Makbuus Dajaaj/ Machbuus ya Kuku (U.A.E)

Makbuus Dajaaj/ Machbuus ya Kuku (U.A.E)

 

Vipimo

Mchele wa Basmati - 4 vikombe

Kuku (mkubwa kiasi) - 1  (wa Lb 6 -7)

Vitunguu vilivyokatwakatwa - 3

Samli - 4 vijiko vya supu

Buharaat (bizari ya Machbuus) - 2 vijiko vya supu

Bizari ya manjano (haldi/tumeric) - 1 kijiko cha chai

Nyanya zikizomenywa na kukatwakatwa - 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa - 2 vijiko vya supu      

Loomi (ndimu kavu) au ya unga - ½  au ½ kijiko cha chai

Mdalasini kijiti - 1

Karafuu nzima - 3

Hililiki nzima - 4

Maji - 5 vikombe

Kotmiri iliyokatwakatwa - ½ kikombe

Chumvi - kiasi

 

Vipimo Baharaat (Binzari)

Baharaat – Bizari ya Makbuus

Pilipili Manga - ½ kikombe

Gilgilani (Corriander seeds) - ¼ kikombe

Mdalasini vijiti - ¼ kikombe

Karafuu - ¼ kikombe

Bizari ya pilau (cumin seeds) -1/3 kikombe

Hiliki - 2 vijiko vya chai

Paprika ya unga - ½ kikombe

 

Namna Ya Kutayarisha Baharaat (bizari)

 1. Chambua hiliki utoe kokwa zake, kisha tia vitu vyote katika mashine ya kusagia (grinder) usage hadi iwe unga.
 2. Changanya na Paprika bizari ikiwa tayar.
 3. Ihifadhi katika chupa yenye mfuniko wa kubana vizuri.

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Makbuus

 1. Osha na roweka mchele kwa muda kiasi.
 2. Msafishe kuku, mkate vipande vinne weka kando.
 3. Katika sufuria ya kupikia, tia samli, kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi ya hudhurungi (brown). Tia baharaat na bizari ya manjano, kaanga kwa dakika moja hivi.
 4. Tia vipande vya kuku, chumvi, thomu, punguza moto na umkaange kuku katika masala ya vitunguu.
 5. Tia nyanya, karafuu, loomi, mdalasini, hiliki, changanya vizuri na endelee kukaanga.
 6. Tia maji (inategemea mchele unaotumia, huenda ukahitaji zaidi). Funika na pika kwa muda wa dakika 20-25.
 7. Mwaga mchele maji uliyorowekea, mimina mchele katika supu, tia kotmiri, changanya vizuri, funika uchemke mchele, punguza moto na pika wali kama inavyopikwa pilau ukoroge mara moja au mbili tu.
 8. Ukishaiva wali, pakua katika sinia/sahani na weka vipande vya kuku juu katikati ya wali.

Kidokezo: 

 1. Ukipenda badala ya kupika wali katika sufuria baada ya kutia mchele na kukaribia kuiva, na kabla ya kukauka supu yote, mimina katika treya ya jalbosi (Treya ya foil) upike ndani ya oveni (bake) kwa mtoto wa takriban 400-450º   kwa muda wa dakika 20-25.
 2. Baharaat hiyo inatumiwa katika vyakula vya nchi za Kiarabu (Gulf States), hivyo unaweza kutumia kupikia  machbuus ya vitoweo vingine kama nyama na samaki na vyakula vinginevyo kama michuzi n.k.

 

 

 

Share