Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
Imekusanywa Na: 'Abdullaah Mu'aawiyah (Abuu Baasim)
Du’aa Za Ruqyah (Kinga) Faida Na Sharh Zake
01-Kuomba Kuwezeshwa Kutenda Kheri, Kuacha Munkari, Kuwapenda Masikini Kupata Maghfirah na Rahmah, Kuepushwa na Fitnah, Na Kulipata Penzi La Allaah
Allaah (Tabaaraka wa Ta’alaa) Alimwamuru Kipenzi Chake Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipomwona usingizini, - na njozi ya Manabii ni kweli – aseme anaposwali:
((اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ فِعْلَ الْخَيْرَاتِ، وَتَرْكَ الْمُنْكَرَاتِ، وَحُبَّ الْمَسَاكِينِ، وَأَنْ تَغْفِرَ لِي، وَتَرْحَمَنِي، وَإِذَا أَرَدْتَ فِتْنَةَ قَوْمٍ فَتَوَفَّنِي غَيْرَ مَفْتُونٍ، وَأَسْأَلُكَ حُبَّكَ، وَحُبَّ مَنْ يُحِبُّكَ، وَحُبَّ عَمَلٍ يُقَرِّبُنِي إِلَى حُبِّكَ))
((Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba kufanya mema yote, kuacha munkari zote, na kuwapenda masikini, na Unighufirie na Unirehemu, na Unapotaka kuwatia watu majaribuni (fitnah), basi Nifishe mimi bila kujaribiwa. Na ninakuomba Penzi Lako na penzi la yule anayekupenda, na kuipenda ‘amali itakayonikurubisha kwenye Penzi Lako)). [Imekharijiwa na Ahmad kwa tamko lake 36/423 nambari 22109 na At Tirmidhiy].
Kisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia Maswahaba:
((إِنَّهَا حَقٌّ فَادْرُسُوهَا وَتَعَلَّمُوهَا))
((Hakika njozi hii ni kweli, basi idurusuni na jifundisheni)). [Ziada hii iko kwa Ahmad na At Tirmidhiy. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyh At Tirmidhiy kwa nambari 2582].
Faida Na Sharh:
Hili ni agizo la Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwetu kuyadurusu yaliyomo ndani yake, kujifunza maana zake na makusudio yake kutokana na umahususi wake.
Du’aa hii bila shaka ni katika du’aa jumuishi zaidi, kamili zaidi na zenye shani kubwa zaidi kutokana na kukusanya kwake maombi kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) Ampe mtu tawfiyq ya kuyafanya mambo yote mema yenye kupendeza Kwake, na kumwomba Amkinge na munkari zote na mabaya yote, pamoja na fitna na misukosuko katika Dini, maisha ya hapa duniani na marejeo ya kesho Aakhirah.
Hivyo inabidi Muislamu akithirishe kuomba du’aa hii, ajitahidi kuyajua makusudio yake na maana zake, na kuyafanyia kazi madhumuni yake. Atakayefanya hivyo, basi bila shaka atapata furaha ya hapa duniani na kesho Aakhirah.
Katika du’aa hii, limetajwa suala la kuwapenda masikini. Kuwapenda masikini kunaingia ndani ya wigo wa kufanya mema ya kheri, kwa kuwa watu hawa hawana chochote hapa duniani cha kuwafanya watu wawapende. Na anayewapenda, anakuwa hafanyi hivyo ila kwa ajili ya Allaah (‘Azza wa Jalla), na hilo ni katika ukamilisho wa iymaan ya mtu. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((من أحب للَّه، وأبغض للَّه، وأعطى للَّه، ومنع للَّه، فقد استكمل الإيمان))
((Mwenye kupenda kwa ajili ya Allaah, akachukia kwa ajili ya Allaah, akatoa kwa ajili ya Allaah na akazuia kwa ajili ya Allaah, basi ameikamilisha vilivyo iymaan yake)). [Hadiyth Marfu’u. Imepokelewa na Abuu Umaamah].
Pia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuusia Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akimwambia:
((يا عائشة أحبِّي المساكين، وقرّبيهم، فإن اللَّه يقربك يوم القيامة))
((Ee ‘Aaishah! Wapende masikini na wakurubishe, Allaah Atakukurubisha Siku ya Qiyaamah)). [Imepokelewa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu)].
Ama ombi la kughufiriwa na kurehemewa, bila shaka maghfirah na rahmah, viwili hivi vinakusanya kheri zote za Aakhirah. Kwa maghfirah, mja atasalimika na adhabu na shari zote, na kwa rahmah, mja ataingia Peponi. Kuingia Peponi na neema zote zilizoko huko, kunatokana na Rahmah za Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa). Hakuna atakayeingia Peponi kwa amali zake, bali ataingia kutokana na Rahmah za Allaah kama alivyoashiria hilo Rasuli (Swalla Allaahu Alayhi wa Sallam) katika Hadiyth nyingine.
Rahmah ya Allaah (‘Azza wa Jalla) ni bora kuliko vyote vya duniani. Allaah Anatuambia:
وَرَحْمَتُ رَبِّكَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُون
Na Rahmah ya Rabb wako ni bora kuliko wanayoyakusanya. [Az- Zukhruf (43:32)].
Aidha, kutokana na umuhimu wa maghfirah na rahmah, Allaah (‘Azza wa Jalla) Amemwamuru Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na sisi aombe maghfirah na rahmah. Anasema:
وَقُل رَّبِّ اغْفِرْ وَارْحَمْ وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِين
Na sema: “Rabb wangu! Ghufuria na Rehemu, Nawe ni Mbora wa wenye kurehemu. [Al-Muuminuwn 23:118)]
Kisha du’aa hii Aliyoagizwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inagusia suala la fitnah. Inasema: “Ukitaka kuwaingiza watu kwenye fitnah na adhabu katika Dini, au adhabu ya kidunia kati ya misukosuko na mengineyo, basi Nifishe Unirejeshe Kwako kabla ya kutokea hayo.”
Makusudio hapa ni kusalimika na fitnah katika maisha yote ya Muislamu, na kusalimika na shari zote kabla hazijamfikia, na kufa akiwa salama kabla ya kufikiwa na fitnah.
Na hili linadulisha kuwa inajuzu kuomba kifo kwa kuhofia fitnah katika Dini.
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((اثْنَتَانِ يَكْرَهُهُمَا ابْنُ آدَمَ: الْمَوْتُ، وَالْمَوْتُ خَيْرٌ لِلْمُؤْمِنِ مِنْ الْفِتْنَةِ، وَيَكْرَهُ قِلَّةَ الْمَالِ وَقِلَّةُ الْمَالِ أَقَلُّ لِلْحِسَاب))
((Mawili anayachukia mwana Aadam: Mauti, na mauti ni kheri zaidi kwa Muumini kuliko fitnah. Na anachukia uchache wa mali, na uchache wa mali ni nafuu zaidi kwa hisabu)). [Imepokelewa na Mahmuwd bin Lubayd (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) na kusimuliwa na Ahmad].
Ama penzi, hili bila shaka ndio ombi la juu zaidi na matarajio ghali zaidi kuliko yote. Mja kupendwa na Rabb wake, na yeye kuwa hakuna akipendaye zaidi kuliko Rabb wake na Rasuli Wake, bila shaka hakuna jingine zaidi ya hilo.
Mwenye kulipata Penzi hilo, amali zake zote, maneno yake yote, na vitendo vyake vyote vinakuwa vikielekezwa kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) tu. Muumini hupata qabuli kwavyo ardhini na mbinguni kama ilivyo kwenye Swahiyh.
Du’aa Za Ruqyah (Kinga) Faida Na Sharh Zake
02-Kuomba Kinga Dhidi Ya Tabia Za Kuchukiza, Matendo,
Hawaa Na Magonjwa Yote Mabaya
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anajilinda kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akisema:
((اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ مُنْكَرَاتِ الْأَخْلَاقِ، وَالْأَعْمَالِ، وَالْأَهْوَاءِ والأدواء))
((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na yenye kuchukiza katika tabia, matendo, hawaa na magonjwa)). [At Tirmidhiy 3591]
Faida Na Sharh:
Katika du’aa hii, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anajilinda kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kutokana na tabia zote zinazochukiza, matendo yote yanayochukiza, hawaa na matamanio yote yanayochukiza na magonjwa yote mabaya.
Tabia mbaya zinazochukiza ni kama hikdi, hasadi, kibri, ubakhili, na woga. Pia ulimi mchafu wa kutukana, wa kusingizia watu, kufitinisha na kusema uongo. Tabia zote hizi mbaya ni kiini cha sababu ya shari zote katika jamii, na ndiyo sababu kuu ya kuiweka mbali kheri na jamii. Na tabia zote hizi hazijengi jamii njema, bali zinazidi kuibomoa na kuisambaratisha.
Ama matendo, ni kama zinaa, mauaji, kunywa pombe, wizi, rushwa, ufujaji mali, dhulma, ufisadi, kudhalilisha watu, uonevu, unyanyasaji, ubaguzi, unyanyapaa na kadhalika. Haya yote huleta madhara makubwa ndani ya jamii kama tunavyoshuhudia na kujionea wenyewe haya ndani ya jamii zetu.
