Hijjah Ya Muislamu Asiyeswali
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Nini hukmu ya mwenye kufanya Hajj lakini hakuwa akiswali aidha kwa makusudi (akiwa anaamini kuwa haikuwa ni wajib kwake kuswali) au kwa kudharau? Je, Hajj yake inakubaliwa?
JIBU:
Yeyote mwenye kufanya Hajj ambaye hakuwa akiswali, kwa sababu akiamini kuwa sio fardhi kwake, basi amekufuru kutokana na rai waliokubaliana ‘Ulamaa, na Hajj yake haikubaliwi. Lakini ikiwa hakuwa anaswali kwa sababu ya uvivu na dharau, basi kwa hali hii, kuna rai tofauti baina ya ‘Ulamaa. Baadhi ya rai zao ni kuwa Hajj yake inafaa na pia kuna baadhi ambao rai zao ni kuwa Hajj yake haifai. Na rai iliyo sahihi kabisa ni kwamba Hajj yake haifai kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
(( إن العهد الذي بيننا و بينهم الصلاة فمن تركها فقد كفر )) أخرجه أصحاب السنن
((Mafungamano baina yetu na wao (Makafiri) ni Swalaah, atakayeiacha amekufuru)) [Aswhaabus-Sunan]
Vile vile amesema:
((بين الرجل و الكافر و الشرك ترك الصلاة)) أخرجه مسلم في صحيحه
((Baina ya mtu na kafiri na shirki ni kuacha Swalaah)) [Muslim katika Swahiyh yake]
Hii ni kwa ujumla na inawahusu wote; mwenye kuamini kuwa Swalaah sio fardhi na asiyeswali kwa sababu ya uvivu au dharau.
Wa biLLaahi At-Tawfiyq wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiyyina Muhammad wa aalihi wa Swahbihi wa sallam.
[Fataawa Al-Hajj Wal-'Umrah waz-Ziyaarah Uk. 15]
Kufanya Hajj Akiwa Bado Ana Deni La Benki
Al-Lajnah Ad-Daaimah
SWALI:
Muislamu alitaka kutekeleza fardhi ya Hajj akiwa ana deni. Je, akiwa ameomba ruhusa kwa wenye kumdai na wamemruhusu kutekeleza Hajj itakuwa imekubaliwa?
JIBU:
Ikiwa hali ni kama ulivyotaja, kuwa na ruhusa ya wenye kumdai atekeleze Hajj kabla ya kulipa deni, basi hakuna ubaya kufanya Hajj kabla ya kumaliza deni na Hajj haitoathirika (kuwa ina kasoro) kwa kutokana na hali yake ilivyo baina yake na waliomkopesha.
Na kwa Allah ndio yako mafanikio yote na Rahma na Amani zimfikie Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam na Swahaba zake.
[Fataawa al-Lajnah ad-Daaimah lil-Buhuwth al-'Ilmiyyah wal-Iftaa. Mjalada 11, Uk. 46, Fatwa Namba 5545 Imejumuisha:
Kiongozi Mkuu: Shaykh 'Abdul 'Aziyz ibn 'Abdillaah ibn Baaz
Msaidizi Kiongozi Mkuu: Shaykh ‘Abdur-Razzaaq 'Afiyfiy
Mjumbe: Shaykh 'Abdullaah Ibn Ghudayyaan
Mjumbe: Shaykh 'Abdullah ibn Qu'uwd]
Mama Alifanya Hajj Na Mtu Asiye Mahram Wake
Shaykh Swaalih Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah)
SWALI:
Mama yangu aliyekwishafariki sasa, (Allaah Amrehemu) amefanya Hajj akiwa na umri wa miaka 60 na mtu asiye Mahram wake. Je, Hajj yake ni sahihi au nimfanyie tena mimi Hajj.
JIBU:
Ikiwa mwanamke alifanya Hajj na mtu asiye na Mahram wake, atakuwa amemuasi Rabb wake na amefanya dhambi. Hii ni kwa sababu Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mwanamke kusafiri bila ya Mahram kwenda Hajj au safari nyingine yoyote. Ama kuhusu Hajj yake aliyofanya itakuwa ni sahihi In Shaa Allaah ingawa ilihusisha dhambi, tunamuomba Allaah Amsamehe.
