'Aqiydah Ya Ahlus Sunnah Wal Jama'ah -1
Itikadi Sahihi
‘Aqiydah Ya Ahlus Sunnah Wal Jama’ah – 1
Muhammad Faraj Salim As-Sa’y
‘Aqiydah ya Ahlus Sunnah ni sahili na nyepesi, haina tabu kufahamika wala haina mikanganyo. Haina tabu kuisherehesha. Bali inafahamika na mtu wa kawaida kama inavyofahamika na mtaalamu. Mtu yeyote anaweza kuifahamu kwa wepesi kabisa.
Vitabu vyao vya Hadiyth kama vile Al-Bukhaariy na Muslim na vingine, pamoja na mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) yaliyonukuliwa ndani ya vitabu hivyo na kuenezwa kila mahali ulimwenguni kwa njia ya isnadi yenye kufuata mfumo na elimu ya hali ya juu, vitabu hivyo vinakubaliwa na sehemu kubwa sana ya umma huu na vinatumiwa katika kuitimiza na kuisherehesha sheria ya Mwenyezi Mungu.
Maulamaa wake kama vile Imam Abu Haniyfah na Imam Maalik na Imam Shafi na Imam Ahmad bin Hanbal na Ibnul Mubaarak na Ibnu Taymiyah na wenzao wengi wengine wanapendwa na kufuatwa na asilimia zaidi ya 95 ya Waislamu ulimwenguni, kutokana na elimu yao kubwa na masharti yao mepesi. Walikuwa daima wakisema: “Ukikuta katika mafundisho yetu yanayokubaliana na Qur-aan au Sunnah sahihi, basi yafuateni. Na kama hayakubaliani na hayo basi yapigeni na ukuta.”
Watu wamedurusu sira zao na mwenendo wao na elimu yao heshima yao, wakawakubali kama ni Maimamu wao walioisherehesha Qur-aan tukufu na mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kwa njia ya kitaalamu na kwa uhodari mkubwa.
Viongozi wao walipambana na maadui wa Waislamu, wakaweza kuzifungua nchi nyingi sana na nyoyo nyingi. Walitayarisha majeshi na wapiganaji walioweza kuziteka nchi kubwa kubwa kuanzia Uturuki, sehemu kubwa ya Uchina na Urusi. Afghanistan na Afrika na Asia na sehemu kubwa ya Ulaya, na kwa njia hiyo mamilioni kwa mamilioni ya watu waliingia katika dini hii tukufu.
Walifanikiwa kote huko kuwatoa watu katika giza la kumkufuru Mwenyezi Mungu na kuwaingiza katika nuru ya Uislamu, kuwatoa katika jeuri ya watawala wao, na kuwaingiza katika uadilifu wa Uislamu, kuwatoa katika kuipenda dunia, na kuwaingiza katika kuipenda akhera yao, na juu ya kuwa wao ndio walioziteka nchi hizo, lakini wananchi wake wanandelea mpaka leo kuwapa watoto wao majina ya wafunguzi wale wa Kiislamu.
Utamkuta mtoto wa Kirusi au wa Kituruki au wa Ki Africa au Asia au Ulaya au hata Marekani akipewa jina la Abu Bakr au ‘Umar au ‘Aliy au ‘Uthmaan au Mu’aawiyah au Khaalid (Khaalid bin Waliyd) au Haarun au Salaahud-Diyn, n.k.
Kutokana na mafundisho ya Maulamaa wao yaliyo mepesi yanayokubalika na akili ya mwanadamu yeyote wa kawaida, madhehebu haya yalipendwa na kufuatwa na asilimia kubwa sana ya Waislamu duniani.
Kuthibitisha Sifa Za Allaah
Kwa mfano katika kuzithibitisha sifa za Mwenyezi Mungu, Ahlus Sunnah wanakubali na kukithibitisha kila Alichokubali na Kukithibitisha Mwenyezi Mungu bila ya kuchelewesha wala kubadilisha.
Mwenyezi Mungu Anaposema kuwa Anao Uwezo, na sisi tunaamini kuwa Anao Uwezo. Anaposema kuwa Anaona, na sisi tunaamini kuwa Anaona Subhaanahu wa Ta’ala.