Ama matamanio na hawaa, haya ni matamanio ya kinafsi ya kupondokea kwenye anasa batili na za haraam, kuifumbia macho haki, kufuata kibubusa mielekeo batili yenye hoja zisizo na mashiko, kujisahau na starehe za dunia na kuisahau aakhirah, kujisahaulisha kifo na yanayofuatia baada ya hapo na kadhalika.
Ama magonjwa, haya ni yale yote yenye kuwakimbiza watu wasimkurubie mgonjwa kama ukoma, ndui, na mbalanga ambayo hugeuza umbo la mtu. Pia magonjwa yote yenye kuambukiza na magonjwa yenye kiwango kidogo cha kupona kama ukimwi, saratani, pumu na kadhalika. Magonjwa haya humweka mgonjwa katika hali ngumu ya kisaikolojia pamoja na jamaa zake wa karibu mbali na gharama kubwa za matibabu yake.
Katika du’aa nyingine kuhusiana na magonjwa, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anajilinda akisema:
((اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْبَرَصِ، وَالْجُنُونِ، وَالْجُذَامِ، وَمِنْ سَيِّئِ الأَسْقَامِ))
((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na mbalanga, magonjwa ya akili, ukoma na magonjwa mabaya)). [Imepokelewa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na kusimuliwa na Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy].
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda na mambo haya manne, kwa kuwa mwana Aadam hawezi kujibandua nayo katika maisha yake ya usiku na mchana. Ikiwa hatakuwa nayo yeye, basi atayakuta kwa wenzake wanaomzunguka wakiwa Waislamu au wasio Waislamu, na madhara yake yatamgusa pia yeye, atake asitake.
Na kwa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda nayo, na kwa kuwa yeye ndiye kiigizo chema kwetu, na yeye ndiye aliye karibu zaidi na Allaah ('Azza wa Jalla), ni vizuri kwa Muislamu awe anaisoma du’aa hii kila siku ili Allaah (‘Azza wa Jalla) Amlinde na hayo yote kutokana na ubaya wake.
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
03-Kuomba Kinga Dhidi Ya Shari Ya Masikio, Macho, Ulimi, Moyo Na Utupu
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anajilinda kwa Allaah ('Azza wa Jalla) akisema:
((اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ سَمْعِي، وَمِنْ شَرِّ بَصَرِي، وَمِنْ شَرِّ لِسَانِي، وَمِنْ شَرِّ قَلْبِي، وَمِنْ شَرِّ مَنِيِّي))
((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na shari ya masikio yangu, na shari ya macho yangu, na shari ya ulimi wangu, na shari ya moyo wangu, na shari ya manii yangu)). [Abuu Daawuwd 1551, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy 5470].
Faida Na Sharh:
Katika Hadiyth hii, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anajilinda na shari ya masikio yake. Shari hii ni ya kusikiliza kila lililoharamishwa na ambalo Allaah (‘Azza wa Jalla) Haliridhii kama shirki, kufr, masengenyo, uongo, uzushi, ala za muziki na kadhalika. Anaomba masikio yake yasisikilize ila lile la haki kama dhikr, nasaha njema, mawaidha mema na kadhalika.
Anajilinda na shari ya macho yake. Anaomba asiangalie chochote ila kile tu ambacho Allaah (‘Azza wa Jalla) Anakiridhia. Asiangalie wanawake walioharamishwa, asiwaangalie watu kwa jicho la dharau au viumbe vinginevyo vya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na pia asisahau kuviangalia viumbe vya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa mazingatio na utaamuli ili kuzidi kupata iymaan na kujuua zaidi Uwezo wa Allaah (Tabaaraka wa Ta’alaa).
Kadhalika, anajilinda na shari ya ulimi wake kama kusengenya, kufitini, kusema uongo, kuyazungumzia yasiyomhusu mtu au kuyanyamazia yanayomhusu na kadhalika, kwa kuwa wengi wataingia motoni kutokana na ndimi zao. Anaomba asitamke ila lililo la haki kama kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) na kumshukuru, kuamrisha mema na kukataza munkari, kusoma Qur-aan na mengineyo ya faida na kadhalika. Atambue kwamba viungo vyake vya mwili vitakuja kumshuhudia matendo yake mazuri na maovu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ أَلْسِنَتُهُمْ وَأَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٤﴾
Siku zitakaposhuhudia dhidi yao ndimi zao, na mikono yao, na miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [An-Nuwr: 241]
Na Anasema pia Allaah ('Azza wa Jalla):
الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلَىٰ أَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا أَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ أَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٦٥﴾
Leo Tunatia vizibo juu ya vinywa vyao, na itatusemesha mikono yao, na itashuhudia miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyachuma. [Yaasiyn: 65]
Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴿١٦﴾
Na kwa yakini Tumemuumba insani na Tunajua yale yanayowaza nafsi yake, na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo.
إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ﴿١٧﴾
Pale wanapopokea wapokeaji wawili (Malaika) wanaokaa kuliani na kushotoni.
مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ﴿١٨﴾
Hatamki kauli yeyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha (kurekodi). [Qaaf (50: 16-18)]
Pia, anajilinda na shari ya moyo wake. Shari hii inatokana na unafiki, hasadi, hikdi, riyaa, kibr, dhana mbaya, itikadi potofu, kuipenda dunia na kufuata hawaa ya nafsi. Na nyoyo zenye kuepukana na shari hizo ni nyoyo zitakazokuwa salama na katika amani Aakhirah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾
“Siku hayatofaa mali wa watoto.
إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾
“Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. [Ash-Shu’araa: 88-89]
Mwisho anaomba Allaah (‘Azza wa Jalla) Amlinde kutokana na shari ya manii yake. Hapa anakusudia utupu wake, yaani kuuweka mahala pasipo pake kwa kuzini, kulawiti, kupiga punyeto na mengineyo ya haramu. Matamanio ya tupu ni moja kati ya mitihani migumu inayomkabili mwana Aadam, na inahitaji subira imara ya kuepukana na shari zake na maharamisho yake na hususan katika zama zetu za leo.
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda na shari ya viungo hivi, kwa kuwa ndivyo kiini cha matamanio ya mtu na mchemko wa ladha yake, na ndiyo asili na chimbuko la shari zote. Allaah (‘Azza wa Jalla) Amemtunuku mwana Aadam viungo hivi ili anufaike navyo kwa kutenda kheri za kumnufaisha katika dunia yake na Aakhirah yake, na si kuvitumia kwa mambo yenye kumkasirisha Yeye, na kisha mwanadamu huyu kukhasirika duniani na aakhirah.
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
04-Kuomba Uthibiti Wa Moyo Juu Ya Uislamu
عن انس قال: كان النبي صلى الله عليه وسلم يكثر أن يقول: ((اللَّهُمَّ يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِك)) قال أنس فقلنا: يا رسول الله آمنا بك، وبما جئت به، فهل تخاف علينا؟ فقال: ((نعم، إن القلوب بين أصبعين من أصابع الله عز وجل يقلبها))
Imepokelewa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akisema: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikithirisha kusema:
((Ee Mwenye Kuzigeuza nyoyo, Uthibitishe moyo wangu juu ya Dini Yako)). Anas anasema: Tukasema: Ee Rasuli wa Allaah! Tumekuamini na yale uliyokuja nayo. Je watuogopea?" Akasema: ((Naam. Hakika nyoyo ziko baina ya Vidole viwili kati ya Vidole vya Allaah ‘Azza wa Jalla, Huzigeuza)). [Imepokelewa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘snhu). Imesimuliwa na At-Tirmidhiy 2140 na Ahmad 12128. Al-Albaaniy kasema Hadiyth Swahiyh kwenye Mishkaat Al-Maswaabiyh 102].
Faida Na Sharh:
Sisi ni lazima tuviogope Vitendo vya Allaah ('Azza wa Jalla). Kati ya vitendo hivyo ni kuzigeuza nyoyo zetu. Na hii ndiyo sababu iliyomfanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutuhofia sisi kuhusiana na suala hili.
Ugeuzaji huu wa nyoyo unaweza kuwa ni wa kheri kwa mja. Moyo wake unaweza kugeuzwa toka kwenye ubatili kwenda kwenye haki, kutoka kwenye upotofu kwenda kwenye hidaayah, kutoka kwenye maasia kwenda kwenye utiifu, kutoka kwenye bid'ah kwenda kwenye Sunnah, kutoka kwenye shirki kwenda kwenye Tawhiyd na kutoka kwenye ukafiri kwenda kwenye Uislamu.
Aidha, ugeuzaji huu unaweza kuwa wa shari kama kugeuzwa kinyume ya hayo yaliyotangulia.
