Kipengele Maalumu

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

03-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Shirki Ndogo - Riyaa (Kujionyesha)

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

03- Shirki Ndogo : Riyaa (Kujionyesha)

www.alhidaay.com

 

 

‘Amali zote zinahitaji kutangulizwa na niyyah safi. Hadiyth mashuhuri ambayo ‘Ulamaa wamesema kuhusu Hadiyth hii kwamba ni nusu ya ya Dini kama alivyosema Imaam Abu Daawuwd, kwani Dini inakusanya vilivyo dhahiri kama vitendo na visivyo dhahiri kama niyyah. 

 إِنَّما الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ وإنَّما لكُلِّ امْرِىءٍ ما نَوَى،    

Hakika ‘amali inategemea (malipo) kwa niyyah na kila mtu atapata kwa mujibu wa kila alichotilia niyyah. [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Imaam Ash-Shaafi’iy naye kasema Hadiyth hii ni nusu ya elimu. Naye Imaam Ahmad na Imaam Ash-Shaafi’iy wamesema Hadiyth hii inakusanya moja ya tatu ya elimu. Imaam Al-Bayhaqiy akafafanua maneno yao hayo kwa kusema, “Hayo ni kwa sababu, mtu huchuma thawabu kwa moyo wake, ulimi na mwili wake. Hivyo, niyyah inahusiana na moja ya viungo hivyo vitatu. [Ibn Hajr, Fat-h Al-Baariy, mj. 1, uk. 11]

 

Na sharti za kupokelewa ‘amali za mja ni ikhlaasw, niyyah safi ya ‘amali kwa kufuata amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyoamrisha:

 

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ ﴿٥﴾

Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara. [Al-Baayyinah: 5]

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا ﴿١١٠﴾

Hivyo anayetaraji kukutana na Rabb wake, basi na atende ‘amali njema na wala asimshirikishe yeyote katika ‘ibaadah za Rabb wake.” [Al-Kahf: 110]

 

Yaani asifanye riyaa (kujionyesha) ‘amali zake kwa watu kama Swalaah, Hajj, Swawm, Zakaah, Swadaqah, kusoma Qur-aan, kufanyia watu wema na ihsaan kwa ajili ya kusifiwa, kujitukuza au kuonekana ni mwema na sifa kama hizo za riyaa.

 

Na Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) aliwatahadharisha Swahaabah (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kuhusu riyaa. Siku ya Qiyaamah pindi mtu atakapokuja na ‘amali zake itatambulikana kama zilikuwa za ikhlaasw au za riyaa kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وآله وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لاَ يَنْظُرُ إِلى أجْسمِكُمْ وَلاَ إِلَى صُوَرِكُمْ وَلَكِنْ يَنْظُرُ إِلَى قُلُوبِكُمْ)) رواه مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Allaah Hatazami viwiliwili vyenu wala sura zenu, lakini Anatazama nyoyo zenu)). [Muslim]

 

Nyoyo ndizo zitakazodhihirisha ikhlaasw ya mtu kwani humo ndipo kunapofichika shirki kama ilivyobainishwa katika Hadiyth ifauatayo:

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ، قَالَ: خَرَجَ عَلَيْنَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَنَحْنُ نَتَذَاكَرُ الْمَسِيحَ الدَّجَّالَ، فَقَالَ: ((أَلا أُخْبِرُكُمْ بِمَا هُوَ أَخْوَفُ عَلَيْكُمْ عِنْدِي مِنَ الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ؟)) قَالَ: قُلْنَا: بَلَى! فَقَالَ: ((الشِّرْكُ الْخَفِيُّ، أَنْ يَقُومَ الرَّجُلُ يُصَلِّي، فَيُزَيِّنُ صَلاتَهُ، لِمَا يَرَى مِنْ نَظَرِ رَجُلٍ)) سنن ابن ماجه (4204).

