Skip navigation.
Home kabah

Mwandamo Wa Mwezi – Waislamu Wote Duniani Wafunge Siku Moja Na Kula ‘Iyd Siku Moja ?

 

SWALI   

nilimskia sheikh mmoja katika kipindi cha televisheni moja Tanzania anasema kwamba haiwezekani watu wote duniani kupata sikukuu siku moja kwa sababu kuna nchi zimepishana kwa takribani masaa 24,na kutoa mfano kwamba,Honolulu Marekani jumamosi saa 3 asubuhi, New Zealand ni saa 2 asubuhi Ijumaa. je hii ni kweli na kweli inawezekana ikawa ni sababu ya kutowezekana kufunga na kufungua siku moja dunia nzima??

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Ni kweli kuwa zipo sehemu ambazo zimetofautiana kwa masaa takriban 23 kama ulivyosikia   lakini huyo shekhe kachanganya baina ya sehemu. Jua linachomoza Wellington, New Zealand mwanzo kabla ya HawaiiHonolulu, USA, yaani ikiwa New Zealand ni saa mbili siku ya Ijumaa, Honolulu itakuwa Alkhamisi saa tatu asubuhi. Hata hivyo tofauti hiyo si sababu kabisa kwa Waislamu duniani kutofunga na kutofungua pamoja.

Ni hakika isiyopingika kabisa kuwa kuanzia wakati ambao mawasiliano yamekuwa ni sahali kupatikana kote duniani mwezi umekuwa ukionekana Mashariki ya kati. Na kwa sasa kama katika nchi ya Tanzania na Kenya baada ya Waislamu kuchukua umuhimu mkubwa wa kuangalia mwezi ukawa mwandamo wa sehemu hii unakwenda sambamba na ule wa Mashariki ya Kati. Tufahamu kuwa tofauti baina ya sehemu hiyo na sehemu za Mashariki na magharibi ya ulimwengu haizidi masaa 12. Hakika mazungumzo hayo ni watu tu kutafuta vizisababu visivyokuwa na msingi wowote wa kidini.

Ni ajabu kuwa mashekhe hao wamejikita kuzungumza kuhusu mwezi wa kimataifa pekee wala huwasikii kuzungumza matatizo ya rai kama:

  1. Kuzingatia mipaka ya kila nchi.
  2. Kuzingatia umbali wa farsakh 24.
  3. Kuzingatia masafa ya qasri.
  4. Kuzingatia tofauti za matlai.
  5. Kuzingatia usawa wa bahari (sea level).
  6. Kuzingatia maeneo ya mashariki na magharibi.
  7. Kuzingatia kusadifu.

Kila moja katika hizo ni rai ya wanazuoni kuhusu kufuatwa kwa mwezi lakini rai kama hizi huwa tunafichwa. Hata inapozungumziwa rai ya mwandamo wa kitaifa huwa haiwekwi katika mizani kupimwa kama inavyopimwa rai ya kimataifa. Hakika inaonekana wazi kuwa ushabiki ni mkubwa zaidi kuliko kutafuta haki na ukweli. Ndio Waswahili wana msemo: “Kila mwamba ngoma huvutia upandewe”. Lakini msemo huu haufai kuingia katika miono ya Mashaykh ambao vipimo vyao vinatakiwa viwe ni kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah sahihi.

Swali la kujiuliza kila Muislamu kwa kirahisi kabisa: “Je, katika ulimwengu wetu huu tuna miezi (wingi wa mwezi - moon) mingapi?”

Na Allaah Anajua zaidi