Majina Ya Mitume 25 Kama Walivyotajwa Katika Qur-aan Na Mpangilio Wao

 

SWALI:

 

Kama nilivyo sema hapo juu mimi naomba majina ya mitume 25 walivyo kuja kwa utaratibu na unaweza kunichambuli vyema kama huyu ni baba wa huyu wabilahi tawfiq asalamaalaykum

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu kwa swali lako.

 

Pamoja na kwamba inasemwa kuwa idadi ya Mitume wanafika hadi 124,000 kutokana na baadhi ya mapokezi, lakini Hadiyth hizo zimedhoofishwa na hivyo hatuwezi kuzitegemea, ila kuna Hadiyth ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyosimuliwa na Abu Dhar ambayo alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) idadi ya Mitume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akamjibu kuwa ni mia tatu na makumi kadhaa. Hadiyth hiyo imeelezwa usahihi wake na Imaam Al-Albaaniy kama ilivyo hapa chini:

 

  عن أبي ذر ، قال : قلت : يا رسول الله ! أي الأنبياء كان أول ؟ ! قال : آدم ، قلت : يا رسول الله ! ونبي كان ؟ ! قال : نعم نبي مكلم ، قلت : يا رسول الله : كم المرسلون ؟ ! قال : ثلاث مئة وبضعة عشر ؛ جما غفيرا .
الراوي: أبو ذر الغفاري  -  خلاصة الدرجة: صحيح  -  المحدث: الألباني  -  المصدر: مشكاة المصابيح  -  الصفحة أو الرقم: 5669

 

Kutoka kwa Abu Dhar ambaye amesema: Nilisema: Ee Mjumbe wa Allaah, Nabii yupi wa mwanzo? Akasema: ((Aadam)). Nikasema: Ee Mjumbe wa Allaah, alikuwa ni Nabii? Akasema: ((Ndio Mtume aliyesemeshwa)) Nikasema: Ee Mjumbe wa Allaah. Wapo Mitume wangapi? Akasema: ((Mia tatu na makumi kidogo)) [Mishkaat Al-Maswaabiyh ikiwa na daraja ya Swahiyh]

 

Hata hivyo idadi iliyotajwa katika Qur-aan ni Mitume 25 pekee na dalili ni kauli ya (Subhaanahu wa Ta'ala):

  وَرُسُلاً قَدْ قَصَصْنَاهُمْ عَلَيْكَ مِن قَبْلُ وَرُسُلاً لَّمْ نَقْصُصْهُمْ عَلَيْك 

((Na Mitume tuliokwisha kukuhadithia kabla yake, na Mitume wengine hatukukuhadithia)) [An-Nisaa: 164] 

 

Mitume 18 wametajwa kwa pamoja katika Aayah 4 zifuatazo zinazofuatana:

 

((وَتِلْكَ حُجَّتُنَا آتَيْنَاهَا إِبْرَاهِيمَ عَلَى قَوْمِهِ نَرْفَعُ دَرَجَاتٍ مَّن نَّشَاء إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٌ)) (( وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَقَ وَيَعْقُوبَ كُلاًّ هَدَيْنَا وَنُوحًا هَدَيْنَا مِن قَبْلُ وَمِن ذُرِّيَّتِهِ دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ وَأَيُّوبَ وَيُوسُفَ وَمُوسَى وَهَارُونَ وَكَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ))   ((وَزَكَرِيَّا وَيَحْيَى وَعِيسَى وَإِلْيَاسَ كُلٌّ مِّنَ الصَّالِحِينَ)) ((وَإِسْمَاعِيلَ وَالْيَسَعَ وَيُونُسَ وَلُوطًا وَكُلاًّ فضَّلْنَا عَلَى الْعَالَمِينَ))  

 

((Na hiyo ndio hoja Yetu Tuliyompa Ibraahiym juu ya watu wake.  Tunampandisha cheo Tumtakaye. Hakika Mola wako ni Hakiymun-‘Aliym (Mwenye hikmah wa yote daima - Mjuzi wa yote daima)). 

((Na Tukamtunukia (Ibraahiym mwana anayeitwa) Is-haaq, na (mjukuu) Ya’quwb. Wote Tukawaongoa. Na Nuwh Tulimuongoa kabla (zamani kabla ya Nabii Ibraahiym). Na katika dhuria wake Daawuwd, na Sulaymaan, na Ayyuwb, na Yuwsuf, na Muwsaa, na Haaruwn. Na hivyo ndivyo Tulipavyo watenda wema))

((Na Zakariyyaa, na Yahyaa, na ‘Iysaa, na Ilyaas. Wote ni miongoni mwa (waja) wema)) 

((Na Ismaa’iyl, na Al-Yasa’a na Yuwnus, na Luwtw. Na wote Tuliwafadhilisha juu ya walimwengu)) [Al-An’aam:  83-86]

 

Manabii na Mitume waliotajwa katika Qur-aan kwa mpangio wa ujio ni kama ifutavyo:

 

1.                 Aadam

2.                  Idriys

3.                  Nuwh

4.                  Huwd

5.                 Swaalih

6.                 Ibraahiym

7.                  Luutw

8.                  Ismaa'iyl bin Ibraahiym

9.                   Is-haaq bin Ibraahiym

10.               Ya'quwb bin Is-haaq bin Ibraahiym

11.                 Yuwsuf bin Ya'quwb bin Is-haaq bin Ibraahiym

12.                  Shu'ayb

13.                  Ayyuwb

14.                  Dhul Kifl

15.                  Muwsaa

16.                  Haaruwn nduguye Muwsaa

17.                  Daawuwd

18.                  Sulaymaan bin Daawuwd

19.                  Ilyaas

20.                   Alyasaa'

21.                   Yuwnus

22.                    Zakariyyaa

23.                     Yahyaa bin Zakariyyaa

24.                     'Iysaa bin Maryam

25.                      Muhammad

(Swalla Allaahu 'alayhim wa sallam)

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share