Imepokelewa kutoka kwa Abu Sa’iyd (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja kwetu wakati tulikuwa tukijadiliana kuhusu Dajjaal, akasema: ((Je, niwajulisheni kile nikikhofiacho zaidi kwenu kuliko hata (hatari za) Dajjaal?)) Tukasema: Ndio. Akasema: ((Basi ni shirki iliyojificha. Mtu anasimama kuswali, anaipamba na kuiremba Swalaah yake kwa kujua kuwa kuna watu wanamtazama)) [Sunan Ibn Maajah (4204)]

 

Hiyo ni kama sifa ya wanafiki wanaomhadaa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema:

 

 إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿١٤٢﴾

Hakika wanafiki (wanadhani) wanamhadaa Allaah, na hali Yeye (Allaah) Ndiye Mwenye kuwahadaa. Na wanaposimama kuswali husimama kwa uvivu, wakijionyesha kwa watu na wala hawamdhukuru Allaah isipokuwa kidogo tu. [An-Nisaa: 142]

 

Share

Tarjama Ya Maana Ya Qur-aan (Translation Of The Meaning Of Al-Qur-aan)

Bonyeza Hapa Kwa Faida Ziada

Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

41-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Nabiy Pekee Aliyejaaliwa Fadhila Tele Za Kumswalia

 

Fadhila Za  Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم) 

41-Nabiy Pekee Aliyejaaliwa Fadhila Tele Za Kumswalia

www.alhidaaya.com

 

 

قال رَسولُ الله صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ صَلَّى عَلَيَّ صَلَاةً صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ بِهَا عَشْرًا))

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وسلم) amesema: ((Atakayeniswalia mara moja basi Allaah Atamswalia mara kumi)) [Hadiyth ya Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  - Muslim (1/288) [408] Amesema Al-Bukhaariy katika Swahiyh yake: Abul Al-‘Aaaliyah amesema: “Swalaah ya Allaah ni kumsifu kwake mbele ya Malaika na Swalaah ya Malaika ni du’aa”]

 

وَقال رَسولُ الله صلى الله عليه وسلم: ((لا تجعلوا قبري عيدا، وصلوا علي فإن صلاتكم تبلغني حيث كنتم))

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وسلم) amesema: ((Msilifanye kaburi langu kuwa ni mahali pa kufanya ‘Ibaada inayorejewa na niswalieni kwani kuniswalia kwenu kunanifikia popote mlipo)) [Hadiyth ya Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)   - Abu Daawuwd (2/218) [2042], Ahmad (2/367) na ameisahihisha Al-Albaaniy (رحمه الله) katika Swahiyh  Abi Daawuwd (2/383)]

 

 

وَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ لِلَّهِ مَلائِكَةً سَيَّاحِينَ فِي الأَرْضِ يُبَلِّغُونِي مِنْ أُمَّتِي السَّلام))

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وسلم) amesema: ((Hakika Allaah Ana Malaika wanamzunguka katika ardhi, wananiletea salamu kutoka kwa Ummah wangu))  [Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Mas-‘uwd (رضي الله عنه)  -  An-Nasaaiy (3/43), Al-Haakim (2/421) na ameisahihisha  katika Swahiyh An-Nasaaiy  (1/274)]

 

 

وَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم َ: ((مَا مِنْ أحَدٍ يُسَلِّمْ علَيَّ إلاَّ رَدَّ اللهُ رُوحِي حَتَّى أَرُدَّ عَلَيْهِ السَّلامَ))

Na pia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وسلم) amesema: ((Hakuna mtu yeyote anayeniswalia ila Allaah hunirudisha roho yangu ili nimrudishie salamu))  [Hadiyth ya Abu Hurayrah (رضي الله عنه)  - Abu Daawuwd  (2041), na Al-Albaaniy (رحمه الله) ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh Abi Daawuwd (1/283)]

 

Share

Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

41-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Unyenyekevu Wake: Akitembelea Wagonjwa Hata Wasio Waislamu

 

Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم)

41-Unyenyekevu Wake  Akitembelea Wagonjwa Hata Wasio Waislamu

www.alhidaaya.com

 

 

 

