كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji
Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأُضْحِيَةُ
Udhwhiyah
Abu Maalik Kamaal Bin As-Sayyid Saalim
Imetarjumiwa na 'Abdullaah Mu'aawiyah (Abu Baasim)
Alhidaaya.com
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأُضْحِيَةُ
Udhwhiyah
Alhidaaya.com [3]
01-Udhwhiyah: Taarifu Yake Na Uhalali Wake:
"الأُضْحِيَةُ" , kwa kutia dhwamma juu ya alif (al-udhwhiyah), pia inafaa kutia kasrah ( "الأِضْحِيَةُ"al-idhwhiyah), na pia inajuzu kuondosha hamzah na kufatihisha dhwaad "ضَحِيَةٌ") dhwahiyatun), ni mnyama anayechinjwa kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah Ta’aalaa katika yale Masiku ya kuchinja kwa masharti maalum. Ni kama vile amenyambulika kutokana na jina la wakati ambao imewekwa sharia ya kumchinja ndanimwe, na kwa hivyo akaitwa kwayo Yawm Al-Adhwhaa (Siku ya kuchinja). [Subulus Salaam (4/160) na Ibn ‘Aabidiyna (5/111].
Uhalali Na Usharia Wake:
Asili ya uhalali wa udhwhiyah ni Qur-aan, Sunnah na Ijmaa. Ama katika Qur-aan, ni Kauli Yake Ta’aalaa:
فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾
2. Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja. [Al-Kawthar : 02].
Baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kuwa muradi wa Aayah hii ni kuchinja udhwhiyah baada ya Swalaatul ‘Iyd.
Ama Sunnah, Anas amesema:
"ضَحَّى النَّبِيُ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِكَبْشَيْنِ أَمْلَحَيْنِ أَقْرَنَيْنِ ذَبَحَهُمَا بِيَدِهِ ، وَسَمَّى وَكَبَّرَ ، وَوَضَعَ رِجْلَهُ عَلَى صِفَاحِهِمَا"
“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja beberu wawili wenye rangi mseto ya weupe na weusi na wenye pembe, aliwachinja kwa mkono wake, akapiga Bismil Laahi, akaleta Takbiyr, na akaweka mguu wake juu ya bapa za shingo zao”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5558) na Muslim (1966)].
Na Waislamu wote wanajua uhalali wa udhwhiyah. [Al-Mughniy (9/345), Al-Haawiy cha Al-Mawruwdiy (19/83) na Al-Muhallaa (7/355)].
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأُضْحِيَةُ
Udhwhiyah
Alhidaaya.com [3]
02-Udhwhiyah: Hukmu Ya Kuchinja Udhwhiyah:
‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu hukmu ya udhwhiya kwa kauli mbili:
[Al-Mabsuwtw (12/8)].
Ya kwanza: Ni waajib kwa mwenye uwezo
Ni kauli ya Rabiy-‘ah, Al-Awzaa’iy, Abuu Haniyfah, Al-Layth na baadhi ya Wamaalik. Dalili walizotoa ni:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾
Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja. [Al-Kawthar : 02].
Wamejibiwa: Kwamba ‘Ulamaa wana kauli tano katika kuiawilisha Aayah hii, na kauli yenye nguvu zaidi ni ile isemayo kuwa muradi ni: Swali kwa ajili ya Allaah, na chinja kwa ajili ya Allaah.
2- Hadiyth ya Jundub bin Sufyaan (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنْ ذَبَحَ قَبْلَ أَنْ يُصَلِّيَ فَلْيَذْبَحْ أُخْرَى مَكَانَهَا، وَمَنْ لَمْ يَذْبَحْ فَلْيَذْبَحْ"
“Atakayechinja kabla hajaswali, basi achinje mnyama mwingine badala yake, na ambaye hakuchinja, basi na achinje”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5562) na Muslim (1960)].
Wamejibiwa: Kwamba makusudio ni kubainisha sharti la kukubalika udhwhiyah kisharia. Hii ni kama kwa mfano kumwambia aliyeswali Swalaah ya Dhuhaa kabla ya jua kuchomoza: Jua likichomoza, swali tena Swalaah yako.
3- Hadiyth ya Al-Baraa kwamba Abu Burdah alisema:
"يَا رَسُوْلَ اللهِ ، ذَبَحْتُ قَبْلَ أَنْ أُصَلِّيَ ، وَعِنْدِيْ جَذَعَةٌ خَيْرٌ مِنْ مُسِنَّةٍ ، فَقَالَ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : اجْعَلْهَا مَكَانَهَا ، وَلَنْ تُجْزِئَ عَنْ أَحَدٍ بَعْدَكَ"
“Ee Rasuli wa Allaah! Nimechinja kabla sijaswali. Nami nina jadh-‘a ambaye kwangu ni mbora zaidi kuliko musinnah. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Mfidie huyo huyo mahala pa uliyemchinja, na hatofaa kwa yeyote baada yako”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5560)].
4- Hadiyth ya Al-Baraa bin ‘Aazib kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَرْبَعَةٌ لا يُجْزِيْنَ فِي الأَضَاحِي : العَوْرَاءُ البَيِّنُ عَوْرَهَا و........."
“Wanne hawatoshelezi katika wanyama wa kudhwahi: Mwenye chongo la wazi linaloonekana……..”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2802), At-Tirmidhiy (1497), An-Nasaaiy (7/215), Ibn Maajah (3144) na wengineo].
Wamesema (kutilia nguvu hoja yao): Neno lake “hawatoshelezi”, ni dalili juu ya uwajibu wa kudhwahi! Kwa kuwa neno “haitoshelezi” halisemwi kwa linalohusiana na sunnah. Wakasema pia kuwa kutokuwa mnyama na kasoro yoyote kunazingatiwa kwa wanyama walio wajibu kuchinjwa, ama wale wa sunnah, hao inajuzu kujikurubisha kwa Allaah kwa aliye chongo au mwenye kasoro nyingineyo yoyote mwilini.
Wamejibiwa: Kwamba wanyama wa kudhwahi ni dhabihu ya kafara ya Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo yeye anajikurubisha kwayo kwa Allaah ‘Azza wa Jalla kwa mujibu wa alivyoletewa sharia kuhusiana na hilo. Nayo pia ni hukmu ambayo imewekewa wakati maalum, hivyo haifai mtu apetuke kwayo Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa kuwa ni mustahili ajikurubishe nayo kwa jambo ambalo limekatazwa kwa ulimi wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). [At-Tamhiyd cha Ibn ‘Abdul Barri (20/167].
5- Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنْ كَانَ لَهُ سَعَةً وَلَمْ يُضَحِّ فَلَا يَقْرُبَنَّ مَسْجِدَنَا وَمُصَلَّانَا"
“Atakayekuwa na uwezo na asidhwahi, basi asiukaribie kabisa Msikiti wetu na sehemu yetu ya kuswalia”. [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Ibn Maajah (3123), Ahmad (2/321), Al-Haakim (2/389), Ad-Daaraqutwniy (4/285), na Al-Bayhaqiy (9/260)].
Ya pili: Kudhwahi ni sunnah na si waajib
Haya ni madhehebu ya Jumhuwr; Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-haaq, Abu Thawr, Al-Mazniy, Ibn Al-Mundhir, Daawuwd, Ibn Hazm na wengineo. Wametoa dalili hizi zifuatazo:
1- Hadiyth ya Ummu Salamah kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا دَخَلَتِ الْعَشْرُ وَأَرَادَ أَحَدُكُمْ أَنْ يُضَحِّيَ فَلاَ يَمَسَّ مِنْ شَعَرِهِ وَبَشَرِهِ شَيْئًا "
“Linapoingia kumi (la mwanzo la mwezi wa Dhul-Hijja) na mmoja wenu akaazimia kudhwahi, basi asikate chochote katika nywele zake na kucha zake”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1977), An-Nasaaiy (7/212), Ibn Maajah (3149), na Ahmad (6/289). Wamekhitalifiana katika kuwa kwake Marfuw’u au Mawquwf. Linaloonekana kuwa na nguvu zaidi ni Marfuw’u].
