Swalaah - Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

 

 

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

Imekusanywa na:

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Share

01-Swalaah - Kuwajibika Na Fadhila Zake: Maana Ya Swalah Na Kuwajibika Kwake

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

01- Kuwajibika Na Fadhila Zake: Maana Ya Swalaah Na Kuwajibika Kwake

 

Alhidaaya.com

 

 

Maana Ya Swalaah Kilugha:

           

 

Ni du'aa kama Anavyosema  Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ ۖ إِنَّ صَلَاتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿١٠٣﴾

Chukua (ee Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo na waombee du’aa (na maghfirah). Hakika du’aa yako ni utulivu kwao. Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. [At-Tawbah: 103]

 

 Hadiyth ifuatayo inathibitisha pia maana hiyo:
 

عن أبي هريرة -رضي الله عنه- قال: قال رسول الله -صلى الله عليه وسلم: ((إذا دعي أحدكم فليجب فإن كان صائمًا فليصلِّ و إن كان مفطرًا فليطعم)) أخرجه مسلم         

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Akialikwa mmoja wenu aitike (mwaliko), ikiwa amefunga  aombe du'aa (kwa waliomualika), akiwa hakufunga basi ale (chakula))) [Muslim] 

 

Yaani: Awaombee du'aa ya maghfirah, baraka na kheri)

 

Swalaah kutoka kwa Allaah ni Himdi na kutoka kwa Malaika ni du'aa kama Anavyosema:

 

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾

56. Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa [Al-Ahzaab: 56]

 

Abu 'Alyah amesema: Swalaah ya Allaah ni kumsifu mja kwa Malaika Wake na Swalaah ya Malaika ni du'aa.

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema: "Wanawaswalia" maana wanawabarikia"  

 

Vile vile Swalaah kutoka kwa Allaah ni maghfirah au Baraka. Swalaah kwa maana ya maghfirah nikutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ ﴿١٥٧﴾

Hao zitakuwa juu yao Barakah kutoka kwa Rabb wao na rahmah, na hao ndio wenye kuongoka. [Al-Baqarah: 157]

 

Na kama ilivyosimuliwa kutoka kwa Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alisema:

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى آل أَبِي أَوْفَى

‘Allahumma Swalli ‘alaa Aali Abi Awfiy’ Akimaanisha ‘Ee Allaah wasamehe jamaa wa Abu Awfiy’.  

 

Hivyo hapa Swalaah ina maana ya maghfirah.
 

 

Maana Swalaah Kishariy'ah

 

Ni kumuabudu Allaah kwa kauli na vitendo maalumu  vinavyoanza na Takbiyrah (Allaahu Akbar) na kumalizika na Tasliym (kutoa salaam).

 

Na imeitwa Swalaah kwa sababu inahusiana na du'aa katika kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) tunaposimama, tunaporukuu, tunaposujudu na tunapokaa, hivyo Swalaah nzima ni du'aa.

 

 

Hukumu Ya Swalaah:

 

Swalaah ni fardhi kwa kila Muislamu mwenye akili timamu, aliyebaleghe kutokana na dalili kutoka katika Qur-aan:

 

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ ﴿٥﴾

Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara. [Al-Bayyinah: 5]

إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا ﴿١٠٣﴾

hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu [An-Nisaa: 103]

 
 

Ama katika Sunnah ni kauli yake Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomtuma Mu'aadh Bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kupeleka risala Yemen kwa kumwambia: ((…na wafundishe kwamba Allaah Amewafaridhisha Swalaah tano kila siku…)) [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

Vile vile,

 

  عبدالله بن عمر قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم (( بُنِـيَ  الإِسْلاَمُ علـى خَمْسٍ: شَهادَةِ أنْ لا إِلٰهَ إلا الله وأنَّ مُـحَمَّداً رَسُولُ الله وإِقامِ الصَّلاَةِ وإِيتاءِ الزَّكاةِ وَحَجِّ البَـيْتِ وَصَوْمِ رَمَضَانَ((  البخاري

Kutoka kwa 'Abdullaah ibn 'Umar ambaye amesema: Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Uislamu umejengeka kwa matano; Kushuhudia (na kukiri kwa moyo)  kwamba hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah na kuswali (Swalaah tano), kutoa Zakaah, kuhiji katika Nyumba (Makkah) na kufunga (mwezi wa) Ramadhwaan)) [Al-Bukhaariy]

 

Kuna Aayah na Hadiyth nyingi zinazothibitisha kuwajibika kwa Swalaah. Ama mwanamke mwenye hedhi na aliye katika nifaas hawawajibiki kuswali kutokana na kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  

 

  أليس إذا حاضت المرأة لم تصل ولم تصم ؟  -متفق       

((Kwani sio kweli kwamba mwanamke anapokuwa katika hedhi haswali wala hafungi?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Share

02-Swalaah - Kuwajibika Na Fadhila Zake: Kusisitizwa Kwake na Malipo yake

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

02- Kusisitizwa Kwake na Malipo yake

 

Alhidaaya.com

 

 

Hakika Swalaah ‘ibaadah muhimu na tukufu katika Uislamu kwa dalili zifuatazo: 

 

Swalaah Ni Nguzo Ya Dini:

 

 

عن معاذِ بن جبلٍ رضي الله عنه (( ...ألا أُخْبِرُكَ بِرَأسِ الأمْرِ وَعَمودِهِ وَذِرْوَةِ سَنَامِهِ؟)) قلتُ: بَلىَ يا رسول الله. قال:  رَأْسُ الأمْرِ الإسلامُ، وعَمُودُهُ الصَّلاةُ، وَذِرْوَةُ سَنَامِهِ الجِهادُ))

رَوَاهُ التِّرْمِذِيُّ وَقَالَ: حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ  ٌ

Kutoka kwa Mu'aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhu) ((…Tena akasema: Je, nikwambie kilele cha hilo jambo; nguzo yake na sehemu yake ya juu kabisa?))  Nikasema: Ndio ee Rasuli wa Allaah.  Akasema:  ((Kilele chake ni Uislamu, nguzo yake ni Swalaah na sehemu yake ya juu kabisa ni Jihaad)) [At-Tirmidhiy na Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

Hivyo inapoanguka nguzo huanguka kile kilichojengewa nacho nayo ina maana ni Dini yake mtu kwani bila ya kuswali ni kama kafiri kutokana na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) itakayotajwa katika hukmu ya mwenye kuacha Swalaah.

   

 

Swalaah Ni Jambo La Kwanza Kuulizwa Na Kuhesabiwa Siku Ya Qiyaamah:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ َقَالَ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ ((إِنَّ أَوَّلَ مَا يُحَاسَبُ بِهِ الْعَبْدُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مِنْ عَمَلِهِ صَلاتُهُ فَإِنْ صَلُحَتْ فَقَدْ أَفْلَحَ وَأَنْجَحَ وَإِنْ فَسَدَتْ فَقَدْ خَابَ وَخَسِرَ فَإِنْ انْتَقَصَ مِنْ فَرِيضَتِهِ شَيْءٌ قَالَ الرَّبُّ عَزَّ وَجَلَّ انْظُرُوا هَلْ لِعَبْدِي مِنْ تَطَوُّعٍ فَيُكَمَّلَ بِهَا مَا انْتَقَصَ مِنْ الْفَرِيضَةِ ثُمَّ يَكُونُ سَائِرُ عَمَلِهِ عَلَى ذَلِكَ)) الترمذي و أبوا داود والنسائي وابن ماجه وأحمد

 

Imepokelewa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah  wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kitu cha kwanza kinachohesabiwa katika ‘amali za mja wa Allaah Siku ya Qiyaamah ni Swalaah zake. Zikiwa zimetimia, hapo tena atakuwa kaneemeka na kafuzu, na zikiwa zina kasoro atakuwa kaanguka na kala khasara. Ikiwa pana upungufu katika Swalaah zake za fardhi Allaah ‘Azza wa Jalla Atasema: “Tazama ikiwa mja wangu ana Swalaah zozote za Sunnah ambazo zinaweza kufidia zile zilizopungua, hapo tena ‘amali yake iliyobaki itaangaliwa hivyo hivyo)). [At-Tirmidhiy, Abu Daawuwd, An-Nasaaiy, Ibn Maajah na Ahmad]

 

Kwa hiyo kuacha Swalaah iwe ni   jambo la kumtia khofu kubwa Muislamu kwa kuwa ni kupata hasara siku ya Qiyaamah kwa kuacha kuswali.

