Akiwa Ndani Ya Ihraam Amechezea Nywele Kisha Zimeng'oka
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Nina tabia ya kuchezea nywele ninapoikuwa na fikra. Nilipokwishaingia katika ihraam, bila ya kujitambua, nilifanya hivyo na baadhi ya nywele ziling'oka na kuanguka. Je, napaswa kulipa kafara?
JIBU:
Hakuna haja kufanya hivyo (kulipa kafara) kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametaja kuhusu Waumini kwamba wamesema:
رَبَّنَا لاَ تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا
“Rabb wetu Usituchukulie tukisahau au tukikosea. [Al-Baqarah:286]
Kisha Allaah Akawajibu du'aa yao hii kama ilivyotajwa katika Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliitikia kwa kusema:
((قَدْ فَعَلْت))
(Nimeiitikia [du'aa]) [Muslim katika Swahiyh yake]
[Fataawa Al-Hajj Wal 'Umrah waz-Ziyaarah Uk. 58]
Amenyoa Kwapa Akiwa Katika Hali Ya Ihraam
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Hujaji ameingia katika Ihraam ya 'Umrah, kisha akakumbuka kuwa ni waajib kunyoa kwapani. Akanyoa akiwa katika ihraam. Kisha akaelekea kufanya 'Umrah. Tunaomba mutuelezee hukmu ya hili, na Allaah Awalipe.
JIBU:
Kunyoa kwapani au kunyofoa nywele zake sio waajib kwa ajili ya kuingia katika ihraam. Bali ni jambo la kupendeza kunyoa na kubakia msafi kabla ya kuingia katika ihraam, kama inavyopendekezeka kupunguza masharubu, kukata kucha, kunyoa nywele za sehemu za siri ikihitajika (yaani ikiwa zimekuwa nyingi kiasi cha kuhitaji kupunguzwa) Sio lazima kufanya hivyo mtu anapoingia katika ihraam, bali inatosheleza akifanya kabla ya kuingia katika ihraam akiwa bado nyumbani kwake au njiani. Na hawajibiki kufanya lolote (kulipa kafara) yule anayekumbuka kunyoa kwapa kwani ni ukosefu wa kutambua hukmu ya jambo hili. Hali kadhalika haiwajibiki lolote kwa aliyekwishaingia katika ihraam kisha akasahau na kufanya lolote ambalo limetajwa kufanywa kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
رَبَّنَا لاَ تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا
“Rabb wetu Usituchukulie tukisahau au tukikosea. [Al-Baqarah:286]
Na imethibitika kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa Allaah Aliikubali du'aa hii.
[Majmuw' Fataawa Samaahat Shaykh Ibn Baaz – Mjalada 6, Uk. 96, Fatwa Namba 48]
Amesahau Kutamka Talbiyah katika Hajj ya Tamattu'
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Hajji ameingia katika ihraam alipofika Miyqaat lakini kasahau kutamka talbiyah kwa ajili ya Hajj ya Tammattu'. Je amalize taratibu zake kama ni Hajji wa Tammattu’? Afanye nini ikiwa atavua ihraam yake na kuvaa ihraam ya Hajj akiwa Makkah?
JIBU:
Ikiwa ametia niyyah ya kutekeleza 'Umrah alipoingia katika ihraam kisha akasahau kutamka talbiyah huku akiwa na niyyah ya 'Umrah, atahesabika kama aliyetamka talbiyah. Anatakiwa afanye twawaaf, sa’ay na kukata nywele kisha avue ihraam yake. Anaruhusiwa kutamka talbiyah akiwa njiani. Ikiwa hakutamka talbiyah basi hakuna kimpasacho kufanya (kama kafara) kwani kutamka talbiyah ni Sunnah iliyothibiti. Afanye twawaaf, sa’y, akate nywele zake ili amalize 'Umrah yake. Hii ni kwa sababu alikuwa na niyyah ya 'Umrah. Ikiwa ametia niyyah ya Hajj wakati alipoingia katika ihraam na muda unatosheleza, inapendekezeka kubadilisha niyyah yake kufanya 'Umrah ambayo ni kufanya twawaaf, sa’y, kukata nywele ili kujitoa katika ihraam.
Himdi Anastahiki Allaah, atahesabika kuwa kama ni Mutamatti'
[Fataawa Muhimmah tata'allaq bil-Hajji wal-‘Umrah – Uk. 16, Fatwa Namba 4]
Kupaka Manukato Katika Ihraam
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Nini hukmu ya kupata mafuta mazuri katika ihraam kabla ya kutia nia na talbiyah?
JIBU:
Sio sawa kupaka manukato mazuri katika ihraam (vipande viwili vyeupe vya shuka vinavyovaliwa). Sunnah ni kupaka mafuta mazuri mwilini kama kichwani, ndevu, kwapani na sehemu nyingine. Ama ihraam haipakwi mafuta mazuri kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Msivae nguo zilizoguswa na az-za’faraan au al-wars [aina ya mafuta mazuri]))
Kwa hiyo Sunnah ni kujipaka mafuta mazuri mwilini pekee na sio katika ihraam. Na ikiwa imepakwa, basi isivaliwe bali ioshwe au mtu abadlishe avae nyingineyo.
[Majmuw' Fataawaa Samaahat Shaykh Ibn Baaz – Mjalada 6, Uk 96, Fatwa 46]
Tanbihi Kutoka Alhidaaya:
Hukmu hiyo ya kupaka mafuta mazuri inawahusu wanaume pekee kwani mwanamke haimpasi kujipaka mafuta mazuri kabisa akiwa Hajj au hata anapokuwa nje ya Hajj kwani jambo hilo limekatazwa kuwa mwanamke asitoke nje akiwa amejipaka mafuta mazuri ili isiwe fitna kwa wanaume watakaosikia harufu nzuri kwake.
