كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji
Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
Abu Maalik Kamaal Bin As-Sayyid Saalim
Imetarjumiwa na 'Abdullaah Mu'aawiyah (Abu Baasim)
Alhidaaya.com
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
Alhidaaya.com [3]
01-Chinjo La Kisharia: Taarifu Yake:
"التَّذْكِيَةُ" katika lugha, ni “maswdar” (kiini) ya kitenzi "ذَكَّيْتُ الْحَيَوَانَ" (nimemchinja mnyama), na nomino ni "الذَّكَاةُ" (chinjo au kuchinja).
Ama katika istilahi, ni sababisho, au ni njia yenye kufikishia kuhalalika kumla mnyama wa nchi kavu kwa hiari.
Mahanafi wameielezea kama ni njia ya kisharia ya kubakia utwahara wa mnyama na uhalali wa kumla kama mnyama mwenyewe analiwa, na uhalali wa kunufaika na ngozi yake na nywele zake kama haliwi.
Ama Mahanbali, wao wameielezea "التَّذْكِيَةُ" kama ni kumchinja au kumdunga chini ya shingo mnyama ambaye imewezekana kumdhibiti na anayefaa kuliwa, mwenye kuishi nchi kavu, lakini asiwe nzige au mfano wake, kwa kukata koo na umio. Au ni kumjeruhi mnyama asiyewezekanika kumdhibiti kama itashindikana kukata koo na umio.
"التَّذْكِيَةُ" iko aina mbili, nazo ni "الذَّبْحُ" na "النَّحْرُ"
Taarifu Ya "الذَّبْحُ":
Katika lugha ina maana ya kupasua, nayo ndio maana asili. Kisha ikatumika katika kukata koo kutokea ndani kwenye maungio kati ya shingo na kichwa chini ya taya mbili.
Ama katika istilahi, neno hili lina maana nyingi. Kati ya maana hizo ni njia ya kufikia kuhalalika mnyama, ni sawa kwa kumkata shingoni, au chini ya shingo, kwa mnyama anayeweza kudhibitiwa, au kwa kuitoa roho ya mnyama asiyeweza kudhibitiwa kwa kumjeruhi sehemu yoyote mwilini mwake kwa kitu chenye ncha kali, au kwa kujeruhiwa na mnyama mwindaji aliyefunzwa. "الذَّبْحُ" inakuwa kwa wanyama wote isipokuwa kwa ngamia tu.
Taarifu Ya "النَّحْرُ":
Katika lugha ina maana ya sehemu ya juu ya kifua, au sehemu ya kidani, au kifua chote. Pia ina maana ya kudunga chini ya shingo ya mnyama.
Na katika istilahi, ni kudunga (kuchana kwa kisu) sehemu ya chini ya shingo ya mnyama, na hii inakuwa spesheli kwa ngamia tu.
Faida:
Kumkhusisha ngamia kwa "النَّحْرُ" (kumdunga), na wanyama wengineo kwa "الذَّبْحُ" (kuchinja), ni jambo linalopendeza kwa Jumhuwr, lakini si waajib. Kupendeza huko ni kwa kuwa Allaah Ta’aalaa Ametaja "النَّحْرُ" kwa upande wa ngamia pale Aliposema:
"فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ"
“Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja (dunga)”. [Al-Kawthar : 02].
Na kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo Ametaja "الذَّبْحُ" Aliposema:
"إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تَذْبَحُوا بَقَرَةً"
“Hakika Allaah Anakuamuruni mchinje ng’ombe”. [Al-Baqarah : 67].
Na kwa kuwa asili katika kuchinja, ni kuangalia lile lenye unafuu zaidi kwa mnyama. Na lile litakalompumzisha na kumwepushia taabu, mateso na uchungu, ndilo bora na litakiwalo zaidi. Hivyo basi, la sahali zaidi kwa ngamia ni kumdunga kwa kuwa sehemu ya chini ya shingo yake haina nyama, wakati wanyama wengine nyama zao zimekusanyika kwenye shingo. Ng’ombe, mbuzi na kondoo, shingo zao zote hazitofautiani.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
Alhidaaya.com [3]
02-Chinjo La Kisharia: Hukmu Ya Kuchinja Na Hikmah Ya Kushurutishwa Kwake:
Kuchinja ni sharti ya kuhalalisha kuliwa mnyama ambaye ni halali kuliwa kisharia, na kunufaika naye kwa njia zote. Allaah Ta’aalaa Amesema:
"وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ"
“Na wala msile katika ambavyo halikutajwa Jina la Allaah (wakati wa kuchinjwa), kwani huo ni ukiukaji wa utiifu kwa Allaah”. [Al-An’aam : 121].
Raafi’u bin Khadiyj alimwambia Rasuli:
"إِنَّا لاَقُو الْعَدُوِّ غَدًا وَلَيْسَتْ مَعَنَا مُدًى قَالَ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : " أَعْجِلْ أَوْ أَرْنِي مَا أَنْهَرَ الدَّمَ وَذُكِرَ اسْمُ اللَّهِ فَكُلْ لَيْسَ السِّنَّ وَالظُّفُرَ وَسَأُحَدِّثُكَ أَمَّا السِّنُّ فَعَظْمٌ وَأَمَّا الظُّفُرُ فَمُدَى الْحَبَشَةِ"
“Sisi kesho tunapambana na adui, na hatuna visu (vya kuchinjia). Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Chinja haraka au kuwa makini (unaponoa), (ukichinjia kwa) chochote chenye kuchuruzisha damu sambamba na kutajwa Jina la Allaah, basi kula isipokuwa jino au kucha, na nitakueleza (sababu ya hilo). Ama jino, hilo ni mfupa, na ama kucha, hizo ni kisu cha Wahabeshi (wanachinja kwa kutumia kucha zao)”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5543) na Muslim (1968)].