 

 

Maswali ya kujiuliza kuhusu Swalaah:

 

  • Unaswali?
  • Unaziswali Swalaah zote kwa wakati wake?
  • Unaziswali kwa twahara iliyokamilika na wudhuu uliotekelezeka vizuri?
  • Unaelekea Qiblah? Unaweka Sutrah mbele yako?
  • Nguo na sehemu unazoswalia ni safi hakuna najisi yoyote wala si isbaal; hazibururi kwa kuvuka mafundo ya miguu?
  • Unaswali mahali au nyumba isiyotundikwa picha za viumbe?
  • Unaswali Jamaa’ah Msikitini? (Swalaah kwa wanaume).
  • Unaswali kwa kutimizia kila kitendo cha Swalaah ipasavyo?
  • Unasoma Qur-aan kwa kuzingatia maana yake?
  • Unaswali kwa khushuu’ (unyenyekevu) na twumaaninah (utulivu)?
  • Unaswali Swalaah za Nawaafil na Sunnah; Sunnah zilosisitizwa na zisositizwa, dhwuhaa, witr’ kwa ujumla Qiyaamul-Layl?  

 

Wasiya Wa Mwisho Wa Rasuli wa Allaah  (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Ummah Wake:

 

Katika khutbah zake za mwisho aliwausia sana Swalaah akisema:

 

((...الصلاة الصلاة و ما ملكت أيمانكم))    أحمد وصححه الألباني

 

((…Swalaah, Swalaah na waliomiliki mikono yenu ya kuume)) [Ahmad na ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy]

 

 

'Ibaadah Pekee Iliyofaradhiwa Katika Mbingu Ya Saba:

 

Swalaah ni nguzo pekee aliyoipokea Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mbingu ya saba katika tukio la Israa Wal-Mi'raaj. Na zilikuwa asili yake ni Swalaah khamsini kisha zikapunguzwa hadi zikafika tano. Hivyo thawabu zake ni khamsiyn katika mizani ingawa ni tano katika kuzitekeleza.

 

Sifa Ya Mwanzo Na Ya Mwisho Ya Waja Watakaofuzu:

 

Kwa jinsi Swalaah ilivyokuwa ni muhimu na tukufu mno, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameanza kutaja Swalaah kwa waja Wake watakaofuzu na kupata Jannah ya Firdaws kwa kutekeleza na kudumisha Swalaah.

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾

Kwa yakini wamefaulu Waumini.

 

الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾

Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea.

 

وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ﴿٣﴾

Na ambao wanajiepusha na mambo ya upuuzi.

 

وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ ﴿٤﴾

Na ambao wanatoa Zakaah.

 

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾

Na ambao wanazihifadhi tupu zao.

 

إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾

Isipokuwa kwa wake zao, au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume basi hao hawalaumiwi.

 

فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾

Lakini atakayetaka kinyume ya hayo; basi hao ndio wapindukao mipaka.

 

وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿٨﴾

Na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga.

 

وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿٩﴾

Na ambao wanazihifadhi Swalaah zao.

 

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾

Hao ndio warithi.

 

الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾

Ambao watarithi (Jannah) ya Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu. [Al-Muuminuwn: 1-11]

 

 

Kwa hiyo, nani basi miongoni mwa Muumini asiyetaka kuipata Jannah ya Al-Firdaws iliyo juu kabisa karibu na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu tu ya kuacha Swalaah? Ibaadah ambayo haimchukui mtu muda mwingi  kuitekeleza?

 

 

 

Share

03-Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake: Amri za Mwanzo Kwa Manabii Waliopita

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

03- Amri Za Mwanzo Kwa Manabii Waliopita

 

Alhidaaya.com

 

 

Swalaah ilikuwa ni amri ya kwanza hata kwa Manabii waliopita. Alipozaliwa Nabii 'Iysaa (‘Alayhis Salaam) maneno ya mwanzo aliyotamka akiwa bado mtoto mchanga ni kuwa ameamrishwa Swalaah: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 فَأَتَتْ بِهِ قَوْمَهَا تَحْمِلُهُ ۖ قَالُوا يَا مَرْيَمُ لَقَدْ جِئْتِ شَيْئًا فَرِيًّا ﴿٢٧﴾

Akawafikia watu wake akiwa amembeba (mtoto); wakasema: “Ee Maryam! Kwa yakini umeleta jambo lisilopata kusikika, kuu na ovu mno. 

 

 

يَا أُخْتَ هَارُونَ مَا كَانَ أَبُوكِ امْرَأَ سَوْءٍ وَمَا كَانَتْ أُمُّكِ بَغِيًّا ﴿٢٨﴾

 “Ee dada wa Haaruwn! Hakuwa baba yako mtu muovu, na wala hakuwa mama yako kahaba.”

 

فَأَشَارَتْ إِلَيْهِ ۖ قَالُوا كَيْفَ نُكَلِّمُ مَن كَانَ فِي الْمَهْدِ صَبِيًّا ﴿٢٩﴾

Akamuashiria. Wakasema: “Vipi tuseme na aliye kwenye susu, bado mtoto?”

 

قَالَ إِنِّي عَبْدُ اللَّـهِ آتَانِيَ الْكِتَابَ وَجَعَلَنِي نَبِيًّا ﴿٣٠﴾

 (Mtoto) Akasema: “Hakika mimi ni mja wa Allaah; Amenipa Kitabu (Injiyl) na Amenijaalia kuwa Nabiy.”

 

وَجَعَلَنِي مُبَارَكًا أَيْنَ مَا كُنتُ وَأَوْصَانِي بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ مَا دُمْتُ حَيًّا ﴿٣١﴾

 “Na Amenijaalia kuwa mwenye kubarikiwa popote nitakapokuweko, na Ameniusia Swalaah na Zakaah madamu niko hai.”  [Maryam: 27-31]

 

Nabii Muwsaa (‘Alayhis Salaam) pia alipoanza tu kupewa risala, ilikuwa ni ukumbusho wa Swalaah: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَهَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ مُوسَىٰ ﴿٩﴾

Na je, imekufikia hadithi ya Muwsaa?

 

 

إِذْ رَأَىٰ نَارًا فَقَالَ لِأَهْلِهِ امْكُثُوا إِنِّي آنَسْتُ نَارًا لَّعَلِّي آتِيكُم مِّنْهَا بِقَبَسٍ أَوْ أَجِدُ عَلَى النَّارِ هُدًى ﴿١٠﴾

Alipouona moto akawaambia ahli zake: “Bakieni (hapa); kwa yakini nimeona moto, huenda nikakuleteeni kutoka humo kijinga cha moto, au nipate kwenye huo moto mwongozo.

