Kurtadi (Kutoka Katika Dini)

 

Kurtadi (kutoka Katika Dini)

 

Imetarjumiwa na Muhammad Faraj Saalim As-Saiy (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

  

Swali:

 

'Je hii hukmu ya kuuwawa kwa murtadi si katika kulazimishana katika Dini?'

 

Jawabu:

Allaah Anasema:

 

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ ۚ فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٥٦﴾

Hapana kulazimisha katika Dini, kwani imekwishabainika kati ya uongofu na upotofu. Basi atakayemkanusha twaghuti na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika, na Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote   [Al Baqarah: 256]

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Atakayebadilisha Dini yake muuweni."  [Al-Bukhaariy]

 

Na akasema:

 

"Si halali (kumwaga) damu ya Muislamu isipokuwa kwa matatu; Nafsi kwa nafsi (Aliyeua auwawe), na mzinzi 'thayyib' (aliyekwishaoa au kuolewa) na aliyeacha Dini akafarikiana na kundi." [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Hapana mgongano wowote baina ya hukmu mbili hizi. Ya mwanzo ni juu ya asiyekuwa Muislamu.  Huyu akitaka kubaki katika Dini yake ya Ukristo au Uyahudi au Dini yoyote ile, anao uhuru kamili wa kubaki huko, na haijuzu kumlazimsha kuiacha Dini yake.

 

Ama hukmu ya pili ni juu ya jambo jingine kabisa. Ni juu ya yule uliyekwishambainikia ukweli, akamjua Allaah, akaikubali hidaya Yake, kisha akaamua kwa hiari yake mwenyewe kuingia katika Dini ya Kiislamu bila kulazimishwa.

 

 

Atakayeamua kusilimu kwa hiari yake mwenyewe, hatakiwi kufanya kufru tena. Haiwezekani mtu leo aseme mimi ni Muislamu, kisha aanze kumtukana Allaah kuwa amefanya makosa au dhulma n.k. Au amtukane Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au Swahaba zake (Radhwiya Allaahu anhum) au Wake zake (Radhwiya Allaahu anhunna), au aseme: “Mimi sioni kama Swalaah ina umuhimu wowote” au aitie ila yoyote Dini. Au afanye jambo lolote litakaloingiza shaka ndani ya nafsi dhaifu. Huyu anakuwa hajaingia katika Dini isipokuwa kwa ajili ya kuwababisha watu. Huyu ni mzizi mbaya unaotaka kuleta fitna katika Dini na lazima ung'olewe.

 

 

Na hii ndiyo maana mtu atakayetoka katika Dini. Akinyamaza kimya asiseme kitu, hawezi kuhukumiwa kama ni murtadi. Na hii ni kwa sababu Waislamu hawatakiwi kufuatilia na kuchunguza aibu au matendo ya watu yaliyotendwa kwa kujisitiri au kwa kujificha. Bali wanahesabiwa kwa matendo yaliyofanywa kwa jahara tena pawe na ushahidi usio na shaka kuwa mtu huyo anajuwa analotenda na alilikusudia.

 

 

Kwa hivyo mwenye kurtadi kisha akatamka jahara mbele ya watu, anakuwa keshatangaza vita dhidi ya Uislamu, na anakuwa keshainyanyua bendera ya upotovu, na kwa ajili hiyo kisheria mtu huyo lazima apigwe vita kwa sababu anahesabiwa kuwa ni mwenye kuipiga vita Dini, na Uislamu haukubali kugeuzwa mchezo, leo mtu anaingia na kesho anatoka.

 

Allaah Anasema:

 

وَقَالَت طَّائِفَةٌ مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ آمِنُوا بِالَّذِي أُنزِلَ عَلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَجْهَ النَّهَارِ وَاكْفُرُوا آخِرَهُ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٧٢﴾

Na kundi miongoni mwa Ahlil-Kitaabi likasema (kuambiana): “Aminini yale ambayo yameteremshwa kwa wale walioamini mwanzo wa mchana na kanusheni mwisho wake, wapate kurejea (waache dini yao).”   [Aal-‘Imraan: 72]

 

 

Ufafanuzi wa Aayah hii:

 

"Miongoni mwa vitimbi walivyokuwa wakifanya Mayahudi na Manasara ili kuwababaisha watu na Dini ya haki  ya Uislamu. Ni kuwaamrisha baadhi yao kwenda kusilimu kisha kurejea katika Dini yao ili wawatie wasiwasi na wahka wale Waislamu wa kweli waone kuwa labda si Dini ya haki hii. Mbona wameingia mahodari wale kisha wakatoka?

