Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

 

Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

Husayn Al-‘Awayishah

 

Kimetarjumiwa Na: Alhidaaya.com

 

 

 

 

Share

01-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Yaliyomo

 

Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

YALIYOMO

 

Jedwali Unukuzi……………………………………………………………………………………

Utangulizi……………………………………………………………………………………………..

Baada Ya Kifo Cha Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)…………………………………………………………………………………………………

Thamani Ya Nasaha Za Mwisho………………………………..………………………..

Nawamuru Kumcha Allah………………….……………………………………….………

Marekebisho Ni Yapi?.................................................................

Si Rukhusa Kutegemea Qur-aan Pekee Na Kuacha Sunnah…………....

Yeyote Anayechukua Kutoka Kwa Maswahaba Bila Shaka Amechukua

Kutoka Kwenye Qur-aan……………………………….…………………………….……..

Ni Sunnah Moja (Njia) Au Mbili?..................................................

Kuna Wakati Waislamu Kutofautiana Juu Ya Mambo Mengi

Msimamo Wetu Kuhusu Bid’ah Uwe Upi?......................................

Kila Bida’h Ni Upotevu…………………………………….………………………………….

Kukanusha Wale Wanaoigawa Bid’ah Kwenye Makundi Mawili –

Bid’ah Nzuri Na Mbaya…………………………….………………………………………….

Hatari Ya Bid’ah (Uzushi)………………………..………………………………………….

Katika Amri Yake Ya Mwisho, Mtume (Swalla Allaahu

‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Alitukataza Kufanya Jambo Moja Tu: Bid’ah………………………………………....................................................

Hitimisho……………………………………………………………..………………………………

 

 

Share

02-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Utangulizi

 

 

Utangulizi

 

Kwa hakika shukrani zote zinamstahiki Allaah; tunamtukuza Yeye, tunamwomba msamaha Yeye, na tunatafuta maghfira kwake na msaada. Tunakimbilia kwa Allaah atuhifadhi na uovu wa nafsi zetu na amali zetu mbaya. Yeyote aliyeongozwa na Allaah, hapana awezaye kumpotosha; na yeyote anayepotezwa na Allaah hapana awezaye kumwongoza. Nanakiri ya kwamba hapana mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah pekee, na Yeye hana mshirika; na nakiri ya kwamba Mtume wetu Muhammad ni mtumwa Wake na Mjumbe wake.

Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu.(3:102)

 

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu Aliyekuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni.” (4:1)

 

Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya sawasawa. 

 

Apate kukutengenezeeni vitendo vyenu na Akusameheni madhambi yenu. Na anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, bila ya shaka amefanikiwa mafanikio makubwa.” (33:70-71.)

 

Kwa uhakika, maneno ya ukweli zaidi ni Kitabu cha Allaah, na mwongozo mzuri ni ule wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Uovu wa mambo ni yale yaliyozushwa (katika Dini), kwani kwa kila jipya linalozushwa ni bida’h, na kila uzushi ni upotevu, na kila upotevu ni kuingizwa Motoni.

 

Katika miaka ya hivi karibuni Waislamu waaminifu, wamekagua hali ya Taifa letu, na walichogundua ni athari za mafanikio ya Shaytwaan, wa amali mbovu, na damu ya majeraha mengi. Waliona kutokupatana, kutokuelewana, mfarakano, mkanganyiko, na wasiwasi. Walipata matokeo mabaya kwa kutokuhukumu kwa mujibu wa Kitabu cha Allaah, majumbani, sokoni au katika jamii. Waliona matokeo haya mashuleni, vyuo vikuu, vitabuni, magazetini, na vyombo vya habari; kwa uhakika, wanayashuhudia hata katika sehemu ‘adhimu, Misikitini ambapo uzushi unashamiri. Na pia wameona athari za uovu miongoni mwa viongozi wa da’wah (walinganiaji katikaUislamu) na wasomi.

 

Wale wanaojitahidi kufanya amali njema, wanashindana kutafuta tiba kwa Taifa letu na masikitiko yake. Madawa au tiba ya kila kitu yanayotolewa ni mengi, lakini hali haibadiliki – isipokuwa katika maeneo fulani, ambapo juhudi zisizoratibiwa zimefanywa, lakini hazitoshi kufanya mabadiliko kwa ujumla.

 

Iwapo tunataka tiba ya dunia nzima kwa matatizo yetu, lazima tutalii mwongozo wa mwisho uliotolewa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Maswahaba zake na Taifa lake - ambao umeelezewa na Al-Irbaad bin Saariyah (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa khutbah ambayo ilisababisha mioyo ya Maswahaba kutetema na macho kububujika machozi. Kisha, akawapa usia wa mwisho.

 

Nasaha zinaihusu enzi yetu kama ilivyokuwa kwa enzi zote; ni nasaha zinazofaa kwa wakati wa kutopatana na migongano,  wakati  ambao Waislamu wamegawika katika makundi  na vyama; kwa kila kikundi kikisema, “sisi  tuko sahihi na katika yale yaliyo sahihi, na ni wengine ndio waliokwenda kombo.”

 

Kila mmoja anajaribu kuonesha tahadhari zake kwa Waislamu, akijaribu kuwashawishi wajiunge na kundi lake na wajitenge na makundi mengine au vyama. Kila mmoja kwa uwazi au kujitokeza, analaumu wengine kwa kutokuwa na ufahamu kamili wa Uislamu, kwa kutowaalika wengine katika njia inayomridhia Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Tunaishi katika zama ambazo kila mmoja wetu anahitaji sana kutafakari juu ya nasaha za mwisho za Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Hitajio hilo ndilo lililo nichochea kuandika kitabu hiki kidogo, kwa matarajio ya kupokewa na masikio yanayosikia kwa kuridhia, mioyo inayomcha Mola wao, na nafsi zinazoitikia wito wa kufuata haki.

 

Namwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) azifanye juhudi za kuifanya kazi hii ni ya uaminifu Kwake, na sio kwa jambo jingine lolote. Namwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) auauni Ummah wa Kiislamu kupitia kwangu, kunifanya ufunguo wa wema, na kufuli ya kuzuia maovu. Kwa hakika, Yeye (Subhaanahu wa Ta’ala) ni muweza wa kila kitu.

 

Husayn Bin ‘Awdah al–‘Awayishah

 

Share

03-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Baada Ya Kufariki Dunia

 

Baada Ya Kufariki Dunia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifariki dunia: macho yalibubujika machozi, mioyo ilihuzunika, ulimwengu uliingia kiza, na waumini wakijilaumu wenyewe kwa mabadiliko yatakayotokea baadaye. Mwalimu aliyekuwa kipenzi cha waumini wote na aliyekuwa rehema kwao, alifariki dunia. Mtu anapompoteza aliyekuwa kipenzi na anayeheshimiwa sana, moyo wake unajaa kumbukumbu; alikuwa akikaa pale; alikuwa akisimama pale; alikuwa akisema na kufanya kadha, na kadha.

 

Watu wanapompoteza wampendaye, kwa kawaida hutafakari na kukumbukia maneno na misemo aliyoitamka. Na kama aliyekufa alichukuliwa kama kiigizo, wanakumbuka nasaha zake, hususa nasaha za mwisho, wakikazana kwa moyo wao wote kuzitekeleza. Wanarejea maneno yake na kuyapa uhai mpya kwa utendaji.

 

Kama mioyo yenu ilijeruhiwa na kifo cha Mtume wenu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi jibidiisheni kutekeleza nasaha zake za mwisho. Irbaad bin Saariyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisimulia;

 

“Mjumbe wa Alah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa khutbah yenye umbuji na hekima, khutbah ambayo ilisababisha macho kububujika machozi na mioyo kutetema. Tulisema, “Ewe Mjumbe wa Allaah! Inakuwa kama kkhutbah ya kuaga! Yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Muogopeni Allaah, na lazima msikilize na muwatii (walio katika mamlaka), hata kama mtumwa wa Kihabeshi atafanywa kiongozi wenu. Yeyote atakayeishi baada yangu ataona migogoro; hivyo kilichopo juu yenu ni Sunnah zangu na Sunnah za Khalifah walioongozwa baada yangu; zuiweni (yaani Sunnah zangu….) kwa magego yenu.[1] Na jihadharini na muwe mbali na mambo yaliyo zaliwa, kwani kila uzushi ni upotevu”.[2]

 

Tulisema, “Ewe Mjumbe wa Allaah! Hii ni kama khutbah ya kuaga! (ya mwisho)  sasa unatuagiza nini?

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Nimewaachieni ushahidi uliowazi, ambao usiku wake ni sawa na mchana wake. Hapana aendaye kombo baada yangu isipokuwa yule aliyekhasirika.

 

Yeyote atakayeishi baada yangu ataona migongano mingi; na juu yenu ni yale myajuayo kutokana na Sunnah yangu na Sunnah ya Khalifah waongofu: Iumeni (yaani Sunnah yangu….) kwa magego yenu. Mnawajibika kumtii mtumwa wa Kihabeshi. Kwa hakika, muumini ni sawa na ngamia Anif (ngamia aliyewekewa mbao katika pua yake, kutokana na kuhisi maumivu, anamtii mpandaji) popote anapoelekezwa, anakwenda.”[3]

 



[1] Maana yake: Shikamana na Sunnah yangu na ning’inia kwayo, kama vile mtu anayening’inia katika kitu kwa meno yake hufanya kwa magego, alichelea kitu kile kitamponyoka.