 

فَلَمَّا أَتَاهَا نُودِيَ يَا مُوسَىٰ ﴿١١﴾

Basi alipoufikia, aliitwa: “Ee Muwsaa!

 

إِنِّي أَنَا رَبُّكَ فَاخْلَعْ نَعْلَيْكَ ۖ إِنَّكَ بِالْوَادِ الْمُقَدَّسِ طُوًى ﴿١٢﴾

 “Hakika Mimi ni Rabb wako; basi vua viatu vyako, kwani wewe hakika uko katika bonde takatifu la Twuwaa.

 

وَأَنَا اخْتَرْتُكَ فَاسْتَمِعْ لِمَا يُوحَىٰ ﴿١٣﴾

 “Nami nimekuchagua; basi sikiliza kwa makini yanayofunuliwa Wahy (kwako).

 

إِنَّنِي أَنَا اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدْنِي وَأَقِمِ الصَّلَاةَ لِذِكْرِي ﴿١٤﴾

 “Hakika mimi ni Allaah hapana Muabudiwa wa haki ila Mimi; basi niabudu, na simamisha Swalaah kwa ajili ya kunidhukuru. [Twaahaa: 9-14]

 

 

Nabii Ismaa'iyl (‘Alayhis Salaam) amesifiwa kwa kuamrisha watu wake Swalaah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِسْمَاعِيلَ ۚ إِنَّهُ كَانَ صَادِقَ الْوَعْدِ وَكَانَ رَسُولًا نَّبِيًّا ﴿٥٤﴾

Na mtaje katika Kitabu Ismaa’iyl. Hakika yeye alikuwa mkweli wa ahadi na alikuwa Rasuli na Nabiy.

 

وَكَانَ يَأْمُرُ أَهْلَهُ بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ وَكَانَ عِندَ رَبِّهِ مَرْضِيًّا ﴿٥٥﴾

Na alikuwa akiwaamrisha ahli zake Swalaah na Zakaah, na alikuwa mridhiwa mbele ya Rabb wake. [Maryam: 54-55]

 

 

Hivyo basi Swalaah ni ‘ibaadah iliyo muhimu kupita zote kutokana dalili hizo na pia kwa ajili ya uhusiano wetu na Rabb wetu Aliyetuumba  Akatuamrisha kumwabudu Yeye pekee kama Anavyosema:

 

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾

Na Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu. [Adh-Dhaariyaat: 56]

 

 

 

 

Share

04-Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake: Maamrisho Ya Swalah Kwetu

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

04- Maamrisho Ya Swalah Kwetu

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Amemuamrisha Rasuli Wake (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na sisi kuamrisha familia zetu na watu wetu kutekelza Swalaah, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا

Na amrisha ahli zako Swalaah, na dumisha kusubiri kwayo [Twaahaa: 132]

 

Aayah hiyo tukufu inatupa dokezo kwamba kudumisha Swalaah ni jambo gumu hasa kwa watoto na vijana wetu. Hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatutia nguvu kwa kututaka tusichoke kuimarisha ibaadah hii, bali tuendelee nayo kwa kuvumilia tabu zake.

 

Swalaah huwa nzito kwa wengi wanapokuwa usingizini. Lakini haitupasi kuwaonea huruma watoto wetu na wanaotuhusu kuwaamsha kwa ajili ya kuswali, kwani  kufanya hivyo haimaanishi kuwa ni kuwapenda bali ni kuwaangamiza kwa sababu Muislamu anapodumisha Swalaah yake, hujiepusha na maovu na machafu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ

na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari.  [Al-'Ankabuwt: 45]

 

 

Na maovu humpeleka mtu motoni, na moto huo ndio tuliotahadharishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) tujikinge nao:   

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴿٦﴾

Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika washupavu hawana huruma, shadidi, hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. [At-Tahriym: 6]

 

 

Naye Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) vile vile ametuamrisha Swalaah, akatusisitiza na kutubainishia fadhila na malipo yake adhimu:

 

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى اللّه عليه وسلم أنه قال: ((مُرُوا أَوْلادَكُمْ بِالصَّلاةِ وَهُمْ أَبْنَاءُ سَبْعِ سِنِينَ، وَاضْرِبُوهُمْ عَلَيْهَا وَهُمْ أَبْنَاءُ عَشْرٍ، وَفَرِّقُوا بَيْنَهُمْ فِي الْمَضَاجِعِ))    البخاري

Kutoka kwa Abuu Hurayrah  (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)    amesema: “Amrisheni watoto wenu kuswali wakiwa na umri wa miaka saba, na wapigeni (pigo khafifu wakiwa hawataki kuswali) wakiwa na umri wa miaka kumi, na watenganisheni vitanda.”(kuwatenganisha wasichana na wavulana vyumbani) [Al-Bukhaariy]

 

 

Amri ya kukidhi Swalaah:

 

Swalaah inapaswa kukidhiwa kwa mwenye kuisahau au kwa mwenye kupitiwa kwa usingizi:

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍعَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ ((مَنْ نَسِيَ صَلَاةً فَلْيُصَلِّ إِذَا ذَكَرَهَا لَا كَفَّارَةَ لَهَا إِلَّا ذَلِكَ))   الصحيحين و سننابن ماجة و الترمذي

 

Kutoka kwa Anas bin Maalik kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kusahau Swalaah, aswali atakapokumbuka na hakuna kafara isipokuwa hivyo)) [Al-Bukhaariy, Muslim, Sunan Ibn Maajah na At-Tirmidhy]

 

Na katika Riwaayah nyingine:

 

(( مَنْ نَسِىَ صَلاَةً  أَوْ نام عَنْها فَكَفَّارَتها أنْ يُصَلِّيها  إِذَا ذَكَرَهَا ، لاَ كَفَّارَةَ لَهَا إِلاَّ ذَلِكَ))  رواه مسلم 

 

((Atakayesahau Swalaah au ikampita akiwa amelala basi kafara yake ni kuiswali atakapokumbuka, hakuna kafara isipokuwa hiyo)) [Muslim]

 

Hii ni rahmah ya Allaah kwetu sisi waja kwamba tumepewa udhuru  kama huo wa kusahau au kupitiwa na usingizi katika ibaadah muhimu kama hii. Inamaanisha kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Hatukalifishi kwa mambo yanayotushinda nguvu. Na ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alipowatakabalia Waumini katika du'aa yao walipomuomba:

 

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ ۗ رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تُحَمِّلْنَا مَا لَا طَاقَةَ لَنَا بِهِ ۖ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا ۚ أَنتَ مَوْلَانَا فَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ ﴿٢٨٦﴾  

Allaah Hakalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake.  Itapata (thawabu) iliyoyachuma, na ni dhidi yake (kwa maovu) iliyojichumia. “Rabb wetu Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Rabb wetu, Usitubebeshe mzigo kama Ulivyoubebesha juu ya wale waliokuwa kabla yetu. Rabb wetu, Usitutwike tusiyoyaweza, na Tusamehe, na Tughufurie na Turehemu, Wewe ni Mola Mlinzi wetu, basi Tunusuru dhidi ya watu makafiri. [Al-Baqarah: 286]

 

 

 

 

 

Share

05-Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake: Ni 'Ibaadah Muhimu Kabisa

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

05- Swalaah Ni ‘Ibaadah Muhimu Kabisa

 

Alhidaaya.com

 

 

 Swalaah ni ‘ibaadah muhimu kabisa kuliko zote nyinginezo kwa sababu:

 

 

1-Swalaah ni nguzo pekee ya Kiislamu iliyofaridhishwa kutoka mbingu ya saba:

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ رضي الله عنه حديث الإسراء المشهور، وفيه أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ:

  ((فَأَوْحَى اللَّهُ إِلَيَّ مَا أَوْحَى فَفَرَضَ عَلَيَّ خَمْسِينَ صَلَاةً فِي كُلِّ يَوْمٍ وَلَيْلَةٍ، فَنَزَلْتُ إِلَى مُوسَى صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: مَا فَرَضَ رَبُّكَ عَلَى أُمَّتِكَ؟ قُلْتُ خَمْسِينَ صَلَاةً. قَالَ ارْجِعْ إِلَى رَبِّكَ فَاسْأَلْهُ التَّخْفِيفَ... قَالَ  فَلَمْ أَزَلْ أَرْجِعُ بَيْنَ رَبِّي تَبَارَكَ وَتَعَالَى وَبَيْنَ مُوسَى عَلَيْهِ السَّلَام حَتَّى قَالَ: يَا مُحَمَّدُ إِنَّهُنَّ خَمْسُ صَلَوَاتٍ كُلَّ يَوْمٍ وَلَيْلَةٍ، لِكُلِّ صَلَاةٍ عَشْرٌ، فَذَلِكَ خَمْسُونَ صَلَاةً))  روى البخاري (349) ومسلم (162)

 

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuhusu Hadiyth ya Al-Israa Wal Mi’raaj iliyo mashuhuri ambayo imeendelea kusema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kisha Allaah Akanifunulia Wahy Akanifaridhisha Swalaah khamsini kwa kila siku moja na usiku wake. Nikateremka kwa Muwsaa ('Alayhis-Salaam) akauliza: “Amekufaridhisha nini Rabb wako kwa ummah wako.” Nikasema:  Swalaah khamsini. Akasema: “Rudi kwa Rabb wako na muombe takhfifu (Akupunguzie)) Akasema: ((Nikawa naendelea kurudi baina ya Rabb wangu Tabaaraka wa Ta’aalaa na baina Muwsaa mpaka (Allaah) Akasema: Yaa Muhammad! Hizo ni Swalaah khamsini kila siku moja na usiku wake, lakini kila Swalaah ni (thawabu) kumi, kwa hiyo (jumla ni thawabu (khamsini)) [Al-Bukhaariy (349), Muslim (162)]

 

 

2-Swalaah imeanzwa kutajwa katika Suwrah ya pili tu katika Mswahafu na ni miongoni mwa sifa za Waumini watakaofuzu:

 

 الم ﴿١﴾

Alif Laam Miym.

 

 

ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ ﴿٢﴾

Hiki ni Kitabu kisicho na shaka ndani yake, ni mwongozo kwa wenye taqwa.

 

 

الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣﴾

Ambao huamini ya ghayb na husimamisha Swalaah na katika vile Tulivyowaruzuku hutoa. [Al-Baqarah: 1-3]

 

 

 

3-Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametuamrisha Swalaah mara nyingi katika Qur-aan. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَارْكَعُوا مَعَ الرَّاكِعِينَ ﴿٤٣﴾

Na simamisheni Swalaah na toeni Zakaah na rukuuni pamoja na wanaorukuu (katika utiifu). [Al-Baqarah: 43]

 

 

 Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾

Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja kwa ajili Yake. [Al-Kawthar: 2]

 

 

 Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

  وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾

Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. [Al-Baqarah: 45]

 

 Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 

 حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ﴿٢٣٨﴾

Shikamaneni na Swalaah na khaswa Swalaah ya katikati (Alasiri), na simameni mbele ya Allaah katika hali ya utiifu [Al-Baqarah: 238]

 

 

 Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ ۚ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ﴿١١٤﴾

Na simamisha Swalaah katika ncha mbili za mchana na sehemu ya kwanza ya usiku; hakika mema yanaondosha maovu. Hivyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.  [Huwd: 114]

 

 Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 

 أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَىٰ غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ ۖ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا ﴿٧٨﴾

Simamisha Swalaah tokea kupinduka hadi kukuchwa jua mpaka kiza cha usiku na Qur-aan ya (Swalaah ya) Alfajiri. Hakika Qur-aan ya Alfajiri ni yenye kushuhudiwa. [Al-Israa: 78]

 

 

 Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلَاةَ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمْ ۚ فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۚ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا ﴿١٠٣﴾

Mtakapomaliza Swalaah, mdhukuruni Allaah msimamapo, na mkaapo na mnapolala ubavuni mwenu Mtakapopata utulivu, simamisheni Swalaah (kama desturi), hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu [An-Nisaa: 103]

 

 

4-Luqmaan alimpa wasiya  mwanawe akataja Swalaah mwanzo kabisa:

 

يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا أَصَابَكَ ۖ إِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴿١٧﴾

  “Ee mwanangu! Simamisha Swalaah, na amrisha mema na kataza ya munkari, na subiri juu ya yale yatakayokusibu. Hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa. [Luqmaan: 17]

 

 

 

5- Swalaah ni nguzo ya pili katika nguzo tano za Kiislamu.

 

 

6-Hakuna mwenye udhuru na Swalaah za fardhi; si mgonjwa wala msafiri, hata Muislamu akiwa vitani amewekewa aina yake ya kuswali. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِذَا ضَرَبْتُمْ فِي الْأَرْضِ فَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَقْصُرُوا مِنَ الصَّلَاةِ إِنْ خِفْتُمْ أَن يَفْتِنَكُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ إِنَّ الْكَافِرِينَ كَانُوا لَكُمْ عَدُوًّا مُّبِينًا ﴿١٠١﴾

Na mtakaposafiri katika ardhi basi si dhambi kwenu kufupisha Swalaah mkikhofu kwamba waliokufuru watakushambulieni. Hakika makafiri wamekuwa kwenu ni maadui dhahiri. 

 

 

وَإِذَا كُنتَ فِيهِمْ فَأَقَمْتَ لَهُمُ الصَّلَاةَ فَلْتَقُمْ طَائِفَةٌ مِّنْهُم مَّعَكَ وَلْيَأْخُذُوا أَسْلِحَتَهُمْ فَإِذَا سَجَدُوا فَلْيَكُونُوا مِن وَرَائِكُمْ وَلْتَأْتِ طَائِفَةٌ أُخْرَىٰ لَمْ يُصَلُّوا فَلْيُصَلُّوا مَعَكَ وَلْيَأْخُذُوا حِذْرَهُمْ وَأَسْلِحَتَهُمْ ۗ وَدَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْ تَغْفُلُونَ عَنْ أَسْلِحَتِكُمْ وَأَمْتِعَتِكُمْ فَيَمِيلُونَ عَلَيْكُم مَّيْلَةً وَاحِدَةً ۚ وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن كَانَ بِكُمْ أَذًى مِّن مَّطَرٍ أَوْ كُنتُم مَّرْضَىٰ أَن تَضَعُوا أَسْلِحَتَكُمْ ۖ وَخُذُوا حِذْرَكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ أَعَدَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا ﴿١٠٢﴾

Na utapokuwa upo kati yao, ukawaswalisha, basi lisimame kundi miongoni mwao pamoja nawe, na wachukue silaha zao. Watakaposujudu basi wawe nyuma yenu (kuwalinda). Na lije kundi jingine ambalo halikuswali, liswali pamoja nawe, nao washike hadhari na silaha zao. Wale waliokufuru wanatamani kama mtaghafilika na silaha zenu na vifaa vyenu wakuvamieni mvamio mmoja. Na wala si dhambi kwenu ikiwa mna maudhiko kutokana na mvua au mkiwa wagonjwa kuweka (chini) silaha zenu. Na mshike hadhari zenu. Hakika Allaah Amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.

