Kuna Wakati Maalumu Kufunga Ndoa Katika Sheria Ili Ndoa Iwe Ya Baraka?

SWALI:

 

Assalaam alaykum, naomba nipatiwe ufafanuzi ni muda gani unafaa kwa ajili ya ndoa kwani natarijia kufunga ndoa mwezi ujao inshaallah. Ila kinachonitatiza nikuwa kuna muda maalum yaani saa ya kufunga ndoa, kwani nimeambiwa ili ndoa yako iwe na baraka unatakiwa umtafute sheikh akuambie muda gani unafaa ili ndoa ifungwe. Nafikiri ni mambo yanayotendeka ndani ya jamii yetu ya kiislam, naomba kama jambo hili lipo ndani ya dini yetu au ni mambo ya uzushi au ilishathibiti kipindi cha Mtume swalallahu aleih wassalaam.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu wakati maalumu wa kufunga ndoa. Hakika ni kuwa katika Dini yetu hakuna wakati maalumu wa kufunga ndoa. Unaweza kufunga wakati na mwezi wowote ambao umeafikiana na mkeo mtararajiwa au baada ya makubaliano ya familia mbili hizo. Ama kuwa katika baadhi ya jamii zetu hufanya ushirikina kwa kwenda kwa wachawi na wapigaji ramli ili wawaeleze wakati na tarehe ya kuoa. Kufanya hivyo ni dhambi kubwa sana katika Uislamu. Hakika ni kuwa Allaah Anatueleza kuwa shirki ni dhambi ambayo haisamehewi na Allaah kabisa (Suratun Nisaa (4): Aayah ya 48 na 116). Na amali ya mwenye kumshirikisha Allaah yote hupomoka na akaharibikiwa.

 

Ni nasaha yetu kuwa wewe usifuate ada na desturi zinazokwenda kinyume na Uislamu bali kuwa imara katika Uislamu wako na Allaah Aliyetukuka Atakupatia tawfiki.

 

Tukitazama historia ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) utakuta kuwa alioa katika tarehe na miezi tofauti.

Zifuatayo ni tarehe za ndoa zake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

1.     Sawdah bint Zam‘ah, ‘Aa’ishah bint Abu Bakr, Hafswah bint ‘Umar, Ummu Salamah Hind bint Abi Umayyah (Radhiya Allaahu ‘anhunna) aliwaoa Shawwaal (Mfungo Mosi).

2.     Juwayriyyah bint al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anha) – Sha‘abaan.

3.     Ummu Habiybah Ramlah bint Abi Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anha) – Muharram (Mfungo Nne).

4.     Maymunah bint al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anha) – Dhul Qa‘adah (Mfungo Pili).

 

Hii ni ishara ya wazi kuwa ndoa inaweza kufungwa wakati wowote kwa mujibu wa ndoa za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share