Kufukiza Ubani Wakati Wa Kuomba Duaa Inafaa?

 

Kufukiza Ubani Wakati Wa Kuomba Duaa Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Asalam Alaykum,

Kuna uhalali/faida/hasara gani wa kutumia ubani kuweka kwenye moto wakati wa kuomba duah au kurehemu ndugu zetu waliotutangulia katika haki?

Wabillah tawfiq

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kufukiza ubani katika moto wakati wa kusoma du’aa haina uhalali wala faida yoyote.  Na hii imekuwa ni ada ya baadhi ya ndugu zetu hasa wanaosoma Maulidi na Khitmah kwa kuamini kuwa du'aa inapanda juu na moshi wake. Yote haya ni mambo ya kijahili yasiyokubalika katika Shariy’ah ya Kiislamu. 

 

 

Inayopatikana ni hasara kubwa kwani ni kwenda kinyume na Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Chetezo cha moto wakati wa ‘aibadah na du’aa imechukuliwa kutoka kwa Mafursi (Iran) ambao walikuwa wanaabudu jua na moto. Walipoingia katika Uislamu waliingia na baadhi ya desturi zao mbaya zinazokwenda kinyume na Uislamu. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametusisitiza sana tusifuate ada na desturi za makafiri au kujifananisha nao kwani tutakuwa sawa na wao kama alivyosema: 

((مَنْ تَشَبَّهَ بِقَوْمٍ فَهُوَ مِنْهُمْ))

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Atakayejifananisha na watu basi yeye ni miongoni mwao". [Abuu Daawuwd na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Abiy Daawuwd (3401)]

 

 

Leo pia utakuta wanawake Waislamu wanaoishi India wanavaa sare kama Mabaniyani huku matumbo yao yapo wazi kabisa jambo ambalo linakataliwa na kwenda kinyume na Dini hii ya Kiislamu. Au vijana wa kiume kusuka nywele, kuvaa hereni, mikufu au kuchonga nyusi kwa kuwaiga makafiri wanamuziki na wachezaji mipira, na vijana wa kike kuvaa masuruali kama wanaume n.k.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share