 

فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلَاةَ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمْ ۚ فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۚ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا ﴿١٠٣﴾

Mtakapomaliza Swalaah, mdhukuruni Allaah msimamapo, na mkaapo na mnapolala ubavuni mwenu Mtakapopata utulivu, simamisheni Swalaah (kama desturi), hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu. [An-Nisaa: 101-103].

 

 

7- Swalaah ni ‘ibaadah pekee iliyowekewa masharti kama twahara, mavazi na khasa kuelekea Qiblah.

 

 

8- Anaposwali mtu, hutumia viungo vyote vya mwili; moyo, akili na ulimi.

 

9-Hairuhusiwi kushughulika kufanya lolote jengine wakati wa kuitekeleza Swalaah wala kuzungumza hata kuleta mawazo mengine ili ipatikane khushuu.

 

 

10- Swalaah ni ‘amali bora kabisa Anayoipenda Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuliko jihaad  pindi akitimiza mja kwa wakati wake:

 

 

عن أبي مسعود رضي الله عنه قال: سألت رسول الله صلى الله عليه و سلم، أي الأعمال أفضل ؟ قال :((الصلاة على وقتها))، قلت ثم أي ؟ قال: ((بر الوالدين))  قلت ثم أي؟ قال: ((الجهاد في سبيل الله)) متفق عليه

Kutoka kwa Abdullaah bin Mas'uud (Radhwiya Allaahu 'anhu ambaye amesema: "Nilimuuliza Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni amali gani inayopendeza kwa Allaah? Akajibu: ((Ni kuswali kwa wakti wake)). Nikamuuliza tena: Kisha ni amali gani? Akajibu: ((Ni kuwafanyia ihsani wazazi)). Nikamuuliza tena: Kisha ni amali gani? Akajibu: ((Ni kupigana Jihaad katika njia ya Allaah)) [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

 

 

Share

06-Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake: Fadhila Za Swalah

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

06-Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake: Fadhila Za Swalaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Fadhila za Swalaah ni nyingi na tukufu mno, lau kila Muislamu atazitambua na kuzipima uzito wake, basi hakuna atakayetaka kuzikosa. Tumebashiriwa fadhila zake katika Aayah na Hadiyth nyingi, miongoni mwazo ni:

 

 

1- Swalaah inabashiria kumwepusha Muislamu kutokana na machafu na maovu na hufutiwa madhambi:  

 

 اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ

Soma (ee Muhammad Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) uliyoletewa Wahy katika Kitabu na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari. [Al-‘Ankabuwt: 45]

 

 

 Na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((أَرَأَيْتُمْ لَوْ أَنَّ نَهْرًا بِبَابِ أَحَدِكُمْ يَغْتَسِلُ مِنْهُ كُلَّ يَوْمٍ خَمْسَ مَرَّاتٍ هَلْ يَبْقَى مِنْ دَرَنِهِ شَيْءٌ؟)) قَالُوا: لَا يَبْقَى مِنْ دَرَنِهِ شَيْءٌ. قَالَ: ((فَذَلِكَ مَثَلُ الصَّلَوَاتِ الْخَمْسِ يَمْحُو اللَّهُ بِهِنَّ الْخَطَايَا))     رواه البخاري ومسلم

 

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:Mnaonaje kungekuwa na mto mlangoni mwa mmoja wenu na akaoga mara tano kwa siku. je, atabakiwa na tone la uchafu (mwilini mwake)?”  Wakasema: “Hatabakiwa na tone la uchafu.” Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ”Basi hivyo ni mfano wa Swalaah tano ambazo Allaah Anafuta madhambi kwazo.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Na pia Hadiyth ya:

 

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ ((الصَّلَاةُ الْخَمْسُ، وَالْجُمْعَةُ إِلَى الْجُمْعَةِ، كَفَّارَةٌ لِمَا بَيْنَهُنَّ، مَا لَمْ تُغْشَ الْكَبَائِرُ)) رواه مسلم

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swalaah tano na Ijumaa hadi Ijumaa ni kafara baina yao madamu hayafanywi Al-kabaair [madhambi makubwa])) [Muslim]

 

 

Pia:

 

 

عَنْ عُثْمَانَ بْنِ عَفَّانَ، قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((مَنْ تَوَضَّأَ لِلصَّلَاةِ فَأَسْبَغَ الْوُضُوءَ، ثُمَّ مَشَى إِلَى الصَّلَاةِ الْمَكْتُوبَةِ، فَصَلَّاهَا مَعَ النَّاسِ أَوْ مَعَ الْجَمَاعَةِ أَوْ فِي الْمَسْجِدِ غَفَرَ اللهُ لَهُ ذُنُوبَه)) مسلم

Kutoka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Atakayetawadha kwa ajili ya Swalaah, akafanya vizuri wudhuu wake kisha akaenda kuswali Swalaah za fardhi akaziswali pamoja na watu au jamaa au Msikitini Allaah Atamfutia madhambi yake)) [Muslim]

 

 

 

2- Swalaah inabashiria kwamba ni nuru:

 

  (( الصلاة نور)) رواه مسلم والترمذي

 

((Swalaah ni nuru)) [Muslim na At-Tirmidhiy

 

 

 

3-Swalaah inabashiria kupandishwa daraja na kufutiwa dhambi kwa kila sajdah moja:

 

 

 ‏‏((ما مِن عبدٍ يسجدُ للَّهِ سَجدةً إلَّا كتبَ اللَّهُ لَهُ بِها حسنةً، ومحا عنهُ بِها سيِّئةً، ورفعَ لَهُ بِها درجةً، فاستَكْثروا منَ  السُّجُود))   رواه ابن ماجه

((Mja yeyote atakayesujudu sajda moja ataandikiwa wema mmoja, na atafutiwa baya moja, na atapandishwa daraja yake, kwa hiyo, zidisheni kusujudu)) [Ibn Maajah]  

 

 

 

4-Swalaah inabashiria kumuingiza Muislamu Jannah:

 

 

 عن أَبِي موسى الأشعرِيِّ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّه صلى الله عليه وسلم: ((منْ صلَّى الْبَرْديْنِ دَخَلَ الْجنَّةَ)) متفقٌ عَلَيهِ

Kutoka kwa Abuu Muusa kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((AtakayeswaliAl-Bardayn (Swalaah ya Alfajiri na 'Ishaa) ataingia Jannah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

5- Swalaah inabashiria kuwa karibu na Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huko Jannah:

 

 

 عن أبي فراس رَبِيعَة بْن كَعْبٍ الْأَسْلَمِيُّ رضي الله عنه    خادم رسول الله صلى الله عليه وسلم قَالَ: كُنْتُ أَبِيتُ مَعَ رَسُولِ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَأَتَيْتُهُ بِوَضُوئِهِ وَحَاجَتِهِ، فَقَالَ لِي: ((سَلْني)) فَقُلْتُ: أَسْأَلُكَ مُرَافَقَتَكَ فِي الْجَنَّةِ، قَالَ: ((أَوْ غَيْرَ ذَلِكَ؟))  قُلْتُ: هُوَ ذَاكَ، قَالَ: ((فَأَعِنِّي عَلَى نَفْسِكَ بِكَثْرَةِ السُّجُودِ)) رواه مسلم في  صحيحه

