Ikiwa Mtachezeana Tu Na Kutokwa Manii Inapasa Kukoga Josho?

Ikiwa Mtachezeana Tu Na Kutokwa Manii Inapasa Kukoga Josho?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI

 

Assalamu aleikum,

Ninaelewa unaweza au mnaweza kugusana tupu baina ya mke na mume na ikawa hamtokuwa wenye kuhitajika kukoga Janaba.I sipokuwa kama ntatokwa na shahawa.

Swala langu lipo hapo najua vigumu kwa mwanamke kukumbana na umbile lauume au akawa mwenye kucheza nacho kiungo hicho bila kumtoka chochote. Kwa sisi inawezekana (wanaume) sasa tulijaalie suala hili kwa mwanamke ambae anajaribu kumridhisha mumewe, namzungumzia mwanamke hapa kwa sababu ana njia nyingi za kumridhisha mumewe kwa mfano: mkono, mguu kiuno au hata mdomo. Hivo wanaweza kuvitumia na khafla mume akajikuta tiari amekusha.Na mke akawa bado hajatokwa na chochote, Vipi hapa atahitajika kukonga na yeye. In Shaa Allaah liwe lenye kufahamika suala hili.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Tunavyoliona na kulisoma swali lako ni kwamba halipo wazi na kufuma pale panapotaka kuulizwa. Ni nasaha zetu kwa waulizaji wapendwa wawe ni wenye kuuliza swali moja kwa moja badala ya kuzunguka sana na hivyo hata kueleweka vibaya na wenye kujibu au kutoeleweka kabisa.

 

Ni muhimu ieleweke kuwa Wanazuoni wote wa Salaf (waliopita) na khalaf (wa sasa) wameafikiana kuwa ni wajibu kujitwaharisha kwa kuoga kwa yeyote yule (mwanamme na mwanamke) anayetokwa na manii akiwa usingizini au akiwa macho au kwa kujamiiana na pia pale mwanamke anapopata ada yake au damu anayotokwa baada ya uzazi. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Umm Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Ummu Sulaym (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) aliuliza: “Ee Rasuli wa Allah! Allaah Haoni haya juu ya ukweli. Mwanamke anaona katika usingizi kama anavyoona mwanamme, je ni juu yake kuoga?” Akasema: “Ndio, anapoona maji” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Wametofautiana Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anuhum) kuhusu kuwajibika kuoga kwa kujimai. Miongoni mwao ni wale wenye rai kuwa zinapokutana ngozi mbili zilizotahiriwa basi inakuwa wajibu kwa wote wawili kukoga ikiwa wametokwa na manii au la. Hii ni rai ya Faqihi wakubwa na  hii ndiyo kauli ya Jamhuwr (‘Ulamaa wengi).

 

 

Rai ya pili ni ile inayosema si wajibu kukoga ikiwa hawakushusha, na hii ni kauli ya baadhi ya watu wa Dhwaahiriy.

 

Dalili zilizotolewa kwa wenye kuunga kauli ya kwanza ni kama zifuatazo:

 

 

1.  Amepokea Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema: “Anapokaa mmoja wenu baina ya viungo vinne vya mwili wake (yaani mkewe) na akafanya juhudi (jimai), basi inakuwa wajibu kuoga” [Ahmad na Muslim]

 

 

2.  Amesema Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Anapokaa baina ya sehemu zake nne na zikakutana ngozi mbili zilizotahiriwa imekuwa wajibu kwao kuoga”.

 

 

3.  Anahadithia Abu Muwsaa Al-Ash‘ariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu): Kulizuka tofauti baina ya kikundi cha Muhajirina na kipote cha Answaariy, na tofauti yao ilikuwa  Answaariy wakisema: “Josho la janaba linakuwa wajibu tu pale wanapotokwa na manii”. Lakini Muhajirina wakasema: “Pindi mtu anapostarehe na mwanamke kuoga inakuwa wajibu (ikiwa atashusha au la)”. Abu Muwsaa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema: “Sawa, mimi nitawatosheleza kwa hilo”. Abu Muwsaa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) “Nilisimama na nikaelekea kwa ‘Aishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)  na kutaka ruhusa ambayo alinipatia”. Nikamwambia: “Ee Mama wa Waumini! Nataka kukuuliza kuhusu jambo fulani lakini naona haya kukuuliza”. Akasema: “Usione haya kuniuliza kuhusu jambo ambalo unaweza kumuuliza mamako aliyekuzaa, kwani mimi pia ni mama yako”. Kwa hili nikasema: “Ni kitu gani kinachofanya kuoga kunakuwa wajibu kwa mtu?” Akanijibu: “Umekuja kwa mtu mwenye ujuzi wa hilo. Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   amesema: ‘Yeyote mwenye kukaa kwenye sehemu nne (za mwanamke) na sehemu za siri zikagusana baina yao, josho la janaba itakuwa ni wajibu’” [Muslim, Ahmad na Maalik kwa maneno tofauti kidogo]