Mwanamke Kuvaa Soksi Na Glavu Akiwa Katika Ihraam
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Nini hukmu ya mwanamke kuvaa soksi na glavu akiwa katika Ihraam? Je, anaruhusiwa kuvua hizo anapokuwa katika ihraam?
JIBU:
Inapendekezeka mwanamke avae soksi au viatu. Ni bora kwake na bora kujifunika vizuri. Itatosheleza kama atavaa nguo pana (za kumfunika vizuri). Hakuna kipingamizi ikiwa atavaa soksi kisha akazivua, kama vile mwanaume anapovaa viatu kisha akavivua anapotaka hakuna ubaya kufanya hivyo. Lakini hairuhusiwi kwake kuvaa glavu kwani mwanamke amekatazwa kuvaa glavu katika ihraam. Vile vile hatakiwi kuvaa niqaab (kujifunika uso) au chochote kitakachomfunika uso kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza hivyo. Lakini mwanamke ateremshe utaji (ushungi) wake (ajifunike uso) anapokuwa mbele ya wasio Mahram wake. Na inafaa afanye hivyo anapofanya twawaaf na sa'y. 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: "Wapandaji (wanaume) walipita mbele yetu tukiwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Walipokuwa sambamba mbele yetu tuliteremsha utaji (shungi) zetu usoni na vichwani mwetu, kisha walipotoweka tulijifunua)) [Abu Daawuwd na Ibn Maajah]
Mwanamume anaruhusiwa kuvaa kanda mbili au viatu ikiwa havijakatwa. Hii ni rai sahihi. Kwa upande mwengine rai ya ‘Ulamaa wengi ni kwamba wavikate. Na rai iliyo sahihi ni kuwa haijawajibika kwake kuvikata ikiwa hakuweza kuvikata (Viatu). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alihutubia watu siku ya 'Arafah na akasema: ((Yeyote ambaye hakuweza kuvaa Izaar (nguo ya ihraam ya wanaume ambayo haikushonwa) basi avae suruwali. Na yeyote ambaye hakuweza kupata kanda mbilli (au viatu vya ngozi, au viatu vya makubadhi) basi avae viatu vya wazi)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwaamrisha wavikate viatu vyao hivyo, amri ya kukata imefutwa hapa.
WabiLLaahi At-Tawfiyq
[Fataawaa Muhimmah Tata'allaq bil-Hajji wal 'Umrah – Uk. 18, Fatwa Namba 6]
Inaruhusiwa Kubadilisha Ihraam Kwa Ajili Ya Kuikosha?
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Je, inaruhusiwa kubadilisha ihraam kwa ajili ya kuikosha?
JIBU:
Hakuna ubaya kuosha (nguo ya) ihraam au kubadilisha na kutumia nyingine ikiwa mpya au kukuu.
[Majmuw' al Fataawa Samaahat Shaykh ibn Baaz, Mjalada 6, Uk. 96, Fatwa Namba 45].
Wanawake Kuvaa Nguo Za Aina Nyingine Katika Ihraam
SWALI:
Je, mwanamke anaruhusiwa kuingia katika ihraam kwa kuvaa nguo yoyote apendayo?
JIBU:
Ndio, anaweza kuingia katika ihraam akavaa nguo yoyote apendayo. Hana haja kuvaa nguo hasa kwa ajili ya ihraam kama wanavyofanya baadhi yao na kudhania kuwa inapasa kuvaa nguo maalum. Lakini inampasa kuvaa nguo ambayo haivutii (isiyokuwa ina rangi nyingi za kupendeza au mapambo). Hii kwa sababu atachanganyika na wanaume kwa hiyo nguo zake zisiwe za kumvutia mtazamaji. Isiwe nzuri ya kupendeza lakini iwe ya kawaida na sio ya kuleta matamanio.
[Fataawa Al-Mar-ah]
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/265
[2] http://www.alhidaaya.com
[3] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9224&title=Fataawaa%3A%20Ihraam%20Na%20Talbiyah%20%20
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9225&title=01-Imaam%20Ibn%20Baaz%3A%20Akiwa%20Ndani%20Ya%20Ihraam%20Amechezea%20Nywele%20Kisha%20Zimeng%27oka
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9226&title=02-Imaam%20Ibn%20Baaz%3A%20Amenyoa%20Kwapa%20Akiwa%20Katika%20Hali%20Ya%20Ihraam
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9227&title=03-Imaam%20Ibn%20Baaz%3A%20Amesahau%20Kutamka%20Talbiyah%20katika%20Hajj%20ya%20Tamattu%27
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9228&title=04-Imaam%20Ibn%20Baaz%3A%20Kupaka%20Manukato%20Katika%20Ihraam
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9229&title=05-Imaam%20Ibn%20Baaz%3A%20Mwanamke%20Kuvaa%20Soksi%20Na%20Glavu%20Akiwa%20Katika%20Ihraam
[9] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9230&title=06-Imaam%20Ibn%20Baaz%3A%20%20Inaruhusiwa%20Kubadilisha%20Ihraam%20Kwa%20Ajili%20Ya%20Kuikosha%3F
[10] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9231&title=07-Fatwa%3A%20Wanawake%20Kuvaa%20Nguo%20Za%20Aina%20Nyingine%20Katika%20Ihraam