Wamesema: Neno lake “akaazimia kudhwahi” ni dalili kuwa kudhwahi si waajib.
2- Imekuja kwa njia sahihi kutoka kwa Maswahaba kwamba kudhwahi si waajib, na wala haikupokelewa kutoka kwa yeyote kati yao kwamba ni waajib. Al-Mawruwdiy amesema: “Imepokelewa toka kwa Maswahaba (Radhwiya Allaah ‘anhum) linalofungika kwalo Ijma’a ya kupomoka uwajibu”. [Al-Haawiy (19/85) na Al-Muhallaa (7/358)].
Kati ya hayo ni:
(a) Abu Sariyhah amesema:
"رَأَيْتُ أَبَا بَكْرِ وَعُمَرَ ، وَمَا يُضَحِّيَانِ"
“Nimewaona Abu Bakr na ‘Umar hawadhwahi”. [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na ‘Abdur Razzaaq (8139) na Al-Bayhaqiy (9/269)].
(b) Abu Mas-‘uwd Al-Answaariy (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:
"إِنِّي لأَدَعُ الأَضْحَى ، وَإِنِّيْ لَمُوْسِرٌ ، مَخَافَةَ أَنْ يَرَى جِيْرَانِي أَنَّهُ حُتِمَ عَلَيَّ"
“Mimi huacha kudhwahi, nami nina uwezo, kwa sababu ninachelea majirani zangu kudhani kwamba ni lazima kwangu”. [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na ‘Abdur Razzaaq (8149) na Al-Bayhaqiy (9/265)].
Ninasema: “Linaloonekana ni kwamba dalili za wenye kuwajibisha hazina nguvu wala vigezo vya kuwajibisha. Na kwa muktadha huu, kauli inayozingatiwa ni ya Maswahaba (Radhwiya Allaah ‘anhum) na Jumhuwr ya ‘Ulamaa”.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأُضْحِيَةُ
Udhwhiyah
Alhidaaya.com [3]
03-Udhwhiyah: Wanyama Wanaochinjwa:
1- Haitoshelezi katika kuchinja isipokuwa wanyama wa miguu minne wa mifugo ambao ni ngamia, ng’ombe, kondoo na mbuzi. Ni kwa Neno Lake Ta’alaa:
"لِّيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ"
“Ili walitaje Jina la Allaah kwa yale Aliyowaruzuku ya wanyama wa miguu minne wa mifugo”. [Al-Hajj : 34].
Jopo la ‘Ulamaa limenukuu Ijma’a ya kwamba kudhwahi hakufai isipokuwa kwa wanyama hawa. Lakini, Ibn Al-Mundhir ameeleza kutoka kwa Hasan bin Swaaleh kwamba inajuzu kudhwahi nyati na mburukenge. Daawuwd pia kasema hivyo hivyo kuhusu nyati. Ama Ibn Hazm, yeye amejuzisha wanyama wote wanaoliwa wenye miguu minne au ndege!! Ametoa hoja kwa kauli ya Bilaal (Radhwiya Allaah ‘anhu) aliyesema:
"مَاكُنْتُ أُبَالِي لَوْ ضَحَّيْتُ بِدِيْكٍ.."
“Sikuwa nikijali hata nikichinja jogoo…”. [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Abdur Razzaaq (8156) na Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (7/358)].
Ninasema: “Madhehebu ya Jumhuwr ndiyo yenye kulazimiana na Aayah Tukufu, na pia kwa vile haikupokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alidhwahi mnyama mwingine zaidi ya ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo”.
(a,b) - Ngamia na ng’ombe
Imethibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba zake, walidhwahi wanyama hawa wawili (ngamia na ng’ombe), mbali na kwamba inajuzu watu saba kushirikiana ng’ombe mmoja au ngamia mmoja ambaye atawatosheleza wote. Na hii ni kwa vielelezo vifuatavyo:
1- Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillaah:
"نحَرْنا مَعَ رَسولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَامَ الْحُدَيْبِيَةِ الْبَدَنَةَ عَنْ سَبْعَةٍ وَالْبَقَرَةَ عَنْ سَبْعَةٍ"
“Tulichinja pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwaka wa Al-Hudaybiyah ngamia mmoja kwa watu saba, na ng’ombe mmoja kwa watu saba”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1318), Abu Daawuwd (2809), At-Tirmidhiy (903), na Ibn Maajah (3132)].
2- Pia Jaabir kasema:
"كُنَّا نَتَمَتَّعُ مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِالْعُمْرَةِ فَنَذْبَحُ الْبَقَرَةَ عَنْ سَبْعَةٍ نَشْتَرِكُ فِيهَا"
“Tulifanya Hajji Tamattu (‘Umrah kabla ya Hijja) pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tukashirikiana watu saba kuchinja ng’ombe mmoja”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1318), Abu Daawuwd (2807) na An-Nasaaiy (7/222)].
Faida mbalimbali:
Ya kwanza: Is-haaq, Ibn Khuzaymah na wengineo wana mwelekeo usemao kuwa ngamia mmoja anatosheleza watu kumi. Na hii ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema:
"كُنَّا مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي سَفَرٍ فَحَضَرَ الْأَضْحَى فَاشْتَرَكْنَا فِي الْبَقَرَةِ سَبْعَةٌ وَفِي الْبَعِيرِ عَشَرَةٌ"
“Tulikuwa safarini pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Adhwhaa ikatukutia huko. Tukashirikiana watu saba ng’ombe mmoja, na watu kumi ngamia mmoja”. [Isnaad yake ni Hasan. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1501), An-Nasaaiy (7/222) na Ibn Maajah (3131)].
Ash-Shawkaan akioanisha kati ya dalili amesema: “Ngamia anawatosha watu kumi kama ni wa udhwhiyah, na watu saba kama ni wa amali za Hijja”.
Ya pili: Imamu Maalik (Rahimahul Laah) -kinyume na Jumhuwr- ameshurutisha kwa wenye kushirikiana ng’ombe mmoja au ngamia mmoja wawe ni watu wa nyumba moja!!
Kauli hii inabidi iangaliwe, kwa kuwa Hadiyth ya Jaabir iliyotangulia ambayo inasema: “Tulichinja pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwaka wa Al-Hudaybiyah ngamia mmoja kwa watu saba, na ng’ombe mmoja kwa watu saba”, inaonyesha kuwa Maswahaba walikuwa ni watu tofauti tofauti toka makabila mbalimbali. Na hata makabila yao yangelikuwa ni mamoja, basi wangetofautiana nyumba, na lau zingekuwa nyumba zao ni moja, basi ingelikuwa vile vile ni vigumu kila nyumba kukamilisha idadi ya watu saba, ima wangezidi, au wangepungua. [Al-Haawiy cha Al-Mawruwdiy (19/145-146) na Fiqhul Udhwhiyah (uk. 89-90)].
Ya tatu: Jumhuwr -kinyume na Abu Haniyfah- wamejuzisha kutofautiana nia kwa watu saba wenye kushirikiana kwenye mnyama mmoja. Wamesema kuwa inajuzu baadhi yao washiriki kwa niya ya udhwhiyah, na wengine kwa niya ya kupata nyama tu. Kwa sababu fungu la kila mmoja wao linazingatiwa kwa mujibu wa niya yake na si kwa mujibu wa niya ya mwenzake. Kwa kuwa, lau kama dhabihu zao zitatofautiana, baadhi yao wakafanya fungu lao kwa ajili ya qiraan, na wengine kwa tamattu, na wengine kwa kunyoa, na waliobaki kwa kivazi, basi itajuzu. Kadhalika, hata kama mwingine fungu lake likawa kwa ajili ya nyama tu, kwa kuwa niya ya asiyejikurubisha haiathiri niya ya mwenye kujikurubisha.
