Skip navigation.
Home kabah

Kuna Ushahidi Aliyerudi Hajj Asomewe Maulidi?

 

SWALI


 
Namshukuru ALLAH subhana Wataala kunipa fersa hii ya kuuliza.Jamaa yangu amerudi Hijja hivi watu wa nyumbani wanataka kumsomea Maulidi jee inafaa?kama haifai kuna Adhabu kwa kufanya Maulidi ua kumsomea dua huyo hujaj,na imetokea wapi?kuna uthibitisho gani  katika Qur an na hadithi? Nitafurahi kwa kupata jibu lenu kwani bado tupo nyuma.
 




 
JIBU:
 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuona kwamba ndugu zetu mko katika hima ya kutaka kujua mas-ala ya dini yetu na kutafuta haki na kujiepusha na upotofu.
 
Hakika Maulidi ni dhahiri kabisa kwamba ni bid'ah (uzushi) uliozushwa miaka baina 400 na 600 baada ya kufariki Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kundi potofu la Mashia Ismailiya (Aga Khan) walipokuwa wakitawala Misr. Kisha yakasambaa na kuenea kufikia pande mbali mbali za dunia hadi kufika kwetu Afrika Mashariki.
 
 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Ametuonya mara nyingi kujiepusha na uzushi na alikuwa akitanguliza khutba zake kwa kutoa maonyo hayo:

((إن خير الكلام كلام الله وخير الهدي هدي محمد صلى الله علي وسلم  وشر الأمور محدثاتها وكل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة وكل ضلالة في النار))  أخرجه مسلم في صحيحه 

((Maneno bora  ni kitabu cha Allah (Qur-aan) na uongofu bora kabisa ni uongofu wa Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم   na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika dini) ni bid'ah (uzushi)  na kila bid'ah ni motoni)) [Muslim katika Swahiyh yake]

 
 
 
Maudhui haya yameelezewa kwa upana ndani ya tovuti, ni vizuri kuyasoma ili Muislamu atambue 'Aqiydah yake swahihi na aweze kuusalimisha Uislamu wake kwani hakika uzushi ni ufisadi mkuu wa 'Aqiydah ya Muislamu. Hivyo bila ya shaka mwenye kutaka kubakia katika usalama wa dini yake ni lazima ajifunze kujua yepi ni ya uzushi na yepi ni ya Sunnah ili asalimike na abakie katika radhi za Mola wake. 
 
 
Juu ya hivyo, mwenye kutenda uzushi hana ila kupoteza muda wake kwa kutenda amali ambazo hazina thamani mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na zaidi ni kutumbukia katika madhambi na kujitayarishia makazi mabaya.
 

((وَقَدِمْنَا إِلَى مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاء مَّنثُورًا ))

((Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika vitendo vyao, tuvifanye kama mavumbi yaliyotawanyika)) [Al-Furqaan: 23]


 

 (( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy]

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate makala muhimu kuhusu mas-ala haya ya Maulidi:


 
Zijue Sababu Za Kumfanya Muislam Asisherehekee Maulidi
 
Mawlid – Mtazamo Wa Kisheria
 
Hoja Za Wanaosherehekea Maulid Na Majibu Yake
 



Muislamu anayerudi kutoka hajj hahitaji kufanyiwa lolote, kwani ikiwa ametimiza Hijjah yake basi atakuwa amerudi akiwa amefutiwa dhambi zake zote. Bali yeye ndiye anayepasa kukuombeeni nyinyi kwa vile yeye atakuwa ametoka kufutiwa dhambi zake bila ya shaka atakuwa bado yuko karibu na Mola wake zaidi.

 

Watu wake wanaweza kumuombe tu du'aa kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amthibitishie Iymaan yake, Azidi kumuongoza na Amtakabalie amali zake. Kumuombea huko kuwe ni kila mtu binafsi katika swala zake au nyakati nyinginezo na sio kwa kukusanyika kumuombea kwani hilo pia ni jambo   lisilofaa na kukubalika katika dini yetu kwa vile hatukupata mafunzo hayo katika Sunnah.

 

Na sisi tunamuombea hayo mema yote na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amjaalie kuendeleza ucha Mungu wake daima.

 
Na Allaah Anajua zaidi