 عَنْ ثَابِتٍ عَنْ أَنَسٍ رَضِي اللَّهُ عَنْهُ قَالَ: كَانَ غُلَامٌ يَهُودِيٌّ يَخْدُمُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَمَرِضَ، فَأَتَاهُ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَعُودُهُ فَقَعَدَ عِنْدَ رَأْسِهِ، فَقَالَ لَهُ: أَسْلِمْ فَنَظَرَ إِلَى أَبِيهِ وَهُوَ عِنْدَهُ فَقَالَ لَهُ: أَطِعْ أَبَا الْقَاسِمِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَسْلَمَ فَخَرَجَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَهُوَ يَقُولُ: الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي أَنْقَذَهُ مِنَ النَّارِ ((البخاري

Kutoka kwa Thaabit, kutoka kwa Anas (Radhwiya-Allaahu ‘anhu) amesema:  Alikuweko mtoto wa ki-Yahudi akimhudumia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa anaumwa. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtembelea. Akaketi karibu ya kichwa chake na akamtaka asilimu. Yule mtoto akamtazama baba yake ambaye alikuwa ameketi karibu yake. Basi baba huyo akamwambia (mwanawe) amtii Abdul-Qaasim, na mtoto akatii na kusilimu. Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatoka nje akisema: ((AlhamduliLLaah Ambaye Amemkinga na moto)) [Al-Bukhaariy]

 

Share

Aayah Na Mafunzo

135-Aayah Na Mafunzo: Allaah Atakughufuria Madhambi Hata Kama Ukikariri Kumuasi

 

Aayah Na Mafunzo

Aal-‘Imraan

Allaah Atakughufuria Madhambi Hata Kama Ukikariri Kumuasi

Alhidaaya.com

 

 

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿١٣٥﴾

Na wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao (kwa maasi), humdhukuru Allaah wakaomba maghfirah kwa madhambi yao. Na nani anayeghufuria madhambi isipokuwa Allaah. Na hawaendelei katika waliyoyafanya na wao wanajua.

 

أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُم مَّغْفِرَةٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَجَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ ﴿١٣٦﴾

Hao jazaa yao ni maghfirah kutoka kwa Rabb wao na Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo. Na uzuri ulioje ujira wa watendaji (wema). [Aal-'Imraan 135-136]

 

 

Mafunzo:

 

Hakika fadhila nyingi kabisa zimetajwa katika Qur-aan na Sunnah kuhusu kuomba tawbah, mojawapo: Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): “Mja alifanya dhambi akasema: Ee Allaah, nighufurie dhambi zangu. Allaah (عزّ وجلّ) Akasema: Mja wangu kafanya dhambi akajua kuwa anaye Rabb wa kumghufuria dhambi na kuziondosha. Kisha akarudia kufanya dhambi tena akasema: Ee Allaah nighufurie dhambi zangu. Allaah (Tabaaraka wa Ta’aala) Akasema: Mja wangu kafanya dhambi akajua kuwa anaye Rabb wa kumghufuria dhambi na kuziondosha. Kisha akarudia kufanya dhambi tena akasema: Ee Allaah nighufurie dhambi zangu. Allaah (عزّ وجلّ) Akasema: Mja wangu kafanya dhambi akajua kuwa anaye Rabb wa kumghufuria dhambi na kuziondosha. Nakushuhudisheni kwamba Nimemghufuria na afanye mja Wangu atakavyo.” [Ahmad].

 

Share

Asbaabun-Nuzuwl

083-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Mutwaffifiyn

 

Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)

Suwrah Al-Mutwaffifiyn

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

083-Al-Mutwaffifiyn

 وَيْلٌ لِّلْمُطَفِّفِينَ ﴿١﴾

1. Ole kwa wanaopunja.

 

 

عَنَّ عِكْرِمَة، حَدَّثَهُ عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ، قَالَ لَمَّا قَدِمَ النَّبِيُّ  صلى الله عليه وسلم الْمَدِينَةَ كَانُوا مِنْ أَخْبَثِ النَّاسِ كَيْلاً فَأَنْزَلَ اللَّهُ سُبْحَانَهُ: ((وَيْلٌ لِلْمُطَفِّفِينَ))‏ فَأَحْسَنُوا الْكَيْلَ بَعْدَ ذَلِكَ ‏.‏

