Vidani Vya Fedha Vinafaa Kuvaliwa Na Wanaume Na Kuswali Navyo?

SWALI:

 

Assalaam aleykum,

 

Natumai hali zenu zote ni nzuri, nimefurahi sana waislam kupata website hii inayotupa mafunzo mbalimbali ya dini yetu. Swali langu ni kuhusu vidani vya madini ya silver ambavyo vijana wengi wa kiislam wanavivaa, je ni halali kuvaliwa? Na ikiwa kuruhusiwa kuswali navyo? Au kuna uzito Fulani (grams) ni ruhusa?

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuvaa vidani wanaume.

Vidani aina yoyote ile kama ni dhahabu, fedha, shaba na kadhalika havifai kwa mwanamme kwani hayo ni mapambo kwa wanawake. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza pamoja na kuwalaani wanaume wote wanaojifananisha na wanawake na kinyume chake. Mbali na hivyo uvaaji wa vidani ni ‘amali ya makafiri ambao pia sheria imetutaka tuwe tofauti nao.

 

Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake na wanawake wanaojifananisha na wanaume” (al-Bukhaariy, Abu Dawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

 

Hivyo, ni vyema kabisa kwa Muislamu mwanamme aachane na kuvaa vidani. Kwa hiyo, haifai kuvivaa katika Swalah au wakati mwingine wowote.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share