Ya nne: Umri ufaao kwa ngamia na ng’ombe
Jaabir amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam amesema:
"لاَ تَذْبَحُوا إِلاَّ مُسِنَّةً إِلاَّ أَنْ يَعْسُرَ عَلَيْكُمْ فَتَذْبَحُوا جَذَعَةً مِنَ الضَّأْنِ"
“Msichinje isipokuwa “musinnah”, ila kama itakuwa vigumu kwenu kumpata, basi chinjeni “jadha’ah” wa mbuzi au kondoo”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1963), Abu Daawuwd (2797), An-Nasaaiy (7/218) na Ibn Maajah (3141)].
“Musinnah” ni mnyama aliyekomaa vizuri. Kwa ngamia ni yule aliyetimiza miaka mitano na kuingia wa sita, na kwa ng’ombe ni yule aliyetimiza miaka miwili na kuingia wa tatu. Haitojuzu kuchinja walio chini ya miaka hiyo kwa wote wawili. Ama “jadha’ah” kwa mbuzi na kondoo, ni yule aliyefikisha miezi sita kwenda juu. Haijuzu wa chini ya miezi sita.
(c) Kondoo
Toka kwa Anas, kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"ضَحَّى بِكَبْشَيْنِ أَمْلَحَيْنِ .... "
“Alichinja kondoo wawili dume wenye rangi mseto ya weupe na weusi….”. [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo].
Kondoo mmoja anamtosheleza mtu; yeye pamoja na watu wa nyumba yake. ‘Aaishah amesema:
"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَمَرَ بِكَبْشٍ أَقْرَنَ يَطَأُ فِي سَوَادٍ وَيَبْرَكُ فِي سَوَادٍ وَيَنْظُرُ فِي سَوَادٍ فَأُتِيَ بِهِ لِيُضَحِّيَ بِهِ فَقَالَ لَهَا : يَا عَائِشَةُ هَلُمِّي الْمُدْيَةَ ، ثُمَّ قَالَ : اشْحَذِيهَا بِحَجَرٍ ، فَفَعَلَتْ ثُمَّ أَخَذَهَا وَأَخَذَ الْكَبْشَ فَأَضْجَعَهُ ، ثُمَّ ذَبَحَهُ ، ثُمَّ قَالَ : بِسْمِ اللَّهِ ، اللَّهُمَّ تَقَبَّلْ مِنْ مُحَمَّدٍ وَآلِ مُحَمَّدٍ وَمِنْ أُمَّةِ مُحَمَّدٍ ، ثُمَّ ضَحَّى بِهِ."
“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliagiza beberu la kondoo mwenye pembe, mwenye miguu myeusi, mwenye tumbo jeusi, na mwenye macho meusi. Akaletewa ili amchinje (kwa udhwhiya). Akamwambia: Ee ‘Aaishah! Niletee kisu. Kisha akamwambia: Kinoe kwa jiwe. ‘Aaishah akakinoa, Rasuli akakichukua, akamkamata beberu, akamlaza ubavu, kisha akamchinja huku akisema: Bismil Laah. Ee Allaah! Mtakabalie Muhammad, na familia ya Muhammad, na ummah wa Muhammad”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1967)].
Na Abu ‘Atwaa bin Yasaar amesema:
"سَأَلْتُ أَبَا أَيُّوبَ الأَنْصَارِيَّ كَيْفَ كَانَتِ الضَّحَايَا فِيكُمْ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ـ قَالَ كَانَ الرَّجُلُ فِي عَهْدِ النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يُضَحِّي بِالشَّاةِ عَنْهُ وَعَنْ أَهْلِ بَيْتِهِ فَيَأْكُلُونَ وَيُطْعِمُونَ ، ثُمَّ تَبَاهَى النَّاسُ فَصَارَ كَمَا تَرَى"
“Nilimuuliza Abu Ayyuuwb Al-Answaariy: Ni mazingira yapi mliyokuwa nayo kwa upande wa kudhwahi wanyama wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Akasema: Mtu katika enzi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alikuwa anachinja kondoo kwa niaba yake na kwa niaba ya watu wa nyumba yake, kisha wanakula na kugawa kwa wengine, mpaka watu wakaanza kushindana, na hali ikawa kama unavyoiona”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1505), Ibn Maajah (3147), na Al-Bayhaqiy (9/268)].
"وَ عَنْ عَبْدِ اللهِ بِنْ هِشَامِ كَانَ قَدْ أَدْرَكَ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَذَهَبَتْ بِهِ أُمُّهُ زَيْنَبُ ابْنَةُ حُمَيْدٍ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَتْ : يَا رَسُولَ اللَّهِ بَايِعْهُ. فَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم : " هُوَ صَغِيرٌ "، فَمَسَحَ رَأْسَهُ وَدَعَا لَهُ، وَكَانَ يُضَحِّي بِالشَّاةِ الْوَاحِدَةِ عَنْ جَمِيعِ أَهْلِهِ"
‘Abdullaah bin Hishaam ambaye alimwahi Rasuli akiwa hai amesema kuwa mama yake Zaynab bint Humayd alimchukua kwenda naye kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alipofika alisema: Ee Rasuli wa Allaah! Peaneni naye fungamano la kuwajibika na Uislamu na kukutii wewe (Bay-‘a). Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Yeye bado hajabaleghe. Akakipangusa kichwa chake na akamwombea. Naye (‘Abdullaah bin Hishaam) alikuwa anachinja kondoo mmoja kwa niaba ya watu wake wote”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (7210), Abu Daawuwd (2942) kwa ufupisho, na Ahmad (4/233)].
Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad wanaona kwamba kondoo mmoja anamtosheleza mtu pamoja na familia yake yote hata kama ni wengi. Lakini Abu Haniyfah na Ath-Thawriy wamelikirihisha hilo!!
Umri Ufaao Kwa Kondoo:
Nyuma kidogo tumeitaja kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:
"لاَ تَذْبَحُوا إِلاَّ مُسِنَّةً إِلاَّ أَنْ يَعْسُرَ عَلَيْكُمْ فَتَذْبَحُوا جَذَعَةً مِنَ الضَّأْنِ"
“Msichinje isipokuwa “musinnah”, ila kama itakuwa vigumu kwenu kumpata, basi chinjeni “jadha’ah” wa mbuzi au kondoo”.
Kauli hii inaonyesha kwamba haijuzu katika udhwhiyah aliye chini ya “musinnah”, na “musinnah” kwa kondoo ni yule aliyefikisha mwaka na anaingia mwaka wa pili. Lakini kama itakuwa vigumu kumpata, basi atatosha “jadha’ah, na huyu ni mwenye kuanzia miezi sita kwenda juu. Na huu ndio msimamo wa ‘Ulamaa. Lakini pamoja na msimamo wao huu, wamejuzisha kuchinja kondoo “jadha’ah kwa hali yoyote hata kama “musinnah” atapatikana, kwa kuwa wameichukulia Hadiyth hii kuwa inastahabisha jambo hilo huku wakitolea dalili kwa jumla ya Hadiyth zinazoashiria kujuzu kuchinja kondoo wa kuanzia miezi sita katika hali yoyote ile, lakini Asaaniyd za Hadiyth hizo zote ni Dhwa’iyf.
Lenye nguvu na kutegemewa zaidi ni kuwa kondoo “jadha’ah” hatoshelezi isipokuwa tu kama “musinnah” hatopatikana kutokana na udhahiri wa Hadiyth hii, na udhaifu wa wenye kuikhalifu. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi. [Al-Mabsuwtw (12/9), Al-Mudawwanah (2/2), Al-Haawiy (19/89) na Al-Mughniy (9/348)].