Kutoka kwa Abuu Firaas Rabiy'ah bin Ka'ab Al-Aslamiy mtumishi wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye amesema: "Nililala na Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) usiku mmoja nikamletea maji ya kutawadha, akaniambia: ((Niombe utakacho)) Nikasema: "Nataka kuandamana na wewe Jannah. Akasema: ((Hutaki lolote lingine?)) Nikasema: "Ni hilo tu."  Akasema:  ((Basi nisaidie (ili hilo liwezekane) kwa kuzidisha kusujudu [Kuswali])) [Muslim katika Swahiyh yake] 

 

 

6-Swalaah inabashiria kuombewa Rahmah na Malaika:

 

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((المَلاَئِكَةُ تُصَلِّي عَلَى أَحَدِكُمْ مَا دَامَ فِي مُصَلَّاهُ الَّذي صَلَّى فِيه مَا لَمْ يُحْدِثْ تُقُول: اللَّهُمَّ اغْفِرْ لَهُ، اللَّهُمَّ ارْحَمْهُ))  متفق عليه

 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Malaika wanamswalia mmoja wenu madamu amebakia sehemu aliyoswali ikiwa hakutengua wudhuu wake, (Malaika) Husema:  "Ee Allaah! Mghufurie, Ee Allaah Mrehemu.")) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

7-Swalaah inabashiria kubakia katika kuhifadhiwa na Allaah:

 

عن جندب بن عبدالله رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((مَن صَلَّى الصُّبحَ فَهُوَ فِي ذِمَّةِ اللَّهِ...))  مسلم (657)

 

Kutoka kwa Junub bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali asubuhi atakuwa katika hifadhi ya Allaah)) [Muslim]

 

 

 

8-Swalaah inabashiria kufutiwa madhambi yaliyotangulia:

 

 

عن أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِذَا قَالَ أَحَدُكُمْ آمِينَ وَقَالَتْ الْمَلَائِكَةُ فِي السَّمَاءِ آمِينَ فَوَافَقَتْ إِحْدَاهُمَا الْأُخْرَى غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ)) متفق عليه

 ((Atakaposema mmoja wenu (katika Swalaah) Aamiyn, na Malaika mbinguni wakasema Aamiyn, zikawafikiana pamoja, atafutiwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 Pale Waumini wanaposema: “Aamiyn” baada ya kusomwa Suwratul-Faatihah.

 

 

9-Swalaah inabashiria kujiepusha na unafiki:

 

  عن أَبي هُريرة رضيَ اللَّه عنهُ   قال : قال رسولُ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم : (( لَيْسَ صَلاةٌ أَثْقَلَ عَلَى المُنَافِقينَ مِنْ صلاة الفَجْرِ وَالعِشاءِ وَلَوْ يَعْلَمُونَ ما فِيهما لأَتَوْهُما وَلَوْ حبْوًا)) متفق عليه .

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna Swalaah iliyo nzito kwa wanafiki kama Swalaah ya Alfajiri na ‘Ishaa. Lau kama wangelijua yaliyomo humo (fadhila na faida) wangeliziendea (kuziswali) japo kwa kutambaa)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Azidi kutuzindua na Atuzidishie iymaan na tawfiyq ya hidaaya tutekeleze ‘ibaadah hii tukufu ili tutimize nguzo hii adhimu ya Kiislamu na tujaaliwe kuchuma thawabu na fadhila nyingi za Swalaah. Na tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atutakabalie Swalaah zetu, na tusiache kuomba du’aa Baba yetu Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) ili tuwe wenye kusimamisha Swalaah pamoja na vizazi vyetu:

 

رَبِّ اجْعَلْنِي مُقِيمَ الصَّلَاةِ وَمِن ذُرِّيَّتِي ۚ رَبَّنَا وَتَقَبَّلْ دُعَاءِ﴿٤٠﴾

 “Rabb wangu! Nijaalie niwe mwenye kusimamisha Swalaah na dhuria wangu. Rabb wetu! Nitakabalie du’aa yangu.” [Ibraahiym: 40]

 

 

 

 

 

 

Share

07-Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake: Adhabu Za Mwenye Kuacha Swalah

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

07-Adhabu Za Mwenye Kuacha Swalaah

 

Alhidaaya.com

 

  

Baadhi ya Waislamu huwa hawatilii mkazo kabisa Swalaah. Kuna wanaozipuuza kwa kutokuziswali kwa wakati wake, na kuna wasioswali kabisa. Na kwa vile Swalaah ni msingi wa Dini, na ni ‘ibaadah tukufu kabisa, basi wanapozidharau na kutokutimiza kuziswali, malipo yake ni mabaya mno ya kuweza kumfikisha mtu motoni. Adhabu kadhaa zimetajwa katika Qur-aan na Sunnah zikiwemo:

 

 

1-Wanaoacha kuswali watakutana na adhabu Motoni: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) :

 

فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ ۖ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا ﴿٥٩﴾

Wakafuata baada yao waovu, walipoteza Swalaah na wakafuata matamanio; basi watakutana na adhabu motoni. [Maryam: 59]

 

 

'Abdullaahi bin Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema kuhusu “watakutana na adhabu motoni.” ina maana ni "bonde la moto lililokuwa refu lenye chakula kichafu kabisa" [At-Twabariy 18:218]

 

 

 

2-Makazi ya wasioswali yatakuwa ni motoni na watakapoulizwa na wakaazi wa Jannah sababu ya kuwafikisha motoni,  watakiri kuwa sababu mojawapo ni kwa sababu ya kutokuswali. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ﴿٣٨﴾

Kila nafsi iko katika rehani kwa yale iliyoyachuma.

 

إِلَّا أَصْحَابَ الْيَمِينِ﴿٣٩﴾

Isipokuwa watu wa kuliani.

 

 

فِي جَنَّاتٍ يَتَسَاءَلُونَ﴿٤٠﴾

Katika Jannaat wanaulizana.

 

 

عَنِ الْمُجْرِمِينَ﴿٤١﴾

Kuhusu wahalifu.

 

 

مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ﴿٤٢﴾

 (Watawauliza): “Nini kilichokuingizeni katika motoni?”

 

 

 

قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ﴿٤٣﴾

Watasema: “Hatukuwa miongoni mwa wanaoswali. [Al-Mudath-thir: 38-43]

 

 

 

Hayo yatakuwa ni malipo yao kwa sababu waliridhika na maisha ya dunia na anasa zake hadi wakasahau kama kuna Rabb Aliyewaumba Akawaamrisha wamuabudu.

 

 

 

3-Wanaocha kuswali watapata adhabu ya moto kwa sababu kupuuza Swalaah zao kwa kutokuziswali ipasavyo; ima kwa kuswali na kuacha, au kutokuziswali kwa wakati wake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ ﴿٤﴾

Basi Ole kwa wanaoswali ...

 

 

الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ ﴿٥﴾

Ambao wanapuuza Swalaah zao. [Al-Maa'uwn: 4-5]

 

 

 

 

Neno 'wayl'  limetajwa mara kadhaa katika Qur-aan kuwa ni adhabu iwapatayo watu kwa sababu mbalimbali za maasi; mojawapo ikiwa ni kuacha Swalaah. Ni neno la kutisha lenye maana ya kudhalilishwa, kuadhibiwa na kungamizwa.  