[2] Ilisimuliwa na Abu Daawuud ndani ya Swahiyh Abu Daawuud (3851), na At-Tirmidhiy ndani ya Swahiyh Sunnan At-Tirmidhiy (2157); na Ibn Maajah ndani ya Swahiyh Sunnah Bin-Majah (40) vile vile wengine. Rejea Swahiyh At-Targhiyb Wat-Tarhiyb (Uk.24) na Kitaab As-Sunnah (54) cha Bin Abu Asim, kilichopitiwa upya na Shaykh Al-Albaaniy-Allaah Amrehemu.  Katika masimulizi ya An-Nasaaiy na Al-Bayhaqiy katika Al-Asma Was-Swifaat kuna yafuatayo: ‘Na kila upotevu ni Motoni.” Na nyongeza hiyo imo katika Silsilah Swahiyhah, kama katika Al-Ajwibah An-Nafi’ah (Uk.545) na Iswlahul-Masaajid (Uk. 11.)

[3] Swahiyh Sunan Bin Maajah (41).

 

 

Share

04-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Thamani Ya Nasaha Za Mwisho

 

Thamani Ya Nasaha Za Mwisho

 

Tafakari hisia za mama mwenye moyo laini anaposema buriani kwa mwanaye mpenzi au msisimko wa baba kipenzi anapofarakana na mtoto wake kipenzi na ujue ya kwamba kuachana tunako kuzungumza hapa ni kukubwa na kunatia uchungu.

 

Kwa hakika Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema buriani kwa Maswahaba zake na kwa Taifa lake. Ni maelezo gani ya ibada aliyowambia? Je, aliwafafanulia hukumu za Shariah ya Kiislamu? Je, aliwafundisha mambo yenye uhusiano na imani, ambayo hakuwahi kuyataja kabla? Au aliwafundisha kanuni mpya zinazohusiana na mwenendo wa Kiislamu? Hali ilihusu jambo jingine, kwani Dini na “rehema” zilikamilika; kwa hiyo nasaha hizi zilikuwa kamilifu na hakuwahi kuzitoa – kama utapenda, mama wa nasaha. Inatakiwa kujumuisha mazuri yote na mema, na kuonya juu ya maovu yote.

 

Nasaha za mwisho zina kupa Uislamu, imani, na ihsani kwa ukamilifu, zinakutoa kwenye mkanganyiko na shauku na zinakuongoza kwenye mwongozo ulio sahihi.

 

Si ajabu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa uwezo wa kuelezea mambo mengi kwa maneno machache. Enyi wasaka mema: tunyweni kutoka chemchemi safi, haya ni maneno yake:

“Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa khutbah yenye ufasaha,” ambayo ilikuwa ni majibu kwa amri ya Allaah.

“…uwape mawaidha na uwaambie maneno ya kuathiri na kuingia katika nafsi zao.” (4:63).

 

Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. …. (16:125).

 

Mwandishi wa Jamii al-‘Ulum-wal-Hikam alisema ya kuwa mlinganiaji kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) lazima awe mbuji, kwani watu wako tayari (wamezoea) kupokea ujumbe unapowasilishwa kwa ufasaha.

 

Katika lugha ya Kiarabu, balaghah (umbuji) maana yake kufikisha maana iliyo kusudiwa kwenye mioyo ya wasikilizaji katika njia nzuri, kwa kutumia maneno muafaka na suala husika; maneno yenye mvuto kwa wasikilizaji na kupenya ndani ya moyo. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakurefusha khutbah zake; bali alizifupisha, hata hivyo yenye maana ya kina.

 

Jaabir Bin Samurah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisimulia, “Nilikuwa nikiswali na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swalah yake ilikuwa ya kati na kati (yaani, haikuwa ndefu au fupi) na khutbah yake ilikuwa vivyo hivyo (haikuwa ndefu au fupi)”[1]

 

Katika hadithi nyingine, Abu Wail alisema, “Ammar alitoa khutbah iliyo kuwa fupi lakini yenye kina. Aliposhuka kwenye mimbari, tulisema, “Ewe Abu al-Yaqdhan! Ulisema mengi kwa kutumia maneno machache; bora ungepumua (ungerefusha khutbah yako). Aliwajibu kwa kusema, “Kwa hakika, Nilimsikia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema,

 

‘Kwa uhakika, mtu kurefusha Swalah na kufupisha khutbah ni dalili za kuelewa (Fiqh); kwa hiyo refusheni Swalah na fupisheni Khutbah, na bila shaka kuna ‘uchawi’ katika baadhi ya khutbah.”[2] 

 

Wakati mmoja mtu alisimama na akatoa khutbah ndefu, ‘Amr Bin Al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema, “Kama angetoa khutbah ya kiasi, ingelikuwa bora kwake. Nilimsikia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema,

 

“Niliona ya kuwa –au niliamrishwa – kutoa khutbah fupi kwa uhakika, ufupisho ni mzuri.”[3].

 

Leo hapa tulipo tuna khutbah iliyoandikwa sana kwa madoido, lakini  hali yetu iko vipi? Na hadhi yetu ikoje miongoni mwa mataifa? Tunaishi katika zama za wasemaji wengi, Wanachuoni wachache, wakati tuna maneno mengi na vitendo vichache.

 

“….Inayosababisha macho kutoa machozi na mioyo kutetema.”  Machozi na kutetema kunaashira kiwango cha juu cha Iman.

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi" (8:2)

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

“Na wanaposikia yaliyoteremshwa kwa Mtume utaona macho yao yanachururika machozi kwa sababu ya Haki waliyo itambua. Wanasema: Mola wetu! Tumeamini. Basi tuandike pamoja na wanao shuhudia.” (5:83).

 

Hii ndio sabili ya wachaji na waumini wa kweli;

“Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidisha unyenyekevu.” (17:109).

 

Hiyo ndio mioyo ya wale walionufaika na nasaha na mawaidha:

wanajua na kutumia, ni wa kweli katika imani zao, na wanatubia kwa Mola wao.

 

Kutokana na unyeti wake, uchaji wao, unyenyekevu wao, na machozi yao, wao wenyewe wanaomba nasaha, wakisema,

“Hii ni kama khutbah ya kuaga, hivyo tunasihi.”

Walihisi kuwa mtu aliyependwa zaidi na watu alikuwa akiwapa mkono wa buriani, ambalo si jambo la kushangaza, kwani walikuwa viongozi wa Fuqaha na wanazuoni walio wafuatia. Hawakuridhika kwa kile walichokijua kutokana na khutbah zilizopita au hukumu: walitaka ziada, kwani hawakuridhika na kutafuta elimu. Hata hivyo maonyo waliyo yasikia kabla, walitaraji kupata nasaha zilizotimia, ambazo wengeweza kuzitumia kuboresha amali zao na kushikamana na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).



[1] Muslim (866)

[2] Muslim (869)

[3] Ilisimuliwa na Abu Daawuud katika Swahiyh Sunan Abi Daawuud.

 

Share

05-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): "Nawaamuru Kumcha Allaah"

 

“Nawaamuru  Kumcha Allaah”

 

Tiini amri za Allaah na mjiepushe na makatazo yake. Jueni ya kuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta’ala) Anajua yote myatendayo, yote ya dhahiri na mliyofanya kwa siri.

Msiruhusu utashi uwaongoze, kwani ni sababu ya uovu na kuingizwa katika moto wa Jahanamu. Jitakaseni. Jiepusheni na Moto wa Jahanamu kwa kufanya amali njema.

 

Kama dunia ina kushawishi na uzuri na vivutio vilivyo haramishwa, na dhahabu yake inayomeremeta, au na starehe zinazopotosha, kumbuka maneno ya Mtume, “Nawaamuru mumche Allaah.” Iwapo unataka kuokolewa na mitihani na misiba, na kama unataka uruzukiwe na riziki ya halali, mche Allaah.

 

“….Na anayemcha Allaah Humtengezea njia ya kutokea.   

Na Humruzuku kwa jiha asiyotazamia. ….” (65: 2-3).

 

Kama unataka kuokolewa kutokana na shida na kama unataka mambo yako yawe sahali, mche Allaah:

“… Na anayemcha Allaah, Allaah Humfanyia mambo yake kuwa mepesi.” (65: 4).

 

Kama unataka kujifunza njia ya ufanisi na uchaji, mche Allaah.

“… Na mcheni Allaah. Na Allaah ni Mjuzi wa kila kitu. (2: 282).

 

Enyi Waislamu, kama mnatamani kutawala na kuongoza, na kama mnataka kuwa vinara katika nyanja zote na utawala, “mcheni Allaah”.

Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao Aliyowapendelea, na Atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na wataokufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu. (24: 55).

 

Kama unatamani kuwa mtu anayeheshimiwa sana na watu, basi mche Allaah:

“…Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allaah ni huyo aliye mcha Mungu zaidi katika nyinyi...” (49: 13).