Ugeuzaji huu wa nyoyo unaonyesha Uadhama wa Allaah ('Azza wa Jalla). Ni Yeye tu Peke Yake Mwenye Uwezo huu. Ni Yeye Aliyezipindua nyoyo za wachawi wa Fir‘awn katika muda mfupi mno toka kwenye ukafiri na kuingia kwenye iymaan thabiti iliyowafanya kuuawa wakiwa mashuhadaa. Hawakutishika kamwe na vitisho vya Fir’awn vya kuwakata miguu na mikono na kuwasulubu, bali walishikamana na iymaan yao na wakafa nayo kama yalivyosimuliwa hayo katika Surah Ash-Shu’araa.
Kisa cha kusilimu ‘Umar bin Al-Khattwaab pia ni mfano hai wa hili.
Suala hili la kuzipindua nyoyo Allaah Peke Yake Ndiye Mwenye kulisimamia. Hata Malaika hawakupewa kazi hiyo, na wala hawajui lolote kuhusiana na siri iliyoko ndani ya nyoyo za watu. Kuna mambo mengi wanayoyafanyia kazi, lakini hili hawawezi kulikurubia kabisa.
Du’aa hii kila mmoja wetu anahitajika aikithirishe kiasi awezavyo kama alivyokuwa akifanya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye Allaah Anamwambia.
وَلَوْلَا أَن ثَبَّتْنَاكَ لَقَدْ كِدتَّ تَرْكَنُ إِلَيْهِمْ شَيْئًا قَلِيلً
Na lau kama Hatukukuthibitisha; kwa yakini ungelikaribia kuelemea kwao kidogo. [Al-Israa 17:74]
Ni du’aa wanayoiomba ‘Ulamaa waliozama na kubobea katika 'ilmu kutokana na kuijua hatari iliyopo. Na ndiyo sababu ya Anas kumuuliza Rasuli: "Je, unatuhofia?"
Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anataja du’aa ya kuthibitisha nyoyo zetu Anaposema:
(( رَبَّنَا لاَ تُزِغْ قُلُوبَنَا بَعْدَ إِذْ هَدَيْتَنَا وَهَبْ لَنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً))
Rabb wetu! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kuwa Umetuhidi, na Tutunukie kutoka kwako rahmah. Hakika Wewe ni Mwingi wa kutunuku na kuneemesha. [Aal-Ímraan 3:8]
Na ili du’aa hii ipate uimara na kinga zaidi, Muislamu anatakiwa awe na pupa ya kuwajibika na yote aliyoamrishwa na kuyaepuka yote aliyokatazwa. Akiwa katika hali hii pamoja na kuweka dhana njema kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) basi ugeuzaji utakuwa daima salama kwake wa kumtoa katika hali na kumwingiza katika hali bora zaidi kuliko ya nyuma. Allaah (‘Azza wa Jalla) Hampotoi asiyetaka kupotoka. Anatuambia:
وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا
Na wale waliofanya juhudi kwa ajili Yetu, bila shaka Tutawaongoza njia Zetu. Na hakika Allaah Yu Pamoja na watendao ihsaan. [Al-‘Ankabuwt 29:69].
Ama wenye kukataa Maamrisho ya Allaah ('Azza wa Jalla) kwa inadi na kibri na kutaka wenyewe kupotoka, basi hawa ugeuzaji huo utazidi kuwadidimiza pabaya zaidi kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّهُ قُلُوبَهُم
Basi walipopotoka, Allaah Akapotosha nyoyo zao; na Allaah Haongoi watu mafasiki. [Asw-Swaff 61:5]
Na Anasema pia:
وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَى عَلَى الْهُدَى))
Na ama kina Thamuwd, Tuliwaongoza, lakini walistahabu upofu kuliko Uongofu.)). [Fusw-swilat 41:17].
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
05-Kuomba Yaqiyn, ‘Afwa na ‘Aafiyah Duniani na Aakhirah
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anajilinda kwa Allaah ('Azza wa Jalla) akisema:
((اللَّهُمَّ إنِّي أسْألُكَ اليقين والعفو و الْعَافِيَةَ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ))
((Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Al Yaqiyn, Al-‘Afw na Al-‘Aafiyah duniani na Aakhirah)). [Imesimuliwa na At-Tirmidhiy katika Kitabu cha Ad-Da’awaat Hadiyth nambari 3514].
Faida Na Sharh:
اليقين Al-Yaqiyn, ni jambo lililothibiti bila shaka yoyote ndani yake.
العفو Al-‘Afw, ni msamaha wa madhambi na kuacha kutoa adhabu juu yake.
العافية Al-‘Aafiyah, ni neno jumuishi lenye maana ya Allaah ('Azza wa Jalla) kumpa salama na amani Mja Wake, kumlinda na majanga, shari na misukosuko, na kusalimika na magonjwa, na mabalaa na pia kubakia salama katika Dini yake. Pia ni afya mbali na maradhi.
Du’aa hii ya barkah, imekusanya maombi mazito ambayo kila mtu anayatamani katika Dini yake, dunia yake na Aakhirah yake. Mja anamwomba Allaah ('Azza wa Jalla) amani, na kinga ya shari zote za dhahiri na zisizo dhahiri, zinazoonekana na zisizoonekana. Amani na usalama ni lengo la viumbe wote katika ulimwengu huu; wanadamu, wanyama, ndege, wadudu na kadhalika.
Kati ya magonjwa ya kindani na kimaanawi ni magonjwa ya moyo. Kati ya magonjwa hayo, ni shakashaka kuhusiana na baadhi ya masuala ya kidini. Na kwa ajili hiyo, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemwomba Allaah ('Azza wa Jalla) Ampe yaqiyn ya moyo, kwani yaqiyn ya moyo ndiyo daraja ya juu kabisa ya iymaan itakayomfaulisha Muislamu duniani na Aakhirah. Haya ni magonjwa mabaya kabisa ya moyo, na kwa ajili hiyo, alikuwa akiomba akisema:
((اللَّهم زدنا إيماناً ويقيناً وفهماً ))
((Ee Allaah! Tuzidishie iymaan, yaqiyn na fahmu)). [Imekharijiwa na Ahmad 14/278].
Hivyo yaqiyn ikijikita ndani ya moyo, Muislamu huisusa dunia na kushikamana na Aakhirah.
Du’aa hii kiujumla ni muhimu sana kwa Muislamu kuiomba kila wakati.
Dalili ya hilo ni kuwa mtu mmoja alikwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia: “Ee Rasuli wa Allaah! Ni du’aa ipi bora zaidi?" Akasema: ((Unamwomba Rabb wako Al-‘Afwa na Al-‘Aafiyah duniani na Aakhirah)). Kisha akamwendea tena kesho yake akamuuliza: "Ee Rasuli wa Allaah! Ni du’aa ipi bora zaidi?" Akasema: ((Unamwomba Rabb wako Al-‘Afwa na Al-‘Aafiyah duniani na Aakhirah)). Kisha akamwendea siku ya tatu akasema: "Ee Rasuli wa Allaah! Ni du’aa ipi bora zaidi?" Akasema:
((تَسْأَلُ رَبَّكَ الْعَفْوَ وَالْعَافِيَةَ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ، فَإِنَّكَ إِذَا أُعْطِيتَهُمَا فِي الدُّنْيَا، ثُمَّ أُعْطِيتَهُمَا فِي الْآخِرَةِ فَقَدْ أَفْلَحْتَ))
((Unamwomba Rabb wako Al-‘Afwa na Al-‘Aafiyah duniani na Aakhirah. Kwani wewe kama utapewa mawili hayo duniani, kisha ukapewa mawili hayo Aakhirah, basi umefuzu bila shaka)). [Imesimuliwa na Ahmad 19/304 Hadiyth nambari 12291 na At-Tirmidhiy Hadiyth nambari 3512].
Hivi ndivyo walivyokuwa Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hima ya juu kabisa ya kutaka kujua du’aa bora zaidi ya kuomba.
Na ndivyo alivyokuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiomba asubuhi na jioni.
Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) akisema: "Hakuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiacha kuomba du’aa hizi inapomfikia jioni, na anapopambaukiwa:
((اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَافِيَةَ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ، اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَفْوَ وَالْعَافِيَةَ فِي دِينِي وَدُنْيَايَ وَأَهْلِي وَمَالِي، اللَّهُمَّ استُرْ عَوْرَاتي، وآمِنْ رَوْعَاتي، اللَّهمَّ احْفَظْنِي مِنْ بَينِ يَدَيَّ، ومِنْ خَلْفي، وَعن يَميني، وعن شِمالي، ومِن فَوْقِي، وأعُوذُ بِعَظَمَتِكَ أنْ أُغْتَالَ مِنْ تَحتي )).
((Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Al-‘Aafiyah duniani na Aakhirah. Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Al-‘Afwa na Al-‘Aafiyah katika Dini yangu, dunia yangu, watu wangu na mali yangu. Ee Allaah! Nisitiri aibu zangu, na Nipe amani na usalama kwa ninavyoviogopa. Ee Allaah! Nihifadhi toka mbele yangu, toka nyuma yangu, toka kulia kwangu, toka kushoto kwangu na kutoa juu yangu. Na ninajilinda kwa Uadhama Wako kushambuliwa toka chini yangu)).