 

 

 

4-Adhabu kali pia itawafikia wenye kuacha kuswali ambao hata unapowapa nasaha ya kuwakumbusha umuhimu wa kuswali n.k. hawasikii wala hawaogopi adhabu zake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ ارْكَعُوا لَا يَرْكَعُونَ﴿٤٨﴾

Na walipokuwa wakiambiwa “Rukuuni (mswali),” hawakuwa wakirukuu.

 

 

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُكَذِّبِينَ﴿٤٩﴾

Ole Siku hiyo kwa wenye kukadhibisha. [Al-Mursalaat: 48-49]

 

 

 

Ukaidi huo ni hapa duniani, lakini siku ya Qiyaamah watatamani wainamishe vichwa vyao wamsujudie Rabb wao lakini Hayhaata! Hayhaata! (Hayawi! Hayawi!) Hawatoweza Abadan kuinamisha vichwa vyao: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

يَوْمَ يُكْشَفُ عَن سَاقٍ وَيُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ﴿٤٢﴾

Siku utakapofunuliwa Muundi na wataitwa kusujudu lakini hawatoweza.

 

 

 

خَاشِعَةً أَبْصَارُهُمْ تَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ ۖ وَقَدْ كَانُوا يُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ وَهُمْ سَالِمُونَ﴿٤٣﴾

Macho yao yatainama chini, udhalilifu utawafunika. Na hali walikuwa wakiitwa wasujudu (kuswali duniani) walipokuwa wazima wa afya. [Al-Qalam: 42-43]

 

 

 

5-Vile vile asiyeswali atafufuliwa na watu waovu kabisa siku ya Qiyaamah kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو بن العاص عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنَّهُ ذَكَرَ الصَّلاةَ يَوْمًا فَقَالَ:  ((مَنْ حَافَظَ عَلَيْهَا كَانَتْ لَهُ نُورًا وَبُرْهَانًا وَنَجَاةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ، وَمَنْ لَمْ يُحَافِظْ عَلَيْهَا، لَمْ يَكُنْ لَهُ نُورٌ وَلا بُرْهَانٌ وَلا نَجَاةٌ وَكَانَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مَعَ قَارُونَ وَفِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَأُبَيِّ بْنِ خَلَفٍ)) أخرجه الإمام أحمد في مسنده

 

Kutoka kwa 'Abdullaah bin 'Amru ibn Al-'Aaasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba siku moja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitaja kuhusu Swalaah akasema: ((Atakayeihifadhi atakuwa na nuru na uongofu, na kufuzu siku ya Qiyaamah, na asiyeihifadhi hatokuwa na nuru wala uongofu wala kufuzu, na siku ya Qiyaamah atakuwa pamoja na Qaaruwn, Fir'awn, Haaman na Ubayy bin Khalaf)) [Musnad Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh]

 

 

Katika kuifasiri Hadiyth hii, Ibn Al-Qayyim Al-Jawziy (Rahimahu Allaah) amesema: “Mwenye kuacha Swalaah huwa ameshughulika na mojawapo kati ya yafuatayo: Ima atakuwa imemshughulisha mali yake au ufalme wake au cheo chake au biashara zake. Yule aliyeshughulika na mali yake, atafufuliwa pamoja na Qaaruwn, na aliyeshughulika na ufalme wake, huyo atakuwa pamoja na Fir'awn, na aliyeshughulika na cheo chake atakuwa pamoja na Haaman na yule aliyeshughulika na biashara zake (akaacha kuswali), huyo atakuwa pamoja na Ubayy bin Khalaf.”

 

Ee ndugu Muislamu usiyeswali au kupuuza Swalaah yako, je haujafika wakati wa kukhofu adhabu hizi kali za Rabb wako? Je, utaridhika kufufuliwa na watu waovu kabisa badala ya wapenzi wako kwa sababu tu ya kushughulika na dunia na kuacha ‘Ibaadah ambayo hata dakika kumi haikuchukui kuitimiza?

 

 

 

Share

08-Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake: Hukmu Ya Taarikus-Swalah (Asiyeswali)

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

08- Hukmu Ya Taarikus-Swalaah (Asiyeswali)

 

Alhidaaya.com

 

 

‘Ulamaa wamekubaliana kuwa mwenye kuiacha Swalaah kusudi kwa jeuri na kwa kuikanusha, huyo anakuwa kafiri aliyekwisha toka katika Dini ya Kiislam.

 

Wakakhitalifiana juu ya yule mwenye kuiacha kwa uvivu tu au kwa kujishughulisha na dunia lakini haikanushi na anaamini kuwa ni fardhi juu yake. Wapo wanaosema hata huyu naye pia anakuwa kafiri aliyekwishatoka katika Dini ya Kiislam, na dalili walizoziegemea ni baadhi ya Hadiyth zifuatazo za Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عن جَابِر بن عبد الله عن النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهم عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قال: ((إِنَّ بَيْنَ الرَّجُلِ وَبَيْنَ الشِّرْكِ وَالْكُفْرِ تَرْكَ الصَّلَاةِ))   رواه مسلم  

Kutoka kwa Jaabir bin 'Abdillaah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Baina ya mtu na shirki, na kufru, ni kuacha Swalaah)) [Muslim]

 

 Na pia:

 

عَنْ بُرَيْدَةَ بن الحصيب  قال: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: ((إِنَّ الْعَهْدَ الَّذِي بَيْنَنَا وَبَيْنَهُمُ الصَّلاَةُ فَمَنْ تَرَكَهَا فَقَدْ كَفَرَ))  رواه أحمد وأبو داود والترمذي والنسائي وابن ماجه  

 

Kutoka kwa Buraydah bin Al-Haswiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu ambaye amesema: "Nimemsikia Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Ahadi (mafungamano) baina yetu na baina yao (wasio Waislam) ni Swalaah, atakayeiacha atakuwa amekufuru)) [Ahmad, Abu Daawuwd, An-Nasaaiy na Ibn Maajah]

 

 

Vile vile:

 

عن عَبْدِ اللَّهِ بْنِ شَقِيقٍ الْعُقَيْلِيِّ قال: " كَانَ أَصْحَابُ مُحَمَّدٍ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لَا يَرَوْنَ شَيْئًا مِنْ الْأَعْمَالِ تَرْكُهُ كُفْرٌ غَيْرَ الصَّلَاةِ"    رواه الترمذي (2622) وصححه الألباني في صحيح الترمذي

 

Kutoka kwa Abdillaah bin Shaqiyq ambaye amesema: “Maswahaba wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hawakuwa wakiona amali yoyote nyingine mtu akiiacha anakuwa kafiri isipokuwa Swalaah.” [At-Tirmidhiy na ameisahihisha Al-Albaaniy  katika Swahiyh At-Tirmidhiy (2622), Swahiyh At-Targhiyb (565)]

 

 

Anasema Ibn Hazm: “Imepokelewa kutoka kwa 'Umar bin Khatwtwaab na 'Abdur-Rahmaan bin 'Awf na Mu'aadh bin Jabal na Abuu Hurayrah na Maswahaba wengi (Radhwiya Allaahu 'anhum) kuwa: “Atakayeacha kuswali (Swalaah moja tu ya) fardhi kusudi (bila ya udhuru wowote) mpaka wakati wake (Swalaah hiyo) ukatoka, anakuwa kafiri.”