[Al-Muntaqaa Min Fataawa ibn Fawzaan]
Mwajiriwa Benki Anataka Kufanya Hajj
Shaykh Swaalih Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah)
SWALI:
Mimi ni mwajiriwa wa Benki, je naruhusiwa kufanya Hajj kwa mshahara wangu?
JIBU:
Kufanya kazi katika benki zinazohusika na riba hairuhusiwi. Hii kwa sababu ni kusaidia katika dhambi na uovu. Pia Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amelaani mwenye kula/kufaidika na riba, pia mwenye kuhusika na utendaji wa makubaliano (transaction), shahidi wa utendaji makubaliano, na mwenye kuandika utendaji wa makubaliano.
Kwa hiyo, kwa mtazamo halisi, mfanya kazi huwa hasa anasaidia benki hata kama yeye ni karani tu wa benki. Hivyo hulaaniwa kutokana na kauli ya Hadiyth. Kutokana kwayo, mshahara anaopokea ni haraam na haruhusiwi kula/kufaidika nao wala kufanyia Hajj. Hii ni kwa sababu kufanya Hajj kunahitaji kipato kilichokuwa safi kutoka katika chanzo cha halaal. Lakini ikiwa tayari ameshafanya Hajj, basi Hajj yake ni sahihi lakini itaambatana na dhambi kwa maana ujira wake utakuwa ni mdogo.
[Al-Muntaqaa min Fataawa Shaykh Fawzaan – Mjalada 4, Uk. 121, Fatwa Namba 123.]
Mwanamke Asiye Na Mahram Hawajibiki Kufanya Hajj
Al-Lajnah Ad-Daaimah
SWALI:
Mwanamke ambaye anajulikana sana kwa taqwa yake, akiwa katika umri wa wastani au kukaribia uzee anataka kufanya Hajj. Lakini hana Mahram. Nchi anayoishi kuna mwanamume ambaye anajulikana kwa kuwa ni mwenye taqwa ambaye anataka kufanya Hajj, naye anasafiri na jamaa yake mwanamke. Je inafaa mwanamke huyo kwenda Hajj na mwanamume huyo ambaye atakuwa ni mlinzi wao? Je, anawajibika kufanya Hajj au hawajabiki kwa vile hana Mahram, ingawa anao uwezo kifedha? Tupeni jibu, Allah Awalipe.
JIBU:
Mwanamke huyo ambaye hana Mahram hawajibiki kufanya Hajj kwa sababu kuwa na Mahram ni katika kipengele cha uwezo wa kufanya Hajj. Kuwa na uwezo ni moja wa sharti halisi ya kuwajibika kufanya Hajj kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ
Na kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. [Al-'Imraan: 97]
Hairuhusiwi kwake kusafiri kwenda Hajj au safari nyingine bila ya mume au Mahram. Hii ni kutokana na Imaam Al-Bukhaariy alivyohifadhi kuwa Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((لا يحل لامرأة مسلمة تسافر مسيرة اليوم وليلة إلا مع ذي حرمة منها))
((Haimpasi mwanamke Muislamu kusafiri msafara wa mchana na usiku ila awe na Mahram)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Vile vile imerekodiwa na ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba kamsikia Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((لا تسافر المرأة إلا مع ذي محرم ، ولا يدخل عليها رجل إلا ومعها محرم))
((Mwanamke asisafiri ila akiwa na Mahram na mwanamke asiwe peke yake ila akiwa na Mahram wake))
Mtu mmoja alisema: "Ee Rasuli wa Allah, mke wangu amesafiri kwenda kufanya Hajj na nimemuwakilisha na kundi fulani." Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Nenda kafanye Hajj na mke wako))
Hii ni rai ya Al-Hasan, Al-Nukhaaiy, Ahmad, Is-haaq, ibn Al-Mundhir na ‘Ulamaa wanasheria wa Asw-haab Ar-raaiy. Ni rai iliyo sahihi kwa sababu imekubalika kutokana na kukubalika na wote Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo inakataza mwanamke kusafiri bila ya mume au Mahram.