Hadiyth hii inatupa faida kwamba kumwagika damu ya mnyama sambamba na kutajwa Jina la Allaah wakati wa kuchinjwa, ni sharti la kuhalalika kuliwa nyama yake.
Ama hikmah ya kuwa kuchinja ni lazima, ni kwamba uharamu wa kumla mnyama anayeliwa utabaki madhali damu yake iko ndani ya mwili wake, na damu hii haitoki mwilini mwake ila kwa kuchinjwa. Kadhalika, sharia imekuja kwa ajili ya kuhalalisha kwa njia maalum vyote vizuri vya halali. Allaah Ta’aalaa Amesema:
"يَسْأَلُونَكَ مَاذَا أُحِلَّ لَهُمْ ۖ قُلْ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ"
“Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: Mmehalalishiwa vilivyo vizuri”. [Al-An’aam : 04].
Na Anasema tena:
"وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ"
“Na anawahalalishia vilivyo vizuri na anawaharamishia vilivyo vibaya”. [Al-A’araaf : 157].
Na nyama hiyo haiwi salama au yenye manufaa mema ila kwa kumwagika damu ya mnyama na kutoka nje ya mwili wake, ima kwa kuchinjwa "ذَبْحً" au kwa kudungwa chini ya shingo "نَحْرٌ". Na kwa sababu hii, mfu umeharamishwa, kwa kuwa damu chafu bado ipo ndani ya mwili wa mnyama.
Hikma nyinginezo za kuchinja mnyama ni kuiweka mbali shirki na matendo ya washirikina, kukipambanua kinacholiwa na mwanadamu na kile kinacholiwa na wanyama wakali, lakini pia mwanadamu akumbuke Ukarimu wa Allaah kwake kwa kumruhusu kuua na kutoa roho ya mnyama ili aweze kumla na kunufaika naye kiujumla baada ya kufa.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
Alhidaaya.com [3]
03-Chinjo La Kisharia: Masharti Ya Kuchinja:
Kuna masharti kadhaa ambayo ni lazima yawepo ili mnyama anayechinjwa awe halali kuliwa. Baadhi yake yanahusiana na mnyama mwenyewe, mengine yanahusiana na mchinjaji, na baadhi nyingine kwa zana ya kuchinjia.
Masharti Ya Mnyama Anayechinjwa
1- Awe hai wakati anapochinjwa. Mnyama mfu hachinjwi.
2- Kuchinjwa kwake kuwe ndio sababu ya kutoka roho yake, na si kutokana na sababu nyingine.
3- Asiwe amewindwa eneo la Al-Haram. Hili limeelezwa katika Kitabu cha Hijja kwamba ni marufuku kuwinda eneo la Al-Haram. Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuhusiana na Makkah:
"فَلَا يُنَفَّرُ صَيْدُهَا"
“Wanyama wake hawasumbuliwi (wala kuwindwa)”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1349) na Muslim (1355)].
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
Alhidaaya.com [3]
04-Chinjo La Kisharia: Masharti Ya Mchinjaji
1- Awe na akili zake timamu. Ni sawa akiwa mwanaume au mwanamke, aliye baleghe au asiye baleghe kama ni mpambanuzi. Chinjo la mwendawazimu au mtoto asiye na akili halifai, na pia mlevi. Kwa kuwa kusudio la kuchinja na kulitaja Jina la Allaah halitoki toka kwa mtu asiye na akili. Hii ndio kauli ya Jumhuwr.
Ibn Hazm amesema: “Chinjo la asiye baleghe halifai. Chinjo hilo ni sawa na la mwendawazimu na mlevi, kwa kuwa si wao wanaosemeshwa na kauli ya sharia katika Neno Lake Ta’aalaa:
"إِلَّا مَا ذَكَّيْتُمْ"
“Isipokuwa mliyewahi kumchinja kihalali (kabla ya kufa)”. [Al-Maaidah : 03]…kwa kuwa wao si wakalifishwa”.
(2) Awe Muislamu, au mtu wa Kitabu (Myahudi au Mnaswara). Chinjo la mwabudu masanamu na viumbe, au mmajusi haliswihi. Hili limekubaliwa na Fuqahaa wote. Sababu ni kuwa asiye Muislamu, halitaji na wala hana habari kabisa na Jina la Allaah, bali mpagani hulitaja jina la asiye Allaah, au huchinja kwa ajili ya masanamu au viabudiwa vyao. Na Allaah Ta’aalaa Amesema:
"حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ ...... وَمَا ذُبِحَ عَلَى النُّصُبِ"
“Mmeharamishiwa nyamafu…………. na waliochinjwa kwa ajili ya ‘ibaadah ya waabudiwa”. [Al-Maaidah : 03].
Na mmajusi halitaji Jina la Allaah wakati anachinja.
Ama watu wa Kitabu (Mayahudi na Manaswara), mnyama wanaomchinja watu hawa ni halali kuliwa kutokana na Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ"
“Na nyama iliyochinjwa na waliopewa Kitabu ni halali kwenu”. [Al-Maaidah: 05].