Na imepokelewa toka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akisema: Nilikuwa namtumikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila anaposhuka. Nami nilikuwa nikimsikia akikithirisha kusema:
((اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْهَمِّ وَالْحَزَنِ، وَالْعَجْزِ وَالْكَسَلِ، وَالْبُخْلِ وَالْجُبْنِ ، وَضَلَعِ الدَّيْنِ، وَغَلَبَةِ الرِّجَالِ))
((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda kwako na hamu na huzuni, na ajizi na uvivu, na ubakhili na woga, na kulemewa na madeni na kudhalilishwa na watu)). [Al Bukhaariy Hadiyth nambari 6363].
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda na mambo haya yote kwa kuwa yanachafua raha ya maisha ya mtu kwa pande zake zote kisaikolojia, kimwili, kiakili na kwenye moyo.
Hamu na huzuni zina madhara makubwa kwa mwili. Zinanyong'onyeza nguvu za mtu, zinachafua fikra na akili, zinamkosesha mtu mambo mengi ya kheri na kumfanya asitekeleze mawajibiko yanayompasa kwa ufanisi unaotakiwa. Hii ni hamu ya dunia.
Ama ikiwa ni hamu ya Aakhirah, hii inatakiwa kwa kuwa inamfanya Muislamu azidishe kasi ya kuyafanya kheri na mema na kumchunga Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika nyenendo zake zote. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((مَنْ جَعَلَ الْهُمُومَ هَمًّا وَاحِدًا: هَمَّ الْمَعَادِ، كَفَاهُ اللَّهُ هَمَّ دُنْيَاهُ، وَمَنْ تَشَعَّبَتْ بِهِ الْهُمُومُ في أَحْوَالِ الدُّنْيَا، لَمْ يُبَالِ اللَّهُ فِي أَيِّ أَوْدِيَتِهِ هَلَكَ))
((Mwenye kuzifanya humuum (dhiki, wahka) kuwa hamu moja; hamu ya siku ya miadi, Allaah Atamtosheleza na hamu ya dunia. Na ambaye humuum zitamchukua huku na kule katika hali za dunia, Allaah Hatojali ni katika bonde gani kati ya mabonde Yake atahiliki)). [Ibn Maajah 4106, Al-Haakim 2/443, Ibn Abiy Shaybah 13/220 na Al-Bazzaaz 5/68. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyh Ibn Maajah 207].
Ama madeni mazito anayodaiwa mtu, hili pia ni tatizo linalomfanya mtu asilingamane na kuwa sawa. Wakati wote anakuwa akiandamwa na jinamizi la wadai wake kumuulizia madeni yao, kumsumbua na hata wakati mwingine kumtishia kuchukua hatua kali dhidi yake ya kumshitaki, na hivyo kuishia jela. Na hata wakati mwingine inabidi ageuze njia akiwaona kwa mbali, au afunge mawasiliano nao ili kupata nafasi ya kupumua, na pia kuwaahidi ahadi za uongo. Hayo yote humkosesha raha na hata uimara wa kumtii Allaah hudhoofika kutokana na msongo wa mawazo.
Jingine alilojilinda nalo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kudhalilishwa na watu kwa njia ya dhulma, kunyanyaswa na kunyanyapaliwa. Hii ni kama polisi wanavyowafanyia watu kwa kuwapiga bila makosa, kuwavua nguo, kuwatesa kimwili na kisaikolojia, kuwanajisi, kuwabaka na mengineyo mengi. Mtu akifanyiwa haya, hunyong'onyea kabisa kisaikolojia na kujiona si mtu tena mwenye thamani, na hali hii hudhoofisha ari yake ya uzalishaji, utendaji mambo ya kheri na mengineyo mazuri.
Inatakikana kwa kila Muislamu akithirishe du’aa hii tukufu. Tunaihitajia sana du’aa hii na hususan katika zama zetu za leo zilizojaa humumu, ghumumu na uadui kutoka pande zote. Tunamwomba Allaah salama katika Dini yetu na dunia yetu.
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
06-Kuomba Mu’aafaat, Nayo Ni Katika Du’aa Bora Kabisa
Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((ما من دعوة يدعو بها العبد، أفضل من: اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْمُعَافَاةَ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ))
((Hakuna du’aa yoyote anayoiomba mja iliyo bora zaidi kuliko: Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Al-Mu’aafaat duniani na Aakhirah)). [Ibn Maajah 3851]
Faida Na Sharh:
المعافاة Al-Mu’aafaat: Ni vile Allaah ('Azza wa Jalla) kukusalimisha na madhara na adha za watu, na kuwaepushia watu madhara na adha zitokazo kwako, Allaah ('Azza wa Jalla) kukutosheleza nao na kuwatosheleza wao nawe, na Allaah ('Azza wa Jalla) kukuondoshea adha zao, na kuwaondoshea wao adha zako. Na uhalisia wake ni Allaah (Tabaaraka wa Ta’alaa) kumhifadhi mja kutokana na kila analolichukia, linalomhuzunisha na linalomsumbua katika diyn yake, dunia yake na aakhirah yake.
Haya ni maombi ya barkah aliyotujulisha bwana wa mwanzo na wa mwisho. Kila Muislamu anatakiwa awe na pupa ya kuiomba du’aa hii wakati wowote anapokumbuka.
Imesimuliwa kuwa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliwahutubia watu juu ya mimbari ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Rasuli wa Allaah alisimama hapa niliposimama mwaka wa kwanza. Kisha akalia na kusema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akisema:
((إِنَّ النَّاسَ لَمْ يُعْطَوْا فِي الدُّنْيَا خَيْرًا مِنَ الْيَقِينِ وَالْمُعَافَاةِ، فَسَلُوهُمَا اللَّهَ))
(( Hakika watu hawakupewa katika dunia kilicho bora zaidi kuliko yaqiyn na Al-Mu’aafaat. Basi mwombeni Allaah viwili hivyo)). [Imesimuliwa na Ahmad katika Al-Musnad 1/212 Hadiyth nambari 38 na Abu Ya’alaa 1/121].
Al-Mu’aafaat duniani ni kupata salama na amani kutokana na shari zote za kidhahiri na za zilofichika. Na jumla yake ni kusalimika na viumbe na kujitosha nao.
Na Al-Mu’aafat huko Aakhirah ni kusalimika na madhambi na athari zake mbaya na kutokuwa na haki yoyote ya mtu au dhulma yoyote kwa waja.
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
07-Kuomba Uongofu, Taqwa, Utakasifu na Utajiri wa Moyo
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimwomba Allaah ('Azza wa Jalla) akisema:
((اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْهُدَى، وَالتُّقَى، وَالْعَفَافَ، وَالْغِنَى))
((Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba hidaayah, taqwa, utakasifu, na utajiri)). [Imekharijiwa na Muslim 2721]
Faida Na Sharh:
Du’aa hii adhimu, imekusanya maombi manne makubwa na yenye shani ya juu kabisa ambayo kila mja anayeelekea kwa Allaah ('Azza wa Jalla) anayapupia kutokana na umuhimu wake kwa hapa duniani na kesho Aakhirah.
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameanza kwa Al-Hudaa au Hidaayah. Bila shaka hili ni ombi kubwa zaidi kwa mja.
الْهُدَى Al-Hudaa ni neno jumuishi linalohusiana na kila ambalo linahitajia uongofu katika mambo ya dunia na Aakhirah kati ya itikadi safi, utengenefu wa amali, kauli na tabia.
التُّقَى At-Tuqaa ambalo ni sawa na At-Taqwaa (taqwa), ni jina jumuishi la utendaji wa yote Aliyoyaamuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuyaacha yote Aliyoyakataza. Na asili ya neno hili ni ngao au kizuizi, kwa maana kwamba Muislamu anaweka ngao kati yake na adhabu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) kwa kuwajibika na yale yote yatakayomwepushia ghadhabu za Allaah ('Azza wa Jalla) . Hivyo kumwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ngao hii, ni muhimu sana kwa Muislamu.
الْعَفَافَ Al-'Afaaf ni kusafika na mambo yote yasiyofaa, na kujizuia na matamanio na tamaa za kidunia. Al-‘Afaaf inajumuisha kuwa mbali kwa mfano na aina zote za zinaa kama zinaa ya kuangalia, zinaa ya kugusa, zinaa ya kusikiliza, zinaa ya utupu, kujihisi au kujiona bora kuliko wengine na mengineyo yanayofanana na hayo kama chumo la haramu na kadhalika. [Sharhu Riyaadhw Asw-Swaahiliyna, Al ‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah) 2/333]
الْغِنَى Alghinaa, ni utajiri na uliokusudiwa hapa ni utajiri wa moyo. Ni mtu kukinai kile alichonacho na kutovikodolea macho wanavyovimiliki watu wengine. Sifa hii Anaipenda Allaah (‘Azza wa Jalla).
