Ni Waajib Wa Mwanamke Kumhudumia Mumewe Kazi Za Nyumba?

 

SWALI:

Ndugu zangu wa ALHIDAAYA swali ni kwamba mwanamke kumpikia mumewe, kumuandalia chakula na kutunza nyumba katika masuala ya usafi pamoja na kuangalia watoto huo ni wajibu wake ama si wajibu?

 

  


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola   wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muuliza swali. Bila shaka ni jambo linaloeleweka kuwa mume katika Uislamu anahitajika kumtimizia mkewe mahitaji ya msingi kama malazi, chakula, matibabu na mengineo. Hii ni kwa mujibu wa maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Aliyesema: “Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Allaah baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayoyatoa” (4: 34).

Pia, “Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala baba kwa ajili ya mwanawe” (2: 233).

Ni katika desturi na ada za Kiislamu tulizozirithi kutoka kwa watangu wema wa Kiswahaba hadi leo kuwa mwanamke anakuwa na jukumu la kumsaidia mumewe kazi za nyumbani mbali na kuwa si wajibu wake. Kufanya hivyo kunawafanya wawe ni wenye kusaidiana mmoja anakwenda kuchuma cha halali na mwengine anatunza vya nyumbani. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatueleza kuwa mke mwema na mzuri ni,

Basi wanawake wema ni wale wenye kutii na wanaojilinda hata katika siri kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajilinde” (4: 34).

Tunapata mifano mingi katika maisha ya Maswahaba wa kike (Radhiya Allaahu ‘anhunna) ambao walikuwa wakifanya kazi zote za nyumbani. Ama kuhusu kulea watoto ni jukumu kubwa zaidi la mama huku akisaidiwa katika hilo na mumewe ambaye ni baba wa mtoto.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share