Swalah Ya Shuruuq Ni Sawa Na Swalah ya Dhwuhaa?

SWALI:

Assalam alaykum

ukiwa umeamka usiku kwa ajili ya swala za usiku hukurudi kulala tena mpaka ukaswali swalul-fajri naukawa pia hukurudi tena kulala ukaendelea na adhkar za asubuhi mpaka jua likatoka baada ya dakika kumi au ishirini ukaswali rakaa mbili hizi zinakua kama uliyefa umra kwa kauli ya mtume s.a.w. swali ni hili kisha kwa baadaye unaweza kuswali tena kwa ajili swala dhuha


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza tunapenda kukumbusha ndugu yetu, kuacha kufupisha kumsalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na ujizoeze kuandika kwa kirefu ili usikose fadhila za kumswalia Mtume wako (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kikamilifu na vilevile kufanya hivyo ni kumtukuza na kumuadhimisha na kumpa heshima zaidi.

Tunashukuru kwa Swali lako hili ambalo wengi wanaulizia kuhusu hii Swalah iliyopewa jina la Swalaatush-Shuruuq au Swalaatul-Ishraaq (Swalah baada ya kuchomoza jua).

 

Kutokana na fadhila zake kwamba:

((عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم ، أنه قال : من صلى الفجر في جماعة ثم قعد يذكر الله   حتى تطلع الشمس ثم صلى ركعتين كانت له كأجر حجة وعمرة تامة تامة تامة)) أخرج الترمذي  صححه الألباني

.

“Imetoka kwa Anas kwamba Mtume ((Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, Atakayeswali Alfajiri katika Jama'ah kisha akakaa anamkumbuka Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy]

 

Inavyopaswa ni kukaa baada Swalah ya Alfajiri hadi jua litoke na upite wakati wa makruuh (unaochukiza kuswali) yaani wakati pale jua linapochomoza hasa, usubiri kama takriban dakika kumi na tano hadi ishirini hivi ndio uswali rakaa mbili. Ndio maana ikaitwa Swalaatush-Shuruuq, lakini asili yake hiyo ni Swalaatudh-Dwhuhaa na hakuna katika shari’ah Swalah kwa jina hilo kwani Swalah hizi hazina tofauti baina yao katika kuswaliwa isipokuwa Swalaatul-Ishraaq inaswaliwa mapema zaidi lakini ndio hiyo hiyo Swalaatudh-Dhwuhaa inayoswaliwa mwanzoni mwa wakati wake.

Na fadhila za Swalah hiyo ya Adhw-Dhwuhaa, ambayo inajulikana kama Swalaatul-Ishraaq au Shuruuq kwa kuswaliwa kwake mwanzo wa wakati wake, ni hizi: 

عـَن أبي ذَرٍّ رضي الله ُ عنه ، عن النـَبي ِّ صلـَّى الله عليه وسلم قال: ((يـُصـْبـِحُ عـَلى كـُلِّ سـُلامى مـِنْ أحـَدِكـُمْ صـَدَقةُ: فـَكُل تـَسْبـِيحـَةِ صـَدَقةٌ ،وَ كُل تـَحمِيدة صـَدَقةٌ ، وكُلُ تـَهْـليْلةٌ صـَدَقـَةٌ، وكُلُّ تـَكْبِيْرةِ صـَدقةٌ ، وأمرٌ بالمـَعرُوف صـَدقةٌ ، ونـَهىٌ عـَنِ المـُنْكرِ صـَدقةٌ ويـُجْزئ مـِنْ ذلكَ رَكـْعتـَانِ يـَركَعُهُما مـنَ الضـُّحى))  رواه مسلم

Kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) amesema: “Kila kiungo katika mwili wenu hupambaukiwa kikiwa na sadaka, kwa hiyo kila tasbiyh (kusema ‘Subhaana Allaah’) ni sadaka na kila tahmiyd (kusema ‘AlhamduliLlaah’) ni sadaka na kila tahliyl (kusema ‘La Ilaaha Illa Allaah’) ni sadaka  na kila takbiyr (kusema ‘Allaahu Akbar’) ni sadaka na kuamrisha mema ni sadaka na kukataza maovu ni sadaka na itamtosheleza (Mtu) kwa Rakaa mbili za Dhwuhaa.” [Muslim]

Vile vile kuna masimulizi yanayonyesha kuwa Swalaatudhw-Dhwuhaa inatakiwa iswaliwe wakati jua limeshakuwa kali nayo kutokana na Hadiyth ifuatayo:

عَنْ زَيْدِ بْنِ أَرْقَمَ قَالَ خَرَجَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَلَى أَهْلِ قُبَاءَ وَهُمْ يُصَلُّونَ فَقَالَ” : صَلاةُ الأَوَّابِينَ إِذَا رَمِضَتْ الْفِصَالُ  رواه مسم

Kutoka kwa Zayd bin Arqam amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka akawaona watu wa Qubaa wanaswali akasema: “Swalah ya Al-Awwaabiyn ni wakati ngamia wachanga wananyanyua miguu yako.” [Muslim]. (Imeitwa Swalah ya Al-Awwaabiyn kwa sababu ya umoto wa mchanga uliopigwa na jua kali).

 

Kwa hiyo ni bora kwa mwenye kupenda kuswali Swalaatudhw-Dhwuhaa aiswali wakati jua limekuwa kali wakati wowote hadi takriban nusu saa kabla ya Swalah ya Adhuhuri. Na ikiwa amekaa mtu baada ya Swalah ya Alfajiri hadi kuchomoza jua akimdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ili apate fadhila za Hajj na 'Umrah, anaweza kuswali kwanza rakaa zake mbili baada ya jua kuchomoza, kisha tena aongezee rakaa mbili, au nne au sita nyingine za Swalah hiyo ya Adhw-Dhwuhaa apendavyo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share