Anaposema kuwa Anasikia, na sisi tunaamini kuwa Anasikia. Na anaposema kuwa Anayo macho, na sisi tunaamini kuwa Anayo Macho, Subhanahu wa Taala, na Anaposema kuwa Anayo Mikono na sisi tunaamini kuwa Anayo Mikono, na Anaposema kuwa Anao Wajihi, na sisi tunaamini kuwa Anao Wajihi Subhaanahu wa Ta’ala. Lakini macho Yake na mikono Yake na Wajihi wake na Kuona Kwake na kusikia Kwake hauna mfano wowote na kitu chochote.
Maulamaa wetu wametufundisha kuzikubali sifa zote za Mwenyezi Mungu bila ya kukisia kwa akili zetu namna yake au mfano wake. Kwa sababu kuzikataa sifa ambazo Mwenyewe Amejipa Subhaanahu wa Ta’ala, ni makosa, na kuzifananisha sifa hizo pia ni makosa.
لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ وَهُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ
“Hapana kitu kama mfano Wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona” Ash-Shuuraa: 10
Maulamaa wetu wametufundisha kuzikubali sifa zote za Mwenyezi Mungu bila ya kukisia kwa akili zetu namna yake au mfano wake. Kwa sababu kuzikataa sifa ambazo Mwenyewe Amejipa Subhaanahu wa Ta’ala, ni makosa, na kuzifananisha sifa hizo pia ni makosa.
“Hapana kitu kama mfano Wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona”
Mwenyezi Mungu Anaposema:
يَدُ اللَّهِ فَوْقَ أَيْدِيهِمْ
“Mkono wa Mwenyezi Mungu Uko juu ya mikono yao” Al-Fat-h: 10
Sisi tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Anao Mkono. Kwa sababu Yeye Mwenyewe Subhaanahu wa Ta’ala Amesema hivyo. Lakini hatuufananishi Mkono Wake na vijikono vyetu.
Anasema mwanachuoni wa Kishia As-Sayed Muhammad Al-Husayniy Ash-Shiraziy katika tafsiri yake inayoitwa; Taqriyb al Qur’an fil Adh’haan katika kuifasiri Aayah hii: “Mkono wa Mwenyezi Mungu Uko juu ya mikono yao.” “Aya hii inazungumza juu ya Mashaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) waliofungamana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) (chini ya mti), na katika kufungamana, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiutandaza mkono wake huku matumbo ya vidole yakielekea juu, na wanapokuja wenye kufungamana naye walikuwa wakiweka mikono yao juu ya mkono wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)”
Aayah hii ilitemshwa baada ya Maswahaba kufungamana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) walipokuja chini ya ule mti na kuiweka mikono yao juu ya mkono wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), ndipo Mwenyezi Mungu Aliposema;
“Mkono wa Mwenyezi Mungu Uko juu ya mikono yao” Al-Fat-h: 10
Maulamaa wanasema: ‘Mguu wa meza hauwezi kufanana na mguu wa Seremala aliyeichonga meza hiyo na kutengeneza miguu yake, kama vile mkono wa fundi aliyetengeneza simu hauwezi kuwa sawa na mkono wa simu. Siku zote sifa za mtengenezaji haziwezi kufanana na sifa za bidhaa yake.
Na Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye mifano mikubwa. Kwa hivyo Anaposema Subhanahu wa Taala kuwa anao Mkono, na sisi tunakubali kuwa Anao Mkono lakini hatuufananishi na mikono wetu, kwa sababu sifa za Muumba haziwezi kufanana na sifa za viumbe
Na katika Aayah nyingine Mwenyezi Mungu Anamuuliza Ibilisi:
قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ أَسْتَكْبَرْتَ أَمْ كُنتَ مِنَ الْعَالِينَ
Ewe Iblisi! Kipi kilichokuzuia kumtii yule niliyemuumba kwa mikono yangu? Je! Umejiona mkubwa, au umekuwa katika wakuu kweli? Swaad: 75
Sisi tunaamini kuwa; kwa vile Mwenyezi Mungu Amesema kuwa Amemuumba Aadam kwa mikono yake basi haiwezekani kuwa Amekusudia kuwa Amemuumba kwa njia nyingine.