Ibn ‘Abbaas amesema: Makusudio ya "طَعَامُهُمْ" katika Aayah hii, ni nyama iliyochinjwa na watu hao, yaani "ذَبَائِحُهُمْ".
Kauli hii inatiliwa nguvu kwa kusema, lau usingelikuwa muradi wa "طَعَامُهُمْ" (chakula chao) kuwa kwa maana ya "ذَبَائِحُهُمْ" (nyama iliyochinjwa na wao), basi kutajwa kwa kuainishwa Watu wa Kitabu hapa kusingelikuwa na maana yoyote, kwa kuwa vyakula vinginevyo vya makafiri wote visivyo nyama ni halali.
Angalizo:
Nyama Ya Myahudi Au Mnaswara Ni Halali Kama Haikujulikana Kwamba Ameitajia Jina Lisilo La Allaah Ta’aalaa
Kama ataitajia jina lisilo la Allaah kama kusema: Kwa jina la masihi, au bikira, au sanamu, basi hailiwi. Na hii ni kwa Neno Lake Ta’aalaa katika kubainisha vilivyoharamishwa:
"وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ"
“Na kilichotajiwa asiyekuwa Allaah katika kuchinjwa kwake”. [Al-Maaidah : 03].
3- Asiwe ni mwenye kuhirimia (Hajji) akichinja mawindo ya nchi kavu
Ni haramu kwa aliyehirimia Hajji kujihusisha na mawindo ya nchi kavu, ni sawa kwa kuwinda, au kuchinja, au kuua. Ni haramu pia kwake kumwelekeza mwenzake asiye kwenye Ihraam sehemu alipo mnyama, au kumwashiria upande aliko, kama lilivyobainishwa hili katika Kitabu cha Hijja.
Hivyo basi, chochote atakachokichinja aliyehirimia katika mawindo ya nchi kavu, basi kinakuwa ni mfu, hakifai kuliwa. Vile vile kinakuwa mfu alichokichinja mtu asiye katika ihraam kwa kuelekezewa na aliyehirimia au kuashiriwa wapi alipokuwa mnyama. Allaah Ta’aalaa Anasema:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْتُلُوا الصَّيْدَ وَأَنتُمْ حُرُمٌ"
“Enyi walioamini! Msiue mawindo na hali mko katika ihraam”. [Al-Maaidah: 95].
Na Neno Lake:
"وَحُرِّمَ عَلَيْكُمْ صَيْدُ الْبَرِّ مَا دُمْتُمْ حُرُمًا"
“Na mmeharamishiwa mawindo ya nchi kavu madamu mtakuwa katika ihraam”. [Al-Maaidah : 96].
Angalizo:
Lililoharamishwa kwa aliye kwenye ihraam kuchinja, ni mnyama pori anayewindwa tu. Ama wanyama wa kufugwa kama kuku, mbuzi, kondoo na ngamia, hawa hakatazwi, anaweza kuchinja tu. Uharamu ni kwa mnyama pori tu anayewindwa. Ama wengineo, hao wanaingia kiujumla ndani ya wigo wa uhalali. Na hili limekubaliwa na madhehebu yote.
4- Alitaje Jina la Allaah wakati wa kuchinja akikumbuka
Kama atafanya kusudi kutolitaja nailhali anaweza kulitamka, basi mnyama huyo hafai kuliwa kwa mujibu wa kauli ya Jumhuwr. Ama aliyesahau, au akiwa ni bubu, mnyama ataliwa. Allaah Ta’aalaa Amesema:
"وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ"
“Na wala msile katika ambavyo halikutajwa Jina la Allaah (wakati wa kuchinjwa), kwani huo ni ukiukaji wa utiifu kwa Allaah”. [Al-an’aam : 121].
Na kwa Hadiyth ya Raafi’u bin Khadiyj kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَا أَنْهَرَ الدَّمَ وَذُكِرَ اسْمُ اللَّهِ فَكُلْ"
“(Ukichinjia) chochote chenye kuchuruzisha damu sambamba na kutajwa Jina la Allaah, basi kula”. [Hadiyh Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo].
Na kwa ajili hii, Jumhuwr wameshurutisha ulazima wa kulitaja Jina la Allaah wakati wa kuchinja kwa aliyekumbuka hilo na kuwa na uwezo wa kutamka. Lakini Ash-Shaafi’iy anasema kuwa hilo ni jambo linalopendeza (mustahabbu) na si waajib kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah:
"أنَّ قَوْمًا قَالُوْا للنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وآلهِ وَسَلَّمَ: إِنَّ قَوْمَنَا يْأتُوْنَنَا بِلَحْمٍ لا نَدْرِيْ أَذُكِرَ اسْمُ اللهِ عَلَيْهَ أَمْ لاَ؟ فَقَالَ: سَمُّوْا عَلَيْهِ أَنْتُمْ وَكُلُوا. قَالَتْ: وَكَانُوْا حَدِيْثِي عَهْدٍ بِالْكُفْرِ"
“Kwamba watu fulani walimwambia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam: Hakika watu wetu wanatuletea nyama ambazo hatujui kama zimetajiwa Jina la Allaah au la. Rasuli akawaambia: Zitajieni nyinyi na kisha zileni”. Akasema ‘Aaishah kwamba watu hao walikuwa bado ndio wametoka kwenye ukafiri. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2057) na wengineo].
Na lau kama kulitaja Jina la Allaah ni sharti, basi nyama isingelihalalika pamoja na kuweko shaka ya kuwepo kwake, kwa kuwa shaka ndani ya sharti, ni shaka kwa lile lililoshurutishiwa.
