Mke Anayefanya Kazi Anatakiwa Atoe Masurufu Ya Nyumba?

 

SWALI:

Navyojua mume ni mtu msimamizi wa nyumba kutosheleza nyumba na mahitaji yake kama kodi, chakula na hali kadhalika je ikiwa mke ana kazi yake basi ana lazima ya kutoa nusu kodi na nusu chakula au vitu hivyo ni wajibu wa mume na mke akiwa atatoa basi mapenzi yake?? Maana natatanika sana kuwa nilazima ulipe!! Kama kuwajibika vile - naomba msaada wenu hapa.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muuliza swali. Bila shaka ni jambo linaloeleweka kuwa mume katika Uislamu anahitajika kumtimizia mkewe mahitaji ya msingi kama malazi, chakula, matibabu na mengineo. Hii ni kwa mujibu wa maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Aliyesema:

Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Allaah baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayoyatoa (4: 34).

Pia, “Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala baba kwa ajili ya mwanawe” (2: 233).

Mke na mwanamke kwa ujumla katika Uislamu amepatiwa haki ya kuweza kurithi au kuchuma chumo la halali. Kwa hilo Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

Wanaume wana sehemu katika wanayoyaacha wazazi na jamaa waliokaribia. Na wanawake wanayo sehemu katika waliyoyaacha wazazi na jamaa walio karibia. Ikiwa kidogo au kingi. Hizi ni sehemu zilizofaridhiwa” (4: 7).

Amesema tena (Subhaanahu wa Ta‘ala): “Wanaume wana fungu katika waliovichuma, na wanawake wana fungu katika waliovichuma. Na muombeni Allaah fadhila Zake. Hakika Allaah ni Mjuzi wa kila kitu” (4: 32).

Baada ya kupatiwa haki mwanamke ya kumiliki mali, hapo hapo amepatiwa uwezo wa kuitumia katika njia za wema kama kutoa Zakaah, sadaka, kusaidia miradi ya Kiislamu na mambo mengineyo. Hata hivyo, hawajibiki kutoa masrufu yoyote ya nyumbani hata akiwa yeye ni tajiri kuliko mumewe ila ikiwa ataridhika mwenyewe kufanya hivyo.

Ikiwa mke anaona mumewe ni dhaifu katika kipato na ni matatizo kutazama nyumba, mke kama huyo anaweza kumsaidia mumewe katika baadhi ya majukumu naye atapata ujira kwa hilo kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala). Tunapata mifano mingi katika maisha ya Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) ambao walikuwa wanasaidiwa na wake zao waliokuwa na uwezo zaidi wa kifedha. Mmoja wao ni ‘Abdullaah bin Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akisaidiwa na mkewe Zaynab (Radhiya Allaahu ‘anha).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share