Je Uchawi Upo? Na Vipi Kujitibu?

 

 

 

SWALI:

 

Assalam aleikum ndugu zangu! Nimefurahi sana kupata website hii sababu ya mafunzo na faida nyingi nilopata ndani yake.suali langu ni: jee sihri ya exist, yaani mtu anaweza kufanyiwa sihri? Na kama ipo mtu atajua vipi kama amefanyiwa sihri? Na yafaa kufanya dawa kujitopoa??? Naomba munifafanulie suali langu. Shukran.

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ahli zake, Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Sihri iko na kuweko kwa sihri haimaanishi kuwa ni halali kama ambavyo tembo lipo, nguruwe wapo lakini kutumia vitu hivyo ni haramu. Hata Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa Sallam) aliwahi kufanyiwa sihri na Myahudi mmoja aliyekuwa akiitwa al-Labiyb bin ‘Aaswim na mabinti zake. Ndio ikawa sababu ya kuteremshwa kwa Mu‘awadhatayn (Suratul Falaq na an-Naas). Kwa kirefu tafadhali angalia tafsiri ya Surah hizi mbili katika vitabu vya tafsiri vikubwa kama Tasiyr ya Ibnu Kathiyr.

Allaah (SubhaanahuWa Ta’ala) Anasema:

 

 

((وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَكِنَّ الشَّيْاطِينَ كَفَرُواْ يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّى يَقُولاَ إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلاَ تَكْفُرْ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِ بَيْنَ الْمَرْءِ وَزَوْجِهِ وَمَا هُم بِضَآرِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلاَّ بِإِذْنِ اللّهِ))

 

(( Na wala Suleiman hakukufuru, bali mashaytwaan ndio waliokufuru, wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili, Haaruta na Maaruta katika Baabiyl. Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru. Wakajifunza kwa hao wawili yale ya kumfarikisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa kutaka Allaah))(2: 102).

 

 

Zipo ishara au alama za kuonyesha kuwa mtu amefanyiwa sihri na zipo aina tofauti za sihri. Kwa mfano, kuna sihri ya mtu kuwa mgonjwa daima. Mtu huyu akienda hospitali na kupimwa anaonekana kuwa yupo sawa kabisa.

 

Kuna zile za mtu kusikia sauti bila kumuona mtu mwenyewe, au kuona vitu ambavyo havipo, na ile ya uenda wazimu.

 

Kujipotoa zipo aina mbili – moja kati ya hizo haifai na nyengine yafaa.

 

Ile aina ambayo haifai ni kutoa uchawi kwa uchawi, kupunga, kwenda katika mizimu na kadhalika.

 

 

Na ile ambayo inafaa ni kwa Ruqya (Poza kutokana na Qur-aan na Sunnah). Kuisoma Qur-aan na Adhkaar au Du’aa zilizosuniwa na kupokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) na watangu wema.

 

Hivyo, kufanya dawa kujitopoa (kujizungua) yafaa lakini katika njia ambazo ni za halali.

 

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

 

Share