(d) Mbuzi
Mbuzi anayetosheleza ni yule mwenye mwaka mmoja kwenda juu kutokana na Hadiyth iliyotangulia. Ama “jadha’ah” wa mbuzi (mwenye umri wa chini ya mwaka mmoja), huyo hatoshelezi katika udhwhiyah kwa makubaliano ya ‘Ulamaa wote. [Limenukuliwa hili na At-Tirmidhiy katika As-Sunan (4/194), na Ibn ‘Abdul Barri katika At-Tamhiyd (23/185). Lakini ‘Atwaa na Al-Awzaa’iy wamelikhalifu hilo].
Al-Baraa bin ‘Aazib amesema:
"ضَحَّى خَالٌ لِي يُقَالُ لَهُ أَبُو بُرْدَةَ قَبْلَ الصَّلاَةِ فَقَالَ لَهُ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : "شَاتُكَ شَاةُ لَحْمٍ " . فَقَالَ يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّ عِنْدِي دَاجِنًا جَذَعَةً مِنَ الْمَعْزِ ، فَقَالَ : "اذْبَحْهَا وَلاَ تَصْلُحُ لِغَيْرِكَ"
“Mjomba wangu aitwaye Abu Burdah alichinja kabla ya Swalaah. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Kondoo wako ni wa nyama tu. Akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Nina mbuzi wa nyumbani wa chini ya mwaka mmoja . Akamwambia: Mchinje, lakini hafai kwa mwingine zaidi yako”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5556) na Muslim (1961)].
Naye ‘Uqbah bin ‘Aamir amesema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa kondoo wa kudhwahi ili awagawe kwa niaba yake kwa Maswahaba zake. Akabakia mbuzi mdogo wa chini ya mwaka mmoja, naye akamweleza hilo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Rasuli akamwambia:
"ضَحِّ بِهِ أَنْتَ"
“Huyo jichinjie mwenyewe”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5555) na Muslim (1965)].
Kauli ya Rasuli: “Huyo jichinjie mwenyewe”, imechukuliwa na ‘Ulamaa kuwa ni jambo mahsusi kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir tu. Na kauli yao hii inatiliwa nguvu na ziada kwenye Hadiyth iliyoko kwa Al-Bayhaqiy isemayo:
"وَلاَ رُخْصَةَ فِيْهَا لأَحَدٍ بَعْدَكَ"
“Na hakuna ruksa kwayo kwa mwingine yeyote baada yako”. [Angalia Fat-hul Baariy (10/17), na Sunan Al-Bayhaqiy (9/70)].
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأُضْحِيَةُ
Udhwhiyah
Alhidaaya.com [3]
04-Udhwhiyah: Kasoro Zinazomfanya Mnyama Asifae Kwa Kudhwahi:
Kasoro anazokuwa nazo mnyama wa kudhwahi zinagawanyika vigawanyo vitatu:
Cha kwanza: Ni kasoro zinazomfanya mnyama akataliwe na asifae, nazo ni nne. Kasoro hizi Hadiyth imezielezea kuwa hazimpasishi mnyama kuweza kuchinjwa. Wanyama hao ni wenye kasoro hizi:
1- Mwenye chongo linaloonekana wazi. Ikiwa weupe utafunika sehemu kubwa ya jicho lake na kubaki sehemu ndogo tu, basi atakuwa hafai. Na kipofu ndiye hafai kabisa.
2- Mgonjwa ambaye ugonjwa wake unaonekana bayana. Kama ugonjwa wake ni hafifu, basi atafaa.
3- Mwenye kuchechemea mchechemeo dhahiri. Na aliyekatwa au aliyevunjika miguu atakuwa hafai kabisa.
4- Aliyedhoofu kutokana na udhaifu wa mifupa yake.
Toka kwa Al-Baraa bin ‘Aazib kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَرْبَعَةٌ لاَ يَجْزِينَ فِي الأَضَاحِي : الْعَوْرَاءُ الْبَيِّنُ عَوَرُهَا ، وَالْمَرِيضَةُ الْبَيِّنُ مَرَضُهَا ، وَالْعَرْجَاءُ الْبَيِّنُ ظَلْعُهَا ، وَالْكَسِيرَةُ الَّتِي لاَ تُنْقِي"
“Wanne hawakidhi vigezo vya kuwa wanyama wa kudhwahi. Mwenye chongo la wazi linaloonekana, mgonjwa anayeonekana wazi kuwa mgonjwa, anayechechemea ambaye mbavu zake zimetokeza, na mdhoofu anayejikokota”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (7/215), Ibn Maajah (3144) na Ahmad (4/284)].
Kwa kasoro hizi, mnyama anakuwa hafai na hana sifa za kudhwahi kwa makubaliano ya ‘Ulamaa. [At-Tamhiyd (20/167), Al-Mughniy (9/349), na Al-Majmuw’u (8/404)].
Cha pili: Ni kasoro ambazo hazipendezi mnyama huyu kuwa nazo, lakini hazizuii kupata sifa ya kufaa. Kasoro zenyewe ni:
1- Kukatwa sikio lote au sehemu ya sikio.
Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema kwamba mnyama mwenye hali hii hafai kwa kudhwahi. Lakini kauli yao hiyo ina walakini, kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameainisha kasoro nne tu kwa mnyama akiwa nazo kuwa hafai kwa kudhwahi katika Hadiyth iliyotangulia. Bali ‘Aliy (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:
"أَمَرَنَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ نَسْتَشْرِفَ الْعَيْنَ وَالْأُذُنَ"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuamuru tukague macho (kama mazima yanaona) na masikio (kama mazima hayajaguswa)”. [Hadiyth Hasan Bitwuruqih. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (7/217), Ahmad (1/95), At-Tirmidhiy (1498), Abu Daawuwd (284), Ibn Maajah (3142) na wengineo].
Hadiyth hii ya ‘Aliy inatufahamisha kwamba mnyama anayeepukwa ni yule aliyetobolewa, au aliyepasuliwa, au aliyekatwa sikio, lakini pamoja na hivyo, haimaanishi kwamba hafai au hatoshelezi vigezo vikuu.
‘Ulamaa wamekhitalifiana pia kuhusu mnyama ambaye kimaumbile amezaliwa bila masikio mawili. Abu Haniyfah, Maalik na Ash-Shaafi’iy wanaona kwamba kama hana masikio kabisa, basi huyo atakuwa hafai, lakini kama atakuwa na masikio angalau madogo, basi atafaa. [Al-Istidhkaar (15/128), Ibn ‘Aabidiyna (9/467), na Al-Majmuw’u (8/401)].
2- Kuvunjika pembe kidogo au sehemu yake kubwa.
Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema inajuzu kudhwahi mnyama aliyevunjika pembe lakini asiwe anatokwa damu. Kwa upande wa Maalik, yeye anasema itakuwa ni makruhu tu.
Ninasema: Limekuja katika baadhi ya riwaayah za Hadiyth iliyotangulia ya ‘Aliy katazo kwa mnyama aliyevunjika pembe. Lakini riwaayah hizo ni Dhwa’iyf.