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amrsema:
((إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْعَبْدَ التَّقِيَّ، الْغَنِيَّ، الْخَفِيَّ))
((Hakika Allaah Anampenda mja mwenye taqwa, tajiri wa moyo, asiyejitangaza)). [Swahiyh Muslim 2965]
Al-‘Allaamah ‘Abdur-Rahmaan bin Naaswir As-Sa'diy (Rahimahu-Allaah) akiizungumzia du’aa hii ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: "Du’aa hii ni du’aa kusanyifu zaidi na yenye manufaa makubwa zaidi. Inakusanya maombi ya kheri za dunia na za Aakhirah, kwani Al-Hudaa ni elimu yenye manufaa, At-Tuqaa ni kufanya amali njema chanya na kuacha aliyoyakataza Allaah na Rasuli Wake. Kwa haya, Dini inatengenea, kwani Dini ni elimu yenye manufaa, na maarifa ya kweli ndio hidaayah. Na kumtii Allaah na Rasuli Wake ndio At-Tuqaa, na Al-Afaaf na Al-Ghinaa kunajumuisha kutowategemea viumbe, kutoufungamanisha moyo nao, kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Peke Yake katika rizk na kutosheka na kinachopatikana. Kwa haya, furaha ya dunia na Aakhirah inatimu, na utulivu wa moyo unapatikana. Na haya ndio maisha mema bora. Na mwenye kuruzukiwa hidaayah, taqwa, utwaharifu na utajiri wa moyo, basi kapata furaha mbili, kapata kila linalotakiwa, na ameokoka na kila linaloogopwa. [Kitabu cha Bahjat-Quluwbil Abraar uk. 249]
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
08-Kuomba Kutengenekewa Dini, Dunia, Aakhirah na Umri Kuwa Ziada Ya Kheri Zote
Na Mauti Kuwa Mapumziko Na Shari Zote
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba na kusema:
اللَّهُمَّ أَصْلِحْ لِي دِينِي الَّذِي هُوَ عِصْمَةُ أَمْرِي، وَأَصْلِحْ لِي دُنْيَايَ الَّتِي فِيهَا مَعَاشِي، وَأَصْلِحْ لِي آخِرَتِي الَّتِي فِيهَا مَعَادِي، وَاجْعَلِ الْحَيَاةَ زِيَادَةً لِي فِي كُلِّ خَيْرٍ، وَاجْعَلِ الْمَوْتَ رَاحَةً لِي مِنْ كُلِّ شَرٍّ
((Ee Allaah! Nitengenezee Dini yangu ambayo ndiyo hifadhi ya jambo langu, na Nitengenezee dunia yangu ambayo ndipo yalipo maisha yangu, na Nitengenezee Aakhirah yangu ambayo ndiyo marejeo yangu, na Ufanye uhai kuwa ni nyongeza kwangu katika kila kheri, na Yafanye mauti ni pumziko kwangu na kila shari)). [Imekharijiwa na Muslim 2720]
Faida Na Sharh:
La kwanza kabisa aliloliomba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika du’aa hii ni utengefu wa Dini, kwa kuwa Dini ndio makusudio makuu ya Muislamu. Mtu ambaye Dini yake imeharibika, basi kapita utupu na amekhasiri duniani na Aakhirah. Kumwomba Allaah utengenefu wa Dini ni kuomba tawfiyq ya kushikamana na Qur-aan na Sunnah bila kuzidisha au kupunguza. Na hili halitimu ila kwa masharti mawili:
1-Kumtakasia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee katika ‘ibaadah zote.
2-Kumfuata Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyoamuru, na kama alivyofanya.
Mwenye kushikamana na haya, basi atahifadhika na shari zote, sababu zake, matokeo yake na hatima zake.
La pili aliloliomba ni kutengenekewa maisha katika nyumba hii fupi ya dunia isiyodumu. Kutengenekewa huku ni kama kula riziki ya halaal, kumwabudu Allaah ('Azza wa Jalla) kama inavyotakikana, kupata mke au mume mwema, watoto wema wenye kutuliza jicho, nyumba pana yenye utulivu na barkah, maisha matulivu ya usalama na utulivu wa kisaikolojia. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuambia:
مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِنْ ذَكَرٍ أَوْ أُنْثَى وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُمْ بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ
Mwenye kutenda mema miongoni mwa wanamume au wanawake naye ni Muumin, Tutamhuisha uhai mzuri, na bila shaka Tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda. [An Nahl (19:97)]
La tatu ni kutengenekewa na Aakhirah ambako ni marejeo ya watu wote kwa ajili ya hisabu itakayoamua hatima ya mtu; Jannah au Motoni. Kutengenekewa huko kunaanzia hapa hapa duniani kwa Muislamu kupewa tawfiyq na Allaah ('Azza wa Jalla) ya kufanya mema yanayomridhisha Allaah ('Azza wa Jalla) na kuishilia mwisho mwema kutakakokuwa daraja la kuokoka.
La nne aliloliomba ni kuwa kila sekunde ya maisha yake ni nyongeza ya kila la kheri. Anamwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ampe Tawfiyq ya kuwa kila analolifanya liwe ni nyongeza ya kheri kwake na manufaa kwa wengineo. Ili kulifanikisha hili, Muislamu anatakiwa aliwekee nia njema kila analolifanya. Akilala, alale kwa nia ya kuupumzisha mwili ili apate nguvu ya kufanya matendo ya kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kadhalika. Akienda kazini, awe na nia ya kufanya kazi ili kuwakimu wanawe na mkewe. Hata akimwingilia mkewe, iwe kwa niyyah ya kushibisha matamanio yake halaal na kuwa ni kinga ya kufanya zinaa na kadhalika.
Hivyo umri bora zaidi wa Muislamu, ni umri mrefu uliosheheni kheri ndani yake kwake mwenyewe na kwa wengineo.
La mwisho ni kuomba mauti kuwa ni pumziko na kila shari. Pumziko hilo ni kutokana na humuum (wahka) na ghumuum (dhiki) za kidunia kutokana na fitnah na misukosuko, na mitihani mingineyo migumu ya kimaisha inayoweza kuteteresha iymaan ya Muislamu. Na hapa tunafahamu kuwa Muumini hupumzika mapumziko mazuri kabisa na anasalimika usalama kamili anapoondoka duniani. Imekuja katika Swahiyh mbili kuwa jeneza lilipita mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
((مُسْتَرِيحٌ، وَمُ
سْتَرَاحٌ مِنْه))
((Amepumzika, na wamepumzika naye))
Wakauliza: "Ee Rasuli wa Allaah! Nini "Al-Mustariyhu" na "Al-Mustaraahu minhu?" Akasema:
(الْعَبْدُ الْمُؤْمِنُ يَسْتَرِيحُ مِنْ نَصَبِ الدُّنْيَا وَأَذَاهَا إِلَى رَحْمَةِ اللهِ، وَالْعَبْدُ الْفَاجِرُ يَسْتَرِيحُ مِنْهُ الْعِبَادُ، وَالْبِلَادُ، وَالشَّجَرُ، وَالدَّوَابُّ))
((Mja Muumini hupumzika na taabu ya dunia na adha zake kwenda katika Rahmahh za Allaah. Na mja mwovu, waja hupumzika naye, nchi, miti na wanyama)). [Al Bukhaariy 6512]
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
Kuomba Kinga Ya Kutolemewa Na Mitihani, Kuishilia Kwenye Naqama,
Qadhwaa Mbaya na Maadui Kufurahia Misiba
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijilinda kwa Allaah ('Azza wa Jalla) akisema:
((اللهمَّ إنِّي أعُوذُ بِكَ مِنْ جَهْدِ الْبَلَاءِ، وَدَرَكِ الشَّقَاءِ، وَسُوءِ الْقَضَاءِ، وَشَمَاتَةِ الْأَعْدَاءِ))
((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na kuelemewa na mitihani, kuishilia kwenye naqama, qadhwaa mbaya na kufurahia maadui misiba yangu)). [Al-Bukhaariy 6347 na Muslim 2707]
Faida Na Sharh:
جَهْدِ الْبَلَاءِ Jahdil-Balaai maana yake ni kila zito na la tabu kubwa linalomsibu mtu, likamlemea vibaya, naye hana uwezo wa kuliondosha au kukabiliana nalo. Ni kama kuandamwa na vyombo vya usalama kwa kupigania haki, nchi kuzama kwenye migogoro isiyomalizika, kusakamwa na magonjwa hatari na mengineyo.
Mitihani hii inaweza kuwa ya kimwili kama magonjwa, au ya kidhahania kama kukamiwa na watu kwa matusi, masimango, kuzushiwa na kunyanyaswa au kunyanyapaliwa.
درك الشقاء Darakish-Shaqaai ni lolote lenye kumfikisha mtu pabaya na kumkosesha furaha ya maisha, sawasawa kwa upande wa maisha yake ya hapa duniani, au kwa watu wake, au mali yake, na kadhalika. Pia kwa Aakhirah yake kama kupata adhabu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kutokana na madhambi aliyoyachuma hapa duniani.