 

 

 

Nani Murtadi?

 

Allaah Anasema:

 

وَلَا يَزَالُونَ يُقَاتِلُونَكُمْ حَتَّىٰ يَرُدُّوكُمْ عَن دِينِكُمْ إِنِ اسْتَطَاعُوا ۚ وَمَن يَرْتَدِدْ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَيَمُتْ وَهُوَ كَافِرٌ فَأُولَـٰئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۖ وَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢١٧﴾

Na wala hawatoacha kukupigeni vita mpaka wakutoeni katika Dini yenu wakiweza. Na atakayeritadi miongoni mwenu kutoka Dini yake, akafariki hali ya kuwa ni kafiri, basi hao zimeporomoka ‘amali zao katika dunia na Aakhirah. Na hao ni watu wa motoni, wao humo ni wenye kudumu.  [Al – Baqarah: 217]

 

 

"Murtadi" ni yule aliyeiacha Dini ya Kiislamu akiwa na akili timamu, bila kulazimishwa na mtu akaingia katika Dini nyingine kama vile Ukristo au Dini ya Kiyahudi au kutokuwa na Dini kama vile Ukoministi, au akakanusha jambo lolote lijulikanalo kama ni la lazima katika Dini kama vile kuwajibika Kuswali, kutoa Zakaah au akafanya jambo dhidi ya Uislamu au dhidi ya sheria zake zilizo dhahiri au akatamka kauli ambayo haina tafsiri nyengine isipokuwa kukufuru.

 

 

Kurtadi kwa itikadi:

 

-Mwenye kumshirikisha Allaah au kumpinga au akakanusha moja wapo katika sifa Zake zilizothibiti. Ikijulikana wazi kuwa mtu huyo bila shaka anazielewa vizuri sifa hizo. Au amsingizie Allaah jambo ambalo Yeye mwenyewe amelikanusha; mfano; kuwa na mtoto, au kukanusha kuwepo kwa Malaika au Vitabu au Manabii au kuikanusha Siku ya Qiyaamah au Qadar kheri yake na shari yake au akatae jambo lolote linalojulikana kuwa ni la lazima katika Dini,  basi mtu huyu huwa ni Murtadi, aliyetoka katika Dini.

 

 

-Inajulikana pia kuwa anahesabika murtadi, Muislamu yeyote anayeipinga au kuikanusha Qur-aan yote, au sehemu yoyote ya Qur-aan au hata Aayh moja katika Aayah za Qur-aan.

 

-Huhesabiwa kuwa amertadi pia, mwenye itikadi kwamba Qur-aan inakhitalifiana yenyewe kwa yenyewe au ina khitilafu ndani yake, au mwenye kuwa na shaka katika miujiza yake au kujigamba kuwa ana uwezo wa kuleta mfano wake, na pia mwenye kuivunjia heshima, au kuongeza au kupunguza ndani yake.

 

-Anahesabiwa kuwa amertadi mwenye kuitakidi kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema uongo katika baadhi ya aliyokuja nayo, na pia yule anayeitakidi kuwa ni halali jambo lolote liloharamishwa kama vile kuzini kunywa pombe n.k.

 

 

Kurtadi kwa matamshi:

 

Kuapa kwa mila nyengine isiyokuwa ya Kiislamu.

 

 Ameelezea Thabit bin Dhwahaak kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Atakaekula kiapo kwa mila isiyokuwa ya Kiislamu anakuwa kama alivyosema". [Abuu Daawuwd]

 

Mfano wake ni baadhi ya watu wanaopenda kuwaiga wasio waislamu katika kula kiapo akasema; ‘Yesu kristo’ au kwa lugha yoyote ile, viapo vya aina hiyo..

 

Na kutoka kwa Buraydah (Radhwiya Allaahu anhu) ameeleza kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Atakayesema “Mimi si Muislamu” ikiwa anasema uongo basi kama alivyosema, na ikiwa anasema kweli basi hatorudi katika Uislamu akiwa amesalimika". Abuu Daawuwd , An-Nasaaiy,  Ibn Maajah]

 

 

-Atakayemtukana Allaah au Qur-aan au akamtukana Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au moja wapo kati ya Manabii wa Allaah, anakuwa amertadi hata kama ametamka hayo kwa mzaha au kweli au kwa istihizai.

 

Allaah Anasema:

 

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ﴿٦٥﴾

Na ukiwauliza, bila shaka watasema: “Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza.” Sema: “Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayaat Zake na Rasuli Wake?”