Cha tatu: Ni kasoro ambazo hazina athari. Hakuna Hadiyth yoyote Swahiyh iliyokataza au kugusia hilo, ingawa kasoro hizi zinapunguza ukamilifu wa vigezo vinavyotakiwa. Mnyama mwenye kasoro hizi anatosheleza katika kudhwahi na wala hakataliwi, ingawa kuna baadhi ya ‘Ulamaa waliomkataa. Ni kama asiye na meno kabisa, aliyekatwa mkia au tako, aliyekatwa pua, aliyehasiwa na kadhalika.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأُضْحِيَةُ
Udhwhiyah
Alhidaaya.com [3]
05-Udhwhiyah: Sifa Za Ukamilifu Zinazopendeza Kuwepo Kwa Mnyama Wa Kudhwahiwa:
[Rawdhwat At-Twaalibiyna (2/465), Al-Haawiy (19/92), Al-Mughniy (9/347), na Al-Muhallaa (7/370)]
(a) Anapendeza mnyama aliyenona zaidi na aliye mkamilifu zaidi. Kuchinja kondoo aliyenona vizuri ni bora zaidi kuliko kuchinja kondoo wawili walio na hali duni kuliko huyo aliyenona, kwa kuwa lengo kuu hapo ni nyama, na aliyenona ndiye mwenye nyama nyingi zaidi na nzuri zaidi, na nyama nyingi ni bora zaidi kuliko shahamu nyingi zaidi. Yanayothibitisha kuwa aliyenona vizuri anastahabiwa zaidi ni:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ ﴿٣٢﴾
32. Hayo ndio hivyo. Na yeyote anayeadhimisha Ishara za Allaah, basi hayo ni katika taqwa ya nyoyo. [Al-Hajj: 22].
Ash-Shaafi’iy (Rahimahul Laah) ametolea dalili kwa Aayah hii kuwa inastahabiwa kumwadhimisha mnyama wa kuchinjwa na kumnenepesha. [Al-Haawiy (19/94)].
2- Abu Umaamah bin Sahl amesema:
"كُنَّا نُسَمِّنُ الأُضْحِيَةَ بالمَدِيْنَةِ ، وَكَانَ المسْلِمُوْنَ يُسَمِّنُوْنَ"
“Tulikuwa tukiwanenepesha wanyama wa kudhwahi Madiynah, na Waislamu walikuwa wakinenepesha”. [Isnaad yake ni Hasan. Al-Bukhaariy (10/12) kasema ni Mu’allaq, na Abu Nu’aym kasema ni Mawswuul katika Mustakhraji wake kama ilivyo katika At-Ta-‘aliyq (5/6)].
(b) Wanyama walio bora zaidi
Jumhuwr ya ‘Ulamaa kinyume na Maalik, wanaona kwamba wanyama bora zaidi wa kudhwahi ni kwanza kabisa ngamia, kisha ng’ombe, halafu mbuzi na kondoo. Wametoa dalili kadhaa kuhusiana na hili:
1- Kauli ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"مَنِ اغْتَسَلَ يَوْمَ الْجُمْعَةِ غُسْلَ الْجَنَابَةِ، ثُمَّ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الأُوْلَى فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَدَنَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّانِيَةِ، فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَقَرَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّالِثَةِ، فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ كَبْشًا أَقْرَنَ ..."
“Mwenye kuoga kikamilifu siku ya Ijumaa kama anavyofanya katika ghuslu ya janaba, kisha akaenda (Msikitini) katika saa la mwanzo, anakuwa kama ametoa swadaqah ngamia, na mwenye kwenda saa la pili, anakuwa kama ametoa ng’ombe, na mwenye kwenda saa la tatu, anakuwa kama ametoa kondoo dume mwenye pembe..”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (881) na Muslim (850)].
2- Hadiyth ya Abu Dharrin (Radhwiya Allaah ‘anhu), alimuuliza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"فَأَيُ الرِّقَابِ أَفْضَلُ؟ قَالَ : أَغْلَاهَا ثَمَنًا ، وَأَنْفَسُهَا عِنْدَ أَهْلِهَا..."
“Ni mtumwa yupi aliye bora zaidi (kuachwa huru)? Akasema: Ni mwenye thamani zaidi, na aliye bora zaidi kwa watu wanaommiliki….”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2518) na Muslim (84)].
Wamaalik wamesema: Mbora zaidi ni mbuzi na kondoo, kisha ng’ombe, halafu ngamia kutokana na uzuri wa nyama. Na kwa vile Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja beberu wawili wa kondoo wenye rangi nyeupe na nyeusi. Kadhalika, wametoa dalili kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ ﴿١٠٧﴾
107. Na Tukamtolea fidia kwa dhabihu adhimu. [Asw-Swaaffaat: 37].
(c) Mbora zaidi ni mweupe, kisha wa rangi ya udongo, halafu mweusi. Hii ni kwa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja beberu wawili wa kondoo wenye rangi nyeupe iliyochanganyika kidogo na weusi.
Shaykhul Islaam (26/308) amesema: “Mwenye rangi ya udongo ni bora zaidi kuliko mweusi. Na kama kuna weusi kuzunguka macho yake na mdomo wake, na kwenye miguu yake, basi huyo atafanana na mnyama aliyemchinja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Ninasema: “Anaashiria kwa maneno yake haya Hadiyth ya ‘Aaishah:
"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَمَرَ بِكَبْشٍ أَقْرَنَ يَطَأُ فِي سَوَادٍ وَيَبْرَكُ فِي سَوَادٍ وَيَنْظُرُ فِي سَوَادٍ فَأُتِيَ بِهِ لِيُضَحِّيَ بِهِ..."
“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliagiza beberu la kondoo mwenye pembe, mwenye miguu myeusi, mwenye tumbo jeusi, na mwenye macho meusi. Akaletewa ili amchinje (kwa udhwhiyah). [Imekharijiwa na Muslim (1967) na wengineo].
An Nawawiy kasema: “Maana yake ni kwamba miguu yake na tumbo lake, na kuzungukia macho yake kuna weusi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.
(d) Kuchinja dume ni bora zaidi kuliko jike. Hii ni kutokana na ujumuishi wa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na mtumwa bora zaidi wa kuachwa huru:
"أَغْلَاهَا ثَمَنًا ، وَأَنْفَسُهَا عِنْدَ أَهْلِهَا..."
“Ni mwenye thamani zaidi, na aliye bora zaidi kwa watu wanaommiliki….”.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأُضْحِيَةُ
Udhwhiyah
Alhidaaya.com [3]
06-Udhwhiyah: Kukata Kucha Na Kunyoa Nywele Kwa Aliyeazimia Kudhwahi
Toka kwa Ummu Salamah, kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا دَخَلَتِ الْعَشْرُ وَأَرَادَ أَحَدُكُمْ أَنْ يُضَحِّيَ فَلاَ يَمَسَّ مِنْ شَعَرِهِ وَبَشَرِهِ شَيْئًا "
“Linapoingia kumi (la mwanzo la mwezi wa Dhul-Hijja) na mmoja wenu akaazimia kudhwahi, basi asikate chochote katika nywele zake na kucha zake”. [Imekharijiwa na Muslim (1977) na wengineo. Imepita nyuma kidogo].
‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na yule ambaye kumi la mwanzo la Dhul-Hijja limeshaingia naye anataka kudhwahi. [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (3/138), Al-Mughniy (9/346), Ma’aalimu As-Sunan (2/196) na Fiqhul Udhwhiya (uk. 99)].
Ibn Al-Musayyib, Rabiy’ah, Ahmad, Is-haaq, Daawuwd, na baadhi ya wafuasi wa Ash-Shaafi’iy, hawa wanasema kwamba ni haramu kwa mtu huyo kukata chochote katika nywele zake au kucha zake mpaka pale atakapodhwahi. Ni kutokana na uwazi wa Hadiyth hii.
Maalik, Ash-Shaafi’iy na maswahibu zake wanaona kwamba hilo ni makruhu -ukaraha khafifu (tanziyh), na si haramu. Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa):
"كُنْتُ أَفْتِلُ قَلاَئِدَ بُدْنَ النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَمَ ، ثُمَّ يُقَلِّدُهُ وَيَبْعَثُ بِهِ ، وَلا يَحْرُمُ عَلَيْهِ شَيْئٌ أَحَلَّهُ اللَّهُ حَتَّى يَنْحَرَ الْهَدْىَ "
“Nilikuwa ninasuka vigwe vya ngamia wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisha yeye huwavika vigwe hivyo na kumtuma mtu ampelekee (Al-Haram ngamia hao). Na wala hakiharamiki kwake chochote ambacho Allaah Amekihalalisha mpaka mnyama wake anachinjwa”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1698) na Muslim (1321)].
