title=22-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kuomba%20Mtoto
[26] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11131&title=23-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kinga%20Dhidi%20Ya%20Udokezi%20Wa%20Mashaytwaan%20
[27] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11132&title=24-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Iymaan%2C%20Maghfirah%20Na%20Rahmah
[28] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11133&title=25-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Maghfirah%20Na%20Rahmah
[29] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11134&title=26-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kuepushwa%20Na%20Adhabu%20Ya%20Jahannam
[30] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11135&title=27-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Wake%20Na%20Watoto%20Kuwa%20Kitulizo%20Cha%20Jicho
[31] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11136&title=28-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Hikmah%20Na%20Kukutanishwa%20Na%20Watu%20Wema
[32] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11137&title=29-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kutohizishwa%20Siku%20Ya%20Qiyaamah
[33] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11138&title=30-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kuzinduliwa%20Kuzihisi%20Na%20Kuzishukuru%20Neema
[34] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11139&title=31-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kukiri%20Kuidhulumu%20Nafsi%20Kwa%20Makosa%20Na%20Kuomba%20Maghfirah
[35] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11140&title=32-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20%20Kuokolewa%20Na%20Watu%20Madhalimu
[36] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11141&title=33-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Njia%20Iliyo%20Sawa
[37] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11142&title=34-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kheri%20Yoyote%20Wakati%20Wa%20Dhiki%20Mbaya
[38] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11143&title=35-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Usaidizi%20Dhidi%20Ya%20Mafisadi
[39] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11144&title=36-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Maghfirah%20Kwa%20Waumini%20Waliotangulia
[40] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11145&title=37-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Kutimiziwa%20Nuru%20Na%20Kughufuriwa
[41] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11146&title=38-Du%E2%80%99aa%20Toka%20Kwenye%20Qur-aan%20Tukufu%20Na%20Sharh%20Yake%3A%20Maghfirah%20Kwako%2C%20Wazazi%20Na%20Waumini