سُوءِ الْقَضَاءِ Suw-il-Qadhwaai ni kila lile Alilokadiriwa mtu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ambalo linamsumbua na kumhuzunisha, au likamwingiza katika taharuki kubwa. Hili linajumuisha Dini na dunia, nafsi, ahli, mali, watoto na mwisho wa kuondoka hapa duniani.
Kuomba kinga kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hakupingani na suala la kuridhia Alilolipitisha na kulihukumu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa Waja Wake. Kwa kuwa Yeye Ametutaka sisi tujilinde na qadhwaa (majaaliwa) kama hizo ingawa Yeye Ndiye Anayezipitisha. Ndio maana tunaomba katika Du’aa ya Qunuwt tunaposwali Swalaah ya Witr:
اَللَّهُمَّ اِهْدِنِي فِيمَنْ هَدَيْتَ ، وَعَافِنِي فِيمَنْ عَافَيْتَ ، وَتَوَلَّنِي فِيمَنْ تَوَلَّيْتَ ، وَبَارِكْ لِي فِيمَا أَعْطَيْتَ ، وَقِنِي شَرَّ مَا قَضَيْتَ ، فَإِنَّكَ تَقْضِي وَلَا يُقْضَى عَلَيْكَ ، إِنَّهُ لَا يَذِلُّ مَنْ وَالَيْتَ ، تَبَارَكْتَ رَبَّنَا وَتَعَالَيْتَ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ .
(Ee Allaah! Nihidi pamoja na Uliowahidi, na Unipe ’aafiyah pamoja na Uliowapa ’aafiyah, na Nifanye kuwa ni mpenzi Wako pamoja na Uliowafanya wapenzi Wako, na Nibariki katika Ulichonipa na Nikinge na shari ya Ulilolihukumu kwani Wewe Unahukumu wala Huhukumiwi. Hakika hadhaliliki Uliyemfanya mpenzi, Umebarikika Ee Rabb wetu na Umetukuka) [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad)]
Ni lazima tujue kuwa qadhwaa kwa upande wa mwono wa waja inagawanyika sehemu mbili; ya kheri na ya shari. Wanachotakiwa watu ni kujilinda na ile ya shari wanayoiona wao kwa akili zao za ki-bin Aadam lakini ukweli wa mambo ni kuwa qadhwaa yote ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ambayo ni hukmu Yake na vitendo Vyake ni kheri; hakuna shari ndani yake. Kila kitu ni kwa hikma yake. Linaloonekana ni shari kwa viumbe, basi ndani yake utakuwa pamejaa kheri kochokocho.
شَمَاتَةِ الْأَعْدَاءِ Shamaatatil-a’daai ni maadui kufurahia janga linalompata hasimu yao au mtu wanayemchukia tu bila ya haki yoyote. Daima maadui hawa huomba apatwe na lolote la kumdhuru au la kumkwamisha na kadhalika. Hili likimpata mtu humchoma na kumuumiza sana kisaikolojia.
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
10-Kuomba Kinga Dhidi Ya Kuporomokewa, Kuanguka Toka Mwinuko Mrefu, Kughariki, Kuteketea Moto, Kuzugwazugwa Na Shaytwaan Wakati Wa Kifo, Kufa Mtu Akiikimbia Njia Ya Allaah Na Kifo Kitokanacho Na Kuumwa Na Kiumbe Chenye Sumu
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ajilinda kwa Allaah akisema:
اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْهَدْمِ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ التَّرَدِّي، وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ الْغَرَقِ، وَالْحَرَقِ، وَالْهَرَمِ، وَأَعُوذُ بِكَ أَنْ يَتَخَبَّطَنِيَ الشَّيْطَانُ عِنْدَ الْمَوْتِ، وَأَعُوذُ بِكَ أَنْ أَمُوتَ فِي سَبِيلِكَ مُدْبِرًا، وَأَعُوذُ بِكَ أَنْ أَمُوتَ لَدِيغًا
((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako kuporomokewa na jengo, na najilinda Kwako na kuanguka toka sehemu ndefu, na najilinda Kwako kufa maji, kuungua moto na uzee. Na najilinda Kwako shaytwaani kunizugazuga wakati wa kufa, na najilinda Kwako kufa wakati nikiikimbia Njia Yako, na najilinda Kwako kufa kwa kuumwa na kiumbe chenye sumu)). [Imekharijiwa na Abuu Daawuwd 1552, An-Nasaaiy 5546, Ahmad 14/303 na Atw-Twabaraaniy katika Al- Kabiyr 19/170. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyh An Nasaaiy 3/1123]
Faida na Sharh:
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda na kuporomokewa na jengo au jengo kuanguka mtu akiwa ndani, kuanguka toka sehemu ya mwinuko mrefu kama juu ya ghorofa refu, kughariki kama meli kuzama au kuvamiwa na mafuriko, kuteketea kwa moto na uzee.
Mambo haya pamoja na kwamba ndani yake ni kufariki katika daraja ya Shuhadaa kwa mujibu wa baadhi ya Hadiyth, - yaani ikiwa yatakuwa sababu ya kifo kwa Muislamu anakufa akiwa shahidi - lakini hata hivyo, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda nayo. Amejilinda nayo kwa kuwa ni magumu na mazito mno kwa mtu kuweza kuwa na uimara wa kutosha kuyakabili ambapo wakati huo shaytwaan anaitumia nafasi hiyo kuiteteresha iymaan ya Muislamu.
Aidha, matukio haya mara nyingi hutokea ghafla bila mtu kuyatarajia. Yanamkuta akiwa pengine hajaacha wasia au hakujiandaa ingawa mtu anatakiwa ajiandae na safari ya mauti wakati wote.
Kadhalika, matukio haya hutisha sana na hususan kwa wale wenye kuwashuhudia wahanga wakiteseka, wakipaparika, wakihaha na kuangamia bila wakati mwingine kuwa na uwezo wa kuwaokoa. Inakuwa ni hali ya kutisha na kuogofya mno.
Kufariki Shahidi katika matukio haya ni Shahidi ndogo kinyume na Shahidi halisia ya kufia vitani Muislamu akiipigania Dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kufariki huku kama Shahidi kila Muislamu anatamani na anaendea mbio ikiwa itabidi kama walivyokuwa Maswahaba pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika vita mbalimbali.
Lakini ajali hizi alizojilinda nazo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hapa, ni lazima Muislamu ajihadhari nazo na kutumia njia zote kuziepusha.
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anatutaka kabla ya kulala, tuzime taa zote na tuhakikishe kuwa vyombo vyote vimefunikwa vyema. Kwa wenye mitungi ya gesi, wahakikishe mtungi au mitungi imefungwa vyema. Pia mabomba ya maji yamefungwa vyema, milango ya nyumba imekomelewa vizuri na kadhalika. Hii yote ni kwa ajili ya kuepusha ajali na kuchukua hadhari.
Vilevile, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda na kufa huku mtu akiikimbia Jihadi au kutetea Dini au haki au kumwokoa nduguye Mwislamu au bin Aadam yeyote vyovyote iwavyo Dini yake na mfano wake. Hili bila shaka ni jambo baya mno, na ni moja kati ya madhambi makubwa yenye kumwangamiza mtu.
Kadhalika, amejilinda kufa kwa kuumwa na viumbe wenye sumu kama nyoka, nge na kadhalika. Mauti haya yanakuwa ni ya kushtukiza, na pia mtu anaweza kuteseka kwa maumivu makali baada ya kuumwa, akateseka yeye pamoja na jamaa zake wanaomuuguza.
Bila shaka umuhimu wa kuomba du’aa hii uko wazi kabisa kutokana na tunayoyaona na kuyasikia kuhusiana na matukio kama haya. Ni matukio ya kutisha na kuogofya mno ambayo inabidi kuyachukulia hadhari zote na kuomba Msaada wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) nyakati zote.
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
11-Kuomba Fadhila Na Rahmah Za Allaah
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimwomba Allaah akisema:
((اللَّهُمَّ إنِّي أَسْأَلُك مِنْ فَضْلِكَ وَرَحْمَتِكَ، فَإِنَّهُ لاَ يَمْلِكُهَا إِلاَّ أَنْتَ ))
((Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Fadhila Zako na Rahmah Zako, kwani hazimiliki yeyote isipokuwa Wewe tu)). [Imekharijiwa na Atw-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr" 10/178 na Ibn Shaybah 7/94. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika As-Silsilat Asw-Swahiyhah 4/57]
Faida Na Sharh:
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameomba katika du’aa hii fadhila kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alivyoamuru katika Kauli Yake:
"وَاسْأَلُوا اللَّهَ مِنْ فَضْلِه"
Na mwombeni Allaah Fadhla Zake. [An Nisaa (4:32)]
Yaani mwombeni Awaongezeeni Ihsaan Zake zaidi na Neema Zake katika mambo ya kidunia na ki Aakhirah, kwani hayo yote yako Mkononi Mwake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
قُلْ إِنَّ الْفَضْلَ بِيَدِ اللَّـهِ يُؤْتِيهِ مَن يَشَاء
Sema: Hakika fadhla zi Mkononi mwa Allaah, Humpa Amtakaye. [Aal-‘Imraan (3:73)]
Na kwa kuwa iko Mkononi Mwake, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Huitumia na Huisarifu Atakavyo Mwenyewe kwa Hikma Yake. Humpa Amtakaye kwa Hikma na Uwezo Wake uliokamilika, na Humnyima Amtakae kwa Hikma Yake na Uwezo Wake Uliokamilika.