 

لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ ۚ إِن نَّعْفُ عَن طَائِفَةٍ مِّنكُمْ نُعَذِّبْ طَائِفَةً بِأَنَّهُمْ كَانُوا مُجْرِمِينَ﴿٦٦﴾

Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.  [At-Tawbah - 65 – 66]

 

‘Ulamaa  wote wamekubaliana kuwa mwenye kumsingizia uongo Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anha) katika kile kisa cha uongo alichozuliwa (Tukio la "Al-Ifki") na ilihali Allaah keshaukanusha uongo huo kisha akamtakasa, basi anakuwa si Muislamu tena.

 

Allaah Anasema:

 

إِنَّ الَّذِينَ جَاءُوا بِالْإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ ۚ لَا تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم ۖ بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۚ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُم مَّا اكْتَسَبَ مِنَ الْإِثْمِ ۚ وَالَّذِي تَوَلَّىٰ كِبْرَهُ مِنْهُمْ لَهُ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١١﴾

Hakika wale walioleta singizo la kashfa; (kumzulia mama wa waumini ‘Aaishah  رضي الله عنها) ni kundi miongoni mwenu. Msiichukulie kuwa ni shari kwenu, bali ni khayr kwenu.  Kila mtu katika wao atapata yale aliyochuma katika dhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kuu.

 

 

لَّوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَـٰذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ ﴿١٢﴾

Kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa), Waumini wanaume na Waumini wanawake wasiwadhanie wenzao khayr, na wakasema: “Hii ni kashfa ya kusingizwa iliyo dhahiri?”

 

 

لَّوْلَا جَاءُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ ۚ فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاءِ فَأُولَـٰئِكَ عِندَ اللَّـهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ ﴿١٣﴾

Kwa nini hawakuleta mashahidi wanne? Na kwa vile hawakuleta mashahidi, basi hao mbele ya Allaah ndio waongo.

 

 

وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ لَمَسَّكُمْ فِي مَا أَفَضْتُمْ فِيهِ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١٤﴾

Na lau si fadhila ya Allaah juu yenu na rahmah Yake duniani na Aakhirah, bila shaka ingekuguseni adhabu kuu kwa yale mliyojishughulisha nayo kuyaropoka,

 

 

 

إِذْ تَلَقَّوْنَهُ بِأَلْسِنَتِكُمْ وَتَقُولُونَ بِأَفْوَاهِكُم مَّا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّنًا وَهُوَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمٌ ﴿١٥﴾

Mlipoipokea (kashfa ya uzushi) kwa ndimi zenu, na mkasema kwa midomo yenu, yale ambayo hamkuwa na elimu nayo; na mnalidhania ni jambo jepesi; na hali hili mbele ya Allaah ni kubwa mno.

 

 

وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَـٰذَا سُبْحَانَكَ هَـٰذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ ﴿١٦﴾

Na kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa) msiseme: “Haitupasi sisi tuzungumze haya; Subhaanak! Utakasifu ni Wako huu ni usingiziaji wa dhulma mkubwa mno!”

 

 

يَعِظُكُمُ اللَّـهُ أَن تَعُودُوا لِمِثْلِهِ أَبَدًا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٧﴾

Allaah Anakuwaidhini msirudie abadani mfano wa haya, mkiwa ni Waumini wa kweli.  [An-Nuwr: 11-17]

 

Kwa hivyo atakaerudia kueneza uongo huo hatakuwa Muislamu tena.

 

 

 

Kuitukana Dini:

 

 

Yeyote atakayeituhumu kuishambulia au kuitukana Dini ya Allaah au kuwataka watu wafuatae siasa ya kutoamini Allaah au kuwataka wakufuru basi anakuwa Murtadi.

 

Allaah Anasema:

 

وَإِن نَّكَثُوا أَيْمَانَهُم مِّن بَعْدِ عَهْدِهِمْ وَطَعَنُوا فِي دِينِكُمْ فَقَاتِلُوا أَئِمَّةَ الْكُفْرِ ۙ إِنَّهُمْ لَا أَيْمَانَ لَهُمْ لَعَلَّهُمْ يَنتَهُونَ﴿١٢﴾

Na wakivunja viapo vyao baada ya ahadi yao, na wakatukana Dini yenu, basi wapigeni vita viongozi wa ukafiri. Hakika viapo vyao havina maana. (Piganeni nao) ili wapate kukoma. [At-Tawbah: 12]

 

 

Kurtadi kwa matendo:

 

-‘Ulamaa wote wa Kiislamu wamekubaliana kuwa; amefanya kitendo cha kurtadi Muislamu yeyote atakayeutupa Mswahafu mahala panapotupwa taka, au kuuchafua (kwa kukusudia) kwa kuumwagia taka, na pia kuvifanyia hivyo vitabu vya Hadiyth za Al-Qudsiy au vya Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na pia atakayeufanyia dharau Mswahafu.