Dalili nyingine waliyoitoa kwamba kulitaja Jina la Allaah ni jambo mustahabbu na si waajib ni kwamba Allaah Ta’aalaa Ametuhalalishia nyama za Ahlul Kitaab, na watu hawa wanakuwa hawalitaji Jina la Allaah wakati wa kuchinja. Na wakajibu kuhusu Kauli Yake Ta’aalaa katika Aayah ya 121 ya Suwrat Al-An’aam:
"وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ"
“Na wala msile katika ambavyo halikutajwa Jina la Allaah (wakati wa kuchinjwa), kwani huo ni ukiukaji wa utiifu kwa Allaah”… ya kwamba muradi wake ni wale wanyama ambao wametajiwa jina lisilo la Allaah, kwa maana wanyama waliochinjwa kwa ajili ya masanamu, kwa dalili ya Kauli Yake Ta’aalaa katika Aayah ya 3 ya Suwrat Al-Maaidah:
"وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ"
“Na kilichotajiwa asiyekuwa Allaah katika kuchinjwa kwake”. Na muktadha wa Aayah unaonyesha hilo, kwani Allaah Kasema hapo:
"وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ"
“kwani huo ni ukiukaji wa utiifu kwa Allaah”. Na hali ambayo ndani yake kunakuweko ukiukaji wa utiifu kwa Allaah, ni huko kutajwa asiyekuwa Allaah kama Alivyosema kwenye Aayah ya 145 ya Suwrat Al-An’aam:
"أَوْ فِسْقًا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ"
“au kilichochinjwa kinyume na utiifu kwa Allaah kwa kutajiwa asiyekuwa Allaah”.
5- Asilitaje jina la asiye Allaah wakati wa kuchinja
Makusudio ya hili ni kumtukuza asiye Allaah, ni sawa kwa kunyanyua sauti au bila sauti. Mchinjaji asiyelitaja Jina la Allaah mnyama wake anakuwa si halali kuliwa kwa itifaki ya ‘Ulamaa wote. Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:
"حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ وَالدَّمُ وَلَحْمُ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ"
“Mmeharamishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na kilichotajiwa asiyekuwa Allaah katika kuchinjwa kwake”. [Al-Maaidah : 03].
Kuchinja kwa asiye Allaah ni haramu kutokana na Hadiyth ya Abu At-Twufayl aliyesema: ‘Aliyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ)aliulizwa:
"أَخَصَّكُمْ رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وآلِهِ وَسَلَّمَ بِشَيْءٍ؟ فَقَالَ : مَا خَصَّنَا رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وآلِهِ وَسَلَّمَ بِشَيْءٍ لَمْ يَعُمَّ بِهِ النَّاسَ كَافَّةً إِلاَّ مَا كَانَ فِي قِرَابِ سَيْفِي هّذَا ، قَالَ : فَأَخْرَجَ صَحِيْفَةً مَكْتُوْبٌ فِيْهَا : لَعَنَ اللهُ مَنْ ذَبَحَ لِغَيْرِ اللهِ ، وَ لَعَنَ اللهُ مَنْ سَرَقَ مَنَارَ الأَرْضِ ، وَلَعَنَ اللهُ مَنْ لَعَنَ وَالِدَيْهِ ، وَلَعَنَ اللهُ مَنْ آوَى مُحْدِتًا"
“Je, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekukhusuni kwa jambo lolote (ambalo hakuwaambia watu)? Akasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutukhusu kwa jambo lolote ambalo hakuwaenezea habari yake watu wote isipokuwa kilichomo ndani ya ala ya upanga wangu huu. Akatoa karatasi ambayo imeandikwa ndani yake: Allaah Amlaani aliyechinja kwa asiye Allaah, na Allaah Amlaani aliyebadili mipaka ya ardhi (ili adhulumu), na Allaah Amlaani aliyemlaani mzazi wake, na Allaah Amlaani aliyempa hifadhi mzushi”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1978)].
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
Alhidaaya.com [3]
05-Chinjo La Kisharia: Masharti Ya Zana Ya Kuchinjia
Zana ya kuchinjia ina masharti mawili:
1- Iwe yenye kukata. Ni sawa ikiwa chuma au kinginecho, au kali au butu, muhimu iwe inakata. Kwa kuwa makusudio ya kuchinja ni kukata mishipa miwili ya damu ya shingoni, umio na koromeo, pamoja na damu kububujika.
2- Isiwe mfupa au kucha. Ni kwa Hadiyth ya Raafi’u bin Khadiyj aliyesema: “Nilimwambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam:
"إِنَّا لاَقُو الْعَدُوِّ غَدًا وَلَيْسَتْ مَعَنَا مُدًى ، قَالَ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : " مَا أَنْهَرَ الدَّمَ وَذُكِرَ اسْمُ اللَّهِ فَكُلْ لَيْسَ السِّنَّ وَالظُّفُرَ ، أَمَّا السِّنُّ فَعَظْمٌ ، وَأَمَّا الظُّفُرُ فَمُدَى الْحَبَشَةِ"
“Sisi kesho tunapambana na adui, na hatuna visu (vya kuchinjia). Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: (Ukichinjia kwa) chochote chenye kuchuruzisha damu, sambamba na kutajwa Jina la Allaah, basi kula isipokuwa jino au kucha. Ama jino, hilo ni mfupa, na ama kucha, hizo ni kisu cha Wahabeshi (wanachinja kwa kutumia kucha zao)”. [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma].