Ikrimah kutoka kwa Ibn ‘Abbaas amehadithia kuwa pindi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  alipofika Madiynah alikuta watu wa Madiynah wakipunjiana kilo na walikuwa ni wenye tabia mbaya kabisa katika jambo hilo. Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha:

 وَيْلٌ لِّلْمُطَفِّفِينَ ﴿١﴾

1. Ole kwa wanaopunja.

 

Na baada ya hapo wakafanya uzuri katika kupima na kuacha tabia yao hiyo mbaya kupunja katika kipimo  [bn Maajah Kitaab At-Tijaraat (2223)]

 

Ibn Kathiyr:

 

Kuongeza na kupunguza katika kupima kwa pishi au mizani ndio sababu ya adhabu kali na kupata hasara.

 

Amepokea An-Nasaaiy na Ibn Maajah kutoka kwa Ibn ‘Abbaas amesema: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  alipofika Madiynah walikuwa watu wa Madiynah ni waovu mno kuliko watu wote katika  kupunja Allaah (سبحانه وتعالى)  Akateremsha:

وَيْلٌ لِّلْمُطَفِّفِينَ ﴿١﴾

1. Ole kwa wanaopunja.

 

Wakapima vizuri baada ya hapo [An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (6/508) na Ibn Maajah (2/748)]

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 وَيْلٌ لِّلْمُطَفِّفِينَ ﴿١﴾

1. Ole kwa wanaopunja.

 

الَّذِينَ إِذَا اكْتَالُوا عَلَى النَّاسِ يَسْتَوْفُونَ ﴿٢﴾

2. Ambao wanapopokea kipimo kwa watu wanataka wapimiwe kamilifu.

 

وَإِذَا كَالُوهُمْ أَو وَّزَنُوهُمْ يُخْسِرُونَ ﴿٣﴾

3. Na wanapowapimia (watu) kwa kipimo au wanawapimia kwa mizani wanapunja.

 

أَلَا يَظُنُّ أُولَـٰئِكَ أَنَّهُم مَّبْعُوثُونَ ﴿٤﴾

4. Je, hawadhanii kwamba wao watafufuliwa?

 

لِيَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿٥﴾

5. Kwenye Siku adhimu.

 

يَوْمَ يَقُومُ النَّاسُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٦﴾

6. Siku watakayosimama watu kwa Rabb wa walimwengu.

 

 

Share

Hadiyth

041-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Alama Tatu Za Kupata Utamu Wa Iymaan

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Hadiyth Ya   41

Alama Tatu Za Kupata Utamu Wa Iymaan

 

Alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((ثَلاَثٌ مَنْ كُنَّ فِيهِ وَجَدَ حَلاَوَةَ الإِيمَانِ: أَنْ يَكُونَ اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَحَبَّ إِلَيْهِ مِمَّا سِوَاهُمَا، وَأَنْ يُحِبَّ الْمَرْءَ لاَ يُحِبُّهُ إِلاَّ لِلَّهِ, وَأَنْ يَكْرَهَ أَنْ يَعُودَ فِي الْكُفْرِ كَمَا يَكْرَهُ أَنْ يُقْذَفَ فِي النَّارِ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mambo matatu atakayekuwa nayo, atapata utamu wa Iymaan: Allaah na Rasuli Wake wawe vipenzi zaidi kwake kuliko wengineo, ampende mtu na wala asimpende isipokuwa kwa ajili ya Allaah, na achukie kurudi katika ukafiri baada ya Allaah kumwokoa kutoka huko kama anavyochukia kuingizwa motoni)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Muumin mwenye Iymaan ya kweli ni mwenye kumpenda Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kuliko hata nafsi yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ

Nabiy ana haki zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao [Al-Ahzaab (33: 6)]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَتَّخِذُ مِن دُونِ اللَّـهِ أَندَادًا يُحِبُّونَهُمْ كَحُبِّ اللَّـهِ ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَشَدُّ حُبًّا لِّلَّـهِ

Na miongoni mwa watu wako wenye kuchukua asiyekuwa Allaah na kuwafanya kuwa ni wanaolingana (na Allaah) wanawapenda kama kumpenda Allaah. Na wale walioamini wana mapenzi zaidi kwa Allaah. [Al-Baqarah (2: 165)]

