Skip navigation.
Home kabah

Mzee Wangu Ni Mlevi, Je, Naweza Kumtolea Fidya Asamehewe Madhambi Yake? Na Je, Naruhusiwa Kumpa Pesa Za Matumizi?

 

SWALI:

Sina budi kumshukuru Allaah S.W kwa kutujaalia uzima na afya njema na kutuwezesha kuufunga mwezi huu mtukufu wa Ramadhan; ninamuomba Allaah S.W yawe makubuli kwake matendo yetu yote mema tutakayoyafanya katika mwezi huu mtukufu. Na pia sina budi kumuomba yeye Allaah S.W kukujaalieni nyinyi ndugu zetu kila lenye kheir kwa kutufikishia mafundisho mema.  

Suala langu ni kama ifuatavyo:-

Mimi dada yenu nina umri wa miaka 35 hivi sasa; na tokea kupata fahamu kwangu baba yangu mzazi mpaka hivi sasa ninaandika maelezo haya basi hajaacha ulevi yaani tokea mimi sijazaliwa mpaka leo anaendelea na ulevi kiasi ya kwamba sisi watoto tumemaliza maneno kwa mzee wetu huyu awache maasi haya lakini wapi ataacha siku tu ambazo hana pesa lakini akipata tu kazi inaendelea. 

Suala lipo kama ifuatavyo:-

Kuna njia zozote za kufanya iwe kama fidia kwa mzee wetu huyu kutokana na hii hali ya kutokuacha ulevi?

Ikiwa mimi ndie ninaemshughulikia mzee wangu huyu je ninapaswa kumpa pesa za matumizi kama kawaida? kwani nikimpelekea pesa kidogo analalamika na nikimpelekea nyingi ndipo anazidi kulewa kwa hivyo nini nifanye kwa mzee wangu huyu? Ninaomba muongozo wenu ndugu zangu waislam na pia naomba dua zenu kwa wingi kwa ajili ya mzee wangu huyu ili awache mambo haya na aweze kushikamana na dini ya Allaah kikweli kweli. Ahsanteni.

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mahusiano yako na babako. Hakika huo ni mtihani kwako na inafaa uwe na uvumilivu na natija ya hilo itakuwa nzuri. Endeleeni kuzungumza naye kwa wema, busara na njia nzuri kwani uovu haudumu milele hata ukichukua muda mrefu.

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuhimiza kutumia hayo pale Alipotueleza:

Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Anayemjua zaidi aliyeipotea Njia Yake, na Yeye ndiye anayewajua zaidi walioongoka” (16: 125).

Katika madhambi anayofanya mja hakuna fidia kutoka kwa mtu mwengine hata akiwa ni binti yake na ni juu yake kubadilika na kutubia kwa kutimiza masharti yafuatayo:

  1. Kujiondoa katika maasiya.
  2. Kujuta kwa kufanya maasiya.
  3. Kuazimia kutorudia tena katika hayo maasiya.

Wewe lako ni kila wakati kumuombea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Amsaidie kuacha. Kuna wakati ambamo du‘aa za mja zinakubaliwa kwa hivyo jitahidi sana katika nyakati hizo kumuombea kwa dhati na ikhlaasw. Nyakati zenyewe ni:

  1. Wakati umefunga na hasa unapofungua wakati wa Magharibi.
  2. Wakati wa usiku unapoamka kwa ajili ya Tahajjud.
  3. Baina ya Adhana na Iqaamah.
  4. Ukiwa safarini.
  5. Siku ya Ijumaa nyakati za Alasiri hadi linapozama jua.
  6. Pia wakati unaposwali ukiwa katika Sujuud na kabla ya kutoa Salaam.

Ili kumsaidia apunguze unywaji ni lazima umpunguzie masurufu unayompelekea wala isikutishe kupiga kwake kelele. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

Na saidianeni katika wema na ucha Mungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuadhibu” (5: 2).

Haifai kumsaidia mtu katika madhambi bali inafaa umsaidie katika kujirekebisha na hayo maovu.

 

Tufahamu kuwa baadhi ya Mitume watukufu walipata matatizo makubwa zaidi kutoka kwa baba zao lakini wakavumilia na kuendelea kuwaheshimu katika mipaka ya Dini. Mmojawapo ni Nabii Ibraahim (‘Alayhis Salaam) ambaye babake alikuwa ni mshirikina mkubwa sana naye akawa anamlingania. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatupasha habari hiyo: “Na mtaje katika Kitabu Ibraahiym. Hakika yeye alikuwa mkweli, Nabii. Alipomwambia baba yake: Ewe baba yangu! Kwa nini unaabudu visivyo sikia, na visivyo ona, na visivyo kufaa chochote? Ewe baba yangu! Kwa yakini imenifikia ilimu isiyokufikia wewe. Basi nifuate mimi, nami nitakuongoza Njia Iliyo Sawa. Ewe baba yangu! Usimuabudu Shetani. Hakika Shetani ni mwenye kumuasi Mwingi wa Rehema. Ewe baba yangu! Hakika mimi naogopa isikupate adhabu inayo toka kwa Mwingi wa Rehema ukaja kuwa mwenziwe Shetani. (Baba) akasema: Unaichukia miungu yangu, ewe Ibraahiym? Kama huachi, basi lazima nitakupiga mawe. Na niondokelee mbali kwa muda! (Ibraahiym) akasema: Salamun ‘Alayka! Amani iwe juu yako! Mimi nitakuombea msamaha kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ananihurumia sana. Nami najitenga nanyi na hayo mnayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Na ninamwomba Mola wangu Mlezi; asaa nisiwe mwenye kukosa bahati kwa kumwomba Mola wangu Mlezi” (19: 41 – 48).

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuekea mipaka katika kuwahudumikia wazazi wetu walioasi mbali na kuwa tunatakiwa tuwaheshimu. Anasema Aliyetukuka:

“(Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio. Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwatii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anayeelekea Kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni mliyokuwa mkiyatenda” (31: 14 – 15).

Tuko nawe katika kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Amuondolee babako na wazazi wa wengine wenye matatizo kama hayo. 

Na Allaah Anajua zaidi