Skip navigation.
Home kabah

Haki Za Mume Na Mke

 

 

Ummu Iyyaad

 

Mwanamume na mwanamke wanapofunga ndoa inawapasa wote watambue desturi, mwendo mwema na adabu katika maisha hayo ya mke na mume  ili ndoa yao iwe katika mipaka ya sharia ya dini yao. Zifuatazo ni haki za baina ya mume na mke kama ilivyo katika Qur'aan na Sunna.

Allaah سبحانه وتعالى   anasema:

((وَلَهُنَّ مِثْلُ الَّذِي عَلَيْهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ وَلِلرِّجَالِ عَلَيْهِنَّ دَرَجَةٌ وَاللّهُ عَزِيزٌ حَكُيمٌ))

{Nao wanawake wanayo haki kwa Sharia kama ile haki iliyo juu yao. Na wanaume wana daraja zaidi kuliko wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima}  (Al-Baqara 2:228)

Aya hii tukufu inatufundisha wazi kuwa mume na mke wote wana haki baina yao.   Lakini aya imezidi kuonyesha kuwa mume    haki zake zimezidi kwa daraja ambazo anatakiwa kuzipata kutoka kwa mke wake .

قال رسول الله صلى الله عليه وسلم  عند ما وقف في عرفة في حجة والوداع :(( يآ أيها الناس إن لنسائكم عليكم حقاً ولكم عليهن حق)) أبو داود

 Mtume صلى الله عليه وسلم  alisema aliposimama Arafa katika hutuba yake  ya mwisho ya Hajj  ((Ee nyie watu, hakika nyinyi mna haki juu ya wake zenu na wake zenu wana haki juu yenu)) (Abu Dawud )


Baadhi ya haki hizo ziko sawa baina ya mume na mke na nyinginezo ziko tofauti baina
yao

 

HAKI ZA  MUME NA MKE BAINA YAO

Zifuatazo ni haki ambazo zinawapasa wote wawili wazitimize baina yao :

1.     Ukweli:

Jambo hili linawabidi wote wawili walitimize baina yao, ili upatikane  utulivu wa kuaminiana baina yao.  Haiwapasi kudanganyana au kuhadaiyana katika mambo yao yote ya kimaisha  ikiwa ni jambo kubwa au dogo likiwa la  baina yao wawili au baina yao na  watu wa nje.

2.     Mapenzi na huruma baina yao:

Mapenzi katika ndoa ni jambo muhimu kuweko kwani bila ya kuweko bila shaka ndoa  itakuwa yenye upungufu  na ikawa sio  imara bali huenda ikavunjika kutokana na sababu ya upungufu huu wa mapenzi baina ya mume na mke. Kila mmoja awe na mapenzi ya dhati kwa mwenzake hata ipatikane raha ya nafsi na maridhio baina yao.     Vile vile iwepo  rahma  baina yao  kwa kuhurumiana katika mambo ya shida na dhiki hata iwe hadi kuwa mmoja wao anapofikiwa hali hii, basi mwenzie awe ndio kitulizo chake.

Allaah سبحانه وتعالى  Amesema

((وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَة ًإِنَّ فِي ذَلِكَ لَآ يَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ))

{Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri}. (Ar-Ruum 30:21)

3.     Uaminifu:

Kila mmoja wao awe muaminifu kwa mwenzake hata isiwekodhana mbaya au shaka baina yao.  Mke na mume wanapotekeleza haki kama hii baina yao huwafikisha kupindukia uhusiano wao ukawa kuliko uhusiano wa ndugu.

Kila mmoja atambue kuwa yeye ni kioo na nafsi ya mwenzake, kwa hivyo vipi mtu asiweze kuwa muaminifu wa nafsi yake?   