 

Na Hadiyth ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

عَنْ أَنَسٍ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((لاَ يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى أَكُونَ أَحَبَّ إِلَيْهِ مِنْ وَلَدِهِ وَوَالِدِهِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ)) أَخْرَجَاهُ

 

Imepokewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mmoja wenu hawi Muumini mpaka anipende mimi kuliko watoto wake na baba yake na watu wote)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 2. Allaah (سبحانه وتعالى) Ameonya kwamba Waumini wasipompenda au wasipofuata amri Zake au wakikengeuka, Atawaondoshelea mbali duniani, kisha Awalete waliobora zaidi yao na wampende Yeye zaidi.

 

[Rejea: Muhammad (47: 38), Al-Maaidah (5: 54)]

 

 

3. Utamu wa Iymaan unapatikana pale Muislamu atakapofuata amri za Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuacha matamanio ya nafsi kando [Rejea: Aal-‘Imraan (3: 31)].

 

 

4. Utamu wa Iymaan unapatikana kutokana na kupenda kutekeleza ‘Ibaadah, Muumini anapozidisha ‘amali za Sunnah kama Swalaah, Swawm, sadaka hufikia daraja ya kupendwa na Allaah (سبحانه وتعالى).

 

[Hadiyth Al-Qudsiy: ((Yeyote yule atakayefanya uadui kwa walii Wangu, Nitatangaza vita dhidi yake. Mja Wangu hanikaribii na kitu chochote Ninachokipenda kama ‘amali Nilizomfaridhishia, na mja Wangu huzidi kunikaribia kwa ‘amali njema za Sunnah ili Nimpende. Ninapompenda, huwa masikio yake yanayosikilizia, macho yake anayoonea, mikono yake anayopigania, miguu yake anayotembelea nayo, lau angeniomba kitu bila shaka Ningempa, lau angeniomba himaya bila shaka Ningelimkinga, na Sisiti juu ya kitu chochote kama Ninavyosita [kuichukua] roho ya mja Wangu Muumin: Anachukia mauti, Nami Nachukia kumdhuru)) [Al-Bukhaariy]

 

5. Inapasa kujenga mapenzi ya ikhlaasw pamoja na waja wema na kuandamana nao katika vikao vyao, kwani mapenzi yao ni kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى), na ndipo Muislamu atakapopata manufaa ya Dini yatakayomfikisha daraja ya Al-Walaa Wal-Baraa (Kupendana kwa ajili ya Dini ya Allaah na kuchukiana au kutengana kwa ajili yake) kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

((أَوْثقُ عُرَى الإِيمان: الموالاَةُ في الله والمعاداةُ في الله، والحب في الله، والبغضُ في اللَّه عز وجل))   

((Shikizo thabiti kabisa la iymaan ni kuwa na urafiki wa karibu kwa ajili ya Allaah na kujitenga kwa ajili ya Allaah, na kupenda kwa ajili ya Allaah, na kuchukia kwa ajili ya Allaah عزّ وجلّ)) [Hadiyth ya Ibn ‘Abaas (رضي الله عنهما) : Atw-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr na ameisahihisha Al-Abaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (2539)]

 

 Na pia:

 

عَنْ أَبِي أُمَامَةَ ، قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ :  ((مَنْ أَحَبَّ فِي اللَّهِ وَأَبْغَضَ فِي اللَّهِ وَأَعْطَى لِلَّهِ وَمَنَعَ لِلَّهِ فَقَدِ اسْتَكْمَلَ الإِيمَانَ))  

Kutoka kwa Abi Umaamah  (رضي الله عنه kwamba “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Atakayependa kwa ajili ya Allaah, akatoa kwa ajili ya Allaah, akazuia kwa ajili ya Allaah, atakuwa amekamilisha iymaan)) [Abuu Daawuwd na ameisahihisha Al-Albaaniy (4681)]

 

6. Kuchukia kufru na ufasiki na watu wake hata kama mtu ana uhusiano wa damu, kwani kafiri na fasiki huenda akamrudisha mtu katika kufru na ufasiki. [Rejea: Al-Mujaadalah (58: 22)].

 

Share

Wadhakkir