Kuhusu Mashaytwaan Na Vipi Kujikinga Nao

 

SWALI:

 

Asalam alaykum.ALLAH awajaze kheri kwa kujibu maswali yetu mana mnatuweka wazi kwa vitu vilokua vigumu kwetu.Swali langu ni QUR-AAN inatufundisha nini kuhusu mashetani au majini? Pia naomba dua za kujikinga na kujitibu sie na watoto wetu dhidi ya viumbe hivi(mashetani au majini)

 

 


 

 

 

 

JIBU:

 

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  Aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa Ba’ad

 

Hakika swali hili jibu lakelinahitaji maelezo marefu kwani kuna aya na Hadiyth nyingi kabisa zilizotaja kuhusu mashaytwaan au majini kwa hiyo tujaribu kuelezea kwa kadiri tuwezavyo Insha Allaah:

 

Qur'aan inatufahamisha kuwa majini wapo na kuwa iko sababu ya kuweko kwao katika maisha haya, sababu ni kuwa wamuabudu Allaah سبحانه وتعالى Pekee bila ya kumshirikisha. Anasema Allaah سبحانه وتعالى :

 

((وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ))

  

((Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi)) [Adh-Dhaariyaat:56]

 

Majini kama binaadamu wana baadhi ya vitu ambavyo vinafanana kama katika ufahamu wa kujua lipi jema na jipi baya kwani waliposikia Qur'aan inasomwa walishangazwa na kisha wakasema kuwa:

 

 

((وَأَنَّا مِنَّا الصَّالِحُونَ وَمِنَّا دُونَ ذَلِكَ كُنَّا طَرَائِقَ قِدَدًا))

   (( وَأَنَّا ظَنَنَّا أَن لَّن نُّعجِزَ اللَّهَ فِي الْأَرْضِ وَلَن نُّعْجِزَهُ هَرَبًا))

 ((وَأَنَّا لَمَّا سَمِعْنَا الْهُدَى آمَنَّا بِهِ فَمَن يُؤْمِن بِرَبِّهِ فَلَا يَخَافُ بَخْسًا وَلَا رَهَقًا))

 ((
وَأَنَّا مِنَّا الْمُسْلِمُونَ وَمِنَّا الْقَاسِطُونَ فَمَنْ أَسْلَمَ فَأُوْلَئِكَ تَحَرَّوْا رَشَدًا))

 

((Na hakika katika sisi wamo walio wema, na wengine wetu ni kinyume na hivyo. Tumekuwa njia mbali mbali))  

((Nasi tulijua kuwa hatutomshinda Mwenyezi Mungu duniani, wala hatuwezi kumponyoka kwa kukimbia)) 

((Nasi tulipousikia uongofu tuliuamini. Basi mwenye kumuamini Mola wake Mlezi basi haogopi kupunjwa wala kudhulumiwa)) 

((Na hakika wamo katika sisi Waislamu, na wamo kati yetu wanaoacha haki. Basi waliosilimu, hao ndio waliotafuta uongofu))
[Al-Jinn:11-14]

 

 

Kwa hiyo siku ya Qiyaamah nao pia watasimamishwa kuwa na hesabu yao mbele ya Mola wao kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى 

 

((وَجَعَلُوا بَيْنَهُ وَبَيْنَ الْجِنَّةِ نَسَبًا وَلَقَدْ عَلِمَتِ الْجِنَّةُ إِنَّهُمْ لَمُحْضَرُونَ))

((Na wameweka makhusiano ya nasaba baina yake na majini; na majini wamekwisha jua bila ya shaka kuwa wao watahudhurishwa))

[As-Swaafaat :158]

 

Wanaishi kama sisi binaadamu, wanakula, na kunywa na wanaoana na kuzailiana. Nao ni viumbe vinavyoishi na kutembea, na sisi binaadamu hatuwaoni bali wao wanatuona kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى :

 

((إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لاَ تَرَوْنَهُم))

 

 ((Hakika yeye na kabila lakewanakuoneni, na nyinyi hamuwaoni)) [Al-A'raaf 27]

 

Kuumbwa kwao ni kutokana na moto;

 

((وَالْجَآنَّ خَلَقْنَاهُ مِن قَبْلُ مِن نَّارِ السَّمُومِ))

 

 ((Na majini Tuliwaumba kabla kwa moto wa upepo umoto)) [Al-Hijr 27]

 

 

((وَخَلَقَ الْجَانَّ مِن مَّارِجٍ مِّن نَّار))

 

((Na akawaumba majini kwa ulimi wa moto)) [Ar-Rahmaan:15]

 

 

Na wao wanaweza kujibadilisha maumbile yao waonekane kama ni vitu vingine kama vile wanyama kama mbwa au nyoka, na kadhalika. Wana uwezo wa kusafiri masafa makubwa kwa haraka kabisa.  

