Anataka Kuhiji Lakini Ana Deni La Nyumba Benki

SWALI:

Assalam alekum,

Swali langu ni: - Mimi nina deni la nyumba bank, hali ninaweza kwenda kuhiji? Ninaomba msaada wenu kwani mimi sina elimu ya kutosaha. Waasalam


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran, dada yetu kwa swali lako zuri ambalo linafaa lieleweke ili ule utata ambao upo uondoke na watu wajue ule uhakika.

Ieleweke kuwa Hijjah ni nguzo ambayo inampasa kuitekeleza yule Muislamu mwanamume au mwanamke aliye na uwezo wa kuiendea njia hiyo – kwa kuwa na hela za kutosha kwa safari hiyo, kuwa na usalama katika safari, kuacha masrufu kwa wale wanaokutegemea huku nyuma unapoondoka.

Katika hilo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Na Allaah Amewawajibisha watu wafanye Hijjah katika Nyumba hiyo kwa yule awezaye kufunga safari kwenda huko” (3: 97).

Na katika Hadiyth ndefu ya ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuhusu Jibriyl (‘Alayhis Salaam) aliyekuja kumuuliza maswali Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alipoulizwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Uislamu alisema, “…na kwenda Hijjah ukiweza kufanya hivyo” (Muslim, At-Tirmidhiy na Abu Daawuud).

Kawaida ya mkopo wowote inakuwa mkopesha na mkopeshwa na hasa ikiwa ni kutoka Benki wanaandikia kuhusu malipo hayo. Kwa mfano, ikiwa kila mwezi mdaiwa anatakiwa kulipa shilingi 100,000 kwa muda wa miaka kumi. Ikiwa mdaiwa ana pato zaidi ya hilo analolipa akaweza kuweka akiba ya hela kwa kiasi ambacho kinatimiza masharti ya kwenda Hijjah kama tulivyotaja hapo juu kutakuwa hakuna shida yoyote kwake kwenda Hijjah, japokuwa kimsingi ana deni.

Ikiwa kwenda kwake Hijjah kutamfanya asilipe deni lakeanalodaiwa au aruke kwa miezi kadhaa itakuwa bado hajakamilisha masharti kwa yeye kufunga safari hiyo ya mara moja katika uhai wake.

Tanbihi: Tunawapatia nasaha dada na ndugu zetu kuwa mikopo ya Benki za kawaida ina riba ambayo mdaiwa anaipatia banki. Hivyo, kuifanya mikopo aina hiyo kuwa haramu. Mara nyingi watu wamefilisika kwa kukiuka agizo la Muumba, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Tuwe na tahadhari sana katika mas-ala hayo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share