Wamesema: “Wamekubaliana kwa sauti moja kwamba hakatazwi kuvaa nguo za kushonwa na kujitia manukato kama inavyoharamishwa kwa aliyehirimia. Hivyo, hilo limedulisha kuwa ni jambo linalopendeza na lililonadibiwa, na si jambo la wajibu lililolazimishwa”.
Lakini Abu Haniyfah amesema kuwa kufanya hivyo si jambo la karaha.
Ninasema: “Jambo hili linazungukia baina ya uharamu na umakuruhu. Ni kwamba, kunyoa au kupunguza nywele, au jambo lolote ambalo linafanyika kwa nadra sana, jambo hili halikusudiwi katika Hadiyth ya ‘Aaishah, bali yeye amekusudia yale yote anayoyafanya nyakati zote kama kuvaa, kujitia manukato na mfano wake (yaani haya ndiyo ambayo Rasuli hajajiharamishia)”.
Faida Mbili: [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (3/138]
Ya kwanza: Makusudio ya katazo la kukata kucha kunajumuisha kuziondosha kwa kuzikata, kuzivunja na mfano wake. Ama nywele, inajumuisha kuzinyoa kipara, kuzipunguza, kuzinyofoa na mfano wake, ni sawa ikiwa za kwapa, za sharubu, za kinena, za kichwa au sehemu nyingine yoyote ya mwili.
Ya pili: Hikma ya katazo hilo, ni kubaki aliyeazimia kuchinja na viungo vyake kamili ili aachwe huru navyo na moto. Baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kuwa hikma ya hilo ni kujifananisha na aliyehirimia. Lakini kauli hii ina angalizo, kwa kuwa waazimiaji hao hawaepuki wanawake, wameruhusiwa kujitia manukato na kuvaa nguo, na mengineyo ambayo ni marufuku kwa aliyehirimia.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأُضْحِيَةُ
Udhwhiyah
Alhidaaya.com [3]
08-Udhwhiyah: Wakati Wa Kudhwahi:
‘Ulamaa wamekubaliana kwa sauti moja kwamba haijuzu kuchinja mnyama wa udhwhiyah kabla ya kuchomoza alfajiri ya Yawm An Nahr (tarehe 10 Dhul Hijja), lakini wamekhitalifiana kuhusiana na yanayofuatia baada ya hapo. [Al-Ijmaa cha Ibn Al-Mundhir (64), At-Tamhiyd (23/162), Sharhu Muslim (13/110) na Al-Muhallaa (7/374)].
1- Ash-Shaafi’iy, Daawuwd, Ibn Al-Mundir na wengineo wamesema kwamba wakati wake unaingia jua linapochomoza na ukapita muda wa kiasi cha kuswali Swalaatul ‘Iyd na khutba mbili. Kama atachinja baada ya wakati huu, basi itamtosheleza, ni sawa ikiwa imamu ameswali au bado, au mchinjaji ameswali au hakuswali, ni sawa akiwa ni mtu wa mjini, au kijijini, au majangwani.
2- ‘Atwaa na Abu Haniyfah wamesema kwamba wakati wake kwa upande wa watu wa vijijini na majangwani, unaingia inapochomoza alfajiri ya pili. Ama kwa upande wa watu wa mjini, wakati hauingii mpaka imamu aswali na watu na akhutubu. Ikiwa atachinja kabla ya hapo, basi haitofaa.
3- Maalik amesema kwamba haijuzu kuchinja ila baada ya imamu kuswali, kukhutubu na kuchinja.
4- Ahmad amesema kwamba haijuzu kabla ya Swalaah, na inajuzu baada yake, kabla imamu hajachinja.
Ninasema: “Toka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaah ‘anhu): Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنْ ذَبَحَ قَبْلَ الصَّلَاةِ فَإِنَّمَا يَذْبَحُ لِنَفْسِهِ وَمَنْ ذَبَحَ بَعْدَ الصَّلَاةِ فَقَدْ تَمَّ نُسُكُهُ وَأَصَابَ سُنَّةَ الْمُسْلِمِيْن"
“Mwenye kuchinja kabla ya Swalaah, hakika huyo anachinja kwa ajili ya nafsi yake, na mwenye kuchinja baada ya Swalaah, basi amali yake ya kuchinja imetimia na ameipata sunnah ya Waislamu”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5546) na Muslim (1962)].
Al-Baraa bin ‘Aazib: Nimemsikia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikhutubu na kusema:
"إِنَّ أَوَّلَ مَا نَبْدَأُ بِهِ فِي يَوْمِنَا هَذَا نُصَلِّي ثُمَّ نَرْجِعُ فَنَنْحَرُ فَمَنْ فَعَلَ ذَلِكَ فَقَدْ أَصَابَ سُنَّتَنَا وَمَنْ ذَبَحَ فَإِنَّمَا هُوَ لَحْمٌ قَدَّمَهُ لأَهْلِهِ لَيْسَ مِنَ النُّسُكِ فِي شَىْءٍ ، فَقَالَ أَبُوْ بُرْدَةٌ : يَا رَسُوْلَ اللهِ، ذَبَحْتُ قَبْلَ أَنْ أُصَلِّيَ ، وَعِنْدِيْ جَذَعَةٌ خَيْرٌ مِنْ مُسِنَّةٍ ، فَقَالَ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : اجْعَلْهَا مَكَانَهَا ، وَلَنْ تُجْزِئَ عَنْ أَحَدٍ بَعْدَكَ"
“Jambo la kwanza tunaloanza nalo katika siku yetu hii (‘Iyd Al-Adhwhaa) ni kuswali, halafu tunarudi (majumbani) tunachinja. Basi mwenye kufanya hivyo, huyo anakuwa ameipata sunnah yetu. Na mwenye kuchinja (kabla ya Swalaah), hakika hiyo inakuwa ni nyama anayowapa watu wake, haihusiki na chochote na amali ya kudhwahi”. Abu Burdah akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Mimi nimechinja kabla sijaswali. Nami nina jadh-‘a ambaye kwangu ni mbora zaidi kuliko musinnah. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Mfidie huyo huyo mahala pa uliyemchinja, na hatofaa kwa yeyote baada yako”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5560). Imetajwa nyuma].
Hadiyth hizi mbili zinafahamisha kwa uwazi kabisa kwamba wakati wa kudhwahi unaingia baada ya watu kuswali -kwa wale ambao kwao Swalaah ya ‘Iyd huswaliwa- na hakuna ulazima au sharti ya kusubiri mpaka Imamu achinje kwanza, kwa kuwa kama Imamu hakuchinja, basi hilo haliondoshi kwa watu sunnah ya kudhwahi. Na hata kama Imamu huyo atachinja kabla ya Swalaah, basi kudhwahi kwake hakutoshelezi. Hivyo basi, yeye na watu wote wako sawa katika wakati wa kuchinja (yaani baada ya Swalaah). [Al Fat-h (10/24), na Al-Ummu (2/332)].
Ama Hadiyth ya Jaabir:
"صَلَّى بِنَا النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَوْمَ النَّحْرِ بِالْمَدِينَةِ فَتَقَدَّمَ رِجَالٌ فَنَحَرُوا ، وَظَنُّوا أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَدْ نَحَرَ ، فَأَمَرَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مَنْ كَانَ نَحَرَ قَبْلَهُ أَنْ يُعِيدَ بِنَحْرٍ آخَرَ ، وَلاَ يَنْحَرُوا حَتَّى يَنْحَرَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ"
“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituswalisha Yawm An-Nahr (‘Iyd Al-Adhwhaa) mjini Madiynah, na baadhi ya watu wakatangulia kuchinja. Walidhani kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameshachinja. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamuru kila aliyechinja kabla yake achinje tena mnyama mwingine, na wasije kuchinja tena mpaka Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) achinje kwanza. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1963), Ahmad (3/204) na Al-Muhallaa (7/374)].