4.     Tabia njema

Wawe na tabia njema na upole   katika kauli na matendo ili iwepo heshima baina yao kama Alivyosema Allaah

(( وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ))   

{Na kaeni nao kwa wema}  An-Nisaa 4:19

Kauli hii ya Allaah سبحانه وتعالى   imekamilishwa na kauli ya Mtume صلى الله عليه وسلم

(Nakuusieni kuwafanyia wema wanawake ) Al Bukhari na Muslim

5.    Kuhifadhiana siri na aibu

 Haiwapasi wote kutoleana siri zao  au kutoa aibu zao      kwa   watu  wengine  bali kila mmoja ahifadhi heshima ya mwenziwe  kwa watu wa nje.

Mtume   صلى الله عليه وسلم kasema {Watu watakaokuwa katika hali mbaya kabisa mbele ya Allaah سبحانه وتعالى  siku ya Kiyama  ni mwanamme anaekwenda kwa mke wake na mke kwa mume wake kisha akapita kutoa siri yake } Muslim

 

Hizo kwa ujumla ni desturi na haki ambazo zinapaswa kutekelezwa sawa sawa baina ya mume na mke  kwani walikwishachukua ahadi nzito  ya Allaah :

((وَكَيْفَ تَأْخُذُونَهُ وَقَدْ أَفْضَى بَعْضُكُمْ إِلَى بَعْضٍ وَأَخَذْنَ مِنكُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا))

{Na mtachukuaje na ilhali mmekwisha ingiliana nyinyi kwa nyinyi, na wao wanawake wamechukua kwenu ahadi iliyo madhubuti?} An-Nisaa:20

 Vile vile hivi itakuwa wametimiza kumtii Allaah سبحانه وتعالى  katika  kauli yake :

((وَلاَ تَنسَوُاْ الْفَضْلَ بَيْنَكُمْ إِنَّ اللّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ))

{Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda}.  Baqarah 2:237

Zifuatazo ni haki ambazo zinampasa mmojawao azitimize kwa Mwenzake:

 

HAKI ZA MKE KUTOKA KWA MUME

 

1.   Ni wajibu wa mume kumlisha mkewe anapokula yeye, kumvisha anapovaa yeye  na kumtimizia  mahitajo yake ya nyumbani.

2.   Mume vile vile ni wajibu wake kumtia adabu mke anapohisi uasi wa mke wake kama alivyoamrisha Allaah سبحانه وتعالى  katika kauli ifuatayo :

وَاللاَّتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلاَ تَبْغُواْ عَلَيْهِنَّ سَبِيلاً إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا

{Na ambao mnachelea kutoka katika ut'iifu wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikut'iini msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu na Mkuu} (An-Nisaa 4:34)

Aya hii inataka maelezo kidogo kwani baadhi wa wanaume wameifahamu sivyo Allaah سبحانه وتعالى  Aliposema "muhame katika malazi na wapigeni"

Ibn Abbas  na wengineo wamesema kuwa Aya imemaanisha  kupiga  mpigo usio mkali (yaani mpigo hafifu)   Al-Hassan Al- Basri kasema kuwa ina maana mpigo usio wa nguvu.

Maulamaa wameelezea maana hasa ya kauli hii kwamba  inamaanisha  :

a)     Kwanza mume amnasihi mkewe bila ya kumshutumu au kumuonea au kumtia aibu kwa watu.  Atakapomtii hapo basi yawe yamekwisha.

b)   Atakapoendelea kutokumtii mume wake basi awe mbali nae kitandani, yaani asiwe analala nae kwa muda hivi  wala asiseme nae mpakamke ahisi vibaya ajue kuwa kweli mumewe kakasirika nae, Pindi mke akikubali makosa yake basi yawe vile vile yamekwisha warudie hali yao  kama kawaida .

c)      Kisha tena ikiwa bado mke hana utiifu, hapa sasa mume anaweza kumpiga mkewe.  Lakini sio kumpiga kwa nguvu kama walivyofahamu waume wengine bali kama alivyotuelezea Mtume صلى الله عليه وسلم  katika hadithi ifuatayo:

في صحيح مسلم عن جابر عن النبي صلى الله عليه وسلم :  أنه قال في حجة الوداع :

 واتقوا الله في النساء فإنهن عندكم  عوان ولكم عليهن ألا يوطئنفرشكم أحدا تكرهونه

 فإن فعلن ذلك فاضربوهن ضربا غير مبرح ولهن عليكم رزقهن وكسوتهن بالمعروف

Imepokelewa na Muslim kutoka kwa Jabir kwamba Mtume صلى الله عليه وسلم   kasema katika Hijja ya kuaga {Mcheni Allaah kwa wanawake kwani wao ni wasaidizi wenu.  Mnayo haki  juu yao kuwa wasimuruhusu mtu msiyempenda kukanyaga  zulia lenu. (kuingia katika nyumba yao)  Lakini wakifanya hivyo, mnaruhusiwa  kuwatia adabu ndogo.  Wao wana haki kwenu kwamba muwatimizie matumizi yao na nguo kwa njia ya kuridhisha

3.     Ni wajib wake mume kumpa mafundisho ya dini mke wake anayoyahitaji kama mke bado hakuwa na elimu ya dini yake.  Ikiwa yeye mwenyewe mume hawezi basi amruhusu mkewe  kuhudhuria madarasa ili apate elimu ya dini yake kwani ni muhimu kwake kuijua kutahirisha nafsi yake na kuweza kujirekebisha yale mabaya yanayokatazwa ili ajieupushe yeye na aila yake yote na moto kama alivyosema Allaah سبحانه وتعالى

 ((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا))

((Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na  Moto)) (At Tahriim 66:6)

 

4.     Ni wajibu wake mume kumrekebisha mkewe anapokosea kufuata sharia za dini yake kama kuhakikisha mavazi ya stara na kuitimiza hijaab, vile vile asimwachie kuchanganyika na wanaume isipokuwa wale waliokuwa kaharimishwa nao.

 

5.     Ni wajibu wake kumhifadhi  kwa kila njia.  Mume awe ndio mlinzi wake na mwenye majukumu kwake katika mambo yake yote kama Alivyosema Allaah سبحانه وتعالى

(( الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاء))

{Wanaume ni wasimamizi wa wanawake} An-Nisaa 34

{ Mtume صلى الله عليه وسلم  kasema : Mwanamme ni mchunga (msimamizi) wa nyumbani kwake na ataulizwa kuhusu uchungaji (usimamizi) wake}    Al-Bukhari na Muslim

6.     Ikiwa mume ana mke zaidi ya mmoja, inampasa afanye uadilifu baina ya hao wake katika matumizi yao ya chakula, nguo, maskani na kadhalika. Allaah سبحانه وتعالى  kakataza kutokuadilisha kwa kusema

 

 ((فَإِنْ خِف ْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ذَلِكَ أَدْنَى أَلاَّ تَعُولُواْ))

{na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi (oeni) mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Kufanya hivi ndiko kutapelekea  kutokufanya jeuri}  An-Nisaa 4:3

Juu ya hivyo Mtume صلى الله عليه وسلم  aliusia kuwa wanawake watendewe mema  kama alivyosema

{Mbora wenu ni yule Aliye mbora  kwa familia yake na mimi ni mbora kabisa kwa familia yangu}  At-Tabarani

 

HAKI ZA MUME KUTOKA KWA MKE  

1.    Mke ajue umuhimu wa kumtii mume wake kuwa ni jambo muhimu na kutokumtii ni jambo la hatari kwani hadithi inasema :

((لَوْ كُنْتُ آمِراً  أَحَداً أَنْ يَسْجُدَ لأَِحَدٍ لأَمَرْتُ الْمَرْأَةَ أَنْ تَسْجُدَ لِزَوْجِهَا مِنْ عِظَمِ حَقَِّهِ عَلَيْهاَ))