 

Sio ya kuchosha na ufukara na makosa ya jinai yanayotishia mfumo wa jamii kutokana na matokeo ya kiwango cha chini cha Taqwa (uchaji, wema, na kumcha Allaah)?

 

Kumcha Allaah kuna kuhitajia kuuridhia ukweli, hata kama utatoka kwa mtu aliye chini yako kiukoo, jinsia, hadhi au umri.

“Nikuamuru kumcha Allaah” ni maneno yaliyotimia ambayo ni mwafaka kwa kila zama na mahali; mwafaka kwa wanaume na wanawake, kwa matajiri na masikini, kwa weupe na weusi; mwafaka kwa wote, mchungaji na wachungwao.

 

Kwa maneno haya – “Nakuamuru kumcha Allaah” –mtu binafsi, jamii na taifa lote linaweza kufikia ufanifu, lakini wanapotenda kwa mujibu wa kidokezi.

 

“Mche Allaah, na lazima uwasikilize na kuwatii (walio madarakani)  hata kama ni mtumwa kwa Kihebeshi anafanywa kiongozi wako.” Haya ni sawa na kauli,

 

“Sikiliza  na utii, hata kama ni mtumwa wa Kihabeshi, kichwa chake ni kama zabibu kavu, anakuwa mtawala wako.”[1].

 

Katika Hadiyth nyingine,

 

“Yeyote atakayeona kiongozi wake anafanya jambo asilolipenda, basi awe na subira kwani yeyote anayeacha jama’ah kwa pima au shubiri kisha akafa, anakufa kifo cha jahiliya.”[2].

 

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia alisema,

 

“Kusikiliza na kutii ni wajibu kwa Muislamu, kwa avipendavyo na avichukiavyo, madhali hakuamrishwa kufanya dhambi. Iwapo ataamrishwa kutenda dhambi, basi asisikilize wala kutii.”[3].

 

Taifa au rangi au sura ya nje, isikuzuie kuukubali ukweli, kwenda kinyume na msingi huu unakupeleka kwenye majaribio/mtihani mgumu na makinzano.

 

“Yeyote atakayeishi baada yangu ataona migogoro mikubwa” Hapa ndipo tulipo, tunaishi katika zama za mikinzano na kutokubaliana – kutokubaliana katika imani, Fiqh, siasa, lakini inasikitisha sana katika mioyo yetu. Lilikuwa kundi moja na jamii moja, sasa tuna makundi chungu nzima, na kila moja linalingania misingi yake yenyewe.

 

Vipi wingi wa vitabu kwenye safu za maktaba, bado kuna tofauti nyingi za rai katika vitabu hivyo: Waislamu hawajui lipi la kulikubali na lipi na kulikataa! Na litalovunja moyo zaidi ni kuwa tofauti na migongano inapelekea kuangamiza taifa:

 

“...wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu…” (8: 46).

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

 

“Msitofautiane, kwani waliokuja kabla yenu walitofuatiana wao kwa wao, na kisha waliangamizwa.” [4]

 

Mataifa tofauti ya dunia hayajaungana dhidi yetu kwa sababu eti idadi yetu ni ndogo, kwani idadi yetu sio ndogo. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

 

“Mataifa karibu yatajiunga juu yenu (walialikana ili kuwaua na kuwapora ardhi yenu) kama watu wanaoitana kwa ajili ya chakula kwenye Qis’ah yao (sinia la watu kumi).” Mtu mmoja alisema, “Wakati huo tutakuwa wachache?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijibu, “Bali, mtakuwa wengi wakati huo, lakini mtakuwa kama povu la mafuriko (yaani – mapovu na uchafu wote yatakoyachukua. Na Allaah Ataondoa katika vifua vya maadui zenu chuki waliyonayo dhidi yenu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ataingiza katika mioyo yenu Wahn (udhaifu). “Muulizaji aliuliza, “Ewe Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni nini Wahn? “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Kupenda dunia na kuchukia kifo.”[5]

 

‘….Tutaona mapambano zaidi.” Kwa nini migongano mingi?  Kwa sababu watu watategemea mifumo na shari’ah zilizotungwa na binaadamu, na huku wakitelekeza yaliyoteremshwa kutoka kwa Mola (Subhaanahu wa Ta’ala). Watayapa kipaumbele yaliyosemwa na Zayd na ’Amr juu ya ya yale yaliyosemwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),

“…Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Allaah bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi.” (4: 82).

 

Sababu migongano tuliyo wadhukuru hapo juu ni kuacha mafunzo ya Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume. Chochote kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni sababu ya umoja na utulivu, lakini kinachokuja kutoka kwa asiye kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni sababu/chanzo cha mfarakano na ugomvi.

 

 

 



[1] Al-Bukhaariy (7142).

[2] Al-Bukhaariy (7143).

[3] Ilisimuliwa na Al-Bukhaariy (7144); mtu anaweza kutumia mapokezi ya Hadiyth hizi na kutolea hoja  kuwa mtu anaweza kuwa kwenye kundi moja, lakini si Swahiyh kwani huongeza tofauti kati ya Waislamu. Tunaomba mwongozo wa Allaah.

[4] Al-Bukhaariy (24:10)

[5] Ilisimuliwa na Abu Daawuud na wengine, imo katika al-Swahiyhah (958).

Share

06-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Marekebisho Ni Yapi?

 

Marekebisho ni Yapi?

 

”Kisha shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifah wema baada yangu: iumeni (ing’ateni) (yaani Sunnah yangu…) kwa magego yenu.”

 

“Kisha shikamaneni na Sunnah zangu”. Shikamaneni na njia yangu, kwani mwanga, ponyo na rehema; inafafanua Qur-aan na inachota kutoka chemchem yake. Inakuwaje anayepokea kutoka katika Qur-aan na Sunnah kwenda kombo ambapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema;

 

“Nimekuachieni mambo mawili; mkishikamana nayo hamtapotea. Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”[1]

 

IliHadiythwa ya kuwa Abu Al-‘Aaliyah alisema, “Ni jukumu lenu kufuata yaliyokuwepo mwanzoni, kabla hawakufarakana.

 

“Kisha mfuate Sunnah yangu.” Lakini  tutajuaje Sunnah yake ni ipi? Njia sahihi ya kuthibitisha lazima ifuatwe na kuhakikisha uhalisi wa Ahaadiyth, na kwa kuwa Wanachuoni wa Hadiyth walifuata njia hiyo, lazima tuwafuate. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

 

 “Litaendelea kuwepo kundi lililoshinda juu ya ukweli katika Ummah wangu; hawadhuriwi na wale walioacha ukweli, mpaka amri ya Allaah itakapokuja (yaani, karibu na Siku ya Qiyaamah, wakati Yeye (Subhaanahu wa Ta’ala) atachukua roho ya kila Muumini mwanaume na mwanamke) nao wakiwa katika hali hiyo.”[2]

 

Kundi la Wanachuoni wanasema kundi hilo ni watu wa Hadiyth. Shaykh wetu, Al-Albaaniy (Allaah Amuwie radhi) anawataja wote wenye rai hii katika As-Silsilah as-Swahiyhah (1/541); nao ni:-

1.     ’Abdullaah bin Al-Mubaarak, aliyeizungumzia Hadiyth iliyopita. “Kwa maoni yangu, hao ni watu wa Hadiyth.”

2.     ’Aliy bin Al-Madini. Muhammad bin Ismaa’iyl Al-Bukhaariy alisimulia kuwa ‘Aliy bin Al-Madini alisema,

“Wao na watu wa Hadiyth.”

3.     Ahmad bin Hanbal, alipoulizwa kuhusu maana ya Hadiyth tajwa, alisema, “Iwapo watu wa Hadiyth sio kundi lililofuzu, basi siwajui ni nani.”

4.     Ahmad bin Sinaan At-thiqah Al-Hafidh alisema,

“Ni watu wa elimu na watu wa Hadiyth.”

5.     Muhammad bin Ismaa’iyl Al-Bukhaariy. Wakati Hadiyth tajwa iliposomwa, alisema, “Hii inawarejea watu wa Hadiyth“

 

Katika Sahihi yake, alipokuwa akiitolea maelezo Hadiyth, Al-Bukhaariy alisema, “Na wao ni watu wa elimu.” Hii haikinzani na usemi wake mwingine, kuwa watu wa elimu ni watu wa Hadiyth. Jinsi mtu anapokuwa na maarifa ya Hadiyth anakuwa bora zaidi kuliko yule mwenye maarifa kidogo katika Hadiyth. Katika kitabu chake Khalq–Af’aal Al-‘Ibaad, Al-Bukhaariy anataja Aayah hii,

“Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu…” ( 2:143).

 

Alipokuwa akijadili Aayah hii, kisha alisema, “Ni kundi ambalo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilitaja…” Na kisha alitaja Hadiyth tuliyokuwa tunaijadili hapa.