Hadiyth hii Jumhuwr wameiawilisha wakisema kuwa muradi wake ni kuwa Rasuli aliwakataza kuharakia kunakoweza kupelekea mtu kudhwahi kabla ya wakati wake. Na kwa ajili hiyo, Hadiyth nyingine zote zimekuja zikifungamanisha Swalaah, na kwamba mwenye kuchinja baada yake, basi huyo amesibu sunnah, na atakayechinja kabla, basi hajasibu chochote katika amali ya kudhwahi.
Mwisho Wa Wakati Wa Kudhwahi
‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na wakati wa mwisho wa kudhwahi kama ilivyotangulia katika Kitabu cha Hajji katika Masiku ya Kuchinja. Na kwa mujibu wa makhitilafiano hayo, lililokubalika ni kuwa wakati wa kudhwahi unaendelea hadi mwisho wa Masiku ya Tashriyq (tarehe 13 ya Dhul Hijjah). Lakini kiakiba zaidi ni kudhwahi Yawm An Nahr (tarehe 10) kutokana na Ijmaa kuwa inatosheleza katika Siku hiyo. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأُضْحِيَةُ
Udhwhiyah
Alhidaaya.com [3]
08-Udhwhiyah: Mahala Pa Kuchinjia:
Mwenye kuchinja ameruhusiwa kuchinja sehemu yoyote ile baada ya Swalaatul ‘Iyd, ni sawa ikiwa nyumbani kwake au kwingineko. Pia anaruhusiwa kuchinja katika sehemu ilikwoswaliwa ‘Iyd. Jundub bin Suyfaan amesema:
"شَهِدْتُ الأَضْحَى مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ، فَلَمْ يَعْدُ أَنْ صَلَّى وَفَرَغَ مِنْ صَلاَتِهِ سَلَّمَ ، فَإِذَا هُوَ يَرَى لَحْمَ أَضَاحِيَّ قَدْ ذُبِحَتْ قَبْلَ أَنْ يَفْرُغَ مِنْ صَلاَتِهِ ، فَقَالَ : " مَنْ كَانَ ذَبَحَ أُضْحِيَّتَهُ قَبْلَ أَنْ يُصَلِّيَ - أَوْ نُصَلِّيَ - فَلْيَذْبَحْ مَكَانَهَا أُخْرَى ، وَمَنْ كَانَ لَمْ يَذْبَحْ فَلْيَذْبَحْ بِاسْمِ اللَّهِ"
“Nilihudhuria Al-Adhwhaa pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hakufanya jingine lolote isipokuwa aliswali nasi, akaimaliza Swalaah na akatoa tasliym. Kutahamaki akaona nyama za wanyama wa udhwhiyah waliochinjwa kabla hajamaliza Swalaah. Akasema: Aliyekuwa amedhwahi mnyama wake kabla hajaswali -au kabla hatujaswali- basi achinje badala yake mnyama mwingine. Na ambaye bado hajachinja, basi achinje kwa kulitaja Jina la Allaah”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1960) na An-Nasaaiy (7/214)].
Hadiyth hii inaonyesha kuwa walichinja katika eneo waliposwalia ‘Iyd.
Imestahabiwa kwa Imamu achinje mahala pa kuswalia ili watu wajue kwamba wakati wa kudhwahi ushaingia, lakini pia wajifunze kutoka kwake namna ya kuchinja. Ibn ‘Umar amesema:
"كَانَ رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَذْبَحُ وَيَنْحَرُ بِالمصَلَّى"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anachinja katika sehemu ya kuswalia (‘Iyd)”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5552), Abu Daawuwd (2811), An-Nasaaiy (7/213) na Ibn Maajah (3161)].
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأُضْحِيَةُ
Udhwhiyah
Alhidaaya.com [3]
09-Udhwhiyah: Yanayopatiwa Manufaa Kutokana Na Mnyama
1- Kula sehemu ya nyama yake 2- Kutoa swadaqah kwa masikini 3- Kuiweka akiba.
Allaah Ta’aalaa Amesema:
لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۖ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ ﴿٢٨﴾
28. Ili wahudhurie kupata manufaa yao, na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu kupitia yale Aliyowaruzuku kati ya wanyama wenye miguu minne wa mifugo. Basi kuleni sehemu yake, na lisheni mwenye shida fakiri. [Al-Hajj: 28].
Salamah bin Al-Akwaa: Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنْ ضَحَّى مِنْكُمْ فَلاَ يُصْبِحَنَّ بَعْدَ ثَالِثَةٍ وَبَقِيَ فِي بَيْتِهِ مِنْهُ شَيْءٌ " . فَلَمَّا كَانَ فِي الْعَامِ الْمُقْبِلِ قَالُوا : يَا رَسُولَ اللَّهِ نَفْعَلُ كَمَا فَعَلْنَا العَامَ الماضِي ؟ قَالَ : "كُلُوْا ، وَأَطْعِمُوْا ، وَادَّخِرُوا ، فَإِنَّ ذلِكَ العَامُ كَانَ بِالنَّاسِ جُهْدٌ ، فَأَرَدْتُ أَنْ تُعِيْنُوا فِيهَا"
“Aliyedhwahi miongoni mwenu, basi kisibakie kwenye nyumba yake chochote baada ya asubuhi ya siku ya tatu”. Na mwaka uliofuatia ulipowadia walisema: Ee Rasuli wa Allaah! Je, tufanye kama tulivyofanya mwaka jana? Akasema: (Hapana, bali) kuleni, lisheni na wekeni akiba, kwa kuwa mwaka jana watu walikuwa na hali ngumu, hivyo nikataka muwasaidie”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5569) na Muslim (1973)].
Agizo hili la kula, kulisha na kuweka akiba nyama hapa, ni la sunnah na si la waajib kwa mujibu wa kauli ya Jumhuwr. Hivyo basi, imestahabiwa kwa aliyedhwahi ale nyama ya mnyama wake, aweke akiba na alishe. Na ‘Ulamaa wengi wanasema kwamba imestahabiwa atoe swadaqah theluthi moja ya nyama, alishe theluthi, na theluthi ya tatu ale yeye na familia yake. Lakini zimepokelewa aathaar dhwa’iyf kuhusiana na hili. Alaa kulli haal, anaweza kuigawa nyama vyovyote apendavyo kwa mujibu wa hali, na hata akitaka kuitoa yote swadaqah basi inajuzu. ‘Aliy amesema:
"أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم أَمَرَهُ أَنْ يَقُومَ عَلَى بُدْنِهِ، وَأَنْ يَقْسِمَ بُدْنَهُ كُلَّهَا، لُحُومَهَا وَجُلُودَهَا وَجِلاَلَهَا، وَلاَ يُعْطِيَ فِي جِزَارَتِهَا شَيْئًا"
“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru asimamie uchinjaji wa ngamia wake, na awagawe wote kuanzia nyama zao, ngozi zao na (hata) matandiko waliyovishwa (au vigwe), na asitoe chochote kama malipo ya kuchinjiwa kutoka kwao”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1717) na Muslim (1317)].
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
الأُضْحِيَةُ
Udhwhiyah
Alhidaaya.com [3]
10-Udhwhiyah: Yasiyopatiwa Manufaa Kutokana Na Mnyama
1- Haijuzu kuuza chochote kitokanacho na mnyama. Si Ngozi, wala sufi, wala nywele, wala nyama, wala mfupa wala kingine chochote kiwacho. Katika Hadiyth ya Abu Sa’iyd, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"...وَلا تَبِيْعُوا لُحُوْمَ الهَدْيِ وَالأَضَاحِي ، فَكُلُوا وَتَصَدَّقُوا وَاسْتَمْتَعُوا بِجُلُوْدِهَا وَلاَ تَبِيْعُوهَا .."
