Nabiy Aadam Alikuwa Na Rangi Gani?

SWALI:

 

Assalaam Alaykum,

Tafadhali naomba kufahamishwa kuhusu ni ipi rangi ya baba yetu Adam Alayhis salaam? je ni mwafrika, mzungu, au mwarabu n.k.

WABILLAH TAWFIQ
WASSALAAM ALAYKUM

 


JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali hilo kuhusu maumbile ya Nabiy Aadam (‘Alayhis Salaam).

 

Hakika isiyopingika ni kuwa Nabiy Aadam (‘Alayhis Salaam) ndiye mwanadamu wa kwanza kuumbwa na Allaah na baada ya kukaa kwa muda fulani mbinguni aliteremshwa ardhini ili awe khalifa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alimuumba Nabiy Aadam (‘Alayhis Salaam) kwa mchanga au udongo, na asli ya vitu hivi ni kuwa vina rangi tofauti. Na hii ni dalili kubwa ya kuwepo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kuwa Yeye Ndiye Muumbaji na Anavyotaka Anafanya na hakuna aliye na  uwezo wa kumuuliza lakini Yeye Ndiye Atakayetuuliza kwa yale ambayo tumeyafanya hapa duniani.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

“Na katika Ishara Zake ni kuwa kakuumbeni kwa udongo. Kisha mmekuwa watu mlio tawanyika kote kote” [30: 20].

 

Na pia:

“Na katika Ishara Zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutafautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa wajuzi” [30: 22].

 

Hivyo, kuwa na rangi tofauti ni Ishara za kuwepo kwa Allaah na sifa Yake ya Uumbaji.

Na kwa kuwa uumbaji Wake ni kwa udongo wenye rangi tofauti kila mtu anayezalikana naye anakuwa na rangi tofauti na hata na nduguze wa kiume na kike.

Hivyo, ndivyo tulivyo pata rangi zetu kutoka kwa baba yetu kwa kurithi. Na leo tazama unaweza kukuta ndugu wawili wa baba na mama mmoja wanavyotofautiana katika rangi zao.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share