 

Hadiyth zifuatazo zinaelezea juu ya hukmu ya kuuliwa kwa Taarikus-Swalaah (Asiyeswali):

 

عن أُمِّ سَلَمَةَ  رضي الله عنها أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم قَالَ: ((سَتَكُونُ أُمَرَاءُ فَتَعْرِفُونَ وَتُنْكِرُونَ فَمَنْ عَرَفَ بَرِئَ وَمَنْ أَنْكَرَ سَلِمَ وَلَكِنْ مَنْ رَضِيَ وَتَابَعَ)) قَالُوا : أَفَلَا نُقَاتِلُهُمْ ؟ قَالَ: ((لَا مَا صَلَّوْا)) صحيح مسلم

Kutoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu 'anha) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watakuweko viongozi kwenu watakaoamrisha mema na maovu. Atakayechukia hivi vitendo (viovu) hatakuwa na hatia. Atakayevipinga atakuwa salama, lakini (siye) atakayevikubali na kufuata)). Wakauliza: "Je tuwaue?" Akasema: ((Hapana madamu  wanaswali)) [Muslim]

 

 

 عن ابنِ عُمَرَ رضي الله عنهما أنَّ رسُوَل الله صلى الله عليه وسلم قال: ((أُمِرْتُ أَنْ أُقاتِلَ النَّاسَ حتَّى يَشْهَدُوا أنْ لا إلَهَ إلاَّ اللهُ وأنَّ محمداً رسوُل اللهِ، ويُقِيمُوا الصَّلاَةَ، ويُؤتُوا الزَّكاةَ، فإذا فَعَلوا ذَلِكَ عَصَموا منِّي دِماءَهُمْ وأمْوَالَهُمْ إلا بِحَقِّ الإِسْلامِ، وحِسابُهُم على اللهِ تعالى)) رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ وَ مُسْلِمٌ   

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhuma) ambaye alisema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Nimeamrishwa nipigane vita na watu mpaka washuhudie kuwa hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na Muhammad ni Rasuli wa Allaah na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa Zakaah, na wakifanya hivyo, watakuwa wamepata himaya kwangu ya damu yao, na mali yao kwa haki ya Uislamu.  Na hesabu yao itakuwa kwa Allaah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kauli Za Baadhi Ya Wanavyuoni Kuhusu Taarikus-Swalaah:

 

 

Imaam An-Nawawy katika Sharh Muslim amesema:

 

“Anakatwa kichwa chake kwa upanga.”

 

Imaam Abu Haniyfah:

 

Anaona kuwa aliyertadi na akastahiki kuhukumiwa kuuliwa ni yule tu anayeikanusha ‘ibaadah hiyo ya Swalaah, lakini yule anayeacha kuswali kwa uvivu tu au kwa kujishughulisha na dunia, huyo si kafiri bali ni faasiq na hukmu yake ni kuhamishwa mbali na mji wake, wakiegemea dalili zinazobeba maana kwa ujumla kama vile kauli Yake Subhaanahu wa Ta’aalaa Anaposema:

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. [An-Nisaa: 116]

 

Na Hadiyth iliyosimuliwa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((لكلِّ نبيٍّ دعوةٌ مستجابةٌ . فتعَجَّلَ كلُّ نبيٍّ دعوتَه . وإنِّي اخْتَبأْتُ دَعوتي شفاعةً لأُمَّتي يومَ القيامةِ . فهي نائلةٌ ، إن شاءَ اللهُ ، من مات من أُمَّتي لا يُشركُ باللهِ شيئًا)) ‏مسلم

 

((Kila Rasuli wa Allaah  ana du'aa yake inayokubaliwa. Kila Rasuli wa Allaah anafanya haraka kuiomba du'aa yake hiyo. Ama mimi nimeiweka du'aa yangu kwa ajili ya kuwaombea shafaa’ah ummati wangu siku ya Qiyaamah. Ataipata In Shaa Allaah kila aliyekufa na hali hajamshirikisha Allaah na chochote)) [Muslim]

 

Na Hadiyth nyingine za mfano huo.

 

 

Sayyid Saabiq:

 

"Kutokana na Ayaah pamoja na Hadiyth zilizotangulia, inatubainikia kuwa asiyeswali ni kafiri na kwamba damu yake ni halali. Hata hivyo baadhi ya ‘Ulamaa waliotangulia na wa siku hizi wakiwemo Imaam Abuu Haniyfah na Imaam Shaafi'y na Imaam Ahmad wanasema kuwa hawi kafiri moja kwa moja, bali anahesabiwa kuwa ni mtu faasiq (muovu) na anakamatwa na kutubishwa na akikataa kutubu basi ‘Ulamaa wote hao wanasema kuwa mtu huyo anahukumiwa kuuliwa.”

 

 

‘Ulamaa wengine wakasema kuwa hauliwi mtu kwa ajili ya kutoswali, na hawa wameegemeza hoja zao kutokana na Hadiyth:

  

عن ابْنِ مَسْعُودٍ رضي اللهُ عنه قالَ: قالَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم: ((لاَ يَحِلُّ دَمُ امْرِئٍ مُسْلِمٍ إلاّ بإحْدَى ثَلاَثٍ: الثَّيِّبُ الزَّاني، وَالنَّفْسُ بالنّفْسِ، وَالتَّارِكُ لِدِيِنِهِ الْمُفَارِقُ لِلْجَماعَةِ)).  رَوَاهُ الْبُخَارِيّ وَمُسْلِمٌ    

Kutoka kwa Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allahu 'anhu) ambaye alisema: Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Damu ya Muislamu haiwezi kwa haki kumwagwa isipokuwa katika hali tatu:  Mzinzi aliyeoaolewa, uhai kwa uhai, na kwa yule anayeacha Dini na akajifarikisha na  jamaa’ah (amejitenga na watu wa Dini yake))  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Wanasema kuwa hapa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakumtaja asiyeswali kuwa ni miongoni wa waliohalalishwa damu yao.

 

Imaam Ash-Shawkaaniy amesema: 

 

"Kwa hakika asiyeswali ni kafiri, kwa sababu Hadiyth zote zilizopokelewa katika maudhui haya zinamwita hivyo (kuwa ni kafiri), na mpaka uliowekwa baina ya mtu anayestahiki kuitwa kafiri na yule asiyestahiki kuitwa kafiri ni Swalaah."

 

Kwa hiyo waliohukumiwa kuwa ni makafiri kwa sababu ya kutokuswali wanapofariki huwa haipasi kuoshwa, wala kukafiniwa wala haswaliwi wala hazikwi katika makaburi ya Waislamu wala watu wake hawamrithi bali mali yake inapelekwa Baytul-Maal ya Waislamu.

 

Ama ‘Ulamaa wengi rai  zao ni kwamba: Ikiwa Muislamu anakanusha Swalaah kwamba sio fardhi kwake, basi yeye ni kafiri na anatoka katika Uislamu, na hukmu yake ni kama iliyotajwa hapo juu hukumu ya kafiri. Ama ikiwa hakanushi Swalaah bali ni kudharau kwake, au uvivu basi atahesabika ni mtenda dhambi kubwa, lakini hatoki katika Uislamu. Anatakiwa kupewa siku tatu atubu. Atakapotubu ni kheri yake, na asipotubu anatakiwa kuuawa na hii inakuwa ni adhabu yake sio kwa sababu ya kuwa kafiri bali kwa kukataa kuswali. Hivyo huoshwa na kukafiniwa, na kuswaliwa na Waislamu na kuombewa maghfirah na kuzikwa katika makaburi ya Waislamu na pia anaweza kurithiwa. Kwa ujumla hukmu zote zinazomhusu Muislamu anayetenda madhambi zinakuwa sawa na yake anapokuwa hai na anapofariki.  [Fataawa Al-Lajnah Ad-Daaimah (6/49)]  

 

 

Share