 

 

4.   Dalili ya kauli ya pili ni Hadiyth hii: Aliulizwa ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akaambiwa: “Waonaje mtu anapostarehe na mkewe lakini hakushusha (hakutokwa na manii)?” Akajibu: “Atatawadha kama anavyotawadha mmoja wenu kwa ajili ya Swalaah, nimemsikia hayo Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    [Imenukuliwa na Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy katika kitabu chake Bidaayatul Mujtahid, Mjalada wa kwanza]

 

 

Wenye kauli ya kwanza wanafuata Hadiyth ya kwanza na nyenginezo ambao tumezitaja na kusema kuwa hukumu ya Hadiyth inayotumiwa na wenye kauli ya pili imefutwa. Na kutilia mkazo Hadiyth hiyo ya kwanza ni ile Hadiyth aliyopokea Ubayy bin Ka‘ab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: “Hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    alitoa ruhusa hiyo mwanzo wa Uislamu kisha akaamrisha kuoga (kwa wenye kujamiiana)” [Abu Dawuud].

 

 

Na pia maelezo ya ‘Aishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)  alipomjibu Abu Muwsaa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuhusu hilo.

 

 

Katika Hadiyth tulizozitaja hapo juu sehemu zilizotahiriwa ni utupu wa mwanamme na sehemu za siri za mwanamke. Hivyo, pindi utupu wa mwanaume unapoingia katika sehemu ya siri ya mwanamke, josho la janaba linakuwa wajibu kwa wote wawili. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

  وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا ۚ  

Na mkiwa na janaba basi jitwaharisheni.  [Al-Maaidah: 6]

 

 

Kusherehesha kuhusu mas-ala haya, Ash-Shaafi‘iy amesema: “Katika lugha ya Kiarabu, janaba inamaanisha tendo aina yoyote ya kukutana kimwili baina ya mume na mke, bila kujali kama manii yametoka au la. Ikiwa mtu atasema: “fulani na fulani” wana janaba kwa sababu ya kadhaa na kadhaa’, hii inamaanisha janaba kwa njia yoyote ya kujamiiana baina yao (mume na mke) hata ikiwa hakutakuwa na kushusha. Hakuna anaye kataa kuwa zinaa ambayo ina adhabu maalumu ni kukutana kimwili baina ya wawili hata ikiwa hakuna kutokwa kwa manii”.

 

Na hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Anatueleza kinaganaga pale Aliposema:

 

  وَلَا جُنُبًا إِلَّا عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىٰ تَغْتَسِلُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا  

  na wala mkiwa mna janaba isipokuwa mmo safarini mpaka muoge josho. Na mkiwa wagonjwa au safarini au mmoja wenu ametoka msalani au mmewagusa wanawake kisha hamkupata maji, basi mtayammam (ikusudieni) ardhi safi ya mchanga,[An-Nisaa: 43]  

 

 

Na maana ya:

 

mmewagusa wanawake: 

 

ni kukutana kimwili baina ya mume na mke kama anavyosema Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma)

 

Kwa hivyo hapana shaka kuwa ni lazima kuwe na kuingiliana kwa sehemu za siri ili mtu iwe ni wajibu kuoga, lakini ikiwa ni kugusana kama alivyosema muulizaji kwa kucheza cheza au kupigana busu au kushikana shikana au jambo jengine lolote mbali na kuingiliana hakutakuwa na uwajibu kwa mke kukoga ikiwa hatotokwa  chochote vilevile na mume kadhalika. Lakini ikiwa mwanaume kama ulivyosema atatokwa na maji ya uzazi basi itabidi akoge. ‘Ulamaa wote wamekubaliana (wameafikiana) katika hili.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

Share