Skip navigation.
Home kabah

Tofauti Ya Takbira Za Iydul-Fitwr Na Iydul-Adhwhaa

SWALI:

Assalaam Alaikum.

Naomba mnisaidie tofauti ya Takbira za eid al fitri na eid al hajj.   Wassalaam alaikum

 

 

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwa kauli ambayo ina nguvu zaidi hakuna tofauti baina ya takbira za ‘Iydul-Fitwr na ‘Iydul-Hajj. Katika Swalah za ‘Iyd zote mbili Imamu anapiga takbira saba (7) baada ya Takbiyratul Ihraam na takbira tano (5) baada ya takbira ya kuinuka kutoka katika sijdah. Hii ni kulingana na Hadiyth ya ‘Amru ibn Shu‘ayb kutoka kwa babake kutoka kwa babu yake kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa takbiyr kumi na mbili (12) katika ‘Iyd; saba katika rakaa ya kwanza na tano katika rakaa ya mwisho, wala hakuswali kabla yake wala baada yake (Ahmad na Ibn Maajah).

Na hii ndio kauli yenye nguvu na sahihi zaidi iliyopokewa kutoka kwa Maswahaba, Tabiina, Maimamu na wanachuoni. Haijapokewa kwa njia hata dhaifu kinyume nayo.

Ama ikiwa umekusudia takbira ambayo inapigwa baada ya kwisha Ramadhaan hadi Swalah ya ‘Iydul-Fitwr na takbira ambayo inapigwa kuanzia jioni mwa siku ya ‘Arafah hadi Ayaamut-Tashriyq ambayo ni masiku matatu baada ya ‘Iydul-Hajj, basi hazina tofauti ya maneno yake ambayo kwa mujibu wa Maswahaba ni kuwa walikuwa wakisema: “Allaahu Akbar Allaahu Akbar, La Ilaaha Illa Allaah, Allaahu Akbar Allaahu Akbar WaliLlaahil Hamd”

 Kwa hivyo, makusudio ya swali lako yakiwa ni kuhusu maneno ya takbira katika sikukuu hizo mbili, basi yako sawa na hayana tofauti kama tulivyoeleza hapo.

Na Allaah Anajua zaidi