Ndani ya Qur-aan tukufu Mwenyezi Mungu Anazungumza na watu wa kila aina, wenye elimu na wasiokuwa na elimu. Na kusudi Lake Subhaanahu wa Ta’ala ni kuwafundisha watu hao waijuwe dini yao, juu ya hitilafu ya ufahamu wao. Kwa hivyo haiwezekani Azungumze nao kwa njia ya mafumbo au majazi akawa Anasema neno huku Akikusudia jambo au neno lingiine.
Mwenyezi Mungu Angelitaka kusema kuwa Amemuumba mwanaadamu kwa Kudra Yake, kwa mfano; basi Angelisema tu, pasingekuwa na haja ya kuutaja mkono.
Na katika Aayah nyingine pia Mwenyezi Mungu Anasema:
أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا خَلَقْنَا لَهُمْ مِمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ
“Je! Hawaoni kwamba Tumewaumbia kutokana na iliyofanya mikono Yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki.” Yaasin: 71
Na hivi ndivyo ilivyo katika sifa Zake zote Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Ta’ala, kila Anapozitaja, ni juu yetu kusema: ‘Sam’an wa twa’an’, tuzikubali bila kubabaisha maana yake wala kubadilisha wala kufananaisha sifa hizo na sifa za viumbe.
Kwa mfano Mwenyezi Mungu Anaposema:
إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَنْ يَقُولَ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ
“Hakika amri Yake Anapotaka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa.” Yaasin: 71
Tunapoisikia kauli hiyo ya Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Ta’ala, hatuna budi kuikubali na kuiamini. Kwa nini? Kwa sababu Mwenyezi Mungu Mwenyewe Amesema hivyo. Ikiwa Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Ta’ala Hasemi, kwa nini basi alisema kuwa; hukiambia tu: Kuwa! Na kikawa?
Na katika Aayah nyingine Mwenyezi Mungu Anasema:
وَكَلَّمَ اللّهُ مُوسَى تَكْلِيمًا
“Na Mwenyezi Mungu Alinena na Muusa kwa maneno.” An-Nisaa: 164
Bali hata Qur-aan Tukufu ni maneno ya Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Ta’ala. Mwenyezi Mungu Anasema:
وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّى يَسْمَعَ كَلاَمَ اللّهِ ثُمَّ أَبْلِغْهُ مَأْمَنَهُ ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لاَّ يَعْلَمُونَ
“Na ikiwa mmoja wapo katika washirikina akikuomba ulinzi, basi mpe ulinzi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Kisha mfikishe pahala pake pa amani. Haya ni kwa kuwa hao ni watu wasiojua kitu.” At Tawbah: 6
Wengine wanasema kuwa Mwenyezi Mungu hakusudii hivyo, bali hayo ni majazi tu. Na maana yake ni kuwa Anaposema kuwa Anasikia, hakusudii kuwa Anasikia kweli bali hayo ni majazi tu, na Anaposema kuwa Anaona hakusudii kuwa Anaona kweli bali hayo ni majazi tu, na Anaposema kuwa Anayo macho, hakusudii kuwa Anayo macho, bali hayo ni majazi tu, na Anaposema kuwa Anayo mikono hakusudii kuwa Anayo mikono bali hayo ni majazi tu, na anaposema kuwa Anao wajihi hakusudii kuwa Anao wajihi kikweli bali hayo ni majazi tu… SubhaanaLlaah!!!
Sisi tunasema; Majazi yapo, lakini majazi ni kwa mfano mtu shujaa akaitwa Simba, au mtu muovu akaitwa nyoka nk. Haya ni majazi. Lakini maneno ya Mwenyezi Mungu Aliyotuletea waja wake kwa ajili ya kutufundisha dini yetu na kutujulisha sifa Zake Subhanahu wa Taala , hayawezi kuingia katika mfumo huu. Ni maneno ya Kiarabu yasiyokwenda upande. Lugha ya Kiarabu safi kabisa.
Mwenyezi Mungu Anasema:
قُرآنًا عَرَبِيًّا غَيْرَ ذِي عِوَجٍ لَّعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ
“Qur-aan ya Kiarabu isiyo na upogo (isiyokwenda upande), ili wamche Mungu,” Az-Zumar: 28
Itaendelea InshaAllaah…
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