 

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliachia ummah wake nuru na mwongozo. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

“Kwa uhakika, nimekuachieni weupe unaofanana yaani, juu ya angavu, wazi, ukweli usiopingika. Usiku mweupe ni ule ambao mwezi unaonekana kuanzia mwanzo mpaka mwisho, mchana wake ni usiku wake; hapana anayekenguka kutokana nao isipokuwa yule aliyeangamizwa.”[3]

 

Inaelekea ya kuwa haya ni maelezo ya Aayah ifuatayo:

“Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyonyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya Amekuusieni ili mpate kumcha Mungu.” (6: 153).

 

 

Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema,

 

“Tulikuwa tumekaa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipochora mstari mbele yake na kusema, “Hii ni njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).” Kisha alichora mstari kuliani kwake, na mstari kushotoni kwake, na kusema, “Hizi ni njia za Shaytwaani. Kisha aliweka kiganja chake juu ya mstari wa katikati, alisoma:

 

“Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyonyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya Amekuusieni ili mpate kumcha Mungu.” (6: 153).[4]

 

“Kisha juu yenu ni Sunnah yangu.” Hakusema: Namfuate njia ya Shaykh fulani au Mwanachuoni au mwalimu, kwa hivyo jihadharini na ushabiki wa kuwafuata waliotangulia, bali tuchukue yale wanayotufundisha kutokana na Sunnah na ukweli.

 

“Na Sunnah za Makhalifah waongofu.” Lazima tuelewe Sunnah kama walivyozielewa Makhalifah waongofu, kwani wao walikuwa karibu na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mioyo safi, imani thibiti, wakifanya amali njema, na wakishikamana na njia ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Waliyaona mambo kwa macho yao wenyewe, ambapo sisi tunasimuliwa habari zake: “Na kusikia habari si sawa na kujionea kwa macho yako.”[5]

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaelezea ya kuwa waliongozwa vema, tunamjua yeyote baada ya Maswahaba wa Mtume mwenye sifa sawa, ili tumfuate?

 

 



[1] Ilisimuliwa na Maalik na Silsila yake ni Mursal, na Al-Haakim kutoka Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa Silsila ya Hasan, kama Shaykh Wetu (Al-Albaaniy)- Allaah Amuwie radhi – alisema katika At-Tawassul Anwa’uhu Wa-Ahkaamuhu (uk.13). (Angalia Tawassul Aina Zake & Hukumu Zake cha Shaykh Al-Albaaniy, Uk. 7.) Ilipigwa chapa na Al-Hildaayah Publishing & Distribution, UK)

[2] Ilisimuliwa na Muslim (1920) na wengineo.

[3] Usahihi wake kwa Silsila nyingi na masimulizi yaliyothibitisha, kama ilivyotajwa katika Kitabus–Sunnah, cha Bin Abi ‘Aaswim (47,48,49).

[4] Imethibitishwa na Hadiyth nyingine, rejea, kitabu As-Sunnah cha Abu ‘Aaswim (16,17).

[5] Ilisimuliwa na Ahmad, at-Twabaraaniy, al-Khaatwib na wengineo, ikiwa na Silsilah Swahiyh, kama ilivyotajwa katika Takhrij al-‘Aqiydah at-Twahaawiyyah (401)

Share

07-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Si Ruhusa Kutegemea Qur-aan Pekee Na Kuacha Sunnah

 

 

Si Ruhusa Kutegemea Qur-aan Pekee Na Kuacha Sunnah

 

Ni kosa kubwa kabisa kufuata Qur-aan peke yake bila kufuata Sunnah. Tunaona madhehebu nyingi zilizo kengeuka zinadai kufuata Qur-aan, madhehebu ambazo zinategemea zaidi upotoshaji na kudhihirisha ufafanuzi usio sahihi.

 

Je, Swalah, Zakaah au Hajj vimeelezewa kwa urefu ndani ya Qur-aan? (kwa hakika jibu ni hapana); kwa hiyo lazima tuelewe Qur-aan kwa kupitia mwanga wa Sunnah ya Mtume [1].

 

Muislamu lazima atambue ya kuwa maamrisho na makatazo ya mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni lazima kufuatwa, kama ilivyo maamrisho na makatazo ya Allaah ni lazima kufuatwa.

 

“Al-Muqdam Bin Ma’ad Yakrib (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisimulia ya kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

“Ina yumkinika ya kuwa Hadiyth inamfikia mtu kutoka kwangu wakati anaegemea Arikah yake (mto au godoro au kochi) na akasema, “Kati yetu na nyie ni Kitabu cha Allaah; chochote tutakacho kikuta ni halali, tutakichukulia kuwa ni  halali – Na chochote tutakacho kikuta kuwa haramu, tutakifanya haramu kwa hakika alichokikataza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni sawa na Alichokataza Allaah,”[2]

 

Hii inatukumbusha mdahalo uliofanyika kati ya ‘Abdullaah Bin Mas’ud (Radhiya Allaahu ‘anhu) na Ummu Ya’aquub.

 

‘Alqamah alisimulia, ‘Abdullaah alimlaani Al-Waashimah– (wale wanaochoma miili/ngozi zao kwa sindano (tattoo), na sehemu ile wakatia ‘kohl’ au rangi ya buluu ili kuifanya ngozi ionekane buluu au kijani), al-Mutanammiswaat (wale wanaowataka wenzao waondoe au kunyoa nywele katika nyuso zao [nyusi]) na al-Mutafallijaat (wale wanaomtaka mtu atengeneze mwanya kati ya meno yao mawili ya mbele au kufanya wenyewe), wanaofanya kwa urembo, kubadilisha maumbile ya Allaah. Ummu Ya’aquub alisema, “Nini hiki? ‘Abdullaah alijibu, “Kwa nini nisimlaani yule aliyelaaniwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na yule aliyelaaniwa ndani ya Kitabu cha Allaah! (Ummu Ya’aquub) Alisema, “WAllaah nimesoma yaliyoandikwa (yaani, mbele na nyuma ya Qur-aan (mwanzo hadi mwisho)) na sijayaona hayo.” Yeye (‘Abdullaah bin Mas’uud) akasema, “WaLlaahi, kama umesoma, ungelikuta hili.

Na anachokupeni Mtume chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho. …. (59: 7).

 

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwalaani watu tuliowataja hapo juu; Mola wetu (Subhaanahu wa Ta’ala) Alituamrisha tumfuate Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa hiyo anachotupa tukipokee; anachotukataza, tujiweke mbali nacho, na yeyote anayemlaani, tumlaani. Kwa hiyo chimbuko la wale watu chimbuko lake ni Kitabu cha Allaah.

 

Tunajifunza ya kuwa kufuata amri za Mtume ni kufuata amri za Qur-aan, ambapo kujiweka mbali na mambo aliyoyakataza ina maana kujiweka mbali na mambo yaliyokatazwa na Qur-aan. Chochote alichokataza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kina uzito sawa na Alichokataza Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na alichoruhusu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kina uzito sawa na Alichoruhusu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Na kwa ajili hiyo hatutakiwa kutofautisha kati ya Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume.

 

 

 



[1] Shaykh wetu –Al-Albaaniy (Allaah Amuwie radhi) – aliandika makala muhimu kuhusu mada inayoitwa, “Manzilat as–Sunnah Fil-Islaam Wa-bayaan Annahu La Yastaghna ‘Anha bil–Qur-aan.”

[2] Ilisimuliwa na At-Tirmidhiy na imo katika, Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy, na Ibn Majaah, Swahiyh ibni Maajah, (12) pia Ad-Daarimiy na wengineo.

Share

08-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Yeyote Anayechukua Kutoka Kwa Maswahaba Bila Shaka Amechukua Kutoka Kwenye Qur-aan

 

Yeyote Anayechukua Kutoka Kwa Maswahaba Bila Shaka Amechukua Kutoka Kwenye Qur-aan

 

Maswahaba wa Mtume walijifunza kutoka kwa makhalifah wanne –Allaah Awawie radhi wote. Kwa vizazi mbalimbali, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alitoa ushahidi wa Iymaan yao na Alituonya tusifuate njia nyingine isipokuwa njia yao. Yeye (Subhaanahu wa Ta’ala) anasema

“Na anayempinga Mtume baada ya kumdhihirikia uongofu, na akafuata njia isiyokuwa ya Waumini, tutamuelekeza alikoelekea, na tutamuingiza katika Jahannamu. Na hayo ni marejeo maovu.” (4: 115).

 

Na katika Hadiyth:

 

“Kwa hakika watu waliokuwepo kabla yenu miongoni mwa watu na kitabu waligawika makundi (madhehebu) sabini na mawili, na bila shaka wafuasi wa dini hii watagawika katika madhehebu sabini na tatu, sabini na mbili wataingizwa Motoni, ambapo moja litakuwa Peponi: nalo ni Jama’ah.”[1]

 

Katika Hadiyth nyingine, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilielezea kundi lililookolewa kama ifuatavyo:

“Ni lile ambalo Mimi na Maswahaba wangu tumo.”[2]

 

Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alisimulia yafuatayo:

“Msiwalaani Maswahaba wa Muhammad; kwani kisimamo cha mmoja wao kwa saa moja ni bora kuliko ‘amali iliyofanywa na mmoja wenu katika maisha yake.”[3]

 

Mpaka hapo tulipofika lazima tubaini muunganiko: Maswahaba walipokea kutoka kwa Makhalifah waongofu (na kutoka kwenye Sunnah), waliofuata Sunnah, na kama tulivyoona kabla, kufuata Sunnah ni kufuata Qur-aan Takatifu. Kwa hiyo, kupitia kiungo hiki, tunaweza kuhitimisha ya kuwa Yeyote aliyechukua kutoka kwa Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) amechukua kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala); na yeyote anayekataa njia ya Maswahaba kwa hakika amekana Kitabu cha Allaah, ukweli unaoonyesha upotovu na kukinzana kwa wale waliowatangaza Maswahaba- ukiacha watatu miongoni mwao - kuwa ni makafiri (na tunaomba hifadhi ya Allaah!).

