Ugali Kwa Mchuzi Wa Nyama, Mchicha, Maharage Na Chatini Ya Pilipili Mbichi

Vipimo Vya Mchuzi Wa Nyama
Nyama ya ng’ombe vipande vidogo - 2lb
Nyanya - 1
Kitunguu Kilichoktwa katwa - 1
Mafuta - 2 vijiko vya supu
Paprika (bizari ya masala ya rangi) - ½ kijiko cha chai
Kidonge cha supu - 1
Chumvi - Kiasi
Ndimu - Kiasi
Namna Ya Kutayarisha Na Kupika
- Osha nyama kwa chungio ili itoke maji. Kwenye sufuria, weka mafuta na ukaange vitunguu mpaka viwerangi ya hudhurungi.
- Kisha tia nyama na kidonge cha supu uwachie moto mdogo mpaka iwive.
- Halafu tia nyanya na paprika ufunike sufuria na uiwache motoni mpaka ikauke, kamulia ndimu na itakuwa tayari.
Vipimo Vya Mboga
Mchicha ulio katwa katwa 400 gm
Nyanya 1
Kitunguu kilicho katwa 1
Nazi ya unga kiasi
Pilipili mbichi 2
Mafuta ½ kijiko cha supu
Chumvi kiasi
Namna Ya Kutayarisha na Kupika
- Osha mboga vizuri mpaka iwe haina mchanga.
- Katika sufuria, kaanga vitungu hadi viwe laini.
- Tia nyanya, mboga, pilipili na chumvi ikisha toa maji
- Tia nazi na utaiwacha motoni mpaka ikauke kiasi na itakuwa
- tayari kuliwa
Vipimo Vya Maharage
Maharage - 1 kopo
Kitunguu - 1
Nazi - 1 mug
Nyanya (itowe maganda) - 1 kiasi
Pilipili mbichi - 2
Mafuta - 1 kijiko cha supu
Chumvi - kiasi
Namna Ya Kutayarisha Na kupika
- Tia mafuta katika sufuria na ukaanga vitungu mpaka vilainike.
- kisha tia nyanya na pilipili na ukaange kidogo.
- Tia chumvi, maharage na nazi uwachie
- moto mdogo mpaka iwe nzito kiasi na itakuwa tayari.
Vipimo Vya chatini Ya Pilipili mbichi
Pilipili mbichi - 4/5
Kotmiri - 1 Kijiko cha supu
Ndimu - kiasi
Kitunguu saumu(thomu/galic) - 1 chembe
Mafuta ya zaituni - 2 vijiko Vya supu
Chumvi - kiasi
Namna Ya Kutayarisha
- Kwenye blender, tia vipimo vyote na sage isipokuwa chumvi tia mwisho kwa juu kwenye bakuli na itakuwa tayari kwa kuliwa.
Vipimo Vya ugali
Maji - 4 Vikombe kiasi inategemea na unga
Unga wa sembe - 2 vikombe
Namna Ya Kutayarisha Na Kupika
- Tia maji kiasi katika sufuria, weka motoni, yakipata moto korogea unga wa sembe kiasi na ufanye uji mzito uache uchemke vizuri huku ukikoroga.
- Chota kibakuli kimoja cha uji huo weka pembeni kisha mimina unga wote uliobaki upigepige uchanganyike vizuri kwenye uji huo mpaka ushikamane
- Punguza moto anza kuusonga taratibu huku ukiongeza ule uji ulioweka pembeni kidogo kidogo mpaka uone sasa umeshikamana vizuri.
- Endelea kusonga mpaka ulainike kisha mimina kwenye bakuli au sahani na itakuwa tayari kwa kuliwa na mchuzi wa nyama, maharage, mboga na chatini.