Kuchinja Kwa Ala Au Mashine Za Umeme
Tumesema punde kidogo kuwa ala ya kuchinjia ni lazima iwe inakata, na isiwe mfupa au kucha. Na hakuna shaka yoyote kwamba mashine za umeme ni kali na zenye kasi katika kufanikisha shughuli ya uchinjaji, na kwa hivyo zina masharti yote yatakikanayo, hivyo zinafaa sana kwa kazi hii.
Na hapa kuna swali la kidadisi: Mashine hizi kutokana na ukali wake na uharaka, zinaweza kukata kabisa kichwa cha mnyama na kukitenganisha na mwili wake. Je, hili linaweza kuwa tatizo?
Tunasema: Hili linafaa. Hii ni kauli ya Imaam Ahmad, Abu Haniyfah na Ath-Thawriy ambao wanasema kuwa hapa inakuwa imekusanyika kukata kile chenye kubakisha uhai wa mnyama (kichwa) pamoja na chinjo, hivyo inakuwa ni halali. Na mashine hizi ni kali mno na zinakikata kichwa mara moja. Hivyo haifikiriki mnyama kufa na roho yake kutoka bila ya kukatwa mishipa ya damu ya shingo yake.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
Alhidaaya.com [3]
06-Chinjo La Kisharia: Taratibu Njema Za Kuchinja
Katika kuchinja, kuna mambo kadhaa ambayo yamestahabiwa, nayo ni haya yafuatayo:
1- Mnyama achinjwe bila maumivu au mateso
Hili linafanikishwa kwa kukinoa vyema kisu au mfano wake, na kumchinja mnyama chinjo la haraka. Hili humpumzisha haraka, na hateseki wala hapati maumivu.
Toka kwa Shad-daad bin Aws, amesema: Mambo mawili nimeyahifadhi toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Amesema Rasuli:
"إِنَّ اَللَّهَ كَتَبَ اَلْإِحْسَانَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ ، فَإِذَا قَتَلْتُمْ فَأَحْسِنُوا اَلْقِتْلَةَ ، وَإِذَا ذَبَحْتُمْ فَأَحْسِنُوا اَلذِّبْحَةَ، وَلْيُحِدَّ أَحَدُكُمْ شَفْرَتَهُ, وَلْيُرِحْ ذَبِيحَتَهُ"
“Hakika Allaah Ameamuru wema katika kila kitu. Mnapoua, basi uweni kwa njia nzuri (yenye maumivu kidogo iwezekanavyo), na mnapochinja, basi chinjeni chinjo zuri (la haraka bila mateso), na mmoja wenu akinoe vyema kisu chake, na asimpe tabu mnyama wake”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1955)].
Inakuwa ni vyema zaidi kwa mchinjaji akinoe vyema kisu chake kabla ya kumlaza chini mbuzi na mfano wake. Jumhuwr ya ‘Ulamaa wamekirihisha mchinjaji kukinoa kisu chake mbele ya mnyama anayekusudiwa kuchinjwa. Na hii ni kutokana na yaliyopokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba mtu mmoja alimlaza chini kondoo anayetaka kumchinja huku akiendelea kukinoa kisu chake. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
"أتُرِيْدُ أَنْ تُمِيْتَهَا مَوْتَاتٍ؟ هَلَّا حَدَّدْتَ شَفْرَتَكَ قَبْلَ أَنْ تَضْجَعَهَا؟"
“Hivi wataka kumuua mauti mengi? Kwa nini basi usinoe kisu chako kabla ya kumlaza chali?” [Imekharijiwa na Al-Haakim (4/257), Al-Bayhaqiy (9/280), na ‘Abdurraaziq (8608). Wamekhitilafiana katika kuwa Hadiyth hii ni Mawswuul au Mursal].
2- Mnyama alazwe chali
Hili linakuwa ni la huruma zaidi kwake, nalo limekubaliwa na Waislamu wote. Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah:
"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَمَرَ بِكَبْشٍ أَقْرَنَ يَطَأُ فِي سَوَادٍ وَيَبْرَكُ فِي سَوَادٍ وَيَنْظُرُ فِي سَوَادٍ فَأُتِيَ بِهِ لِيُضَحِّيَ بِهِ فَقَالَ لَهَا : يَا عَائِشَةُ هَلُمِّي الْمُدْيَةَ ، ثُمَّ قَالَ : اشْحَذِيهَا بِحَجَرٍ ، فَفَعَلَتْ ثُمَّ أَخَذَهَا وَأَخَذَ الْكَبْشَ فَأَضْجَعَهُ ، ثُمَّ ذَبَحَهُ ، ثُمَّ قَالَ : بِسْمِ اللَّهِ ، اللَّهُمَّ تَقَبَّلْ مِنْ مُحَمَّدٍ وَآلِ مُحَمَّدٍ وَمِنْ أُمَّةِ مُحَمَّدٍ ، ثُمَّ ضَحَّى بِهِ."
“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliagiza beberu la kondoo mwenye pembe, mwenye miguu myeusi, mwenye tumbo jeusi, na mwenye macho meusi. Akaletewa ili amchinje (kwa udhwhiya). Akamwambia: Ee ‘Aaishah! Niletee kisu. Kisha akamwambia: Kinoe kwa jiwe. ‘Aaishah akakinoa, Rasuli akakichukua, akamkamata beberu, kisha akamchinja huku akisema: Bismil Laah. Ee Allaah! Mtakabalie Muhammad, na familia ya Muhammad, na ummah wa Muhammad”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1967) na wengineo. Itakuja kwenye mlango wa kuchinja wanyama wa swadaqah].