 

Wale wanaowaita Maswahaba makafiri, wao ndio wasioamini Qur-aan na Sunnah, na wameachwa bila vigezo sahihi vya kuendesha maisha yao. Wale wasio katika njia sahihi wamepotoka kwa sababu hawashikamani na njia ya watangulizi wema; badala yake wanafuata akili zao kuifahamu Qur-aan na Sunnah. Na kwa sababu hiyo mapote na fikra na madhehebu yamekuwa mengi, na kila moja likisema, “Tunafuata Qur-aan na Sunnah”, Kwa bahati mbaya si wa kweli katika madai yao.

 

 



[1] Ilisimuliwa na Abu Daawuud, Ad-Daarimiy, Ahmad na wengine –Rejea, As-Swahiyhah (204).

[2] Silsilah yake ni Hasan na masimulizi mengine yanathibitisha kwayo, hukmu yake imetajwa ndani ya As-Swahiyhah (203, 204).

[3] Ilisimuliwa na Ibn Abi ‘Aaswim katika Kitabus-Sunnah, wasimulizi katika Silsilah ni waaminifu, wengine zaidi ya Naaswir Bin Dhu’luq, ni wasimulizi wa Al-Bukhaariy na Muslim. Na maimamu wengi wamemtangaza Naaswir kuwa mwaminifu, bila kutaja ya kuwa wapokezi wengi waaminifu walipokea kutoka kwake. Shaykh wetu Al-Albaaniy – Allaah Amrehemu, ametaja hili katika kitabu kilichotajwa (Hadiyth Na. 1006).

Share

09-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Ni Sunnah Moja Au Mbili?

 

Ni Sunnah Moja (Njia) Au Mbili?

 

Ni Sunnah moja, kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Na ing’ateni (yaani Sunnah) kwa magego yenu.” Imekusudiwa kwa “umoja’ (singular). Yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakusema “Yang’ateni (yaumeni), kwa kutumia “uwingi”; bali alisema, “hicho” (i) –inayoashiria “umoja’ kuthibitisha kuwa ni Sunnah moja. Kufuata Sunnah ya Makhalifah waogofu ina maana kufuata Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu Sunnah yao haikuwa nyingine ila Sunnah ya Mtume.

 

Kwani “Ing’ate au Iume” ni tamathali ya usemi, ambayo inaelezea kushikamana kwa dhati na Sunnah, aidha ndio njia sahihi ya kufuatwa. Njia pekee ya kufikia ufanifu ni kufuata njia ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na njia ya Makhalifah waongofu, hasa tukizingatia njia nyingi zilizozuka na zinafuatwa na watu wanaoongozwa na utashi wa kiu yao.

 

Mtu lazima ajitahidi sana ili kushikamana na Sunnah – kwa kuchelea kupotea kwake – kuliko Mwarabu wa Jangwani anayetafuta chakula chake na maji yake, kwa sahabu huyu wa pili anaupatia uhai wa mwili wake, ambapo yule wa mwanzo anaupatia uhai moyo wake.

 

“Na tahadharini na mjiepushe na mambo yaliyozuliwa.” (Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakukoma kutuamuru tufuate Sunnah zake na Sunnah za Makhalifah waongofu, badala yake Yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitukataza mambo yaliyozuliwa. Watu wanaweza wasitambue kuwa kuleta uzushi katika maisha, ni kuwa wanaondoa Sunnah; kila uzushi unasababisha Sunnah kufa (Na tunaomba hifadhi ya Allaah!)

 

Neno ‘bid’ah’ lina maana ya kitu kipya na hakijawahi kutokea kabla yake, na watu wanaridhia vyote vilivyo vipya. Ama kupata ridhaa ya Dini, ni kwa kufuata vya zamani, maana iliyoelezwa kwa maneno yafuatayo ya Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu).

“Fuata na usizue, kwani mliyopewa yanatosha: kwenu nyie kufuata mambo yaliyoanzishwa zamani.”

 

Hadiyth sahihi iliyosimuliwa kutoka kwa Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) – katika masimulizi yanayoweza kuhusishwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

“Utakuaje wakati utakapogubikwa na mtihani (kupitia kwayo) wakubwa (wazee) watafikia ukongwe na vijana watakua. Watu watachukulia ya kuwa ni Sunnah, na sehemu yoyote ikiachwa, itasemwa, “Je Sunnah imeachwa?” Watauliza, “Na ni lini?” Alisema, “Wanachuoni wenu wakiondoka; wasomaji wenu watakapoongezeka, Fuqahaa watakapokuwa wachache, watawala watakapoongezeka; waaminifu watakapokuwa wachache; dunia itakapotafuta kupitia vitendo vya Siku ya Qiyaamah; na wakati maarifa ya Dini yatakapotafutwa lakini si kwa ajili ya Dini.”[1]

 

Allaah Amuwie radhi Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘anhu), mtunza siri za Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Yeye (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema: “Msifanye ibada yoyote ambayo haikufanywa na Maswahaba wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).”

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) amrehemu Tab’i maarufu, Hassan bin ‘Atwiyyah Al-Maharibi, ambaye alisema, “Pindi watu watakapoanzisha bida’h katika Dini yao, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ataondosha Sunnah yao iliyokuwa sawa nayo; na hatawarudishia (yaani Sunnah) mpaka Siku ya Malipo.”[2]





[1] Imesimuliwa na Ad-Daarimiy (1/64) kwa silsilah mbili, moja ambayo ni Swahiyh na nyingine ni hasan; cha al-Haakim (4/514), na kwa wengineo, kama ilivyoelezwa na Shaykh wetu, Al-Albaaniy (Allaah amrehemu) katika Qiyaamu Ramadhaan.

[2] Ilisimuliwa na Ad-Daarimiy yenye Silsilah Swahiyh, kama Shaykh wetu Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu), alisema kwenye Al-Mishkaat (188). Na alisema, “Ilisimuliwa pia kutokana na Hadiythi ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambayo ilisimuliwa na Abu Al-‘Abbaas Al-Asm katika Hadiyth yake.”

 

Share

10-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Kuna Wakati Waislamu Hutofautiana Juu ya Mambo mengi, Msimamo Wetu Kuhusu Bid’ah Uwe Upi?

 

Kuna Wakati Waislamu Hutofautiana Juu ya Mambo mengi, Msimamo Wetu Kuhusu Bid’ah Uwe Upi?

 

Wanachuoni wengi wa bandia, na wale wa namna yao wanasema, “Acheni jambo hili kwani wakati wake bado. “Kwa hakika, wengi wao wanasema, “Mazungumzo kuhusu bid’ah yanawagawa Waislamu.”

 

Hata hivyo Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitufundisha tofauti, kama tutafikwa na mtafaruku na kugawanyika, lazima tuepukana na bid’ah. Yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Kwa hakika yule atakayeishi (baada yangu) ataona mfarakano mkubwa….”

 

Mpaka Yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema,

“Na kuweni macho na mambo mapya yaliyozuliwa.”

Tunapozingatia tofauti kubwa kati ya yaliyosemwa na kundi tulilolitaja hapo juu kuhusu suala hili na anachosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tunatakiwa tukumbuke kuwa si rukhsa kufanya ijtihaad (kuweka mbele maoni yake mtu) wakati (ambapo) ijtihaad hiyo inapingana na Aayah iliyo wazi ya Qur-aan au Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Tusisahau ya kuwa, amri ya Mtume kuhusu bid’ah, inatokana na maamrisho muhimu aliyoyatoa kwa Ummah wake.

 

Baada ya hapo tukumbuke kuwa bid’ah zina sura na rangi nyingi –kuna bid’ah katika imani (‘Aqiydah), katika tawhiyd, katika ibada na katika mu’amalah. Ni bid’ah ipi tutakayoifumbia macho bid’ah katika imani? Itawezekanaje wakati tunajua kuwa usafi katika imani ni wa umuhimu wa juu na ipewe kipaumbele juu ya masuala yote.

 

Tuliwapiga makafiri na mapagani (washirikina) kwa sababu na utupu  na upotofu wa imani zao. Haya basi, vipi bid’ah katika ibada? Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliondosha shaka yoyote kuhusu aina hii na kuhusu aina zote za bid’ah aliposema,

“Na kila bid’ah ni upotevu!”

 

Na kamwe hatuwezi kuunganisha Ummah kutokana na upotevu, kwani Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

 

“Kwa hakika, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliukinga Ummah wangu kutokana kuunganika pamoja katika upotevu.”[1]

 

Watu wasipofuata maamrisho ya Allaah, wanajitakia ghadhabu ya Allaah. Fikiria askari anayemuasi afisa mwandamizi wake ambaye si tu ana uwezo, lakini anachukia uasi vile vile, afisa yule atamuadhibu mnyonge wake. Sasa fikiria sisi kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kisha kutamani kutoka Kwake Neema, Rehema na Msaada!