 

 

Allaah Anasema:

 

 وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ﴿٦٥﴾

Na ukiwauliza, bila shaka watasema: “Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza.” Sema: “Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayaat Zake na Rasuli Wake?”

 

 

لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ ۚ إِن نَّعْفُ عَن طَائِفَةٍ مِّنكُمْ نُعَذِّبْ طَائِفَةً بِأَنَّهُمْ كَانُوا مُجْرِمِينَ﴿٦٦﴾

Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.  [At-Tawbah - 65 – 66]

 

 

-Wamekubaliana ‘Ulamaa kwamba Muislamu yeyote akilisujudia sanamu, jua au mwezi, au akasema neno au kufanya kitendo kinachoonyesha wazi kuwa kaifanyia istihizai Dini, basi anakuwa ametoka katika Dini ‘Amertadi’.

 

-Muislamu yeyote atakayekimbilia nchi ya makafiri wanaowapiga vita Waislamu na akaungana nao katika kupigana vita hivyo dhidi ya Waislamu, basi kesha kuwa kafiri, na hii ni kutokana na kauli ya Allaah isemayo:

 

   وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿٥١﴾

Na yeyote atakayewafanya marafiki wao wandani; basi hakika yeye ni miongoni mwao. Hakika Allaah Haongoi watu madhalimu. [Al-Maaidah: 51]

 

-Muislamu yeyote atakayeipiga vita Shariy’ah ya Kiislamu akaibadilisha kwa kanuni za wanaadamu kwa niyyah ya kuizuia Shariy’ah ya Kiislamu isitumike, basi amekuwa kafiri.

 

Allaah Anasema:

  وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ ﴿٤٤﴾

  Na yeyote asiyehukumu kwa yale Aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio makafiri.  [Al-Maaidah: 44]

 

 

 

Hukmu ya mwenye kurtadi:

 

 

Kutokana na dalili zilizotangulia tunafahamu kuwa mwenye kurtadi akiwa na akili timamu, damu yake inakuwa halali, na hukmu ya kuuliwa inatolewa na Imaam mwenye kuwahukumu Waislamu au msaidizi wake kama vile Qaadhi, na haoshwi, hasaliwi wala hazikwi katika makaburi ya Waislamu. 

 

Hauliwi hapo hapo, bali kwanza hutubishwa na kuonyeshwa dalili mbali mbali kuwa kitendo chake hicho kinamtoa katika Dini, hasa kwa vile huenda kitendo chake hicho au kauli aliyotamka ilikuwa kwa kukisia tu au kwa jitihada akidhani kuwa ndiyo haki inayofaa kufuatwa. Akaiendelea kuishikilia kufru yake hiyo akakataa kuifuata haki, ndipo hukmu inapotendeka.

 

Anasema Ibn Qudaamah (Allaah amrehemu) katika Al Mughniy:

"Mwenye kurtadi hauliwi mpaka Qadhi amtubishe muda wa siku tatu. Na hii ndiyo kauli ya ‘Ulamaa wengi akiwemo ‘Umar na Ali na Atwaa na Al Nakhaiy na Imaam Maalik na Ath-Thawry na Al-Awza'iy na Is-haaq na wengi kati ya ‘Ulamaa wenye rai, kwa sababu kurtadi kwake huenda kukawa kwa dhana na dhana kwa kawaida haiondoki mara moja. Kwa ajili hiyo inawajibika kusubiri muda mrefu ili apate wakati wa kutosha kujirudi na kuitambua haki."

 

 

 

Vipi aliyertadi anaweza kurudi katika Uislamu?

 

Aliyertadi anaweza kurudi katika Uislamu kwa kutamka shahada mbili :

 

اَشهَدُ اَن لاَ اِلَهَ اِلاّ الله وَاَشهَدُ اَنَّ مَحَمّدً رَسُولُ الله

"Ash-hadu an laa ilaaha illa Allaah wa Ash-hadu anna Muhammadan Rasuwlu-Allaah."

 

Ni ikiwa kurtadi kwake kunatokana na kupinga jambo linalojulikana kuwa ni la dharura katika Dini, hakubaliwi mpaka kwanza akiri makosa yake na alikubali jambo hilo."

 

Wa-Allaahu Ta'alaa A'lam

 

 

Share