Kumlaza kunakuwa ni kwa ubavu wake wa kushoto, kwa vile inakuwa ni wepesi kwa mchinjaji katika kukikamata kisu kwa mkono wake wa kulia, na kukikamata kichwa cha mnyama kwa mkono wake wa kushoto.
3- Mchinjaji aweke mguu wake kwenye ubapa wa shingo ya mnyama
Anas amesema:
"ضَحَّى رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِكَبْشَيْنِ أَمْلَحَيْنِ ، فَرَأَيْتُهُ وَاضِعًا قَدَمَهُ عَلَى صِفَاحِهِمَا يُسَمِّي وَيُكَبِّرُ، فَذَبَحَهُمَا بِيَدِهِ."
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja beberu wawili wenye rangi mseto ya weupe na weusi. Nikamwona akiuweka mguu wake juu ya bapa za shingo zao huku akipiga Bismil Laahi na kutamka takbiyr. Akawachinja wote wawili kwa mkono wake”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5558), na itakuja mbeleni].
An Nawawiy kasema: “Bila shaka alifanya hivi ili awe katika hali ya uimara na kujimudu zaidi, na ili pia mnyama asiweze kufanya matata kwa kichwa chake na hivyo kumzuia kukamilisha zoezi au hata kumjeruhi yeye”.
4- Mnyama aelekezwe Qiblah
Kuelekezwa kunakuwa ni kwa machinjio yake na si kwa uso wake. Jaabir bin ‘Abdillaah amesema:
"ذَبَحَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَوْمَ الذَّبْحِ كَبْشَيْنِ أَقْرَنَيْنِ أَمْلَحَيْنِ مُوْجِئَيْن فَلَمَّا َوجَّهَهُمَا قَالَ: إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِيْ فَطَرَ السَّمَوَاتِ وَالْأَرْضَ ، عَلَى مِلَّةِ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ، وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ، إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ، وَبِذَلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا مِنَ الْمُسْلِمِينَ ، اللَّهُمَّ مِنْكَ وَلَكَ عَنْ مُحَمَّدٍ وَأُمَّتِهِ ، بِسْمِ اللَّهِ وَاللَّهُ أَكْبَرُ ، ثُمَّ ذَبَحَ"
“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja siku ya kuchinja kondoo wawili madume, wenye pembe, wenye rangi nyeupe na nyeusi na waliohasiwa. Alipowaelekeza (Qiblah) alisema: Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu kwa Yule Aliyeziumba mbingu na ardhi, juu ya mila ya Ibraahiym aliyejiengua na shirki, na mimi si katika washirikina. Hakika swala yangu, ibada zangu, uhai wangu na kufa kwangu, yote hayo ni ya Allaah, Mola wa walimwengu Asiye na mshirika. Hayo ndiyo niliyoamrishwa kuyafanya, na mimi ni katika Waislamu. Ee Allaah, hii inatoka Kwako na ni Yako, toka kwa Muhammad na umati wake. Kwa Jina la Allaah, na Allaah Ni Mkubwa”. Kisha akachinja”. [Al Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2778) na wengineo. Angalia Al-‘Ilal cha Ibn Abiy Haatim (2/39,44) na Ad-Daaraqutwniy (7/20)].
Na toka kwa Naafi’i, kwamba Ibn ‘Umar:
"كَانَ هُوَ يَنْحَرُ هَدْيَهُ بِيَدِهِ يَصِفُهُنَّ قِيَامًا وَيُوَجِّهُهُنَّ إِلَى الْقِبْلَةِ ، ثُمَّ يَأْكُلُ وَيُطْعِمُ"
“Alikuwa akiwachinja wanyama wake wa (udhwhiya) kwa mkono wake, anawasimamisha na anawaelekeza Qiblah, kisha anakula na kugawa nyama”.
Angalizo:
Kumwelekeza mnyama Qiblah si sharti la lazima katika kuchinja. Na kama kungekuwa lazima, basi Allaah Ta’aalaa Asingelisahau kulibainisha hilo. Ni jambo linalopendeza tu.
5, 6 – Mchinjaji apige Bismil Laah na alete Takbiyr
Katika Hadiyth iliyotangulia ya ‘Aaishah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomlaza kondoo dume chini, alisema: Bismil Laah. [Imetajwa nyuma kidogo].
Na pia katika Hadiyth ya Anas:
"فَرَأَيْتُهُ وَاضِعًا قَدَمَهُ عَلَى صِفَاحِهِمَا يُسَمِّي وَيُكَبِّرُ ، فَذَبَحَهُمَا بِيَدِهِ."
“Nikamwona akiuweka mguu wake juu ya bapa za shingo zao huku akipiga Bismil Laahi na kutamka takbiyr, na akawachinja kwa mkono wake”. [Imetajwa nyuma kidogo].
Vile vile, Hadiyth ya Jaabir iliyotajwa nyuma kidogo kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
"بِسْمِ اللَّهِ وَاللَّهُ أَكْبَرُ ، ثُمَّ ذَبَحَ."
“Kwa Jina la Allaah, na Allaah Ni Mkubwa”. Kisha akachinja”. [Imetajwa punde kidogo].