 

Haiyumkiniki kimaadili wala kimatendo kwetu sisi kuruhusu kuenea kwa bid’ah na kupenya katika jamii na wakati huo huo kutaraji umoja miongoni mwa Waislamu na nguvu katika Ummah wetu.

Allaah Anasema:

…Hakika Allaah habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo nafsini mwao... (13: 11).

 

Kama tulivyokwishajadili; kule kuwepo tu kwa bid’ah kunasababisha kutoweka kwa Sunan (wingi wa Sunnah). Kukosekana kwa Sunan za Mtume, na kuwepo kwa bid’ah, kuna mtu mwenye akili timamu anayetarajia Waislamu kuungana!

 

 

Kila Bid’ah ni Upotevu

 

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anafafanua kuwa mambo mapya yaliyoanzishwa ni uzushi (bid’ah) na njia ya upotevu.

Kwa kuacha Sunnah, tunawaiga Wana wa Israaiyl, ambao waliangamizwa walipojishughulisha na visa, wakitelekeza kutimiza dini yao. Inatajwa kwenye Hadiyth”

 

“Kwa hakika, Wana Israaiyl waliangamizwa, walipojishughulisha na kusimulia visa.”[2]



[1] Hasan, katika silsilah zake mbali mbali; ilisimuliwa na Abu ‘Aaswim katika As-Sunnah katika mlolongo wa nambari, 82, 83 na 84 (nakala ina maoni ya Shaykh wetu -Allaah Awe radhi naye) katika At-Tirmidhiy, na katika vyanzo vingine. Rejea Asw-Swahiyhah (1331) za Adh-Dhwa’iyfah, katika maelezo ya Hadiyth Na.1510.

[2] Ilisimuliwa na At-Twabaraaniy, katika Al-Mu’jam Al-Kabiyr; Abu Nu’aym katika Al-Hilyah; na wengineo. Aidha imetajwa ndani ya As-Swahiyhah (1681). Katika Nihaayah imetajwa, “Ikiwa na maana, waliamini khutbah na kuacha matendo, na hiyo ilikuwa sababu ya kuangamizwa kwao, au kinyume chake: walipoangamizwa kwa sababu ya kuacha matendo, wakajishughulisha na visa.”

Shaykh wetu (Allaah Amuwie radhi) alisema, “Inakubalika kusema ya kuwa sababu ya kuangamizwa kwao ni kuzipa umuhimu watoa khutbah na visa vyao, badala ya kuzingatia Fiqh na elimu yenye manufaa, elimu ambayo ingewasaidia kujua dini yao…Hilo lilipojiri waliangamizwa, mashaka yanayowapata wahubiri leo, na maonyo yao mengi yanatokana na masimulizi ya Wana wa Israaiyl au kutoka kwa Masufi na tunamwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atulinde.”

 

Share

11-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Kukanusha Wale Wanaoigawa Bid’ah Kwenye Makundi Mawili: Bid’ah Nzuri Na Mbaya

 

Kukanusha Wale Wanaoigawa Bid’ah Kwenye Makundi Mawili: Bid’ah Nzuri Na Mbaya

 

Baadhi wanasema ya kuwa kuna bid’ah nzuri na kuna bid’ah mbaya.[1]

Sema, kama inakuridhisha, “Bidah nzuri na bid’ah mbovu, lakini kumbuka haya: Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

“Kwa uhakika kila bida’ni upotovu, na kila upotovu ni Motoni.”

 

Bid’ah zote; ziwe ni nzuri na au mbaya na zote unazoweza kutaja ziko chini ya “yote/kila”, ambayo ilitajwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ilisimuliwa ya kuwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisimulia,

“Kila bid’ah ni upotevu, hata kama baadhi ya watu watachukulia kuwa ni nzuri.[2]

 

Mtu anaposema huu si wakati wa kukataza bid’ah bali ni bora kupiga vita madhehebu zinazokiuka maadili, hayuko sawa – kutokana na sababu zifuatazo:

 

1.     Kwa kutokataza bid’ah, hawatoeneza tu bali wataziongeza, pamoja na hayo, Sunah nyingi (Sunan) zitafutwa. Hali hii itapelekea kuenea kwa upotofu na makosa, kwa sababu, lazima tukumbuke, kila bid’ah ni upotofu (dhwalaalah).

 

2.     Kila Muislamu anawajibu, kama anaweza, kuzuia na kukataza maovu. Iwapo mtu ataona kitendo kiovu kinafanywa mbele ya macho yake, lazima akikataze, bila kujali udogo wake, ukilinganishwa na maovu makubwa yaliyoenea (yaliyo shamiri) – kama vile Ukomunisti, umasonia (Masonry), na itikadi zote potofu.

 

 

Vivyo hivyo, kuwepo kwa madhehebu zilizopotoka kusiwazuie Wanachuoni kuwakumbusha watu juu ya maonyo ya kutowaasi wazazi, kusema uongo, kula Ribaa na vitendo vyote viovu.

 

3.     Ukosefu wa elimu katika jamii, pamoja na bid’ah kunasababisha na kueneza upotovu wa madhehebu. Lakini Maswahaba ambao walisimamisha jamii kinyume na ile tuliyoielezea, walikuwa baidi  (mbali) na bid’ah, kwa hakika, walianzisha jamii safi, ambayo haikuwa na madhehebu zilizopotoka.[3]

 

4.     Hebu tujaalie kuwa tunaelewa vema imani ya makundi mbali mbali yaliyoparaganyika - je, tutafanya nini baada ya hapo? Jibu, bila shaka, ni kuwa tuna haja ya kufafanua kukengeuka kwao, lakini inatubidi tuwe na maarifa, fiqh na mwongozo. Pamoja na hayo, elimu hiyo lazima iwe sahihi na halisi kwa sababu mihemko na ushupavu havitoshi kukanusha waliokengeuka na waliopotoshwa. Yule anayeifahamu Dini ana uwezo mzuri wa kuchanganua upotofu wa madhehebu zilizopotea, na ana uwezo wa kuwakusanya Waislamu kwa lile lililo sawa, katika Imani, Fiqh na mwenendo mzuri.

 



[1] Mmoja anaweza kuunga mkono kauli ya ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyosema: “Ubarikiwe uzushi (bid’ah) huu.” Yeye ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema haya katika masimulizi yalitolewa na ‘Abdur- Rahmaan bin ‘Abdil-Qaariy, ambaye alisema, “Wakati wa usiku mmoja wa Ramadhaan, nilikwenda na ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) Msikitini, ambapo watu walisambaa katika makundi, kila kundi lilikuwa na Waumini chini ya kumi, na watu wengine wakiswali kwa makundi. ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoona hali hiyo, yeye (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema, “Nahisi ya kuwa ingekuwa bora kama ningewakusanya wote wawe na Imaam mmoja.” Kisha alidhamiria kulifanya hilo na aliwakusanya nyuma ya Ubay Bin Ka’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu), ‘Abdur-Rahmaan aliendelea kusema, “Nilipotoka naye usiku mwingine (tuliona kuwa) watu walikuwa wakiswali nyuma ya Imaam mmoja, na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema ‘Uzushi (bid’ah) huu ubarikiwe.”

Alichokusudia ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa kusema bid’ah (uzushi) ni maana ya kilugha (isimu) ambayo ina maana ya upya au ugeni, kile ambacho hakikufahamika mwanzo. Yafuatayo ni kiini cha aliyosema mwandishi wa Jami’ Al-‘Uluum Wal-Hikam: Baadhi ya watangulizi wetu watukufu walipopasisha baadhi ya bid’ah (uzushi), ulikuwa uzushi kwa maana ya kilugha (isimu) na si uzushi kwa maana ya Shari’ah. Mfano mmoja wapo ni yale aliyosema ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) usiku wa manane walipokuwa wakiswali katika mwezi wa Ramadhaan: “Bid’ah hii imebarikiwa.”