Pia ameomba Rahmah, kwa kuwa Rahmah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) imekienea kila kitu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Amemwomba Allaah ('Azza wa Jalla) Amfunike nayo ili aweze kufaulu hapa duniani na huko Aakhirah.
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
12-Kuomba Kujilinda Dhidi Ya Njaa Na Khiyana
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijilinda kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akisema:
((اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْجُوعِ؛ فَإِنَّهُ بِئْسَ الضَّجِيعُ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ الْخِيَانَةِ؛ فَإِنَّهَا بِئْسَتِ الْبِطَانَةُ))
((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na njaa, kwani njaa ni mwenza mbaya sana ninayelala naye. Na najilinda Kwako na khiyana, kwani khiyana ni mwandani mwovu kabisa)). [Imekharijiwa na Abuu Daawuwd 1547, An-Nasaaiy 5483, na Ibn Maajah 3354]
Faida Na Sharh:
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda na njaa. Njaa ni ngumu kuikabili, huleta maumivu ya kipekee mwilini, humdhoofisha mtu, huchafua akili, huibua fikra mbaya na mawazo potovu, huteteresha ‘ibaadah, hulegeza uimara wa mtu katika kumcha Allaah ('Azza wa Jalla) , huchemsha hamaki na ghadhabu, husababisha tabia mbaya na hata wakati mwingine humwondolea mtu haiba yake na hishma yake akajikuta anafanya mambo ya ovyo asiyoyatarajia.
Aidha, inaweza kumsukuma akaiba, akasema uongo, akajidhalilisha na hata wakati mwingine kujiuza kimwili kwa akina mama. Pia inamfanya asiwajali wengine na kuangalia tumbo lake tu. Tunaona misaada ya vyakula inapogawanywa kwa wahanga wa janga fulani mathalan ambao wamepoteza kila wanachokimiliki, watu wananyosukumana na kukanyagana bila kujali kati ya mtoto na mtu mzima, mzee na kijana, mwanamke au mwanamume, mlemavu au mzima; kila mtu anajiwania yeye apate kwanza kabla ya mwingine. Hayo yote ni madhara ya njaa aliyojilinda nayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Mtu akibanwa na njaa, usingizi pia humruka. Usingizi huja pale tumbo linapokuwa na kitu. Kama halina kitu, basi usingizi nao hupaa. Na madhara ya mtu kutopata usingizi ni makubwa kwa mwili wake.
Kadhalika, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda na khiyana. Khiyana ni kuvunja ahadi kwa siri. Inaweza kuwa khiyana kati ya mtu na mtu, au kati ya mtu na Rabb wake (Azza wa Jalla). Inakusanya makalifisho yote ya ki-Shariy’ah Aliyoyaamuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anayetuambia:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَخُونُوا اللَّهَ وَالرَّسُولَ وَتَخُونُوا أَمَانَاتِكُمْ وَأَنْتُمْ تَعْلَمُونَ
Enyi walioamini! Msimfanyie khiyana Allaah na Rasuli na wala msikhini amana zenu na hali nyinyi mnajua. [Al-Anfaal (8:27)]
Mtu akiwa na sifa hii, anakuwa kana kwamba ndani ya mwili wake anaishi na mwandani mbaya kabisa. Kuishi na mwandani kama huyu ni khatari kubwa kabisa. Ni lazima Muislamu aachane na tabia kama hii. Ni sawa na mtu kuishi na ugonjwa hatari kabisa kama saratani. Asipoutibu haraka, basi utamuua na kummaliza.
Ni lazima Muislamu achunge makalifisho yote ya ki-Shariy’ah aliyokalifishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na ayatekeleze kama inavyotakikana. Pia achunge amana, ahadi na yote yanayohusiana na wenzake wana Aadam, kwani hayo yote ataulizwa Siku ya Qiyaamah.
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
13-Kujilinda Dhidi Ya Kupotea Au Kupoteza, Au Kuteleza Au Kutelezesha, Au Kudhulumu
Imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini Ummu Salamah Hind Al-Makhzuwmiyyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akisema: Hakutoka kamwe Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nyumbani kwangu ila hunyanyua macho yake mbinguni na kusema:
((اللَّهُمَّ اني أَعُوذُ بِكَ أَنْ أَضِلَّ أَوْ أُضَلَّ أَوْ أَزِلَّ أَوْ أُزَلَّ أَوْ أَظْلِمَ أَوْ أُظْلَمَ أَوْ أَجْهَلَ أَوْ يُجْهَلَ عَلَيَّ ))
((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako kupotea au kupoteza, au kuteleza kufanya kosa au kutelezeshwa, au kudhulumu au kudhulumiwa, au kufanya kitendo cha kisafihi au mimi kufanyiwa usafihi)). [Imesimuliwa na Ahlus-Sunan wanne na wengineo]
Faida Na Sharh:
Hii ni du’aa adhimu ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa haiachi kila anapotoka nyumbani. Kunyanyua kwake macho mbinguni kunaashiria 'Uluwa wa Allaah (Jalla wa ‘Alaa) juu ya Viumbe Vyake vyote, na kuwa Yeye Anaviona viumbe hivyo katika hali zao zote, na kuwa hakuna chochote kinachofichikana Kwake. Na hili linatukumbusha sisi kuwa mtu anapotoka nyumbani, basi amche Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) popote pale awapo katika mihangaiko yake ya kutafuta rizki, na ajue kwamba Allaah (‘Azza wa Jalla) Anaziona nyenendo zake zote. Huko anakokwenda ni lazima atatangamana na watu wa aina zote na tabaka zote; wema na wabaya, atasuguana nao, na ataamiliana nao.
Katika mtangamano huu, panatokea mengi mabaya ya haramu ambayo yeye anaweza kuyafanya au kufanyiwa ambayo inabidi ajihadhari nayo.
Na hayo ndio haya aliyotukusanyia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika du’aa hii adhimu. Yote haya ni katika madhambi makubwa angamizi.
Ameomba akingwe asitumbukie kwenye dhwalaalah (upotofu) ambayo ni kinyume na hidaayah, au mtu mwingine kumtumbukiza. Na hili ndilo daima tunaloliomba katika Swalaah zetu zote tunaposoma Suwrah Al-Faatihah kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuongoe Njia iliyonyooka isiyo ya waliopotea kutokana na hatari ya dhwalalah (upotofu).
Akaomba akingwe asiteleze au kumtelezesha mwingine. Kuteleza huku ni kufanya dhambi bila ya kujua au kuhisi. Hii inawezekana kutokana na kitendo au kauli, na haya yanafanyika sana katika maisha yetu ya kila siku. Kuna mengi ambayo tunayaona ni madogo na hayana neno, lakini dhambi zake ni kubwa kwa Allaah ('Azza wa Jalla).
Akaomba alindwe asije kumdhulumu mtu sawasawa katika mali yake, hishma yake, utu wake na kadhalika, au yeye kufanyiwa dhulma, kwani dhulma ya aina yoyote inamuumiza sana mdhulumiwa ingawa haki yake atakwenda kuipata Siku ya Qiyaamah. Lakini pamoja na hivyo, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anajilinda, kwani mdhulumiwa wakati mwingine anaweza kujisahau na kupetuka mipaka zaidi ya alivyodhulumiwa, na hapo yeye kuwa mkosa.
Mwisho akaomba kinga asifanye kitendo cha kijahili au kisafihi kama kukebehi watu, kuwadhihaki, kuwakejeli au kuwadharau na kadhalika, au yeye kufanyiwa hayo.
Kuongezea na haya, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa pia akisema anapotoka nyumbani:
بِسْمِ اللَّهِ تَوَكَّلْتُ عَلَى اللَّهِ لا حَوْلَ وَلا قُوَّةَ إِلا بِاللَّهِ
((BismiLLaah. Nimetawakkal kwa Allaah, hakuna uwezo wala nguvu ila kutoka kwa Allaah)). [Imepokelewa na Anas bin Maalik. Imesimuliwa na At-Tirmidhiy katika Sunan yake 3348. Abuu ‘Iysaa kasema ni Hadiyh Hasan Swahiyh]
Na mwenye kusema hivi basi huambiwa: "Umetoshelezwa na umekingwa", na shaytwaan hukaa mbali naye.
Haya ndiyo maelekezo ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo inabidi tuyazingatie ili tupate kinga ya duniani na kesho Aakhirah.