 

Wanapenda sana kuishi katika sehemu chafu kama vyooni, katika mashimo, jaani, makaburini, katika magofu na kadhalika na ndio maana Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametufundisha tunapoingia chooni kuomba du'aa hii:

 

(بِسْمِ الله ) اللّهُـمَّ إِنِّـي أَعـوذُ بِـكَ مِـنَ الْخُـبْثِ وَالْخَبائِث    

   

Bismillah, Allaahumma Inni A'udhu Bika Minal-Khubthi Wal-Khabaaith

 

 

 (Kwa jina la Mwenyezi Mungu ) Ewe Mwenyezi Mungu  najilinda Kwako kutokana na mashetani ya kiume na ya kike.

 

 

Wana uhusiano na sisi binaadamu na kila mmoja wetu anaye jini ambaye anakuwa ni mwenye kumuandama kama rafiki yake.

 

  عن ابن مسعود أنه قال : قال رسول الله: (( ما منكم من أحد إلا وقد وكل به قرينه من الجن)) . قالوا : وإياك يا رسول الله؟ قال :  ((وإياي إلا أن الله أعانني عليه فأسلم فلا يأمرني إلا بخير))   رواه مسلم

 

Ibn Mas'uud amesema: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Hakuna mmoja wenu ila anaye jini anayemuwakilisha qariyn (rafiki) katika majini)) Wakasema: Hata wewe ewe Mjumbe wa Allaah? Akasema: ((Hata mimi isipokuwa mimi Allaah Amenisaidia kwa kumsilimisha kwa hiyo haniamrishi ila mema tu)) [Muslim]

 

 

Na shatwaan anaweza kuwa ni binaadamu au jini, na ndio Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

 

((مِن شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ))

((الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ))  

 ((مِنَ الْجِنَّةِ وَ النَّاسِ))

 

))Na shari ya wasiwasi wa Shetani, Khannas))

((Anayetia wasiwasi katika vifua vya watu)).

((Kutokana na majini na wanaadamu)) 
 [An-Naas 114:46]

 

Na kuhusu mashetani wa kibinadamu:

 

((وَإِذَا لَقُواْ الَّذِينَ آمَنُواْ قَالُواْ آمَنَّا وَإِذَا خَلَوْاْ إِلَى شَيَاطِينِهِمْ قَالُواْ إِنَّا مَعَكْمْ إِنَّمَا نَحْنُ مُسْتَهْزِؤُونَ))

 

(( Na wanapokutana na walioamini husema: Tumeamini. Na wanapokuwa peke yao na mashaytwaan wao husema: Hakika sisi tu pamoja nanyi. Hakika sisi tunawadhihaki tu))    [Al-Baqaraha 2.14]

 

 

KUJIKINGA NA MASHAYTWAAN

 

Kuna njia nyingi za kujikinga na mashaytwaan kutokana na madhara yaokama ilivyo katika Qur'aan na Sunnah:

 

 1-Kujikinga nao kama Alivyotufundisha Allaah سبحانه وتعالى kuwa tuseme:            

                              

  ((  رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ  مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ))    

((وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ))       

 

((Mola wangu Mlezi! Najikinga kwako na wasiwasi wa mashaytwaan))

((Na najikinga kwako, Mola wangu Mlezi, wasinikaribie))[Al-Muuminuun]

 

 

2-Kusoma Surah mbili za mwisho (Al-Falaq na An-Naas)

 

3-Kusema 'Bismillah' kabla ya kula, kunywa, kuingia katika nyumba, kujamiiana, unapoingia chooni pamoja na du'aa yake.

 

 4-Kusoma Ayatul-Kursiy unapolala pamoja na Aya mbili za mwisho katika Suratul-Baqarah.

 

5-Kusoma Qur'aan sana na khaswa Suratul Baqarah ambayo Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema atakayesoma  sura hiyo haingii shaytwaan nyumbani kwake.

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال)) : لا تجعلوا بيوتكم قبورًا فإن البيت الذي تقرأ فيه سورة البقرة لا يدخله الشيطان))   صحيح الجامع

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema ((Msifanye nyumba zenu makaburi kwani nyumba inayosomwa Suratul-Baqarah haingii shaytwaan)) [Sahiyh Al-Jaami'i]

 

6-Kusoma nyiradi za asubuhi na jioni kila siku ambazo ni za Sunnah nazo zinapatikana katika kitabu cha Hisnul-Muslim kinachopatikana hata kwa lugha yetu ya Kiswahili. Na pia utaweza kukipata kitabu hicho katika kiungo kifuatacho katika ALHIDAAYA:

 

 Bonyeza hapa:

 

          Kitabu Cha Hiswnul-Muslim- Du'aa Katika Qur-aan na Sunnah

 

 

Na humo utapata pia Du'aa za kuwakinga watoto kama alivyokuwa akifanya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم .

 

 

7-Kutia wudhuu kila mara.

 

Kwa ujumla ni kuimarisha iymaan yako kwa kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى  kila wakati katika harakaat zako, kwani hivyo utajikinga na mashaytwaan na hawatoweza kukudhuru. 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share