“…wala msiuze nyama za wanyama wa amali za Hijja na wa kudhwahi, bali kuleni, zigaweni swadaqah, na tumieni ngozi zao, lakini msiziuze..”. [Hadiyth hii ni Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Ahmad katika Al-Musnad (4/15)].
Lakini mali inayostahiki kwa ‘ibaadah kwa ajili ya Allaah, haijuzu kwa mtoaji wake kuiuza kama zakah na kafara. Na inadulisha juu ya hili pia kwamba haijuzu kumlipa mchinjaji ujira wake kutokana na nyama ya udhwhiya. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad. Abu Haniyfah amesema: Anaweza kuuza chochote kitokanacho na mnyama na kutoa swadaqah kwa thamani yake!! Lenye nguvu ni kuwa hilo halipo. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.
2- Mchinjaji hapewi ujira wake kutokana na udhwhiyah. Kwa kuwa kama atapewa, atakuwa kama anamegewa fungu la thawabu za mnyama huyo huyo. Mwenye mnyama anatakiwa amlipe mchinjaji ujira wake kutokana na mali yake, lakini pia anaruhusiwa kumpa chochote cha mnyama kama ni swadaqah, lakini si kama ujira wake.
‘Aliy amesema:
"أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم أَمَرَهُ أَنْ يَقُومَ عَلَى بُدْنِهِ، وَأَنْ يَقْسِمَ بُدْنَهُ كُلَّهَا، لُحُومَهَا وَجُلُودَهَا وَجِلاَلَهَا، وَلاَ يُعْطِيَ فِي جِزَارَتِهَا شَيْئًا"
“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru asimamie uchinjaji wa ngamia wake, na awagawe wote kuanzia nyama zao, ngozi zao na (hata) matandiko waliyovishwa (au vigwe), na asitoe chochote kama malipo ya kuchinjiwa kutoka kwao”. [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo].
Na katika tamshi jingine:
"نَحْنُ نُعْطِيْهِ مِنْ عِنْدِنَا"
“Sisi tunampa kutoka mifukoni mwetu”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1317)].
Haya ndiyo yaliyosemwa na Jumhuwr ya ‘Ulamaa. Lakini Hasan Al-Baswriy, na ‘Abdullaah bin ‘Ubayd bin ‘Umayr wamejuzisha mchinjaji apewe ngozi kama ujira wake.
Faida:
1- Kudhwahi mnyama ni bora zaidi kuliko kutoa swadaqah thamani yake.
Huu ndio msimamo wa ‘Ulamaa. Kwa kuwa udhwhiyah ni sunnah kokotezwa kinyume na swadaqah ya hiari, mbali na kuwa udhwhiya ni nembo kati ya nembo za Uislamu. [At-Tamhiyd (23/192), Al-Majmuw’u (8/425) na Majmuw’ul Fataawaa (36/304)].
2- Mnyama akipotea kabla ya kuchinjwa, basi aliyekusudia kudhwahi halazimiwi chochote.
Tamiym bin Huwaysw amesema:
"اشْتَرَيْتُ شَاةً بِمِنَى أُضْحِيَةً فَضَلَّتْ ، فَسَأَلْتُ ابْنَ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ عَنْ ذَلِكَ فَقَالَ : لاَ يَضُرُّكَ"
“Nilinunua kondoo Mina kwa ajili ya kudhwahi akapotea. Nikamuuliza Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) akasema: “Hakuna neno”. [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy (9/289) na Ibn Hazm (7/358)].
Ibn ‘Umar amesema:
" مَنْ أَهْدَى بَدَنَةً ثُمَّ ضَلَّتْ أَوْ مَاتَتْ فَإِنَّهَا إِنْ كَانَتْ نَذْرًا أَبْدَلَهَا وَإِنْ كَانَتْ تَطَوُّعًا فَإِنْ شَاءَ أَبْدَلَهَا وَإِنْ شَاءَ تَرَكَهَا"
“Mwenye kujitolea mnyama kisha akapotea au akafa, ikiwa ni wa nadhiri, basi alete mwingine badala yake, na kama alikuwa ni wa swadaqah tu, basi ikiwa atataka, ataleta mwingine badala yake, au akitaka ataacha”. [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Maalik (866) na Al-Bayhaqiy (9/289)].
Ninasema: “Linaunganishwa na hili kama ataugua au akafa kabla ya kuchinjwa. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.
3- Je mnyama wa kudhwahiwa anaweza kupelekwa mji mwingine?
Asili, ni kwamba mahala pa mnyama ni pale alipo mmiliki wake aliyekusudia kudhwahi. Hii ni kwa vile masikini wa sehemu ile watakuwa na kiu kubwa ya kugawiwa nyama yake. Lakini pamoja na hivyo, hakuna kizuizi cha kumpeleka sehemu nyingine kama kutakuwa na maslaha makubwa zaidi. Katika Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdullaah kuhusiana na nyama za wanyama wa kuchinjwa amesema:
"كُنَّا لاَ نَأْكُلُ مِنْ لُحُومِ بُدْنِنَا فَوْقَ ثَلاَثِ بمِنًى، فَرَخَّصَ لَنَا النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ " كُلُوا وَتَزَوَّدُوا ". فَأَكَلْنَا وَتَزَوَّدْنَا"
“Tulikuwa hatuli nyama za wanyama wetu Mina kwa zaidi ya siku tatu, kisha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaturuhusu kwa kutuambia: Kuleni na chukueni masurufu ya safari. Tukala na tukachukua”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1719) na Muslim (1972)].
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/284
[2] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11331&title=08C-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20%D9%83%D9%90%D8%AA%D9%8E%D8%A7%D8%A8%D9%8F%20%D8%A7%D9%84%D8%A3%D9%8E%D8%B7%D9%92%D8%B9%D9%90%D9%85%D9%8E%D8%A9%D9%90%20%D9%88%D9%8E%D8%A7%D9%84%D8%A3%D9%8E%D8%B4%D9%92%D8%B1%D9%90%D8%A8%D8%A9%D9%90%20-%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20%D8%A7%D9%84%D8%A3%D9%8F%D8%B6%D9%92%D8%AD%D9%90%D9%8A%D9%8E%D8%A9%D9%8F%20-%20Udhwhiyah%20%20
[3] http://www.alhidaaya.com/
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11347&title=01-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Udhwhiyah%3A%20Taarifu%20Yake%20Na%20Uhalali%20Wake%20
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11348&title=02-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Udhwhiyah%3A%20Hukmu%20Ya%20Kuchinja%20Udhwhiyah
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11349&title=03-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Udhwhiyah%3A%20Wanyama%20Wanaochinjwa
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11350&title=04-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Udhwhiyah%3A%20Kasoro%20Zinazomfanya%20Mnyama%20Asifae%20Kwa%20Kudhwahi%20%20
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11351&title=05-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Udhwhiyah%3A%20Sifa%20Za%20Ukamilifu%20Zinazopendeza%20Kuwepo%20Kwa%20Mnyama%20Wa%20Kudhwahiwa
[9] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11352&title=06-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Udhwhiyah%3A%20Kukata%20Kucha%20Na%20Kunyoa%20Nywele%20Kwa%20Aliyeazimia%20Kudhwahi
[10] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11353&title=07-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Udhwhiyah%3A%20Wakati%20Wa%20Kudhwahi
[11] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11354&title=08-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Udhwhiyah%3A%20Mahala%20Pa%20Kuchinjia
[12] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11355&title=09-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Udhwhiyah%3A%20Yanayopatiwa%20Manufaa%20Kutokana%20Na%20Mnyama
[13] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11356&title=10-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Vyakula%20Na%20Vinywaji%3A%20Udhwhiyah%3A%20Yasiyopatiwa%20Manufaa%20Kutokana%20Na%20Mnyama