Amekhasimikiana Na Mumewe Muda Wa Miaka 15 Mume Hamuulizi Lolote Na Hakumtamkia Kuwa Kamuacha, Je Ameachika?

SWALI:

 

ASALAAM ALYEKUM WARAHMATULLAH WABARAKATU. KWANZA NAWAPONGEZA KWA KAZI NZURI MNAYOIFANYA.SWALI LANGU NDUGU YANGU TOKA AOLEWE ANA MUDA WA MIAKA 20 AMEISHI NA MUME WAKE MIAKA 6 WAKAASIANA MUME WAKE AKAENDA KUOA .HAMUULIZIA KWA LOLOTE.KWA MUDA WA MIAKA 15 HIYO.JE ATAKUWA AMEACHIKA JAPO HAJAWAHI KUMWAMBIA NIMEKUACHA.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mke kukhasimiana na mumewe kwa muda wa miaka 15.

Hakika kila Dini ina nidhamu yake katika kila jambo na kwa kuwa Uislamu ni nidhamu kamili ya maisha kuhusu kila jambo, ikiwemo mas-ala ya talaka.

 

Tujue kuwa talaka Kiislamu inapita tu ikiwa mume atatamka kuwa amemtaliki mkewe, au amemwandikia barua kuhusu suala hilo, au amemtumia mjumbe mwaminifu, au ametoa ishara ambayo inafahamika kuwa ni talaka. Ikiwa hakuna lolote katika hayo kule kukhasimiana na mume kuoa si kuwa mke ametalikiwa japokuwa mume ana makosa makubwa kwa kumuacha mkewe kwa muda wote huo bila kumtaliki wala kumpatia masurufu yake ya kawaida.

 

Katika hali hiyo dada yetu ilikuwa ampigie simu mumewe au akutane naye kujua hatima yake katika kuachwa huko. Kwa kuwa hakufanya hivyo, itabidi kwa sasa awe ni mwenye kufuatilia suala hilo kwa kuwasiliana na mumewe ili atoe maelekezo kama ni mkewe au amemtaliki na wakati gani. Ikiwa mume atasema kuwa hajamtaliki itabidi adai masrufu yake ya miaka yote 15 na hiyo ni haki yake kupatiwa. Ikiwa mume anasema bado ni mkewe inabidi mke afanye yafuatayo:

 

1.     Je, mke bado anataka kubaki na mume huyo? Ikiwa atataka hivyo atakuwa na haki hiyo bila ya pingamizi yoyote. Hata hivyo, inatakiwa ahakikishe kuwa atapata haki yake kikamilifu kama inavyohitajika kutoka kwa mumewe kama mke wa halali.

2.     Mume hakujibu chochote hata baada ya kupigiwa simu au kuendewa, itabidi mke afanye juhudi aitishe kikao baina yake na mumewe na wazazi au wawakilishi wao ili wasuluhishe tatizo hilo. Ikiwa itajitokeza katika kikao hicho kuwa mume hataki ima atatoa talaka au akikubali, basi ataendelea kuishi naye kwa wema.

3.     Ikiwa hakukupatikana suluhisho lolote itabidi mke apeleke kesi yake kwa Qaadhi au Shaykh muadilifu, aliye mjuzi ili kuamua tatizo hilo lao. Ikiwa mume hataki kutoa talaka wala kukaa naye kwa wema itabidi Qaadhi apitishe talaka katika hilo.

 

Hata hivyo, nasaha zetu hasa kwa kina mama ambao wamedhulumiwa wasiwe ni wenye kudhalilishwa kwa muda mrefu kama huo bali wanatakiwa wachukue hatua kwa haraka kuhusu hayo wanayokumbana nayo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share