Michezo Gani Inayoruhusiwa Kishari’ah Na Ipi Isiyoruhusiwa?

 

SWALI:

 

Ni michezo gani dini inayokubaliana nayo na ipi dini isiyokubaliana nayo? Na kuna masharti yoyote?

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu michezo inayokubalika katika dini na ile isiyokubalika.

Hakuna uharamu wowote kwa mtu kucheza mchezo wowote ule ambao unakwenda sambamba na shari’ah, kuangalia au kuwa shabiki kwa mipaka ya Uislamu.

 

Tufahamu kuwa Uislamu ni Dini ya vitendo wala sio ya nadharia. Inawachukulia wanaadamu kama wanaadamu. Kwa ajili hiyo, Uislamu ni Dini na dunia. Kuna namna nyingi ya michezo waliowekewa Waislamu na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kujifurahisha na kujipumzisha, nayo kwa wakati huo yanaitayarisha nafsi zao kuweza kufanya ‘Ibaadah zao na wajibu wao kwa nashati kubwa zaidi na hima kubwa zaidi. Nyingi katika hizo ni Riyadha zinazowazoweza kupambana na mazito, na kuwatayarisha kwa vita vya Jihaad na kupigana kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka. Katika michezo iliyo halali ni kama ifuatayo:

 

1.     Mbio, naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anashindana na mkewe ‘Aa’ishah (Radhiya Allaahu ‘anha).

 

2.     Miereka, naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alishindana na Rukaana na kumshinda (Abu Daawuud na Ahmad).

 

3.     Kurusha mishale. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwapita Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakishindana kurusha mishale, naye akawahimiza kwa kuwaambia: “Rusheni nami ni pamoja nanyi” (al-Bukhaariy).

 

4.     Kucheza na mikuki.

 

5.     Kupanda farasi.

 

6.     Kuogelea pia kumehimizwa sana.

 

7.     Kuwinda kwa kutumia ala kama mishale, mikuki na kwa sasa bunduki.

 

Uislamu pia umeweka kanuni za kijumla ya kuufanya mchezo wowote ule kuwa halali au haramu. Kanuni hizo ni kama zifuatazo:

 

1.     Uhalali unategemea manufaa au hasara inayopatikana. Ikiwa manufaa ni makubwa zaidi mchezo utakuwa halali na lau itakuwa kinyume chake basi utakuwa ni haramu.

 

2.     Mchezo wowote wenye kamari unakuwa ni haramu.

 

3.     Isicheleweshwe Swalah kutoka kwa wakati wake kwa ajili ya mchezo wowote ule. Hatari hiyo inakuwa kubwa kwa kupoteza wakati na kujishughulisha watu kukosa kutekeleza wajibu wao.

 

4.     Mchezaji ahifadhi ulimi wake wakati wa kucheza, asitukane na kutokwa na maneno machafu.

 

5.     Mchezo kama wa ngumi ni mchezo uliokuwa haufai kwani kuna kudhuriuana uso ambako kumekatazwa na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuleta madhara ya ubongo na mifano ni mingi.

 

6.     Mavazi yalingane na stara ya iliyowekwa kishari’ah. Haifai kuvaa vikaptula vinavyonyesha mapaja ya mwanaume kama ilivyo kwenye mpira wa miguu na mbio na pia nguo za kubana zenye kuonyesha maungo ya ndani kama kwenye michezo ya kukimbia, kuogelea, michezo ya viungo kama jimnastiki (sarakasi) n.k.

 

 

7.     Wanawake hawakatazwi kucheza maadam wako wenyewe, na wawe wamevaa stara za kishari’ah. Hata hivyo wanawake haiwapendezei kucheza michezo ya nguvu iliyo kinyume na maumbile yao kama mieleka, mpira wa miguu na mingine ambao wanawake wa siku hizi wameanza kuiga.

 

Ikiwa moja katika masharti yaliyo juu haikutimizwa, basi mchezo huo utakuwa ni haramu. Hivyo, uhalali na uharamu kucheza mchezo wowote itagemea na vigezo vilivyo juu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share