Talaka Ziko Aina Ngapi Na Wakati Gani Zinasihi?

 

SWALI: 

Ziko aina ngapi za Talaka?

Naomba maelezo ni wakati gani hizo aina za Talaka zinasihi.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Tungependa kuwakumbusha ndugu na dada zetu katika Imani kuwa kabla ya kuuliza swali atazame kama swali lake au mfano wake limejibiwa. Hii inawiya vigumu kwetu kujibu swali moja mara mbili au zaidi ambapo wakati huo tungeutumia kujibu maswali mengine mapya. Swali kama hili tayari tumelijibu, ingia hapa usome Mas-ala Ya Talaka Mbali Mbali

Hata hivyo, tutagusa tena kwa faida ya muulizaji na wengine wenye utata kama huo.

 

Mwanzo kabisa maana ya talaka ni kufungua fungo la ndoa kwa tamko bayana au kwa kinaya (isiyo moja kwa moja). Ama vigawanyo vyake ni kama vifuatavyo:

 

i)             Talaka ya Sunnah: Nayo ni mume kumuacha mkewe katika utwahara ambao hujawahi kukutana naye kimwili.

ii)           Talaka Bid‘ah (Uzushi): Ni mume kumuacha mkewe akiwa katika siku zake za ada, au katika kipindi cha damu ya uzazi, au katika twahara aliyomuungilia au kumuacha talaka tatu kwa mpigo mmoja. Mwenye kutoa talaka aina hii huwa ana madhambi lakini talaka yenyewe huwa imepita ila ile ya tatu huhesabiwa kuwa ni moja tu.

iii)          Talaka Baain: Ni ile ambayo mume anamuacha mkewe akakosa haki ya kumrejea kwa kuwa eda imekwisha. Hivyo, mume huyo akawa ni mposaji kama waposaji wengine na mke akikubali inabidi mume apose, atoe mahari na ifungwe nikaha upya.

iv)         Talaka Rejea: Hii ni ile ambayo mume anamiliki haki ya kumrejea mtalaka wake. Huku ni mume kumrejea mkewe katika kipindi cha eda la kuachwa talaka ya kwanza au ya pili.

 

Pia zipo aina tofauti za kutoa talaka. Nazo ni kama zifuatazo:

 

a)             Talaka Bayana: Hii ni talaka iliyo wazi kabisa isiyo na utata aina yoyote. Nayo ni kama kusema: “Nimekuacha”. Na talaka hii si lazima ukusudie kwani tamko lako linatosha.

b)            Talaka Kinaya (isiyo bayana): Hii ni lazima ukusudie talaka kwa kuwa tamko lako si bayana kama kusema: “Nenda kwa ndugu zako” au “Usiseme na mimi” na yanayofanana na hayo. Ikiwa talaka imenuiwa basi itakuwa imetuka.

c)            Talaka ya hapo kwa hapo: Ni ile ambayo inapotolewa mke huachika hapo hapo bila kuchelewa. Hiyo ni kusema: “Wewe umeachika” baada ya mume kutamka hayo mke atakuwa ameachika.

d)            Talaka ya Kutungika: Ni ambayo mume ameitungika juu ya kitu kingine kuwa kitu hicho akikifanya au akikiacha atakuwa ameachika. Mfano ni mume kusema: ukitoka hapa nyumbani utakuwa umeachika” na mfano kama huo.

e)            Talaka ya Khiyari: Hii ni mume kumwambia mkewe nimekupatia khiyari kutengana nami au kubaki nami. Akichagua kutengana talaka itakuwa imepita. Hii ni kama Anavyotueleza Allaah Aliyetukuka kuhusu uteuzi waliopatiwa wakeze Mtume na Mtume mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo katika Suratul Ahzaab (33), Aayah ya 28.

f)             Talaka kwa Uwakala au Maandishi: Mume kama atamuwakilisha mtu mwingine kumuacha mkewe au akamuandikia mkewe talaka akimuarifu katika maandishi hayo kuwa amemuacha, mke atakuwa ameachika.

g)            Talaka kwa Kuharamisha: Hii ni kusema kwa mume kumwambia mkewe: Wewe ni haramu kwangu au unakuwa haramu, kama atakusudia kwa tamko hilo talaka itakuwa talaka, na kama atakusudia dhihari itakuwa dhihari naye atawajibika kwa tamko hilo kafara la dhihari.  

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share