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
Alhidaaya.com [3]
07-Chinjo La Kisharia: Taratibu Njema Za Kuchinja Ngamia Na Mnyama Mfano Wake
Yamestahabiwa katika kumchinja ngamia na mnyama mwenye shingo ndefu mfano wake, yale yote yaliyostahabiwa katika kuwachinja wanyama wenye shingo fupi (kama ng’ombe, mbuzi n.k). Isipokuwa ngamia huchinjwa akiwa amesimama kwa miguu miwili na mkono mmoja wa kulia, na mkono wake wa kushoto hufungwa. [Al-Badaai’u (5/41), Nihaayatul Muhtaaj (8/111), na Al-Muqni’u (1/474)].
1- Allaah Ta’aalaa Anasema:
"وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ ۖ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ"
“Na ngamia na ng’ombe Tumekufanyieni kuwa ni miongoni mwa Ishara za Allaah; kwa hao mnapata khayr nyingi. Basi tajeni Jina la Allaah juu yao wanapopangwa safu (kuchinjwa)”. [Al-Hajj: 36].
Ibn ‘Abbaas amesema صَوَافَّ yaani قِيَامًا kwa maana wakiwa wamesimamishwa.
2- Katika Hadiyth ya Anas bin Maalik wakati Rasuli akifanya Hijja:
...وَنَحَرَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم بِيَدِهِ سَبْعَ بَدَنَاتٍ قِيَامًا ، وَضَحَّى بِالْمَدِينَةِ بِكَبْشَيْنِ أَقْرَنَيْنِ أَمْلَحَيْنِ"
“ …na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akachinja ngamia saba kwa mkono wake wakiwa wamesimama, na huko Madiynah alichinja madume mawili ya kondoo yenye pembe na rangi nyeupe na nyeusi”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1714) na Muslim (690)].
3- Toka kwa Ziyaad bin Jubayr, amesema:
"رَأَيْتُ ابنَ عُمَرَ (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) أَتَى عَلَى رَجُلٍ قَدْ أَنَاخَ بَدَنَتَهُ يَنْحَرُهَا قَالَ: ابْعَثْهَا قِيَامًا مُقَيَّدَةً سُنَّةَ مُحَمَّدٍ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ"
“Nilimwona Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhu) akipita na kumkuta mtu anamchinja ngamia wake akiwa amempigisha magoti. Akamwambia: Mnyanyue umchinje akiwa amesimama na amefungwa (mkono wa kushoto). Hii ndiyo Sunnah ya Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1713) na Muslim (1320)].
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
Alhidaaya.com [3]
08-Chinjo La Kisharia: Kama Ikishindikana Kumdhibiti Mnyama Ili Kumchinja
[Al-Muhallaa (7/446), Naylul Awtwaar (8/163) na As Saylul Jarraar (4/68)]
Kama mchinjaji hakuweza kumdhibiti mnyama na ikawa ni vigumu kumchinja kwa kutoroka au mfano wa hivyo, hapo itajuzu kumchoma kwa chochote chenye ncha kali, au kumpiga mshale, au risasi na kadhalika katika sehemu yoyote ya mwili wake kiasi cha kuweza kumjeruhi na kumuua. Kwa kufanya hivyo, nyama yake itakuwa ni halali kuliwa. Na hii ndio kauli ya Jumhuwr ya ‘Ulamaa. Lakini Maalik na Al-Layth hawalikubali hili!
Dalili ya Jumhuwr ni Hadiyth ya Raafi’u bin Khadiyj aliyesema:
"كُنَّا مَعَ النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي سَفَرٍ ، فَنَدَّ بَعِيرٌ مِنْ إِبِلِ الْقَوْمِ ، وَلَمْ يَكُنْ مَعَهُمْ خَيْلٌ ، فَرَمَاهُ رَجُلٌ بِسَهْمٍ فَحَبَسَهُ ، فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : "إِنَّ لِهَذِهِ الْبَهَائِمِ أَوَابِدَ كَأَوَابِدِ الْوَحْشِ فَمَا فَعَلَ مِنْهَا هَذَا فَافْعَلُوا بِهِ هَكَذَا "
“Tulikuwa pamoja na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) safarini. Ghafla, ngamia mmoja katika ngamia wa watu alichopoka na kukimbia, nao hawakuwa na farasi. Mtu mmoja akampiga mshale (wa mguuni), ukamfanya asiweze tena kwenda. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Hakika baadhi ya wanyama hawa (tuwafugao), wana tabia za ukali kama walivyo wanyama wakali, na kama atafanya yeyote kati yao tabia hizo, basi nanyi pia mfanyieni hivyo hivyo”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5543) na Muslim (1968)].
Na katika tamshi jingine,
"فَإِذَا غَلَبَكُمْ مِنْهَا شَىْءٌ فَاصْنَعُوا بِهِ هَكَذَا"
“Na kama atawashindeni nguvu, basi nanyi mtumilieni nguvu”.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
Alhidaaya.com [3]
09-Chinjo La Kisharia: Chinjo La Mama Ndilo Chinjo La Mtoto Aliye Tumboni Mwake
[Al-Majmuw’u (9/147), Naylul Awtwaar (8/164) na Subulus Salaam (4/1412)]
Mnyama akichinjwa kisha akatoka matumboni mwake kitoto kikiwa kimekufa, basi kwa mujibu wa kauli mbili zilizo sahihi zaidi za Jumhuwr, kitoto hicho ni halali kuliwa, kwani kinakuwa kimechinjwa kwa chinjo la mama yake. Lakini Abu Haniyfah amekhitilafiana nao.
