Ufafanuzi wa Aayah 'Oeni Wawili…'

SWALI:

Naomba kuuliza suala moja. Katika suala la ndoa Allaah (S.W) ameanza kwa kusema oeni wawili,........ Sasa kwa aya hii kuna taawili gani kwa kuanzia wawili na mujibu wa qurani hisabu huanza na moja lakini hapa moja imekuja mwisho, Jee hii ya wawili inawiana na ile ya mirathi ambayo mwanamme hupata mara mbili ya mwanamke? Nadhani nitafahamika. Ahasante

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Aayah uliyoitaja ya kuoa wake wengi. Qur-aan kwa hakika ina mtindo wake wa pekee katika mambo tofauti. Si lazima kuwa Qur-aan katika mas-ala ya hesabu ianze moja kwani zipo Aayah nyingine ambazo pia hazikuanza hesabu na moja. Mfano mzuri ni Aayah ifuatayo:

Sifa zote njema ni za Allaah, Muumba wa mbingu na ardhi, Aliyewafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa, mbili-mbili, na tatu-tatu, na nne-nne. Huzidisha katika kuumba Apendavyo” (35: 1).

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) haulizwi kwa Afanyalo bali sisi ndio tutakaoulizwa kwa yale tuliyoyafanya hapa duniani mema au mabaya. Hakika ni kuwa hesabu hii na ile ya mirathi ni vitu viwili tofauti kabisa. Maelezo ambayo tunaweza kuyatoa ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) ndiye Muumba na ndiye mjuzi wa maumbile ya mwanaadamu. Maumbile ya mwanadamu (mwanamme) ni kutotosheka na mke mmoja na hivyo Akaanza na agizo la oeni katika muwapendao wawili, au watatu, au wanne. Hili la kuoa mmoja limekuja mwisho kwa wale ambao hawataweza kufanya uadilifu baina ya wake wengi. Kwa hivyo asli ya mwanamme ni kuwa na wake wengi na udhru wa mmoja ni kutoweza kuwa na wengi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 
Share