Skip navigation.
Home kabah

Kuhusu Al-Hidaaya

 

 

 

 

 

 

 

 

Tovuti hii ya ALHIDAAYA imeanzishwa kutoa mafunzo ya Kiislam yaliyo Sahihi kwa kufuata Kitabu cha Allaah na Sunnah Swahiyh za Mtume Muhammad صلي الله عليه وآله و سلم bila kujiegemeza katika dhehebu au kundi lolote lile, bali ALHIDAAYA itakuwa inasimama kwa mwendo waliokwenda nao wema waliotangulia (Salafus-Swaalih).

 

 

 

 

 

 

 

Tovuti hii imeanzishwa na ndugu wenye niyyah ya kuisimamisha dini yao kwa Waislam popote walipo duniani. Pia kuwapatia ndugu zetu faida mbali mbali pamoja na mawaidha kwa lugha yetu ya Kiswahili kwa wepesi kabisa ili waweze kustawisha na kuimarisha maisha yao na familia zao.     

Hakipati misaada kutoka sehemu yoyote kutoka upande wowote bali ni cha kujitolea tu.

Chombo hiki hakiko chini ya serikali wala chama chochote na hakina mielekeo yoyote ya kisiasa.

Lengo lake ni kutoa mafundisho kwa njia mbalimbali za kisasa, zikiwemo njia za kiusomaji na za kiusikilizaji.

Mnakaribishwa  ALHIDAAYA.

 

 

Sababu Ya Kuchagua Aayah Hii Kuwa Nembo  Ya ALHIDAAYA

 

 ((...فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلَا يَشْقَى))

[…Na ukikufikieni kutoka Kwangu uongofu, basi atakayeufuata uongofu Wangu huo hatapotea wala hatataabika] [Twaahaa: 123]

 

Sababu ya kuchagua Aayah hii kuwa ndio kielelezo cha Tovuti hii ya ALHIDAAYA ni kwamba, asili ya neno la ALHIDAAYA linatokana na neno ‘Hudaa’ au 'Al-Hudaa' yaani 'uongofu'. Na katika Aayah hii ya Suratut-Twaahaa utaliona neno ‘Hudaa’ ambalo ndilo asili ya neno ALHIDAAYA.

Vile vile maana ya Aayah hiyo ni kwamba: Yeyote atakayepokea na kukubali yale Aliyoyaleta Allaah سبحانه وتعالى katika Vitabu Vyake na Mitume Yake basi hatapotoka mtu katika maisha haya ya dunia na hatokuwa na dhiki katika maisha ya Aakhirah.

Na katika Aayah nyingine yenye  maana takriban kama hiyo,

 

((... فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَن تَبِعَ هُدَايَ فَلاَ خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلاَ هُمْ يَحْزَنُونَ))

(( .. na kama ukikufikieni uongofu utokao Kwangu, basi watakaofuata uongofu Wangu huo haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika)) [Al-Baqarah: 38]

Vile vile ina maana kwamba: Yeyote atakayekubali na kufuata yale Aliyoyaleta Allaah سبحانه وتعالى  katika Vitabu Vyake na Mitume Yake, hatokuwa na khofu ya Aakhirah na wala hatohuzunika katika maisha ya dunia. [Ibnu Kathiyr 1: 203]

 

Na uongofu huu ni uongofu wa mwisho kabisa Aliotuletea Allaah سبحانه وتعالى ambao haukuletwa kuwaongoza Waarabu pekee, bali  kuwaongoza binaadamu wote ulimwenguni. Nao maana yake ni Mtume wa mwisho  Muhammad صلى الله عليه و آله وسلم   na kitabu cha mwisho nacho ni Qur-aan. Navyo vyote tumeletewa kwetu kupitia mji wa Makkah ambako amezaliwa Mtume صلى الله عليه و آله وسلم na pia Qur-aan nayo ameteremshiwa mwanzo akiwa huko huko Makkah. Na ndio maana tumeweka hapo juu kwenye bango (banner) nembo ya Qur-aan na Ka'abah kuwa ni viwakilishi vya jina hilo la ALHIDAAYA; Qur-aan ndiyo yenyewe ALHIDAAYA na pia kwayo tunapata hidaaya, na Ka'abah ndiyo kielelezo cha eneo palipoanzia hidaaya ambayo hadi leo sisi ndiyo tunayoifuata
 

Na sisi kwa sababu tunahitaji sana huo ‘UONGOFU’ au ‘ALHIDAAYA’, ndio tumeonelea tuiite tovuti hii kwa jina hilo.  Na tunajaribu kwa kila hali kukusanya yote yale ambayo yatatusaidia kutufikisha, au kwa uchache kutuelekeza katika ‘HIDAAYA’ ambayo itatuokoa na Moto wa Jahannam na kutufikisha katika Jannah In Shaa Allaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

 

 

 

Rudi Juu