Skip navigation.
Home kabah

Kumsomea Khitmah Maiti, Kumchinjia Na Kumuombea Duaa Kwa Pamoja

SWALI:

Assalaam alaykum.

Naomba kuuliza: 1. Ikiwa hairuhusiwi kumfanyia khitima marehemu, je, inaruhusiwa kuchinja mnyama au kutoa sadaka kwa ajili ya kumuombea dua marehemu? Yaani nikakusudia mathalani kufanya sadaka ya chakula/ kichinjo kwa makusudio kuwa thawabu za sadaka hiyo iwe ni dua kwa marehemu wangu.

 2. Ikiwa sadaka hiyo inruhusiwa, je ni sahihi kuwakusanya waislamu kwa ajili ya dua na sadaka hiyo?

Naomba mjibu Insha Allah niweze kuelimika.

Wabillah Tawfiq.

 

 



 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Swali lako lina mas-ala matatu; Kusoma Khitmah, kuchinja na kusoma du'aa kwa pamoja kwa ajili ya maiti.

Kwa ujumla, ikiwa mtu anataka kumfanyia mzazi wake aliyekwishafariki vitendo ambavyo vitamfikia thawabu zake, ni lazima atende vitendo ambavyo vimepatikana dalili zake katika Sunnah. Kufanya kinyume na hivyo ni kupoteza mtu muda wake, mali yake kwa jambo ambalo halina thamani mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama alivyosema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 (( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy]

Shaykh Al-Fawzaan alipoulizwa kuhusu vitendo gani vyema ambavyo aliye hai anaweza kumfanyia maiti alijibu:

"Maiti anaweza kunufaika kwa vitendo vya walio hai ambavyo vinatokana na dalili sahihi inayodhihirisha kuruhusiwa kama; kumuombea du'aa, kumuombea maghfira, kumfanyia sadaka, kumfanyia Hajj na 'Umrah, kumlipia madeni yake na kumtekelezea mirathi yake ya Kiislam. Vitendo vyote hivyo vimethibiti kisheria. Na baadhi ya Maulamaa wameunganisha na hayo pia vitendo vyote vengine vya ibada ambavyo Muislamu hutenda kwa ajili ya Muislamu mwengine ambaye yu hai au amefariki. Lakini, iliyo sahihi ni kujiweka katika mipaka ya yale yaliyoruhusiwa yakiwa na dalili sahihi, kwani hivyo itakuwa ni kutokana na maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anaposema:

 ((وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَى))

((Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyoyafanya mwenyewe)) [An-Najm:39]

[Shaykh ibn Fawzaan

Al-Muntwaqaa min Fataawa  Shaykh ibn Fawzaan – Mjalada 2, Uk. 161, Fatwa Namba 139] 

Mas-ala ya Kuchinja.

Kwa vile haikupatikana dalili kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja kwa ajili ya maiti yeyote kwa nia ya kumfikia thawabu, hivyo kitendo hicho hakipasi kumtendea maiti.

Mas-ala ya kuomba du'aa pamoja.

Aghlabu ya watu hukusanyika katika shughuli kama hizo na nyinginezo na huomba du'aa kwa sauti pamoja, jambo ambalo halikupatikana dalili katika mafunzo ya dini yetu.

Muislamu anaweza kumuombea du'aa mzazi wake akiwa pekee na hii ni dalili kutoka katika Hadiyth ifuatayo:

 ))إذا مات ابن آدم انقطع عمله إلا من ثلاث: صدقة جارية، أو علم ينتفع به، أو ولد صالح يدعو له))  رواه النسائي و الترمذي

((Anapokufa binaadamu hukatika vitendo vyake (vyema) isipokuwa (vitendo) vitatu; sadaka inayoendelea, elimu inayoendelea kunufaisha au mtoto mwema anayemuombea)) [An-Nasaaiy na At-Trimidhiy]

Hii kwa maana amuombee yeye mwenyewe peke yake na sio kujumuisha watu kumuombea kwani Hadiyth iko wazi kuwa ni 'mtoto mwema anayemuombea'.

Kuhusu Khitmah

Nalo ni jambo lisilokuwa na dalili katika mafunzo ya dini yetu, kwani hakuwahi Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumsomea khitma mtu yeyote katika maisha yake. Watoto wake na maswahaba walifariki katika uhai wake na hakuna hata masimulizi yoyote yale kuwa alikusanya watu kuwasomea Khitma; alifiwa na wanawe, ‘ami zake, baba, mama na hata marafiki zake Maswahaba, lakini hakuwahi kuwafanyia Khitmah. Pia alipofariki yeye, wapenzi wake kama kina Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan na hata binamu yake ‘Aliy (radhiya Allaahu ‘anhum), hawakuwahi kumfanyia jambo kama hilo au hata lenye kufanana na hilo! Nao walikuwa wanampenda sana na pia kuwa na uchungu naye kuliko sisi. Hivyo kutenda ibada hiyo ni kuzusha katika dini jambo ambalo amelikemea sana Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani alikuwa akitanguliza maonyo katika khutba zake:

 (( إن خير الكلام كلام الله وخير الهدي هدي محمد صلى الله علي وسلم  وشر الأمور محدثاتها وكل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة وكل ضلالة في النار))  أخرجه مسلم في صحيحه 

 ((Maneno bora  ni Kitabu cha Allah (Qur-aan) na uongofu mbora kabisa ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika dini) ni bid'ah (uzushi) na kila bid'ah ni motoni)[Muslim katika swahiyh yake

Bonyeza hapa usome madhara ya khitma.

KHITMAH: Kutokufaa Na Madhara Yake

Na Allah Anajua zaidi