{Mtume صلى الله عليه وسلم kasema "kama ningeliweza kumuamrisha mtu  amsujudie binaadamu mwenzake, ningeliamrisha mwanamke amsujudie mume wake kwa jinsi haki ya mume ilivyo tukufu kwa mke wake}Tuhfat Al-Ahwadhi  4.323  kutoka Tafsiir ya Ibn Kathiir

2.     Mke inampasa kumtimizia haja ya mumewe wakati    wowote anapomhitajia kujimai naye, kwani kuna hatari kwa kutokumtii mumewe katika jambo hili kama ifuatavyo:

((إذا دَعَا الرَّجُلُ امْرَأتَهُ إِلىَ فِرَاشِهِ فَأَبَتْ عَلَيْه لَعَنَتْهَا الْمَلائِكَةُ حَتَّى تُصْبِحَ))

{Mume atakapomwita mkewe kitandani na akikataa mke, basi malaika watakuwa wanamlaani huyo mke mpaka asubuhi} Imepokelewa na   Imam Al-Bukhari 

3.     Kumhudumia mumewe kwa upole (yaani bila ya  kujikalifisha zaidi ya uwezo wake)

 

4.     Haimpasi mke kutoa sadaka kitu chochote bila idhini ya mumewe .  Kasema Mtume صلى الله عليه وسلم

} قال صلي الله عليه وسلم " لا تنفق المرأة من بيتها شيئا إلا بإذن زوجها قالوا يا رسول الله ولا الطعام قال ذلك من أفضل أموالنا{

   صحيح ابن ماجه -  (حديث حسن  الألباني)

{Asitoe sadaka mwanamke kitu chochote  kutoka nyumbani  ila kwa idhini ya mumewe. Wakasema ewe Mjumbe wa Allaah hata chakula?  Kasema hicho ni mali bora yetu }  Hadithi imepokelewa na Ibn Majah na imepewa daraja ya 'Hasan' kutoka kwa Shaykh Albani .

Ama mwanamke anayo haki kutoa sadaka katika kipato chake mwenyewe kisicho cha mumewe.

Katika hadithi nyingine sahihi inatujulisha kuwa  mwanamke anaweza kutoa sadaka ikiwa anatambua kuwa hatoghadhibikiwa na mumewe.

((عن همام قال سمعت أبا هريرة رضي اللهم عنهم عن النبي صلى اللهم عليه وسلم قال إذا أنفقت المرأة من كسب زوجها عن غير أمره فله نصف أجره))  - البخاري

Kutoka kwa Hamaam kasema : {Nimemsikia Abu Hurayra  رضي اللهم عنهم kwamba Mtume صلى الله عليه وسلم kasema {mwanamke akitoa sadaka kutoka katika kipato cha mumewe bila ya amri yake basi na yeye atapata thawabu nusu yake } Al-Bukhari

5. Haimpasi mwanamke kutoka nyumbani kwake bila ya idhini ya mumewe. (hata kwenda kwa wazazi wake) 

6. Haimpasi mwanamke kumfanyia ujeuri, ufedhuli au usafihi  mumewe

(عن عبد الرحمن ابن عوف قال قال رسول الله صلى اللهم عليه وسلم إذا صلت المرأة خمسها وصامت شهرها وحفظت فرجها وأطاعت زوجها قيل لها ادخلي الجنة من  أي أبواب الجنة شئت) صحيح الترغيب

{Kutoka kwa Abdur-Rahman Ibn 'Awf kasema: Kasema Mtume صلى الله عليه وسلم   : Atakaposwali mwanamke Swalah zake tano, akafunga mwezi wake (wa Ramadhaan), akahifadhi sehemu zake za siri (asifanye uzinifu), akamtii mume wake, ataambiwa ingia peponi kupitia mlango wowote autakao )  Sahih Targhiib

 

Bila ya shaka baada ya kutimiza haki hizi, ndoa itakuwa yenye kudumu bila ya kuwa  na matatizo makubwa ya kuiharibu au kuivunja   نَعُوذُ بالله (Tunajikinga  kwa Allaah)