Alichokusudia Yeye (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni kuwa kitendo kile makhsusi hakikuwahi kufanywa katika utaratibu ule kabla ya wakati ule; hata hivyo, kilikuwa na mzizi katika Shari’ah. Mathalan, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasihi Waislamu wasimame na kuswali Taaraawiyh (tarawehe) katika mwezi wa Ramadhaan. Hata wakati wa uhai wa Mtume, watu walisimama kwa makundi au mmoja mmoja, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe aliwaswalisha Maswahaba Taaraawiyh katika mwezi wa Ramadhaan zaidi ya mara moja. Ni kweli ya kuwa baadaye Mtume alikataa kufanya hivyo, lakini alieleza kwa nini aliacha; alichelea ya kuwa ingefaradhishwa kwao na kuwa wangeshindwa kuidumisha. Kwa kuwa Swalah ya Taaraawiyh ingefaradhishwa tu wakati wa uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)-baadaye wakati wa Ukhalifah wa ‘Umar –hapakuwa na sababu ya kuogopa alichoogopa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lazima tukumbuke ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituamuru tufuate Sunnah za Makhalifah waongofu, na Swalah ya Taaraawiyh kwa jamaa moja ilikuwa Sunnah ya Khalifah mwongofu, hivyo watu walijumuika kutimiza Sunnah ile wakati wa kipindi cha ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu), ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu), na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Shaykh wetu, Al-Albaaniy (Allaah Amuwie radhi) alisema katika Swalaat at-Taaraawiyh (Uk. 43), Kauli ya ‘Umar ‘Bid’ah hii imebarikiwa’, haikukusudiwa bid’ah kwa mujibu wa maana yake katika Shari’ah: kuanzisha jambo katika Dini bila ya kuwa na umuhimu au tukio la mfano wake. Kama inavyofahamika ya kuwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuanzisha jambo jipya, lakini alihuisha zaidi ya Sunnah moja, tunajua kuwa kwa bid’ah alikusudia ile ya maana ya kiisimu: mpya na ngeni ambayo haikujulikana kabla ya kuwepo. Hapana shaka ya kuwa Swalah ya Taaraawiyh nyuma ya Imaam mmoja haikufahamika wala haikufanyika wakati wa Ukhalifah wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) na nusu ya Ukhalifah wa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa mtazamo huo ni mpya. Lakini kwa maoni inayoafikiana na aliyofanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ni Sunnah, si bid’ah, ambayo ndio sababu pekee ilifanya ielezwe kuwa ni nzuri. Na hayo ni maelezo ya Wanachuoni maarufu kuhusu kauli ya ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu). ‘Abdul-Wahhaab As-Subkiy, katika Ishraaq Al-Masaabiyh … Alisema ya kuwa Ibn ‘Abdil-Barr alisema, ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuanzisha Sunnah hii kwa sababu yeyote nyingine kuliko kuanzishwa Sunnah hii na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe, kwani aliipenda, aliridhishwa nayo, na hakuacha kuitekeleza mara kwa mara kwa sababu yoyote ile zaidi ya kuchelea kufanywa faradhi kwa Ummah wake. Yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mrehemevu kwa ummah wake. ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alijifunza kutoka kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akijua ya kuwa vitendo vya faradhi haviwezi kuongezwa wala kupunguzwa baada ya kifo cha Mtume –alifufua Sunnah ya Mtume inayohusu Swalah ya Taaraawiyh katika mwaka wa 14H, rehema aliyopewa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) na Allaah na ambayo hakumfunulia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kufanya hivyo, japokuwa, alikuwa kwa ujumla, alikuwa bora na makini zaidi kufanya ‘amali njema kuliko ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu). Kila mmoja kati ya wawili hao alikuwa na sifa za kipekee nazo hazikupatikana kwa mwengine. Aidha As-Subkiy alisema, “Kama haikuwa Swahiyh ingekuwa bid’ah kama ‘amali njema zinapopandishwa katika nusu ya Sha’abaan au Ijumaa ya mwanzo ya Rajab, kwa hali yoyote ilikuwa lazima kukana kitendo cha kuwakusanya pamoja kwenye Swalah ya Taaraawiyh.”

 

Katika Fatwa yake, mwanachuoni Ibn Hajr al-Haythamiy alisema, “Kuwaondosha Mayahudi na Wakristo kutoka Ghuba ya Uarabu na kuwapiga Waturuki… Hayakuwa matendo ya bid’ah, japokuwa hayo hayakujiri wakati wa uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliposema, “Bid’ah hii imebarikiwa”, alikuwa na maana ya bid’ah katika maana yake halisi katika lugha ya Kiarabu. Na katika hali hiyo bid’ah inatumika kwa mujibu wa maana ya kilugha (isimu) katika Aayah ifuatayo:

“Sema: Mimi si bid’ah (kiroja, kilichozuka) miongoni mwa Mitume...” (46: 9).

 

Mifano yote iliyopita ni bid’ah katika lugha, na bid’ah kwa wajibu wa maana yake kishari’ah ni upotevu. Kwa hiyo wanazuoni wanaposema kuwa bid’ah nzuri na mbaya, wameigawa bid’ah kwa mujibu wa maana ya asili ya lugha ya Kiarabu. Na wanaposema ya kuwa kila bid’ah ni upotofu, wanakusudia ile ambayo Shari’ah inaipa maana ya bid’ah. Huoni kuwa Maswahaba na Taabi’iyn walipozuia Adhana kwa Swalah ambazo si Swalah tano za kila siku kwa mfano, Swalah za ’Iyd mbili, japokuwa hapana zuio la hilo. Na walichukizwa na Shami’an mbili za kona ya Ka’bah kukumbatiwa na kubusiwa baada ya Sa’ay kati ya Swafaa na Marwaa …Vivyo hivyo, kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijitenga kufanya tendo kwa sababu, hivyo kuacha tendo hilo ni Sunnah, na kulitekeleza ni bid’ah. Tuliposema, ‘kwa sababu’ hiyo haihusu kuwaondoa Mayahudi na kuikusanya Qur-aan katika Kitabu kimoja. Aidha, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliacha kuwakusanya watu kwa ajili ya Swalah ya Taaraawiyh kwa sababu, na sababu hiyo ilipotoweka, ilikuwa Swahiyh kwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwajumuisha watu kwa Swalah…”

[2] Hadiyth hii ina Silsilah Swahiyh, kama ilivyotajwa katika Iswlaah al-Masaajid (Uk. 13) kilichoandikwa na Shaykh wetu, Al-Albaaniy (Allaah Amuwie radhi).

[3] Pamoja na hayo, wakati wao, kulikuwa na shirk, ukafiri, uovu na upagani. Hata hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliwaauni Waumini wakapata ushindi, kwa upanga na mkuki vile vile kupitia uthibitisho na ushahidi.

Share

12-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Hatari Ya Bid’ah (Uzushi)

 

Hatari Ya Bid’ah (Uzushi)

 

‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisimulia ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

”Yeyote atakayeanzisha kitu katika jambo  (Dini) letu hili ambalo halimo, basi litakataliwa (litarejeshwa).”[1]

 

Na katika Hadiyth ya Muslim,

“Anayefanya ‘amali ambayo si katika jambo (Dini) letu, basi itarejeshwa.” [2]

                           

Ni desturi ya hatari sana kutafuta ukuruba wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) bila kufuata Qur-aan, Sunnah, na njia ya watakatifu (wacha-Mungu) waliotutangulia. Aidha kutowafuata wao inaonesha ujasiri wa kijuvi, pupa na kuchupa mipaka ya Allaah.

 

Kama fahamu za mtu zinamruhusu kuiba dola moja au dola kumi, atakuwa hana kipingamizi cha kuiba dola elfu moja. Ni sawa na kadhia ya mzushi: akiridhika kuchepuka kutoka Sunnah za Mtume, wakati huo akiridhika na bid’ah moja, bid’ah kubwa na pengine hata shirk itakuwa sahala (nyepesi) kwake. Hatua hiyo ya kwanza ya kuridhia kukengeuka na bid’ah inarahisisha hatua za mbele zinazopelekea kwa kila aina ya upotovu. Hii ndio ilikuwa hali ya watu wa Nuuh (‘Alayhis Salaam), ambao walifanya masanamu ya baadhi ya watukufu wao kuwa miungu baada ya wao kufariki dunia.

 

Mwanzoni, walipokufa tu, Shaytwaan aliwashawishi watu wajenge masanamu baada yao, ili wawakumbuke na waige ‘amali zao njema. Kisha, baada ya kupita karne kwa karne, watu waliposahau lengo la awali la masanamu hayo, Shaytwaan aliwashauri kuabudu masanamu badala ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), akiwadanganya na madai potofu ya kuwa baba yao ndiye aliyekuwa akiyaabudu.

 

Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema,

“Masanamu kutoka kwa watu wa Nuuh (‘Alayhis Salaam) yalishuka miongoni mwa Waarabu baadaye. Ama Wudd (jina la moja ya masanamu), alikuwa wa Kalb katika Dawmat Al-Jandal; Suwa’ alikuwa wa Hudhayl; Yaghuuth alikuwa wa Murad; Thamma alikuwa wa Bani Ghalif huko Jurf, akiwa na Saba; Ya’uuq alikuwa wa Hamdaan; na Nasr wa Hamayr; kwa ukoo wa Kila’. Wao (masanamu) ni majina ya wacha-Mungu miongoni mwa watu wa Nuuh (‘Alayhis Salaam). Walipofariki dunia, Shaytwaan aliwashawishi wasimamishe (wajenge) masanamu ya hao, walipokuwa wakikusanyika na waliyapa majina yao. Walijenga masanamu lakini hawakuyaabudu.

Kizazi hiki kilipopotea na elimu ilipofutika, masanamu yalifanywa vitu vya kuabudiwa.” [3]

 

Hivyo ndivyo Shaytwaan alivyowaghilibu taratibu, kwanza kuzua na kisha kufanya shrik na kukufuru. Endapo wangekata uhusiano kati yao na Shaytwaan kutokea mwanzo, kama wangeminya tatizo katika tumba lake, wasingeanguka kwenye lindi la uovu na ukafiri.

