Mwanamke Ni Lazima Ajifunike Kichwa Akiwa Nyumbani Kwake Au Malaika Hawatoingia Asipofanya Hivyo?

SWALI:

 

A/A/W/WABARAKATU.


KWANZA NAOMBA JINA LANGU MUSILIONYESHE WAKATI WA KUNIPATIA MAJIBU KAMA MAJIBU YATAPITIA GAZETINI. MASUALA YANGU NI MAWILI

MWANAMKE ANAPOKAA KICHWA WAZI NDANI YA NYUMBA YAKE MALAIKA WEMA HAWAINGII? HATA KAMA YUKO NA MAHARIMU ZAKE AU YUKO PEKE YAKE NAOMBA UFAFANUZI

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

Shukrani zetu za dhati kwa maswali yako kuhusu kuacha kichwa wazi kwa mwanamke akiwa nyumbani na Hadiyth kuhusu elimu.

 

Ama kuhusu swali la kwanza hakuna tatizo lolote kwa mwanamke kuwa kichwa wazi akiwa mbele ya maharimu zake kwani hiyo ni sehemu ambayo yaweza kuonekana bila wasiwasi wowote. Allaah Aliyetukuka Anatueleza:

 

"Wala wasidhihirishe viungo vyao ila vinavyodhihirika. Na waangushe shungi zao mpaka vifuani mwao, na wasionyeshe mapambo yao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au watoto wa kaka zao, au wana wa dada zao, …" (24: 31).

Bila shaka, kichwa ni lazima kifunikwe ikiwa yu mbele ya waume wasio maharimu zake au akitoka nje kwa shughuli zake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share