Ninaweza Kuanza Kusoma Surah Katikati Ninaposwalisha?

 

Ninaweza Kuanza Kusoma Suwrah Katikati Ninaposwalisha?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

S. Aleykum,

 

Nina swali,wakati mtu anaswalisha yuaweza kuanza kusoma suwrah popote anapotaka (yaani si lazima aanze mwanzo wa suwrah). Swali langu ni hili je kuna masharti yoyote ama mtu aweza kusoma atakavyo? Shukran

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Anaweza mtu kuanza kusoma popote katika Suwrah, ikiwa anaswalisha au anaswali mwenyewe, kwani kawaida katika Suwrah moja ya Qur-aan huwa ina maelezo mbali mbali, kwa hiyo hakuna kipingamizi kufanya hivyo.

 

Kuhusu sharti za kusoma katika Swaalah, ni vizuri kufuata adabu za Swaalah kama alivyokuwa akifanya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

1. Kisomo cha Suwrah kinaweza kuwa kirefu mara nyingine na mara nyingine kifupi kutokana na hali ya mtu kama yuko katika safari, au anaumwa au kama mtoto analia.

 

2. Kisomo kinakuwa tofauti kutokana na hali ya Swaalah.

 

3. Kisomo cha Swalah ya Alfajiri ni kirefu kuliko Swaalah zote. Kisha kinafuatia kisomo cha Swaalah ya Adhuhuri, kisha Alasiri, kisha 'Ishaa na mwisho ni Magharibi.

 

4.  Kisomo cha Swaalah ya usiku (Tahajjud) ni kirefu zaidi kuliko Swaalah zote hizo.

 

5. Ni Sunnah kufanya kisomo cha Raka'ah ya mwanzo kirefu kuliko Raka'ah ya pili.

 

6. Suwrahl Al-Faatihah ni fardhi katika kila Raka'ah.

 

7. Imaam haruhisiwi kusoma kisomo kirefu sana zaidi ya kilivyoelezwa katika Sunnah, kwa sababu kutowatia mashakani wanaoswali nyuma yake kama watu wazima, wagonjwa, na walio dhaifu.

 

Kisomo cha sauti na cha kimya:

 

1). Qur-aan isomwe kwa sauti katika Swaalah ya Alfajiri, Swaalah ya Ijumaa, Swaalah za 'Iyd, ya mvua, ya kupatwa jua na katika Raka'ah mbili za mwanzo kwenye Swaalah ya Magharibi na 'Ishaa.

 

2). Ni Sunnah kusoma Qur-aan kwa tartiyl, yaani kusoma inavyopaswa kusomwa kwa kufuata sheria zake za Tajwiyd, na kwa kuipendezesha sauti.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

Share