Uzito Wa Thawabu Za Kutoa Mali Yako Kwa Ajili Ya Allaah سبحانه وتعالى

Anasema Allaah سبحانه وتعالى:

((مَّثَلُ الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللّهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنبَتَتْ سَبْعَ سَنَابِلَ فِي كُلِّ سُنبُلَةٍ مِّئَةُ حَبَّةٍ وَاللّهُ يُضَاعِفُ لِمَن يَشَاءُ وَاللّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ))

((Mfano wa wanaotumia mali zao katika njia ya Allaah ni kama mfano wa punje moja iliyochipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Na Allaah Humzidishia Amtakaye, na Allaah ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua)) [Al-Baqarah: 261]

.

Hivyo tunaona kwamba kila unapotoa mali yako Allaah سبحانه وتعالى   Hukuzidishia hiyo mali. Mfano huo Alioutoa Allaah سبحانه وتعالى  katika Aayah hiyo inatupa hesabu ifuatayo:

Punje moja imechipuza mashuke saba            1 x 7=7

Katika kila shuke moja zimo punje mia            7 x 100=700

Kwa hiyo jumla ya kuzidishiwa ni mia saba. 

Na hali kadhalika mafundisho haya yapo katika Sunnah ya Mtume wetu  صلى الله عليه وآله وسلم:

Mtu mmoja alimleta ngamia wake pamoja na hatamu yake   kwa ajili ya Allaah سبحانه وتعالى na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema:

((لك بها يوم القيامة سبعمائة ناقة)) مسلم والنسائي

((Kwa huyo ngamia uliyemtoa, utalipwa ngamia mia saba Siku ya Qiyaamah))  [Muslim na An-Nasaaiy]

.

Hadiyth nyingine:

 عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((كل عمل ابن آدم يضاعف، الحسنة بعشر أمثالها إلى سبعمائة ضعف، إلى ما شاء الله)) أحمد

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه amesema: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Kila ‘amali njema ya mwanaadamu inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi mia saba hadi Atakavyo Allaah…)). [Ahmad].

Na hii ndio maana Anasema Allaah سبحانه وتعالى katika Aayah nyingine kuwa mtu anapotoa mali yake kwa ajili Yake ni kama mfano amemkopesha Allaah سبحانه وتعالى mkopo mzuri ambao malipo yake ni kuzidishiwa zaidi ya hiyo mali aliyoitoa,  kisha juu yake ni kupata ujira mwema kutoka kwa Mola wake Mtukufu. Ni muhimu kujua kuwa Yeye Mwenyewe Allaah سبحانه وتعالى Ndiye Anayeturuzuku hiyo mali, kisha Anatutaka tumkopeshe katika hicho alichotupa ili Atulipe zaidi ya Aliyoturuzuku kabla. Basi nani atakayesita kutoa mkopo kumkopesha Mola wake kwa kutegemea malipo kama hayo?

Anasema Allaah سبحانه وتعالى:  

((مَن ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللَّهَ قَرْضاً حَسَناً فَيُضَاعِفَهُ لَهُ وَلَهُ أَجْرٌ كَرِيمٌ))

 ((Ni nani atakayemkopesha Allaah mkopo mwema, ili Amrudishie maradufu, na apate malipo ya ukarimu)) [Al-Hadiyd: 11]

Kutoa mali kwa fiy Sabili-Allaah ni jambo lenye kutaka kuazimiwa kikweli kwani hakuna asiyependa kumiliki mali. Na wakati wa kutoa mali shaytwaan husimama haraka kumtia wasiwasi binaadamu asitoe mali yake. Unapofika wakati huo basi ndugu Muislamu kumbuka kuwa thawabu zake ni nyingi mno na nzito mbele ya Allaah na ndio maana tunaona kwamba Allaah سبحانه وتعالى Ametanguliza mali kabla ya nafsi katika kuhimiza kufanya jihaad fiy Sabiyli-Allaah:

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَى تِجَارَةٍ تُنجِيكُم مِّنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ))

((تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَتُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ))

((يَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَيُدْخِلْكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ))

 

((Enyi mlioamini! Nikuonyesheni biashara itakayokuokoeni na adhabu iliyo chungu?))

 

((Muaminini Allaah na Mtume Wake, na piganeni Jihaad katika Njia ya Allaah kwa mali yenu na nafsi zenu. Haya ni bora kwenu, ikiwa nyinyi mnajua))

 

((Atakusameheni dhambi zenu, na Atakutieni katika Mabustani yapitiwayo na mito kati yake, na maskani nzuri nzuri katika Bustani za milele. Huko ndio kufuzu kukubwa)) [Asw-Swaff:  10-12]

.

 

Vile vile:

 

 

((إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ أُوْلَئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ))

 

((Hakika Waumini ni wale walio muamini Allaah na Mtume Wake tena wasitie shaka kabisa, na wakapigana Jihaad katika Njia ya Allaah kwa maliyao na nafsi zao. Hao ndio wakweli)) [Al-Hujuraat: 15].

 

Kama tunavyoona katika Aayah hizo za juu kwamba Allaah Anatupa nguvu kutoa mali fiy Sabili-Allaah kwa kutuhakikishia kuwa kutoa ni kufanya biashara Naye ambayo matokeo yake ni kupata faida nyingi na juu ya hivyo ni kupata maghfira kutoka Kwake:

 

((إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ))

((لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُور))

((Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Allaah na wakasimamisha Swalah, na wakatoa kwa siri na kwa dhaahiri katika Tulivyowaruzuku, hao hutaraji biashara isiyododa [isiyoanguka]))

((Ili Yeye Awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na Awazidishie kutokana na fadhila Zake. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye shukrani)) [Faatwir: 29-30]

.

 

 

Share