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
14-Kujikinga Na Shari Ya Sehemu Mtu Anaposhukia
Imepokelewa toka kwa Khawlah binti Al-Hakiym akisema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((من نزل منزلاً ثم قال: أعوذ بكلمات الله التامات من شر ما خلق لم يضره شيء حتى يرتحل من منزله ذلك))
((Mwenye kufikia mashukio (nyumba) yoyote kisha akasema: Najilinda kwa Maneno ya Allaah yaliyotimu na shari ya Alivyoviumba, hakitomdhuru chochote mpaka aondoke kwenye mashukio yake hayo)). [Imesimuliwa na Muslim katika Swahiyh yake toka kwa Khawlah bint Al-Hakiym]
Faida Na Sharh:
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anasafiri, alikuwa hapiti kwenye mwinuko wowote ila hupiga takbiyr, na hashuki bonde lolote ila humsabihi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hii ndiyo hali aliyokuwa nayo kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuwa na mwonjo wa hali ya juu wa kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika hali zote. Hili linatakiwa liwe kiigizo chema kwetu katika hali zetu zote.
Pia mtu anapohamia katika nyumba mpya asome du’aa hiyo na si kufanya kama wafanyao wenye kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kuchinja na kukanyaga damu, au kuvunja mayai au kutundika vitu na kadhalika kwa ajili ya kinga.
Hata mtu anapokaa kufanya mkataba wa manunuzi, anapoingia kutoa darsa au muhaadharah, anapoanza mradi, anapokwenda mahakamani, anapokwenda kazini na kwenye mishughuliko yake yote ya kidunia na ki-Aakhirah, basi asisahau kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Na safari kwa hali yoyote ina mazito yake. Mazito haya yote Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameyafanya kuwa ni sehemu ya ‘ibaadah ya kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kutaamuli yote anayoyaona msafiri safarini.
Mwana Aadam anapokithirisha kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla), basi inaundika kwake hisia ya sita inayomkumbusha daima Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kumkumbusha Uwezo Wake kwa kila anachokiona katika mazingira yanayomzunguka na anayoyapita.
Maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) yaliyotimu kama walivyosema baadhi ya ‘Ulamaa ni:
سبحان الله والحمد لله ولا إله إلا الله والله أكبر
Ndani yake kuna tasbiyh, himdi, tawhiyd na takbiyr.
Kila mahala anapokwenda mtu kuna hatari. Mtu anaweza kusafiri kwenda nje ya nchi, na huko akaibiwa mkoba wake wenye kila kitu muhimu ndani yake; pasi ya kusafiria, pesa, kadi na vinginevyo muhimu. Hapo hukumbana na kila aina ya mateso. Hata kuufikia ubalozi wake kumsaidia wakati mwingine inakuwa ni kazi kubwa kwa kuwa hata pesa ya kuendea huko anakuwa hana. Hata ndani ya nchi yake, itabidi ahangaike sana mpaka aweze kuweka mambo sawa.
Wakati mwingine anapofika uwanjani sehemu ya kupokea mizigo, anakuta mizigo yake haikuwasili na ndege aliyopanda yeye. Linaibuka tatizo jingine hapo, kwa kuwa kila kitu chake kimo humo. Ndege ilipotua salama, alikuwa na furaha isiyo na kifani, kwa kuwa lau pangelitokea tatizo lolote ndege ikiwa juu, basi asingelibakia mtu. Baadhi ya watu hupiga makofi, badala ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kuwafikisha salama. Hilo wamelianzisha wamagharibi, na sisi tunaiga kibubusa tu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anawasili salama, baada ya kufanikisha vyema safari yake na kurudi salama kwa wakeze, wanawe na watu wake, alikuwa akisema:
الحمد لله الذي بنعمته تتم الصالحات
Himdi Ni Yake Allaah Ambaye kwa Neema Zake yanatimu mema matengefu.
Haya ni baadhi ya yanayotukabili katika safari zetu za siku hizi kwa wale wenye kusafiri safari za kawaida. Lakini kuna wasafiri wengine na hususan watafiti na wataalamu wa mambo mbalimbali wanaozamia ndani ya misitu mizito, vina virefu vya bahari, majangwa, mabonde na kadhalika, hawa hatari inakuwa kubwa zaidi. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha du’aa nyingine ya kujikinga na hatari ya haya. Inasimuliwa na ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaposafiri na usiku ukaingia husema:
يا أرض ربي وربكِ الله، أعوذ بالله من شرك وشر ما فيكِ، وشر ما خلق فيكِ، وشر ما يدب عليكِ
((Ee ardhi! Rabb wangu na Rabb wako ni Allaah. Najilinda kwa Allaah na shari yako, na shari ya vilivyomo ndani yako, na shari ya vilivyoumbwa ndani yako, na shari ya vinavyotambaa juu yako)). [Imesimuliwa na Abuu Daawuwd na kupokelewa toka kwa 'Abdullaah bin ‘Umar]
Pia alikuwa akijikinga na nge, nyoka, na wanyama wakali.
Alikuwa akisema:
أعوذ بالله من أسد وأسود ومن الحية والعقرب ومن ساكن البلد ومن والد وما ولد
((Najilinda Kwako na simba, mijoka, nyoka, nge, mkazi wa nchi, na kilichozaa na kilichozaliwa)). [Imepokelewa na ‘Abdullaah bin ‘Umar]
Mkazi wa nchi hapa ni ima wana Aadam, au majini. Na kilichozaa ni Ibliys na kilichozaliwa ni mashaytwaan, au vyote vyenye kuzaa na kuzaliwa ardhini na vyenye madhara kwa mwana Aadam.
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/24
[2] http://www.alhidaaya.com
[3] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9486&title=Du%E2%80%99aa%20Za%20Ruqyah%20%28Kinga%29%20Faida%20Na%20Sharh%20Zake
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9487&title=01-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%3A%20Kuomba%20Kuwezeshwa%20Kutenda%20Kheri%2C%20Kuacha%20Munkari%2C%20Kuwapenda%20Masikini%20Kupata%20Maghfirah%20na%20Rahmah%2C%20Kuepushwa%20na%20Fitnah%2C%20Na%20Kulipata%20Penzi%20La%20Allaah
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9488&title=02-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%3A%20Kuomba%20Kinga%20Dhidi%20Ya%20Tabia%20Za%20Kuchukiza%2C%20Matendo%2C%20Hawaa%20Na%20Magonjwa%20Yote%20Mabaya
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9489&title=03-Du%27aa%20Za%20Ruqya%3A%20Kuomba%20Kinga%20Dhidi%20Ya%20Shari%20Ya%20Masikio%2C%20Macho%2C%20Ulimi%2C%20Moyo%20Na%20Utupu
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9490&title=04-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%3A%20Kuomba%20Uthibiti%20Wa%20Moyo%20Juu%20Ya%20Uislamu
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9491&title=05-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%3A%20Kuomba%20Yaqiyn%2C%20%E2%80%98Afwa%20na%20%E2%80%98Aafiyah%20Duniani%20na%20Aakhirah
[9] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9492&title=06-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%3A%20Kuomba%20Mu%E2%80%99aafaat%2C%20Nayo%20Ni%20Katika%20Du%E2%80%99aa%20Bora%20Kabisa
[10] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9493&title=07-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%20Na%20Tafsiri%20Zake%3A%20Kuomba%20Uongofu%2C%20Taqwa%2C%20Utakasifu%20na%20Utajiri%20wa%20Moyo
[11] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9494&title=08-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%3A%20Kuomba%20Kutengenekewa%20Dini%2C%20Dunia%2C%20Aakhirah%20na%20Umri%20Kuwa%20Ziada%20Ya%20Kheri%20Zote%20%20Na%20Mauti%20Kuwa%20Mapumziko%20Na%20Shari%20Zote
[12] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9495&title=09-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%3A%20Kinga%20Ya%20Kutolemewa%20Na%20Mitihani%2C%20Kuishilia%20Kwenye%20Naqama%2C%20Qadhwaa%20Mbaya%20na%20Maadui%20Kufurahia%20Misiba
[13] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9496&title=10-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%3A%20Kinga%20Dhidi%20Ya%20Kuporomokewa%2C%20Kuanguka%20Toka%20Mwinuko%20Mrefu%2C%20Kughariki%2C%20Kuteketea%20Moto%2C%20Kuzugwazugwa%20Na%20Shaytwaan%20Wakati%20Wa%20Kifo%2C%20Kufa%20Mtu%20Akiikimbia%20Njia%20Ya%20Allaah%2C%20Kifo%20Kitokanacho%20Na%20Kuumwa%20Na%20Kiumbe%20Chenye%20Sumu
[14] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9497&title=11-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%3A%20Kuomba%20%20Fadhla%20Na%20Rahmah%20Za%20Allaah
[15] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9498&title=12-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%3A%20Kuomba%20Kujilinda%20Dhidi%20Ya%20Njaa%20Na%20Khiyana
[16] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9499&title=13-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%3A%20Kujilinda%20Dhidi%20Ya%20Kupotea%20Au%20Kupoteza%2C%20Au%20Kuteleza%20Au%20Kutelezesha%2C%20Au%20Kudhulumu
[17] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9500&title=14-Du%27aa%20Za%20Ruqyah%3A%20Kujikinga%20Na%20Shari%20Ya%20Sehemu%20Mtu%20Anaposhukia