Kauli hii ya Jumhuwr inaungwa mkono na Hadiyth ya Abu Sa’iyd aliyesema: “Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kitoto cha matumboni mwa mnyama. Akasema:
"كُلُوْهُ إِنْ شِئْتُمْ"
“Kileni mkipenda”.
Na katika riwaayah nyingine: Nilisema (Abu Sa’iyd):
"يَا رَسُولَ اللَّهِ ، نَنْحَرُ النَّاقَةَ وَنَذْبَحُ الْبَقَرَةَ وَالشَّاةَ فَنَجِدُ فِي بَطْنِهَا جَنِينا أَنُلْقِيهِ أَمْ نَأْكُلُهُ ؟ قَالَ: كُلُوهُ إِنْ شِئْتُمْ فَإِنَّ ذَكَاتَهُ ذَكَاةُ أُمِّهِ"
“Ee Rasuli wa Allaah! Tunachinja ngamia, tunachinja ng’ombe na mbuzi, na tunakuta matumboni mwao kitoto. Je, tukitupe au tukile? Akasema: Kileni mkipenda, kwani chinjo lake ni chinjo la mama yake”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2827), At-Tirmidhiy (1476) na Ibn Maajah (3199)].
Lakini kama kitatoka kikiwa kizima na uhai kamili, basi hapo itakuwa si halali kukila ila kwa kukichinja. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ
Chinjo La Kisharia
Alhidaaya.com [3]
10- Chinjo La Kisharia: Sehemu Ya Mnyama Iliyokatwa Akiwa Hai
[Al-Muhallaa (7/449), Al-Mughniy (9/320) na Naylul Awtwaar (8/166)]
Toka kwa Abu Waaqid Al-Laythiy: Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَا قُطِعَ مِنَ الْبَهِيمَةِ وَهِيَ حَيَّةٌ فَهُوَ مَيْتَةٌ"
“Chochote kilichokatwa kwa mnyama akiwa hai, basi kipande hicho ni mfu”. [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2858), na At-Tirmidhiy (1480). Ina Hadiyth wenza].
Ibn Hazm (Rahimahul Laah] amesema:
“Sehemu yoyote iliyokatwa ya mnyama akiwa bado hai, au ikakatwa kabla ya kukamilika zoezi la kumchinja, basi sehemu hiyo ni mfu, si halali kuliwa. Na kama kazi ya kumchinja itakamilika baada ya kukata sehemu hiyo, basi hapo mnyama ataliwa kama kawaida, lakini sehemu hiyo iliyokatwa haitofaa kuliwa. Na hili halina makhitilafiano kabisa, kwa kuwa kipande hicho kinakuwa kimetengana na mnyama ambaye ni haramu kumla (kabla ya kuchinjwa), na kinakuwa hakihusiani tena na chinjo litakalofanyika, kwani kinakuwa kiko nje ya asili yake”. [Al-Muhallaa (7/449].
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/284
[2] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11330&title=08B-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20%20%D9%83%D9%90%D8%AA%D9%8E%D8%A7%D8%A8%D9%8F%20%D8%A7%D9%84%D8%A3%D9%8E%D8%B7%D9%92%D8%B9%D9%90%D9%85%D9%8E%D8%A9%D9%90%20%D9%88%D9%8E%D8%A7%D9%84%D8%A3%D9%8E%D8%B4%D9%92%D8%B1%D9%90%D8%A8%D8%A9-Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20%D8%A7%D9%84%D8%AA%D9%91%D9%8E%D8%B0%D9%92%D9%83%D9%90%D9%8A%D9%8E%D8%A9%D9%8F%20%D8%A7%D9%84%D8%B4%D9%91%D9%8E%D8%B1%D9%92%D8%B9%D9%90%D9%8A%D9%91%D9%8E%D8%A9%D9%8F%20Chinjo%20La%20Kisharia
[3] http://www.alhidaaya.com/
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11337&title=01-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Chinjo%20La%20Kisharia%3A%20Taarifu%20Yake
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11338&title=02-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Chinjo%20La%20Kisharia%3A%20Hukmu%20Ya%20Kuchinja%20Na%20Hikmah%20Ya%20Kushurutishwa%20Kwake%20
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11339&title=03-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Chinjo%20La%20Kisharia%3A%20Masharti%20Ya%20Kuchinja%3A%20
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11340&title=04-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Chinjo%20La%20Kisharia%3A%20Masharti%20Ya%20Mchinjaji%20
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11341&title=05-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Chinjo%20La%20Kisharia%3A%20Masharti%20Ya%20Zana%20Ya%20Kuchinjia%20%20
[9] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11342&title=06-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Chinjo%20La%20Kisharia%3ATaratibu%20Njema%20Za%20Kuchinja
[10] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11343&title=07-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Chinjo%20La%20Kisharia%3A%20Taratibu%20Njema%20Za%20Kuchinja%20Ngamia%20Na%20Mnyama%20Mfano%20Wake%20
[11] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11344&title=08-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Chinjo%20La%20Kisharia%3A%20Kama%20Ikishindikana%20Kumdhibiti%20Mnyama%20Ili%20Kumchinja%20
[12] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11345&title=09-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Chinjo%20La%20Kisharia%3AChinjo%20La%20Mama%20Ndilo%20Chinjo%20La%20Mtoto%20Aliye%20Tumboni%20Mwake%20
[13] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11346&title=10-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Chinjo%20La%20Kisharia%3A%20Sehemu%20Ya%20Mnyama%20Iliyokatwa%20Akiwa%20Hai