Maalik, Ash-Shaafiy na Al-Awzaaiy wametoa rai tofauti. Wote wametoa sharti ambayo haina dalili. Ibn Al-Mundhir amesema: "Wote wameacha yaliyo dhahiri, maana ya Hadiyth iliyo wazi na wameweka sharti ambayo hawana dalili."
Wa biLLaahi At-Tawfiyq wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiyyina Muhammad wa aalihi wa Swahbihi wa sallam.
[Al-Lajnah Ad-Daaimah - Fataawa al-Mar-ah]
Watoto Na Vijana Kutekeleza Hajj Inahesabika Ni Hajj Ya Fardhi?
Al-Lajnah Ad-Daaimah
SWALI:
Nilifanya Hajj nilipokuwa na umri wa miaka kumi, kisha nilifanya tena nikiwa na umri wa miaka kumi na tatu, je inatosheleza kuwa nimetimiza fardhi ya Hajj?
JIBU:
Hajj hizo kama zilivyotajwa zinatosheleza kuwa ni Hajj za fardhi ikiwa zimefanywa baada ya kubaleghe aidha kwa kutokwa na manii ndotoni au kwa kuona nywele kuota sehemu za siri. Hii ni kwa sababu mwanamume na mwanamke hutambulika kuwa amebaleghe kutokana na matukio hayo mawili. Vile vile kufikia umri wa miaka kumi na tano na kuanza nidhamu ya hedhi kwa mwanamke.
Wa biLLaahi At-Tawfiyq wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiyyina Muhammad wa aalihi wa Swahbihi wa sallam.
[Fataawa al-Lajnah ad-Daaimah lil-Buhuwth al-'Ilmiyyah wal-Iftaa. Mjalada 11, Uk. 23, Fatwa Namba 10938 - Imejumuisha:
Kiongozi Mkuu: Shaykh 'Abdul 'Aziyz ibn 'Abdillaah ibn Baaz
Msaidizi Kiongozi Mkuu: Shaykh ‘Abdur-Razzaaq 'Afiyfy
Mjumbe: Shaykh 'Abdullaah Ibn Ghudayyaan]
Links
[1] http://alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/265
[2] http://www.alhidaaya.com
[3] https://www.addtoany.com/share#url=http%3A%2F%2Falhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9217&title=Fataawaa%3A%20Uwezo%20Na%20Hukmu%20Za%20%27Umrah%20Na%20Hajj
[4] https://www.addtoany.com/share#url=http%3A%2F%2Falhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9218&title=01-Imaam%20Ibn%20Baaz%3A%20Hijjah%20Ya%20Muislamu%20Asiyeswali
[5] https://www.addtoany.com/share#url=http%3A%2F%2Falhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9219&title=02-Al-Lajnah%20Ad-Daaimah%3A%20Kufanya%20Hajj%20Akiwa%20Bado%20Ana%20Deni%20La%20Benki
[6] https://www.addtoany.com/share#url=http%3A%2F%2Falhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9220&title=03-Shaykh%20Swaalih%20Al-Fawzaan%3A%20Mama%20Alifanya%20Hajj%20Na%20Mtu%20Asiye%20Mahram%20Wake
[7] https://www.addtoany.com/share#url=http%3A%2F%2Falhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9221&title=04-Shaykh%20Swaalih%20Al-Fawzaan%3A%20Mwajiriwa%20Benki%20Anataka%20Kufanya%20Hajj
[8] https://www.addtoany.com/share#url=http%3A%2F%2Falhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9222&title=05-Al-Lajnah%20Ad-Daaimah%3A%20Mwanamke%20Asiye%20Na%20Mahram%20Hawajibiki%20Kufanya%20Hajj
[9] https://www.addtoany.com/share#url=http%3A%2F%2Falhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9223&title=06-Al-Lajnah%20Ad-Daaimah%3A%20Watoto%20Na%20Vijana%20Kutekeleza%20%20%20Hajj%20%20Inahesabika%20Ni%20Hajj%20Ya%20Fardhi%3F