 

Sawa na hilo lilitokea kwa bahati mbaya kwa makundi ya Ummah wetu; mfano mmoja ni kundi moja lililokuwa likikusanyika ndani ya Msikiti. Kwa kila mkusanyiko alikuwepo kiongozi, na kila mshiriki alikuwa na vijiwe mkononi. Kiongozi alisema, “Semeni Takbiyr (Allaahu Akbar) Allaah Mkubwa mara 100, na kila aliyekuwepo alisema mara 100. Waliendelea kufanya hivyo kwa Tahliyl (wakisema, Hapana apasaye kuabudiwa ila Allaah) na kwa Tasbiyh (wakisema, Ametakasika Allaah!) ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwalaani kwa matendo yao.

 

Katika Hadiyth Swahiyh, al-Hakam bin al-Mubaarak alipokea kutoka kwa ‘Umar Bin Yahya, aliyesema, “Nilimsikia baba yangu akisimulia ya kuwa alimsikia baba yake akisema,

Tulikuwa tukikaa kwenye mlango wa ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) kabla ya Swalah ya Alfajiri, na alipotoka nje, tulikwenda naye Msikitini.

 

Asubuhi moja, Abu Muusa Al-Ash’aariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alitujia na kusema, “Je, Abu ‘Abdir-Rahmaan (‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) ameshatoka nje? Tulijibu, “Hapana” na hivyo Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikaa nasi mpaka alipotoka. Alipotoka, Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema, “Ewe Abu ‘Abdir-Rahmaan! Nimeona jambo Msikitini nililolizuia, hata hivyo – AlhamduliLlaah – kila nilichokiona ni kizuri. ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliuliza, na kilikuwa kitu gani? Alijibu, “Iwapo utaishi (kwa kitambo kidogo) utakiona. Niliona makundi katika mduara, walikaa wakisubiri Swalah. Katika kila duara alikuwepo mtu (kiongozi), na wote walikuwa na kokoto mikononi mwao.

Kiongozi alisema: fanyeni Takbiyr mara 100, nao walifanya Takbiyr mara 100. Kisha alisema, fanyeni Tahliyl mara 100 na wakafanya Tahliyl mara 100.

Na kisha aliposema Tasbiyh mara 100, na wakafanya ‘Tasbiyh mara 100. Na uliwaambia nini?  Aliuliza ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu). Sikusema lolote, kwani nilisubiri kujua rai yako kwanza kuhusu suala hili au nipokee amri yako! Yeye (Radhiya Allaahu ‘anhu), Ni wewe uliowataka wahesabu madhambi yao…”

Yeye (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikwenda tukimsindikiza mpaka alipokuta waliokusanyika ‘Abdullaah bin Mas’uud aliwasimamia na kusema, “Ni jambo gani hili mlifanyalo?” Walijibu, ‘Ewe Abu ‘Abdir-Rahmaan (yaani ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) tumetumia hizi kokoto kuhesabu idadi ya Takbiyr, Tahliyl na Tasbiyh tunazofanya.

”Yeye (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema, “Basi hesabuni madhambi yenu… Mlaaniwe, Enyi Ummah wa Muhammad, vipi maangamifu yamewafika mapema! Hawa ndiyo Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika idadi yenye kutosheleza hii ni nguo ambayo ilikuwa bado imetatuka na hii ni sahani yake bado haijavunjika (yaani, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifariki dunia hivi karibuni na tayari mmepotoka). Naapa kwa Yule ambaye Roho yangu iko mikononi Mwake, ama mpo kwenye Dini yenye mwongozo kuliko Dini ya Muhammad, au ni wafunguzi wa mlango wa upotofu.”

Walisema, “WaLlaahi, Ewe Abu ‘Abdir-Rahmaan, tulikusudia kufanya mema, lakini hatukufikia lengo!

 

Kwa hakika, Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizungumza nasi, akisema kikundi cha watu walikuwa wakisoma Qur-aan, hata hivyo haipitii mitulinga yao.

WaLlaahi, sijui lakini pengine wengi wao ni miongoni mwenu. Kisha aligeuka na kuondoka.

 

‘Amr Bin Salamah alisema, “Tuliwaona washiriki wengi wa mikusanyiko (hiyo) wakipigana dhidi yetu siku ya An-Nahrawaan wakiwa upande wa Khawaarij.”[4]

Kilichoonekana ni kitu kidogo japo ni kikubwa si kwa sababu walikuwa wakimdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika njia ambayo haikuamriwa kwenye Qur-aan au Sunnah, na hivyo waliongozwa kwenye uovu. Kama vile, waliishia kuwapiga Waislamu katika Siku ya Nahrawan wakishirikiana na Khaawarij. Hivyo waliacha njia ya Waumini, mwanzoni walifanyaje At-Tasbiyh, At-Tahliyl na At-Takbiyr –huku wakidai ya kuwa walichokuwa wakikitaka ni kutenda mema na baadaye kupigana dhidi ya Waislamu – na pengine walitatizika na kufikiria ya kuwa walikuwa wakitenda mema.

 

 



[1] Ilisimuliwa na Al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).

[2] Muslim (1718).

[3]Ilisimuliwa na Al-Bukhaariy (4920), na Al-Haafidh alitaja ya kuwa Hadiyth hii haikuungana japokuwa ni Swahiyh kwa sababu ya Silsilah nyingine yenye nguvu kutoka kwa Ibn ‘Abbaas na ilishuhudiwa na mwanafunzi wake, ‘Ikrimah katika Tafsiri ya At-Twabariy. Shaykh wetu (Allaah Amuwie radhi) alitufahamisha hivyo, na taarifa hii aliiweka katika toleo la Pili lililopitiwa la “Tahdhiyr al-Masaajid Fiyttikhaadh Al-Qubuur Masaajid.”

[4] Alisimulia Ad-Daarimiy (1/68) na Silsilah yake ni Swahiyh, kwani wasimulizi wake wote ni waaminifu. Rejea Ar-Radd ‘Alaa at-Ta’aqqub al-Hathiyth (uk. 47) kilichoandikwa na Shaykh, Al-Albaaniy (Allaah Amuwie radhi).

Share

13-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Katika Amri Yake ya Mwisho Alitukataza Kufanya Jambo Moja tu; Bid’ah

 

Katika Amri Yake ya Mwisho, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Alitukataza Kufanya Jambo Moja tu; Bid’ah.

 

Iwapo mtu anaweza kufikiria maneno ya Mtume katika maamrisho ya mwisho, mtu atagundua ya kuwa amri za kufanya zinazidi makatazo, ambayo inahesabika kuwa yule anayeshikamana na Sunnah, hahitaji ufafanuzi kuhusu njia za upotofu –Amri za kufanya ni hizi hapa:

 

1.     Mche sana Allaah

 

2.     Sikiliza na tii

 

3.     Jihimize kufanya Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Sunnah za Makhalifah waongofu.

 

Ama kuhusu makatazo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hapa alitukataza jambo moja, alisema, “Jihadharini na muwe mbali na mambo yaliyozuliwa”, ambayo inaelezea au inaashiria: kaeni mbali na mambo mapya na yaliyozuliwa, na matokeo yake mtaokolewa na kufanikiwa. Bid’ah ni siri iliyopo nyuma ya upotofu, kukengeuka na upotevu kamili, kwani inapelekea na wakati mwingine inahusu shirki na ukafiri. Kwa hiyo yeyote anayefunga mlango wa uzushi ameongozwa kwa ridhaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Kuhusu bid’ah, mtu anatakiwa azingatie Hadiyth hii:

“Kwa hakika, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amezuia toba ya mwenye kufanya kila bid’ah.”[1]

 

 

 

Hitimisho

 

Kwa hakika, amri ya mwisho ya Mtume ilikuwa sawa na khutbah zake: zilisababisha mioyo kutetema na macho kububujika machozi, lakini zikiacha mioyo na macho aminifu. Mioyo inatetema kwa sababu ya madhila tunayoyapata ukilinganisha na heshima tuliyoisikia. Macho yanabubujika machozi kwa sababu ya kuparaganyika Waislamu na kwa sababu ya kugawanyika miongoni mwao, ambayo imetusibu baada ya kipindi cha utukufu, heshima na uongozi.

 

Hata hivyo kuna matarajio: maamrisho ya mwisho yana mambo yanayoweza kutuokoa na madhila tuliyomo. Kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), vita kuhusu utashi, kushikamana na Sunnah za Mtume na Sunnah za Makhalifah waongofu, uelewa sahihi wa Qur-aan na Sunnah, ambayo inaambatana na uelewa wa Maswahaba;  na kutojihusisha na bid’ah – yote  haya yamo katika amri ya mwisho ya Mtume. Shikamana na maamrisho hayo na ng’ata kwa magego yako (Allaah Awe radhi nawe) ili uwe miongoni mwa wale watakaokombolewa, wale waliofuzu, kwa ridhaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).



[1] Ilisimuliwa na Abu Ash-Shaykh, katika “At-Taariykh Asbahaan,” na At-Twabaraaniy katika “Al-Awsatw”, na wengineo. Rejea “As-Swahiyhah (1620).”

 

Share